Petro Kanisio
Petro Kanisi (kwa Kiholanzi Pieter Kanijs, au Kanisius, au Kanîs) alizaliwa Nijmegen (leo nchini Uholanzi) tarehe 8 Mei 1521 akafariki Freiburg (Uswisi) tarehe 21 Desemba 1597.
Alikuwa mtawa, mwanateolojia na padri wa Kanisa Katoliki.
Alitangazwa na Papa Pius IX kuwa mwenye heri mwaka 1864, halafu na Papa Pius XI kuwa mtakatifu na mwalimu wa Kanisa tarehe 21 Mei 1925.
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe ya kifo chake 21 Desemba[1], lakini Ujerumani tarehe 27 Aprili.
Kwa kawaida anachorwa akiwa na fuvu la kichwa, sanamu ya Yesu msulubiwa na katekisimu.
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Petro alizaliwa na meya wa Nijmegen, katika Dola takatifu la Roma.
Akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Cologne, Ujerumani, alikuwa akitembelea mara kwa mara Wakartusi wa Mt. Barbara, wamonaki waliochangia sana maisha ya Kiroho ya Wakatoliki, akishirikishana hasa na Yohane Lansperger na Nikola wa Esche; vilevile alishirikiana na watu walioishi Kikristo kadiri ya “Devotio moderna” (yaani Juhudi za kisasa).
Tarehe 8 Mei 1543, siku ya kutimiza miaka 22, akiwa huko Mainz, Ujerumani, baada ya kushiriki mazoezi ya kiroho yaliyoongozwa na Petro Favre, alikuwa Mholanzi wa kwanza kujiunga na Shirika la Yesu na mwanashirika wa nane.
Alipewa upadrisho huko Cologne mwaka 1545.
Mapema, mnamo Juni 1546 aliitwa na askofu wa Augsburg, kardinali Otto Truchsess von Waldburg, ashiriki Mtaguso wa Trento kama mtaalamu wa teolojia.
Mwaka 1548, mwanzilishi wa shirika, Ignasi wa Loyola, alimuita Roma, Italia, akamilishe malezi yake ya kiroho, halafu akamtuma kwenye shule ya bweni ya Messina, Italia, atoe huduma duni za nyumbani.
Tarehe 4 Oktoba 1549 alipata udaktari wa teolojia huko Bologna, Italia, alipofundisha pia kwa muda mfupi.
Kabla ya hapo, tarehe 2 Septemba alimtembelea Papa Paulo III ili kupata baraka kwa ajili ya utume mpya aliopangiwa Ujerumani, akahiji katika Basilika la Mt. Petro huko Vatikano ili mitume Petro na Paulo wamuimarishie moja kwa moja baraka hiyo.
“Huko nilihisi kujaliwa faraja kubwa na uwepo wa neema kupitia waombezi hao. Walithibitisha utume wangu Ujerumani na walionekana kunishirikisha msaada wa wema wao kama mtume wa Ujerumani. Ee Bwana, wewe unajua kwa njia nyingi kiasi gani, na mara ngapi siku hiyohiyo ulinikabidhi Ujerumani, ambao baadaye niliendelea kuushughulikia nikiwa tayari kuishi na kufa kwa ajili yake”.
Ni kwamba kazi aliyopangiwa, yaani kuhuisha imani Katoliki katika nchi kubwa na ndogo zilizounda Dola la Kijerumani, ilionekana haiwezekani kwa sababu ya Urekebisho wa Kiprotestanti uliozidi kuenea. Iliwezekana tu kwa njia ya sala, kutokana na urafiki wa dhati na Yesu Kristo katika mwili wake, yaani Kanisa, uliolishwa na fumbo la mwili wake, yaani Ekaristi. Ndiyo sifa ya maisha ya kiroho ya Petro.
Kwa mfano katika shajara yake, tarehe 4 Septemba 1549 aliandika kwamba alialikwa na Yesu kunywea Moyo wake wazi halafu akapewa nguo yenye vipande vitatu vilivyoitwa amani, upendo na udumifu: ndizo silaha alizozitumia katika utume wake huo.
Kwanza alifanya kazi kwa miaka kadhaa katika Ufalme mdogo wa Bavaria.
Baada ya kuteuliwa mkuu wa kwanza wa kanda ya Ujerumani ya Wajesuiti, wadhifa alioushika hadi mwaka 1569, alitoa mchango mkubwa katika urekebisho wa Kikatoliki hasa kwa kuanzisha vyuo vingi vya shirika, hata mwaka 1897 Papa Leo XIII alimtaja "mtume wa pili wa Ujerumani" baada ya Mt. Bonifas. Uwepo wa Wakatoliki wengi Ujerumani na Austria hadi leo unatokana kwa kiasi kikubwa na kazi yake.
Kanisi alikuwa gombera na mwalimu wa teolojia katika chuo kikuu cha Ingolstadt, akifanya pia kazi ya kuimarisha imani na kurekebisha maadili ya waamini wa kawaida.
Kwa muda mfupi (1554-1555) aliongoza jimbo la Wien, Austria, ingawa alikataa kuwa askofu ili aweze kuendelea na utume wake huko na huko. Akiwa Wien alifanya uchungaji katika hospitali na magereza hata nje ya mji, akaandaa Katekisimu yake.
Mwaka 1556 alianzisha shule ya bweni huko Praha, leo mji mkuu wa Ucheki.
Mwaka 1557 huko Worms, Ujerumani, alishiriki majadiliano ya kiimani na wataalamu wa Kiprotestanti, akiwemo Filipo Melanchthon.
Mwaka 1558 alikuwa balozi wa Papa nchini Polandi, na mwaka 1560 aliongozana na balozi mwingine, Kardinali Stanislaw Hozjusz kuongea na Kaisari Ferdinand I.
Mshauri wa mapapa na watawala, alishiriki mara mbili Bunge la Augsburg (1559 na 1565).
Alishiriki pia vikao vya mwisho vya Mtaguso wa Trento alipochangia masuala mbalimbali (1562).
Aliheshimiwa kwa adabu yake, iliyomfanya akwepe kuita Waprotestanti "wazushi" katika mahubiri yake. Alijua kutofautisha sababu za kukosa imani sahihi, hata aliarifu uongozi wa Kanisa la Roma kuwa wengi katika umati wa Wajerumani walioingia Uprotestanti hawakustahili kulaumiwa.
Alipenda elimudini na kusoma hasa Biblia na vitabu vya mababu wa Kanisa. Alikusanya na kutoa kitaalamu maandishi yote ya Sirili wa Aleksandria na ya Leo Mkuu, mbali ya barua za Jeromu na sala za Nikola wa Flue.
Pia alitoa vitabu vingi vya ibada kwa lugha mbalimbali, akisisitiza kushiriki liturujia lakini pia kuwa na sala ya binafsi. Hatimaye aliandika maisha ya watakatifu wa Uswisi na hotuba nyingi.
Vilevile aliandika vitabu vingine ili kufundisha imani na maisha ya Kiroho kulingana wa mahitaji ya walengwa.
Lakini kitabu chake bora ni Katekisimu, ambayo ilitungwa kama jibu kwa Martin Luther na kutolewa kuanzia mwaka 1555 hadi 1558 kwa jina la Summa doctrinae christianae, ilirudia kuchapwa mara 200 hivi wakati wa maisha yake tu. Ilikuwa na matoleo matatu kulingana na kiwango cha elimu cha wasomaji. Ilieleza imani Katoliki kwa ufupi na uwazi, kwa mtindo wa maswali na majibu na kwa kutegemea misamiati ya Biblia, bila kubishana na Waprotestanti.
Ilitafsiriwa pia katika lugha mbalimbali na kutolewa mara 400 na zaidi.
Mwaka 1580 alianzisha huko Freiburg (Uswisi) chuo cha Mt. Mikaeli, ambapo alielekeza nguvu zake za mwisho kuhubiri na kuandika na ambapo alifariki tarehe 21 Desemba 1597 na hatimaye kuzikwa.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
Maandishi
[hariri | hariri chanzo]- (1555) Summa doctrinae christianae
Toleo refu (lenye madondoo ya kuthibitishia):
- Gombo la 1: Imani, Tumaini, Upendo na Amri za Kanisa
- Gombo la 2: Sakramenti
- Gombo la 3: Utakaso wa Kikristo, matendo mema, maadili bawaba, vipaji na Matunda ya Roho Mtakatifu, Heri Nane, Mashauri ya Kiinjili n.k.
- (1556) Catechismus minimus
- (1558) Parvus catechismus catholicorum
- De verbi Dei corruptelis (1571)
- De Joh. Baptista (1577)
- De Maria Virgine (1577)
- Notae in evangelicas lectiones (magombo 2, 1591–1593)