Nenda kwa yaliyomo

Kupashwa habari

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kupashwa habari Maria)
Kupashwa Habari, mchoro wa msanii asiyejulikana, 1420 hivi, Museu Nacional d'Art de Catalunya, Barcelona, Hispania.
Kanisa la Kiorthodoksi la Kupashwa Habari, lililojengwa Nazareth mahali panapodhaniwa Maria alitokewa.
Kupashwa Habari kadiri ya El Greco, takriban 15901603, Ohara Museum of Art, Kurashiki, Japani.
Mfululizo wa kurasa juu ya Yesu
Yesu
Yesu Kristo na Ukristo

Umwilisho  • Utoto wa Yesu  • Ubatizo
Arusi ya Kana • Utume wa Yesu • Mifano ya Yesu  • Miujiza ya Yesu
Kugeuka sura • Karamu ya mwisho • Msalaba wa Yesu  • Maneno saba
Kifo cha Yesu  • Ufufuko wa Yesu
Kupaa mbinguni  • Ujio wa pili
Injili  • Majina ya Yesu katika Agano Jipya  • Yesu kadiri ya historia  • Tarehe za maisha ya Yesu • Kristolojia

Mazingira ya Yesu

Wayahudi • Kiaramu • Bikira Maria • Yosefu (mume wa Maria) • Familia takatifu • Ukoo wa Yesu • Ndugu wa Yesu • Yohane Mbatizaji

Mitazamo juu ya Yesu

Mitazamo katika Agano Jipya · Mitazamo ya Kikristo • Mitazamo ya Kiyahudi • Mitazamo ya Kiislamu • Yesu katika sanaa

Kupashwa Habari kadiri ya Salomon Koninck, 1655, Hallwyl Museum, Stockholm, Uswidi.
Kupashwa Habari kadiri ya Murillo, 16551660, Hermitage Museum, Saint Petersburg, Urusi.

Kupashwa habari kwa Bikira Maria kwamba atapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na hatimaye kuzaa mtoto wa kiume, jina lake Yesu, ni tukio la kuheshimika sana kati ya Wakristo na Waislamu kutokana na masimulizi ya Injili na Kurani.

Katika Injili

[hariri | hariri chanzo]

Ni hasa sura ya 1 ya Injili ya Luka inayoripoti tukio hilo baada ya lile lililotangulia miezi sita, la Malaika Gabrieli kumpasha habari mzee Zakaria kwamba mke wake mkongwe tena tasa, Elizabeti, atamzalia mtoto wa kiume, Yohane.

26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28 Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe." 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30 Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho." 34 Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?" 35 Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36 Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37 Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu." 38 Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.

Ingawa Injili ya Mathayo 1:18-21 inategemea chanzo tofauti, habari zake zinalingana vizuri na zile za Luka.

Katika Kurani

[hariri | hariri chanzo]

Tukio hilohilo linasimuliwa na Qur'an, Sura 003:045 (Al-i-Imran – Familia ya Imran) aya 45–51:

45 Tazama! Malaika alisema: "Ewe Mariamu! Allah alikupa habari njema ya Neno kutoka kwake: jina lake litakuwa Kristo Yesu, mwana wa Mariamu, wa kuheshimika katika ulimwengu huu na ahera, na mmoja kati ya walio karibu zaidi na Allah;"

Hata Sura 019:016 (Maryam – Mariamu) aya 16–26 inahusika na tukio hilo ambalo mapokeo ya Kiislamu yanashikilia lilitokea katika mwezi wa Ramadhani.

Katika liturujia ya Kikristo

[hariri | hariri chanzo]

Wakristo wengi, labda tangu karne ya 2[1] wanaadhimisha tukio hilo tarehe 25 Machi[2], na ndicho chanzo cha kuadhimisha Noeli miezi tisa baadaye, tarehe 25 Desemba.

Waorthodoksi hawasogezi sikukuu hiyo, hata kama inagongana na Ijumaa Kuu. Kama ni Pasaka wanasherehekea pamoja huo Umwilisho na Ufufuko wa Yesu. Kwao ni mojawapo ya Sherehe kuu. Kumbe Kanisa la Roma linaruhusu kuisogeza ikiangukia Jumapili ya Kwaresima, Juma Kuu au Oktava ya Pasaka, mradi isiachwe.

Denis Mfupi alipoanzisha hesabu ya miaka kuanzia ujio wa Kristo, alipanga mwaka uanze tarehe hiyo muhimu hivyo. Mwanzo wa mwaka ulihamia tarehe 1 Januari katika karne ya 16.

Ni kwamba kwa imani hiyo, ndilo tukio la Neno wa Mungu kutwaa mwili tumboni mwa Bikira Maria na kuanza kuwa binadamu (kwa msamiati wa teolojia: Umwilisho). Hivyo, katika utimilifu wa nyakati, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Mwana pekee na wa milele wa Mungu alifanyika mtu kwa ajili ya watu na kwa wokovu wao.

Ndiyo sababu tukio hilo linakumbukwa mfululizo, kwa mfano kwa sala ya Salamu Maria, kwa ile ya Malaika wa Bwana, kwa Akatistos n.k.

Pia sanaa zimetumika sana kutokeza mshangao wa waamini kwa habari hiyo ya ajabu kuliko zote.

  1. Michael Alan Anderson, Symbols of Saints (ProQuest 2008 ISBN 978-0-549-56551-2), pp. 42–46
  2. Martyrologium Romanum

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kupashwa habari kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.