Karl Peters
Karl Peters (27 Septemba, 1856 – 10 Septemba, 1918) alikuwa Mjerumani aliyeanzisha koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
[hariri] Utoto na masomo
Peters alizaliwa mwaka 1856 katika Ujerumani ya Kaskazini kama mtoto wa nane wa mchungaji wa Kilutheri. Baada ya kumaliza shule ya sekondari alisoma historia na falsafa kwenye vyuo vikuu vya Göttingen, Tübingen na Berlin. Akiwa chuoni alivutwa na mafundisho ya Udarwini wa Kijamii yanayotangaza kwamba ni haki na halali kama wenye nguvu duniani wanatawala na kukandamiza watu dhaifu. Baada ya masomo yake ya historia alifanya kazi London (Uingereza) mnamo 1882/1883. Alijifunza mengi kuhusu himaya ya kikoloni ya Uingereza na utawala wake juu ya nchi nyingi.
[hariri] Itikadi ya ukoloni
Peters alisikitika kuwa Ujerumani haikuwa na koloni hadi wakati ule. Aliamini ya kwamba koloni huongeza utajiri na enzi ya nchi yenye koloni jinsi ilivyoonekana katika mfano wa utawala wa Kiingereza juu ya India. Alitaka kuwapatia Wajerumani nafasi waliyostahili machoni pake kati ya mataifa ya Ulaya.
Aliporudi Ujerumani mwaka 1883 alijishughulisha na siasa ya kudai koloni kwa Ujerumani. Peters alikuwa amejifunza habari za Afrika ya Mashariki alipokaa Uingereza. Hadi wakati ule hakukuwa na koloni la Wazungu katika Afrika ya Mashariki isipokuwa pwani ya Msumbiji iliyotawaliwa na Ureno, lakini nchi za Ulaya zilikuwa zinaandaa mkutano wa Berlin ili kugawana Afrika. Aliamini ya kwamba watu weusi ni dhaifu, hivyo wanapaswa kutawaliwa na wale weupe wenye nguvu.
[hariri] Peters alianzisha Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Machi 1884 Peters aliunda "Shirika la Ukoloni wa Kijerumani" (Gesellschaft für Deutsche Kolonisation). Wakati huo himaya pekee ya kutambuliwa kimataifa ilikuwa Usultani wa Zanzibar. Kamati kuu ya shirika ilimpa wito wa kupata maeneo katika Afrika ya Mashariki kwa imani ya kuwa utawala wa Zanzibar ni wa pwani tu.
Peters alipoandaa safari yake mataifa ya Ulaya yalikuwa yakiandaa mkutano wa Berlin kuhusu masuala ya Kongo. Mkutano huu, ulioanza Disemba 1884, ulisababishwa na mipango ya mfalme Leopold II wa Ubelgiji kujijengea himaya ya binafsi katika beseni ya Kongo akigongana na shabaha za Ureno na Uingereza.
[hariri] Safari ya Peters ya Usagara
Tarehe 10 Novemba, 1884 Peters alifika Unguja pamoja na wanakamati wawili ili aendelee kuzunguka kwenye bara la Tanganyika. Serikali ya Kijerumani ya Chansella Bismarck haikukubali mipango yake kwa sababu iliogopa vurugu kwenye mkutano ulioalikwa tayari. Hivyo Peters alipofika kwenye ubalozi wa Ujerumani mjini Zanzibar alipokewa kwa barua kutoka Berlin iliyosema ya kwamba hawezi kutegemea msaada wowote kwani juhudi zake ni nje ya siasa ya nchi.
Peters akimwogopa Sultani pamoja na Waingereza alivuka kwa siri kutoka Unguja kwenda bara. Alifaulu kutembelea masultani au machifu kadhaa waliotia aina ya sahihi kwenye karatasi walizoonyeshwa na Peters. Karatasi hizi ziliandikwa kwa lugha ya Kijerumani zikasema ya kwamba chifu fulani aliweka eneo lake chini ya mamlaka ya shirika la Kijerumani pamoja na kulipatia shirika hilo haki ya kutumia maeneo na malighafi yote. Kuna uhakika ya kwamba machifu hawakuelewa walichofanya kwa kuchora alama zao kwenye karatasi hizo; walifikiri ya kwamba waliahidiwa ulinzi kutoka kwa mtawala wa mbali ambaye labda siku moja atakuwa na faida kwao, lakini hawakuelewa ya kwamba walitamka kibali kwa wageni kutawala nchi. Peters mwenyewe alisimulia jinsi alivyowapa machifu pombe kali hadi wakawa tayari kuchora alama zao kwenye karatasi walizoonyeshwa bila ya kuelewa maana yake. Kwa njia hiyo katika muda mfupi kati ya 23 Novemba na 17 Desemba 1884 Peters alipata hati kutoka machifu wa Usagara, Nguru, Useguha na Ukami kwa ajili ya shirika lake, jumla eneo la km² 140,000.
[hariri] Peters kukubaliwa na serikali ya Ujerumani
Peters alirudi Ujerumani Februari 1885 katika siku za mwisho wa Mkutano wa Berlin. Aliomba barua ya ulinzi kutoka serikali kwa ajili ya maeneo aliyodai kuwa chini ya shirika la ukoloni. Chansella Mjerumani Bismarck aliendelea kumkatalia. Hati za Peters alizita karatasi zenye michoro bila thamani ya watu weusi. Lakini Peters alimtishia kuweka maeneo hayo chini ya ulinzi wa Leopold II wa Ubelgiji aliyekuwa tayari kupanua himaya yake ya Kongo iliyotambuliwa na serikali za Ulaya wakati wa mkutano. Kutokana na tishio hilo Bismarck alikubali, na Peters akapewa hati rasmi ya kifalme iliyoweka maeneo ya shirika la koloni chini ya ulinzi wa Dola la Ujerumani.
[hariri] Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki
Sultani wa Zanzibar hakufurahishwa na habari hizo akapinga kwa telegramu aliyotumia Berlin akidai ya kuwa Peters aliingia bila ya kibali na kufanya mikataba na machifu waliokuwa chini ya Zanzibar. Lakini baada ya kutoa barua za ulinzi Berlin iliona haja ya kusimama imara ikapeleka manowari 8 huko Zanzibar chini ya admeri Knorr. Sultani alikosa uwezo wa kushindana na jeshi hilo akakubali mikataba ya Peters na kwamba Wajerumani watumie bandari ya Daressalaam.
Wakati huo Peters mwenyewe alibaki Ujerumani na kuandaa upanuzi wa himaya ya shirika lake. Aliunda kampuni jipya la "Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki" lililochukua nafasi ya shirika la awali. Shirika lilituma maafisa kwa misafara mipya na kuongeza mikataba na machifu, na hivyo kuongeza eneo lililodaiwa na shirika.
Mwaka 1887 Karl Peters alirudi Afrika kama mkurugenzi wa utawala wa kampuni. Aliingia katika majadiliano na Sultani Barghash ibn Sa'id kuhusu utawala wa pwani. Baada ya kifo cha Bargash mwaka 1888 Peters alifaulu kumshawishi Sultani mpya Khalifa ibn Sa'id kulikodisha eneo lote la pwani kwa Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki.
[hariri] Msafara wa Emin Pasha na kulenga Uganda
Peters alirudi Ujerumani alipoombwa kuongoza msafara mpya wa kumtafuta Emin Pasha katika eneo kati ya Uganda na Sudan. Emin Pasha alikuwa Mjerumani kwa jina la Dr. Eduard Schnitzer akaingia katika utumishi wa serikali ya Misri, kuwa Mwislamu na gavana wa jimbo la Ikweta katika Sudan ya Kimisri. Baada ya mapinduzi ya Mahdi mwaka 1885 mawasiliano kati ya Emin Pasha na serikali ya Misri ilikatwa; kamati mbalimbali ziliundwa Ulaya kwa shabaha ya kumwokoa.
Peters alifika tena Afrika ya Mashariki mwaka 1889 akaanza msafara wake Juni 1889 kutoka Witu kwenye pwani ya Kenya iliyokuwa eneo lindwa chini ya Ujerumani. Bila ya Peters na watu wengine kujua, Emin Pasha hakuwa na haja yoyote ya kuokolewa lakini kwa hiari yake alikuwa tayari safarini kuelekea Bagamoyo pamoja na mpelelezi Mwingereza Henry Morton Stanley. Lakini Peters mbali na kumtafuta Emin Pasha alikuwa na shabaha yake mwenyewe: kupanua eneo la shirika lake. Kote alikopita alifanya mikataba mipya na machifu na masultani wa kikabila, kwa mfano na chifu wa Kavirondo (Kisumu) tarehe 1 Februari 1890.
Haya yote aliyafanya ingawa alijua ya kwamba serikali za Ujerumani na Uingereza ziliwahi kupatana kuhusu maeneo ya Afrika ya Mashariki zilipolenga kutafuta masilahi yao bila kuingiliana. Msafara wa Peters ulipita kabisa katika eneo lililoahidiwa kwa Uingereza. Lakini kufuatana na mapatano ya mkutano wa Berlin wa 1885 utawala wa nchi ya Ulaya katika Afrika ulitambuliwa mradi nchi iliweza kuonyesha utawala wake halisi. Kumbe Waingereza hadi kupita kwa Peters hawakuchukua hatua zozote za kujenga utawala wao katika sehemu za Kenya.
[hariri] Mkataba na Buganda
Kilele cha juhudi za Peters kilikuwa mapatano na Kabaka Mwanga II wa Buganda ya Machi 1890. Mwanga hakupendezwa na wamisionari Waingereza na Wafaransa walioshindana kati yao juu ya athari kubwa huko Buganda. Labda kwa matumaini ya kwamba huyu mfalme wa Ujerumani asiyejulikana kwake atakuwa msaada dhidi ya siasa za Waingereza lakini atakuwa mbali mno asiweze kuleta hasara, Kabaka alitia sahihi kwenye mapatano ya urafiki na ulinzi kati ya Ujerumani na Buganda. Tendo hilo lilitekelezwa na Karl Peters bila ya kibali wala ujuzi wa serikali yake nyumbani.
Peters alirudi kutoka Buganda kuelekea pwani. Tarehe 20 Juni 1890 huko Mpwapwa alikutana na Emin Pascha aliyekuwa tayari njiani kurudi kwake Ikweta. Mwezi wa Julai 1890 Peters alifika Bagamoyo.
[hariri] Jinsi alivyowatendea Waafrika
Katika msafara huo tabia za Peters zilionyesha jinsi alivyodharau Waafrika. Aliamini na kuandika kwamba Mwafrika hutawaliwa kwa kiboko tu. Kwake Mwafrika hakuwa mtu kamili. Akijiona mwenyewe ni bwana ambaye wenyeji wanapaswa kumtumikia aliwadharau. Alipopita Ugogo alikasirika juu ya Mgogo aliyecheka alipomtazama akinyoa ndevu zake, akaamuru apigwe kiboko. Tendo hilo liliwasababisha Wagogo kuchukua silaha ikawa vita watu wakauawa kwa wingi. Watu waliosafiri naye na kumjua walisimulia jinsi alivyowapiga mara nyingi mahamali au watumishi wake, akapewa nao jina “mkono damu”.
[hariri] Mwisho wa himaya ya Peters na shirika la ukoloni
[hariri] Uasi kwenye pwani dhidi ya utawala wa shirika
Wiki chache tu baada ya Peters kuanzisha safari yake ya kumtafuta Emin Pasha utawala wa shirika lake uliporomoka vibaya. Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki lilianza kutekeleza mapatano na Sultani wa Zanzibar kuhusu utawala wa pwani Agosti 1889. Kushushwa kwa bendera ya Sultani na kupandishwa kwa bendera ya shirika kulishtusha wenyeji wengi. Maafisa Wajerumani wa shirika walionyesha ukali wakidai utawala juu ya bandari. Haya yote yalisababisha mara moja ghasia. Wenyeji wakaongozwa na watu kama Abushiri na Bwana Heri. Uasi ulianza Pangani na kuenea kote pwani na kuwa vita kabisa. Shirika lilishindwa kupambana na upinzani huo wa wenyeji.
Hapo serikali ya chansella Bismarck iliingilia kati na kutuma manowari pamoja na wanajeshi waliokomesha upinzani wote. Maeneo ya shirika yaliwekwa chini ya serikali ya Ujerumani kama koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Utawala wa shirika la Peters ulikwisha.
[hariri] Mkataba wa Helgoland-Zanzibar kuingilia kati
Karl Peters aliporudi pwani mwezi Julai 1890 alipokea habari hizo pamoja na habari za mkataba wa tarehe 01.07.1890 kati ya serikali za Uingereza na Ujerumani zilimoelewana juu ya mipaka ya maeneo yao katika Afrika. Waingereza walikuwa wakishtushwa na matendo ya Peters ya kulenga Uganda. Serikali mpya ya Ujerumani ya chansella Caprivi iliona kuwa uhusiano mzuri na Uingereza ni muhimu kuliko kuongeza makoloni yaliyotazamwa na sehemu ya wanasiasa Ujerumani kwa mashaka.
Katika mkataba huo ulioitwa wa „Helgoland-Zanzibar“ Wajerumani walikubali kuwa Uganda, Zanzibar na nchi kaskazini ya mstari kati ya Ziwa Viktoria (Nyanza) na mlima Kilimanjaro pamoja na Witu yawe maeneo chini ya athira ya Uingereza. Waingereza waliahidi ya kwamba watamshawishi Sultani wa Zanzibar kuwapatia Wajerumani pwani ya sehemu iliyoitwa baadaye „Tanganyika“. Mapatano mengine yalihusu mipaka kati ya maeneo ya Waingereza na Wajerumani huko Afrika ya Magharibi na kisiwa cha Helgoland katika Bahari ya Kaskazini.
Peters aliona ya kwamba safari yake ilikuwa bure kabisa. Alisikitika na kufoka dhidi ya wanasiasa huko Berlin. Aliporudi Ujerumani tena alijiunga na wengine waliodai siasa kali ya ukoloni akawa mmojawapo wa waanzilishi wa „Jumuiya ya Wajerumani Wote“ (Alldeutscher Verband). Jumuiya hiyo ilitangaza utaifa mkali, chuki dhidi ya mataifa majirani na Wayahudi, dhaurau dhidi ya watu wenye rangi tofauti na madai ya kuwa Ujerumani ilistahili maeneo makubwa zaidi katika Ulaya na katika mabara mengine.
[hariri] Unyama wa Peters Kilimanjaro na kufukuzwa kwake
[hariri] Kamishna wa Kaisari
Baada ya Peters kurudi Berlin sehemu ya wanasiasa na magazeti walimshangilia na kumsheherekea kama shujaa wa kitaifa aliyezuiwa na waoga serikalini waliothamini uhusiano na watu wa nje kama Waingereza kuliko masilahi ya taifa.
Mwaka 1891 serikali iliamua kutumia maarifa ya Peters kwa kumpa cheo cha „Kamishma wa Kaisari katika eneo la Kilimanjaro“. Kazi yake kuu ilikuwa kuelewana na Waingereza kuhusu mpaka kamili kati ya sehemu za Wajerumani na Waingereza. Pia alikuwa mkuu wa utawala wa kikoloni wa eneo hilo.
[hariri] Mapenzi na mauti
Akiwa mwakilishi Mjerumani Kilimajaro Peters alikuwa na mabinti wenyeji aliowatumia kama wapenzi wake. Usiku wa tarehe 18 Oktoba 1891 Peters alimkuta binti Yagodja pamoja na Mabruk mtumishi wa kiume wakilala pamoja. Peters alikasirika mno akaita mara moja kamati ya mahakama akiwa yeye mwenyewe mwenyekiti. Mtumishi wake Mabruk alihukumiwa anyongwe. Yagodja alikimbia lakini akakamatwa Januari 1891 akapigwa viboko na kunyongwa naye.
Katika hasira yake Peters aliamuru hata kijiji cha binti huyo katika eneo la Rombo kichomwe moto. Wachagga wa Rombo walichukua silaha na kujitetea. Hasira ya Peters ilisababisha vita vya miezi kadhaa, vijiji vingi viliharibika na watu kufa.
[hariri] Kesi dhidi ya Peters
Aprili 1892 gavana Mjerumani von Soden mjini Daressalaam alipokea barua kutoka kwa mmisionari Mwingereza Smythies alimoandika sababu za vita Kilimanjaro kuwa ni unyama wa Peters. Von Soden alifanya utafiti akatuma taarifa juu ya matendo ya Peters kwenda Berlin. Gavana aliandika ya kwamba kwa maoni yake adhabu za kifo hazikuwa za haki kwa sababu Peters alitumia madaraka yake vibaya kwa kiburi na kisasi cha binafsi.
Awali serikali ya Berlin ilipendelea kutochukua hatua dhidi ya Peters. Gavana von Soden aliona aibu ya kuwa Peters alitenda maovu hayo wakati ana wajibu kwa ajili ya koloni, lakini hakuwa na uwezo wa kumwondoa madarakani kwa sababu ya cheo chake Peters. Von Soden alimsisitizia hadi mwishoni akajiuzulu na kuacha cheo chake mwaka 1893.
Mambo yalibadilika baada ya wabunge wa upinzani katika „Reichstag“ kupata habari za Peters na kuuliza maswali bungeni. Peters aliitwa arudi Berlin akapewa kazi wizarani. Kamati ya nidhamu ilifungua kesi dhidi yake na kumfanyia utafiti.
Peters alipoona mambo yanaweza kwenda vibaya aliomba kupumzika akahamia London. Kamati ya nidhamu iliamua tarehe 24 Aprili 1897 kuwa Peters alikosa. Alifutwa katika utumishi wa serikali pamoja na kupoteza haki za pensheni (malipo ya uzeeni). Mahakama kuu ya nidhamu ilirudia tamko hilo vikali zaidi Peters alipokata rufaa.
[hariri] Maisha ya Peters baada ya kuondolewa katika utumishi wa serikali
Alipokaa tena London Peters aliunda makampuni ya kutafuta dhahabu Kusini mwa Afrika akasafiri mara sita kwenda Zimbabwe, Msumbiji na Afrika Kusini. (Dr. Carl Peters Estates and Exploration Co. na South East Africa Ltd.).
Mwaka 1905 Kaisari Wilhelm II aliyekuwa mshabiki wa Peters alimpa haki ya kutumia tena kwa heshima yake cheo cha “Kamishna wa Kaisari”.
Mwanzo wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia alirudi Ujerumani kwa sababu makampuni yake katika himaya ya Uingereza yalinyimwa nafasi kama mali ya adui. Kaisari alimsaidia tena kwa kumpa pensheni kutoka makisio yake ya binafsi.
Karl Peters aliaga dunia kabla ya mwisho wa vita tarehe 10 Septemba, 1918. Hakukumbukwa sana isipokuwa na vikundi kadhaa vilivyodai Ujerumani irudishiwe makoloni yake iliyonyang’anywa baada ya vita.
Tangu 1933 serikali ya Adolf Hitler ilimkumbuka na kumheshimu ikimtambua kama mtangulizi wa itikadi yake. Barabara na viwanja katika miji mbalimbali vikapewa jina lake. 1936 Adolf Hitler alitamka kwa amri ya pekee kuwa hukumu dhidi ya Peters ifutwe na mjane wake apewe pensheni yake.
Katika miaka ya nyuma barabara zilizoitwa kwa jina la Peters zilibadilishiwa jina kwa sababu miji kadhaa iliona ya kwamba ni aibu kutunza kumbukumbu yake kwa njia hiyo.
| Nchi za Afrika | |
|---|---|
| Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesoto | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Uhabeshi | Uswazi | Zambia | Zimbabwe | |
| Maeneo ya kiafrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika | |
| Ufaransa: Mayotte · Réunion | Hispania: Visiwa vya Kanari · Ceuta · Melilla | Ureno: Visiwa vya Madeira | Uingereza: · Kisiwa cha St. Helena · Kisiwa cha Diego Garcia | |
