Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Shirikiano za kijeshi katika Ulaya wakati wa mwaka 1915. Nyekundu: Mataifa ya Kati; kijani: Mataifa ya Ushirikiano; njano: mataifa yasiyoshiriki vitani
Picha:WW1 TitlePicture For Wikipedia Article.jpg
Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia:
1.Mifereji huko Verdun (Ufaransa) baada ya kulimwa kwa mizinga mikubwa;
2. Eropleni za kijeshi na faru za kwanza;
3. bunduki ya mtombo na manowari
Ramani ya dunia ikionyesha nchi na maeneo yaliyoshiriki katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Kijani: Mataifa ya Ushirikiano; njano: Mataifa ya Kati; nchi zisizoshiriki kwa rangi ya kijivu

Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilikuwa vita kati ya 1914 hadi 1918 ya Ujerumani, Austria-Hungaria, Bulgaria na Uturuki (ziliitwa "Mataifa ya Kati") dhidi ya Ufaransa, Urusi, Uingereza, Marekani na nchi mbalimbali zilizoshirikiana nazo (zilitwa "Mataifa ya Ushirikiano").

Vita hii ilianza katika Ulaya ikapanuka haraka hadi Mashariki ya Kati, Afrika na Asia ya Mashariki ikasababisha kifo cha takriban watu milioni tisa.

Sababu na matokeo[hariri | hariri chanzo]

Sababu yake ilikuwa mashindano makali kati ya mataifa ya Ulaya kuhusu kipaumbele duniani.

Matokeo yake yalikuwa mwisho wa kipaumbele cha Ulaya duniani na kupanda ngazi wa Marekani, mapinduzi katika nchi mbalimbali, mwisho wa falme za Ujerumani, Austria na Urusi pamoja na mwanzo wa utawala wa kikomunisti katika Urusi, mwisho wa Dola la Austria - Hungaria na Dola la Uturuki ya Kiosmani pamoja na mwisho wa ukoloni wa Kijerumani duaniani.

Katika Ulaya nchi mpya zilijitokeza kama vile Czechoslovakia, Finland, Latvia, Lithuania, Estonia na Yugoslavia pamoja nchi zilizorudi katika uwanja wa kimataifa ndizo Austria, Hungaria na Poland.

Mwanzo wa vita[hariri | hariri chanzo]

Vita ilianza kutokana na ugomvi kati ya Austria-Hungaria na Serbia. Kutokana na muundo wa mikataba ya usaidizi kati ya nchi za Ulaya mwanzo huo ulisababisha nyororo ya matangazo ya hali ya vita kati ya mataifa mengine.

Tar. 28 Juni 1914 katika mji wa Sarayevo mwana wa Kaisari wa Austria aliyekuwa mfalme-teule akauawa pamoja na mke wake na mgaidi Mserbia mwanachama wa kundi la "Mkono Mweusi" lililosikitika utawala wa Austria-Hungaria katika Bosnia. Austria ilidai Serbia ifuate mashariti makali katika utafiti wa tendo lile. Serbia ilipokataa sehemu ya masharti Austria ilitangaza hali ya vita dhidi ya Serbia tar. 28 Julai 1914.

Agosti ya 1914 iliona kupanuka kwa vita hii: Warusi walikuwa na mkataba wa usaidizi na Serbia wakatangaza hali ya vita dhidi ya Austria-Hungaria. Sasa wakaingia Wajerumani waliokuwa na mapatano ya Usaidizi na Austria-Hungaria wakitangaza hali ya vita dhidi ya Urusi. Urusi kwa upande wake ulikuwa na mkataba wa kusaidiana na Ufaransa hivyo hali ya vita ikajitokeza pia kati ya Ufaransa na Ujerumani. Uingereza ulijiunga na vita baada ya Wajerumani walipoanza kuingia ndani ya eneo la Ubelgiji kwa shabaha ya kuvuka haraka ili wavamie kaskazini ya Ufaransa.

Kuanzia Oktoba 1914 Milki ya Osmani (Uturuki) ilijiunga na vita kufuatana na mkataba wake wa siri na Ujerumani. Mwaka 1915 Italia ilijiunga na Wafaransa na Waingereza kwa kushambulia Austria-Hungaria.

Vita katika nchi mbalimbali[hariri | hariri chanzo]

Vita ilipigwa kwa ukali miaka ya 1914- 1918. Wajerumani waliingia ndani ya Ufaransa lakini walikwama kabla ya kufika mji mkuu wa Paris. Kwa muda mrefu mstari wa mapambano ulibaki palepale.

Katika Mashariki Wajerumani walifauli kurudisha mashambulio ya kirusi na kuteka sehemu za Urusi. Katika Kusini ya Ulaya Waustria walifaulu kwa matatizo makubwa kuteka Serbia na Montenegro pamoja na Albania.

Waturuki walishindwa kwa ujumla katika mashambulio yao dhidi ya Warusi katika eneo la Kaukazi na dhidi ya Waingereza katika Misri. Lakini walifaulu kuzuia Waingereza wasifike Uturuki penyewe. Waingereza walipeleka jeshi katika Irak ya kusini wakafaulu kuwarudisha Waturuki hadi kaskazini ya nchi hii.

Vita katika koloni[hariri | hariri chanzo]

Vita ilienea haraka baharini na katika koloni za Ujerumani zilizovamiwa na Waingereza, Wafaransa, Afrika Kusini na Japani. Koloni zilikuwepo Afrika na kwenye visiwa vya Pasifiki pamoja na China. Ujerumani ilikuwa na vikosi vya kijeshi katika koloni za Afrika na pia kwenye kitovu chake katika China.

Kwa ujumla koloni zote zisizokuwa na jeshi zilitekwa bila mapigano na mataifa ya ushirikiano.

  • Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani ilivamiwa na Afrika Kusini na jeshi la ulinzi la Kijerumani likajisalimisha Julai 1915.
  • Kamerun ilivamiwa na Wafaransa na Uingereza kutoka koloni zao za Nigeria na Afrika ya Kati ya Kifaransa. Jeshi la ulinzi likajisalimisha katika Februari 1916.
  • Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ilikuwa mahali pa mapigano yaliyoendelea kwa miaka yote ya vita. Jeshi la Ulinzi wa Kijerumani chini ya uongozi wa Paul von Lettow-Vorbeck lilifaulu kutetea eneo la koloni dhidi ya mashambulio ya kwanza ya Waingereza kutoka Kenya hadi 1916. Kwenye Novemba 1914 jeshi la askari 8,000 kutoka Uhindi lilishindwa kwenye mapigano ya Tanga. Hadi mwanzo wa 1916 Waingereza walikusanya jeshi kubwa kutoka Afrika Kusini na Uhindi wakafaulu kutwaa sehemu kubwa ya koloni hadi Agosti 1916. Jeshi la ulinzi likanedelea kushika kusini ya koloni hadi 1917 ilipohamia kwenye eneo la Kireno katika Msumbiji. Waingereza na Wareno walishindwa kuwashika kundi la Kijerumani. Mwaka 1918 Lettow-Vorbeck alirudi Tanganyika akaingia Rhodesia ya Kaskazini alipoambiwa na Waingereza wakati wa Novemba 1918 ya kwamba vita ya Ulaya ilikwisha tayari.

Mwisho wa vita[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa 1917 mataifa ya Ulaya yalionyesha dalili za uchovu. Katika hali hii mabadiliko mawili makubwa yalitokea: Marekani ilijiunga na vita dhidi ya Wajerumani na Urusi uliona mapinduzi iliyolazimisha serikalimpya kutia sahihi mapatano ya kumaliza mapigano dhidi ya Wajerumani walioteka maeneo makubwa katika Urusi.

Nguvu ya Marekani ilionekana haraka na bahati ya Ujerumani ilipungua sana. Austria-Hungaria ilidhoofishwa vilevile.

Mwaka 1918 iliona mwisho wa vita. Madola ya Austria na Uturuki yalikwisha na sehemu zao zilikuwa nchi mpya au nchi zilizoundwa upya.

Mkutano wa Paris[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1919 mataifa washindi walikutana Paris (Ufaransa) wakikubaliana masharti ya kumaliza hali ya vita dhidi ya Mataifa ya Kati. Mikataba mbalimbali iliandaliwa kati ya washindi na kuwekwa mbele ya nchi zilizoshindwa.

Mikataba hii ilikuwa:

  • Mkataba wa Versailles na Ujerumani (28 Juni 1919)
  • Mkataba wa Saint-Germain na Austria (10 Septemba 1919),
  • Mkataba wa Neuilly na Bulgaria (27 Novemba 1919),
  • Mkataba wa Trianon na Hungaria (4 Juni 1920)
  • Mkataba wa Sèvres na Milki ya Osmani (Uturuki) (10 Agosti 1920; ukasahihishwa na mkataba wa Lausanne wa 24 Julai 1923).

Mkutano wa Paris uliamua masharti makali dhidi ya Ujerumani katika Mkataba wa Versailles. Koloni za Ujerumani zilikabidhiwa na Shirikisho la Mataifa kama maeneo ya kukabidhiwa kwa Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Japani, Afrika Kusini na Australia.

Mkutano wa Paris Ulikuwa jaribio la kuunda utaratibu mpya duniani uliotakiwa kulindwa na Shirikisho la Mataifa. Lakini ukosefu wa nguvu kwa upande wa Shirikisho la Mataifa pamoja na kuanza na kupanuka kwa mwendo mpya wa kifashisti iliyochukua utawala katika Italia na Ujerumani ulishinda nia hiyo. Wataalamu wasio wachache wanasema ya kwamba mwisho wa vita kuu ya kwanza ulipanda tayari mbegu wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]