Shirikisho la Mataifa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyumba ya Mataifa huko Geneva, Uswisi ilijengwa 1929 - 1938 kama makao makuu ya Shirikisho la Mataifa. Leo ni makao makuu ya UM katika Ulaya.

Shirikisho la Mataifa (kwa Kiingereza: League of Nations) lilikuwa umoja wa madola 63 ya dunia kati ya 1920 na 1946 BK.

Umoja huo ulianzishwa na mataifa washindi wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Katika miaka 1920-1930 mataifa mengine yalijiunga nao.

Shirikisho la Mataifa lilikwisha 1946 baada ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa iliochukua nafasi yake.

Mwanzo wake[hariri | hariri chanzo]

Wazo la kuwa na shirikisho la mataifa lilitolewa mara ya kwanza na mwanafalsafa Mjerumani Immanuel Kant mnamo mwaka 1795. Wazo la Kant lilirudiwa na wanafalsafa mbalimbali. Wakati wa vita kuu ya kwanza rais wa Marekani Woodrow Wilson alipendekeza hatua za kuanzisha shirikisho hili kwa kusudi la kuzuia vita kwa wakati ujao baada ya mwisho wa vita ile.

Katiba ya shirikisho la mataifa ilikuwa sehemu ya mkataba wa Versailles mwaka 1919. Nchi washindi au mataifa ya ushirikiano zilijiunga na umoja huo mpya. Baada ya kukubaliwa na nchi za kutosha shirikisho lilianza rasmi tarehe 10 Januari 1920.

Katiba ilikuwa na madhumuni kama yafuatavo:

  • fitina zote kati ya nchi zitasuluhishwa kwa njia ya amani kwa azimio ya kamati au mahakama ya kimataifa
  • nchi wanachama zote zitaungana dhidi ya nchi yoyote itakayoanzisha vita mpya au kukataa azimio la mahakama ya kimataifa
  • nchi zinapatana kupunguza jeshi zao na idadi ya silaha zilizopo
  • mkutano mkuu wa wawakalishi wa nchi zote wanachama itakuwa bunge la shirikisho
  • kamati kuu au halmashauri ya nchi wanachama nne (baadaye sita)na nafasi nne (baadaye 9) za nchi zinazobadilishana kwa zamu
  • ofisi kuu inayoongozwa na Katibu Mkuu
  • mahakama ya kimataifa inaundwa ya kutoa azimio katika matatizo kati ya madola

Maeneo ya kudhaminiwa[hariri | hariri chanzo]

Mkataba wa Versailles ulianzisha aina mpya ya maeneo yaliyowahi kuwa ama koloni au majimbo ya nchi zilizoshindwa katika vita. Koloni zote za Ujerumani pamoja na sehemu kubwa ya majimbo ya Milki ya Osmani ya awali ziliwekwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa na kukabidhiwa kwa nchi washindi wa vita. Zilipewa hali ya pekee kama maeneo ya kudhaminiwa (League of Nations mandate territories). Tofauti na koloni za kawaida nchi wadhamini hazikupewa mamlaka yote jinsi iliyokuwa katika koloni zao za kawaida bali zilipokea maeneo ya kudhaminiwa chini ya masharti fulani pamoja na kulinda haki kadhaa za wenyeji na kuandaa nchi hizi kwa uhuru. Hapo mwanzoni tofauti kati ya koloni na eneo la kudhaminiwa haikuwa kubwa lakini baadaye masharti ya udhamini yalikuwa muhimu. Kwa mfano hali ya Tanganyika kuwa eneo ka kudhaminiwa ilisababisha Uingereza kutokubali walowezi wengi kuja hapa. Vivyo hivyo hali ya Afrika ya Kusini Magharibi kuwa eneo la kudhaminiwa ilizuia sehemu hii kuwa jimbo la Afrika Kusini na kuwa msingi kwa uhuru wake kama nchi ya Namibia.

Mafanikio[hariri | hariri chanzo]

Shirikisho lilikuwa awali umoja wa mataifa washindi wa vita. Baadaye hata nchi zisizoshiriki katika vita na pia nchi zilizoshindwa kama Ujerumani zilipokelewa kama wanachama. Idadi ya wanachama ilipanda hadi kufikia 63.

Nembo la Shirikisho la Mataifa 1939 - 1941

Kati ya mafanikio ni haya:

Shirikisho la mataifa liliunda pia utaratibu wa utawala wa maeneo yaliyokuwa chini ya Uturuki na Ujerumani hadi 1919.

Kazi ya Shirikisho la Mataifa katika Afrika[hariri | hariri chanzo]

Liberia na Afrika Kusini zilikuwa wanachama tangu mwanzo, Ethiopia ilipokelewa mwaka 1923.

Katika Afrika shirikisho liliunda utaratibu mpya kwa ajili ya koloni za Ujerumani yaani Tanganyika, Rwanda, Burundi, Togo, Kamerun na Namibia.

Ujerumani haukubaliwa kuwa nazo tena kwa sababu ya kuwatendea wenyeji Waafrika vibaya. Hata kama sababu hiyo ilikuwa tamko la washindi wa vita waliotaka kujigawia wenyewe koloni hizi ilhali wenyewe waliwahi kuwatendea watu vibaya katika koloni zao msingi muhimu uliwekwa uliozaa matunda baadaye: yaani hata serikali ya kikoloni inatakiwa kuheshimu haki za binadamu.

Halafu koloni za Ujerumani hazikukabidhiwa tu kwa Uingereza (Tanganyika, sehemu za Kamerun na Togo), Ufaransa (sehemu kubwa za Kamerun na Togo), Ubelgiji (Rwanda, Burundi) na Afrika Kusini (Namibia) hivi lakini kama maeneo ya kukabidhiwa chini ya uangalizi wa Shirikisho la Mataifa. Utaratibu huu ulikuwa muhimu baadaye wakati wa uhuru. Namibia ilikuwa sehemu ya Afrika Kusini chini ya sheria za nchi ile lakini jumuiya ya kimataifa haikukubali kwa sababu Namibia ilikuwa kati ya maeneo ya kukabidhiwa - mwishoni Afrika Kusini iliiacha Namibia iwe huru mwaka 1990 miaka 44 baada ya mwisho wa shirikisho lenyewe.

Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia akishtaki Italia kwa sababu ya uvamizi wa nchi yake 1935 mbele ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mataifa

Matatizo[hariri | hariri chanzo]

Tatizo kubwa tangu mwanzo ilikuwa ya kwamba Marekani haukuthebitisha unachama wake. Rais Wilson aliyeandaa kuundwa kwa shirikisho alikuwa amekasirisha wabunge wake nyumbani hivyo Senati ya Marekani iliendelea kukataa uanachama ya Marekani.

Matatizo mengine yaliyosababisha kushindwa kwa shirikisho la mataifa yalitokana hasa na udhaifu mkubwa wa kukosa jeshi lake. Tangu mwanzo shirikisho lilitegemea nguvu ya nchi wanachama kama nchi ilivunja mapatano na kukataa kuitikia maazimio ya shirikisho.

Kuanzia mnamo mwaka 1930 mataifa wanachama makubwa yalianza kuvunja vibaya sheria za shirikisho lakini hatua kali hazikuchukuliwa dhidi yao. Shirikisho lilishindwa kuzuia vita na mashambulio dhidi ya nchi wanachama wake. Kati ya matukio muhimu yaliyoharibu sifa za shirikisho ni:

Nchi mbalimbali zilitoka katika Shirikisho la Mataifa baada ya kupingwa mkutanoni kama vile Italia, Japan na Ujerumani.

Azimio la mwisho lenye maana kidogo yalikuwa kufukuza Urusi katika shirikisha baada ya uvamizi wake katika Finland mwaka 1939.

Mwisho[hariri | hariri chanzo]

Septemba 1939 Ujerumani ilivamia Poland. Baada ya siku chache ilionekana ya kwamba vita kuu ya pili imeanza - Shirikisho la Mataifa lilishindwa katika dhumuni lake la kuzuia marudio ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Washindi wa vita kuu ya pili waliamua kuanzisha chombo kipya. Umoja wa Mataifa uliundwa 1945 ukachukua nafasi yake. Vitengo kadhaa za shirikisho viliendela vikihamia kwa UM kwa mfano Shirika ya Kazi ya Kimataifa (ILO).

Mwaka 1946 mkutano mkuu uliamua mumaliza shirikisho. Mali yale ilikabidhiwa kwa UM.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Shirikisho la Mataifa kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.