Mataifa ya ushirikiano

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mataifa ya Dunia wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia;
Njano-dhahabu: Ujerumani, Italia, Japani na nchi zilizoshikamana nazo; Kijani cheusi: Mataifa ya ushirikiano kabla ya Desemba 1941 (Pearl Harbour); Kijani kibichi: Mataifa yaliyojiunga na ushirikiano tangu Pearl Harbour hadi 1945

Mataifa ya ushirikiano (kwa Kiing.: Allied powers, Allies of WW II) ni jina la kutaja mataifa yaliyoungana dhidi ya Ujerumani na nchi zilizoshikamana nayo hasa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na pia wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Ujerumani ilishambulia Poland tarehe 1 Septemba 1939. Ufaransa na Uingereza ziliwahi kutia saini mikataba ya ulinzi pamoja na Poland, hivyo zilitangaza hali ya vita dhidi ya Ujerumani. Kanada, Australia, New Zealand na Afrika Kusini zilizokuwa nchi huru ndani ya British Commonwealth zilifuata kutangaza vita dhidi ya Ujerumani katika siku za kwanza za Septemba 1939.

Ufaransa na Uingereza zilikuwa na makoloni yao, hivyo sehemu kubwa ya eneo la dunia lilijumlishwa tayari katika juhudi za mataifa ya ushirikiano. Ni hasa Uhindi wa Kiingereza (Uhindi, Pakistan na Bangla Desh leo) iliyochangia mali na watu wengi katika vita. Maaskari Waafrika kutoka majeshi ya kikoloni waliungwa pia na juhudi hizi.

Baada ya mashambulio ya Ujerumani dhidi ya Denmark, Norwei, Ubelgiji na Uholanzi nchi hizo zilitazamwa kama sehemu ya mataifa ya ushirikiano hata kama yalitekwa na kutawaliwa na Ujerumani.

Mwaka 1941 uliona vita ya Ujerumani na Italia dhidi ya Umoja wa Kisovyeti (Urusi) na nchi za Ulaya kusini-mashariki kama Ugiriki na Yugoslavia. Marekani ilikuwa bado nje ya vita lakini serikali yake ilikuwa inatoa tayari misaada mingi kwa Uingereza.

Mwezi wa Novemba 1941 viongozi wa nchi kubwa Franklin D. Roosevelt (Marekani), Winston Churchill (Ufalme wa Maungano- Uingereza) na Stalin (Umoja wa Kisovyeti - Urusi) walikutana mjini Teheran (Uajemi) wakajadili ushirikiano wao na mipango ya vita.

Tarehe 7 Desemba 1941 Japan ilishambulia bandari ya Kimarekani ya Pearl Harbour, Hawaii. Ujerumani ilitangaza hali ya vita dhidi ya Marekani. Tangu hapo nchi nyingi za Amerika yote zilijiunga na mataifa ya ushirikiano. Mwisho wa vita nchi zote za dunia isipokuwa Hispania, Ureno, Uswidi, Uswisi, Eire, Afghanistan na Tibet zilijiunga na mataifa ya ushirikiano dhidi ya Ujerumani, Japani, Hungaria na Bulgaria. Italia ilikuwa imejitenga tayari na Ujerumani mwaka 1943 isipokuwa sehemu kubwa ilikuwa bado chini ya utawala wa jeshi la Ujerumani.

Ushirikiano huo ulikuwa chanzo cha Umoja wa Mataifa ulioundwa mwaka 1945 mara baada ya mwisho wa vita.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mataifa ya ushirikiano kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.