Kiburi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kiburi kadiri ya Adolfo Wildt (1868-1931) katika Chuo kikuu cha serikali huko Milano (Italia).
Kiburi kilivyochongwa katika kinara cha 10 cha Palazzo Ducale huko Venezia (Italia).
Kiburi kilivyochorwa katika kanisa kuu la Chartres (Ufaransa).

Kiburi (kutoka neno la Kiarabu; kwa Kiingereza: hubris[1], hybris[2] na pengine excessive pride[3] pamoja na arrogance[4]) ni hamu isiyoratibiwa ya kujipatia ukuu dhidi ya wengine[5][6], pengine hata dhidi ya Mwenyezi Mungu[7]. Kiburi ni hisia na fikra zilizopotoka kuhusu ukweli na uhalisia wa mambo[8] .

Katika Biblia, shetani anatajwa kuwa na fikra za kuwa juu ya Mungu[9]; hakika huo ni upotofu wa hali ya juu sana, kwa kuwa haiwezekani kwa namna yoyote kuwa zaidi ya Mungu hata kwa mfumbo wa jicho moja, na matokeo yake ni ya kutisha[10][11]. Ni sawa na kusema mtoto amzae baba au mama yake. Haiwezekani chombo cha udongo kikawa na uwezo zaidi ya mfinyanzi kwa kuwa ni kizuri na kinavutia na kusifiwa na watu wengi, huku aliyekifinyanga hajulikani[12]. Kitabu cha Isaya 29:16 kinasema, "Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, 'Hakuna mfinyanga huyu'; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, 'Yeye hana ufahamu'?"

Katika Ukristo kiburi ndicho kilema kikuu cha roho ya shetani na binadamu aliyepotoka.

Mfumo halisi wa kiburi[hariri | hariri chanzo]

“Chanzo cha kiburi ni dhambi; yeye aishikaye atafurika machukizo” (YbS 10:13), kwa kuwa kinazuia kiumbe asimnyenyekee wala kumtii Mungu. Dhambi asili ilikuwa ya kiburi: kutaka kujua “mema na mabaya” (Mwa 3:5) ili kujiongoza badala ya kutii. Wengi wanadanganyika, kimawazo au walau kimatendo, kuhusu mfumo wa kiburi, hivyo wanakubali unyenyekevu bandia, ambao ni kiburi kilichofichika, cha hatari kuliko kile cha wazi kinachokuja kutia aibu. Ni kwamba kiburi hakipingani tu na unyenyekevu, bali pia na moyo mkuu ambao mara nyingi unachanganywa nacho. Pengine tunahitaji kipaji cha shauri ili tusidhani moyo mkuu wa wengine ni kiburi, wala utovu wetu wa moyo ni unyenyekevu halisi.

Kiburi ni hamu isiyoratibiwa ya ukuu: mwenye kiburi anataka kuonekana bora kuliko alivyo kuhusu vitu (k.mf. nguvu ya mwili) au mema ya juu (k.mf. akili au maendeleo ya Kiroho). Maisha yake yana uongo: anazingatia mno sifa zake na kasoro za wengine ili kujipandisha juu yao. Kupenda hivyo ukuu ni kinyume cha utaratibu wa akili, cha sheria ya Mungu na cha unyenyekevu wa kiumbe asiye kamili mbele ya Mungu. Ni tofauti na hamu halali ya kutenda makuu kulingana na wito wetu. Basi, kiburi ni “hamu ya ukuu mwovu” (Augustino); kinamfanya mtu amuige Mungu kinyume, asivumilie kuwa sawa na wenzake, bali atake kuwaweka chini yake, badala ya kuishi nao chini ya matakwa ya Mungu. Kwa hiyo kinapingana na unyenyekevu kuliko kinavyopingana na moyo mkuu, ingawa maadili hayo mawili yanafungamana na kukamilishana. Kumbe kiburi na utovu wa moyo ni vilema vinavyopingana.

Kiburi ni kama kitambaa kinachofumba macho ya roho yasione ukweli, hasa ukuu wa Mungu na ubora wa watu kadhaa. Kinatuzuia tusikubali kufundishwa au kuongozwa nao bila kubishabisha. Hivyo kiburi kinapotosha maisha yetu, kama springi iliyokunjuliwa. Kinatuzuia tusimuombe mwanga Mungu, hivyo yeye anatuficha ukweli. Hakuna kitu kinachotuzuia kuliko kiburi cha roho tusizamie mafumbo. Hivyo kinatuondolea ujuzi halisi wa Mungu katika sala hasa ambayo unyenyekevu unatuandaa kumiminiwa. “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga” (Math 11:25).

Namna mbalimbali za kiburi[hariri | hariri chanzo]

Gregori Mkuu aliorodhesha ngazi za kiburi: kudhani tumejipatia wenyewe yale tuliyojaliwa na Mungu; kudhani tumestahili yale tuliyozawadiwa; kujivunia mambo tusiyonayo (k.mf. elimu kubwa); kutaka upendeleo na kudharau wengine.

Kwa nadra mtu anapotoshwa na kiburi hata kukanusha uwepo wa Mungu, kukataa katakata kumtii au kupinga mamlaka ya Kanisa kwa uzushi. Kwa kawaida kimawazo tunajua kuwa Mungu peke yake ni mkuu na anastahili utiifu wetu. Lakini kimatendo tunajithamini mno kana kwamba tungekuwa asili ya sifa njema tulizonazo; tunajipongeza kwa hizo tukisahau tunavyomtegemea Mungu kama asili ya mema yote; tunaziona kubwa kuliko zilivyo; tunafumbia macho kasoro zetu hata tukaziona ni sifa njema. Kwa mfano tunadhani tuna mawazo mapana kwa sababu tunapuuzia majukumu madogomadogo ya kila siku; hivyo tunasahau kwamba ni lazima tuanze kuwa waaminifu katika madogo tuweze kuwa waaminifu katika makubwa pia, kwa vile siku inaundwa na saa kadhaa, saa inaundwa na dakika kadhaa, nayo dakika inaundwa na sekunde kadhaa.

Hayo yote yanatufanya tujipendee na kuwashusha wengine, tukijiona bora kuliko wao hata kama kwa kweli ni kinyume. Dhambi hizo za kiburi, ambazo mara nyingi ni nyepesi, zinakuwa za mauti zikitufikisha kutenda namna inayostahili lawama kubwa.

Bernardo wa Clairvaux aliorodhesha matokeo kumi na mawili ya kiburi kikija kustawi: kudadisi, kunena kijuujuu, kufurahi usipofaa, kujivunia yasiyo kweli, kupenda upekee, kuringa, kujiamini kipumbavu, kutokubali makosa, kuficha dhambi kwenye kitubio, kuasi, kujiachia kutenda lolote, kuzoea dhambi hadi kumdharau Mungu.

Tunaweza kutofautisha aina za kiburi kwa kuzingatia mtu anajikuza kwa kitu gani: k.mf. asili yake, utajiri wake, mwili wake, elimu yake au roho ya ibada anayodhani kuwa nayo.

Kiburi cha akili kinafanya wasomi kadhaa wakatae ufafanuzi rasmi wa dogma, au kuzipunguza au kuzipotosha; wengine washikilie mno maoni yao wasikubali kusikia hoja tofauti; hatimaye wengine, ingawa wanashika ukweli, wanafurahia uimara wa hakika zao na elimu waliojipatia hata wasiwe tayari kupokea kwa unyenyekevu mwanga mkuu wa Mungu katika sala. “Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi” (1Kor 4:8). Mtu aliyejaa umimi atapokeaje zawadi za juu ambazo Mungu anaweza na kutaka kumjalia kwa faida yake na kwa wokovu wa wengine?

Kiburi cha roho ni kizuio kikubwa zaidi. Yohane wa Msalaba alikizungumzia hivi kuhusu wanaoanza, “Kwa kuwa wanakosa ukamilifu, umotomoto wao wenyewe unakuwa chemchemi isiyotambulikana ya kiburi, maana wanaridhika na matendo yao na kujithamini sana. Ndiyo sababu katika maongezi tunawasikia pengine kutokeza majivuno ya kuchukiza wakianza kujadili masuala ya Kiroho… Wanafurahi zaidi kufundisha kuliko kujifunza; moyoni wanahukumu wale wote wanaoelewa ibada namna tofauti na wao… hata inaonekana kumsikia Farisayo yule aliyedhani kumsifu Mungu kwa kujivunia matendo yake na kumdharau mtozaushuru… Wanaona kibanzi jichoni mwa ndugu yao lakini si boriti jichoni mwao wenyewe. Ikitokea kwamba viongozi wao wa Kiroho hawakubali roho yao wala mwenendo wao… wanatamka kuwa viongozi hao hawaelewi roho yao tena si watu wa Mungu. Wanajifanya wa pekee kwa jinsi wanavyojitokeza kwa nje kwa kutenda, kupiga kite na kukaa namna za ajabuajabu. Wengi wao wanajitafutia upendeleo na urafiki wa pekee wa muungamishi, jambo linalosababisha wivu na mahangaiko. Wanaweza hata kufikia hatua ya kutothubutu tena kuungama kwa unyofu dhambi zao wakiogopa kupunguziwa heshima wanayopewa, hivyo wanajitetea badala ya kujishtaki. Pia wana muungamishi maalumu kwa dhambi mbaya, wakati yule wa kawaida anatumiwa tu kumuelezea yaliyo mema. Kutokana na kiburi cha roho, wengine wanaoanza wakianguka huwa wanachukia na kusikitika mno, wanajikasirikia wakidhani kabisa wangepaswa kuwa watakatifu tayari”.

Kasoro zinazotokana na kiburi[hariri | hariri chanzo]

Kasoro kuu zinazotokana na kiburi ni kujiamini, kutamani vyeo na kujivuna.

Kujiamini kipumbavu ni hamu na taraja isiyoratibiwa ya kutenda mambo makuu kuliko nguvu tulizonazo. Tunadhani kwamba tunaweza kusoma na kujibu masuala magumu, hivyo tunayatolea msimamo harakaharaka. Tunadhani kwamba tuna mwanga wa kutosha tujiongoze bila shauri la kiongozi wa Kiroho. Badala ya kujenga juu ya unyenyekevu, kujikana na kutekeleza wajibu wa kila nukta hata katika madogo, tunasema juu ya juhudi za kitume au tunatamani kufikia mara ngazi za juu za sala, bila kupitia zile za kati, tukisahau kwamba tupo mwanzoni tu na kwamba utashi wetu bado ni dhaifu na umejaa umimi.

Ndipo panapotokea kutamani vyeo. Kwa kuwa tunajiamini mno na kujiona bora kuliko wengine, tunataka kuwatawala, kwa kuwalazimisha wafuate mafundisho yetu au kwa kuwaongoza. Tunajitafutia vyeo tusivyostahili kwa ajili ya ukuu wetu, si kwa utukufu wa Mungu na faida ya wengine. Jinsi zilivyo nyingi njama na mbinu za siri zinazotokana na tabia hiyo katika mazingira yoyote!

Kiburi kinazaa majivuno, yaani kutaka heshima kwa ajili yetu sisi badala ya kuielekeza kwa Mungu aliye asili ya mema yote; tena mara nyingi tunaitaka kwa mambo yasiyo na maana (k.mf. kuonyesha elimu yetu kwa kutia maanani mno mambo madogo tunayojua na kudai wengine wawe na msimamo uleule). Majivuno yanazaa kasoro nyingi: majigambo ya kuchekesha; unafiki unaoficha kilema kwa kinyago cha adili; ubishi unaotetea hoja kwa mashindano na ukali, ukisababisha daima ugomvi; pia ukaidi na lawama kwa wakubwa.

Ni rahisi kuona matokeo ya kutisha ya kiburi kisiposhindwa: mafarakano, chuki na vita vingapi vimezaliwa nacho? Ndicho adui mkuu wa ukamilifu, kwa sababu ni asili ya kasoro zisizohesabika na kinatukosesha neema nyingi: “Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu” (Mith 3:34; Yak 4:6; 1Pet 5:5). Mafarisayo waliokuwa wakisali na kufunga na kutoa sadaka ili waonekane na watu, Yesu alisema juu yao, “wamekwisha kupata thawabu yao” (Math 6:3,5,16). Maisha yanayotawaliwa na kiburi ni tasa, na yanatabiriwa maangamizi yasiporekebishwa mapema.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Definition of HUBRIS.
  2. Hybris definition and meaning | Collins English Dictionary.
  3. Hubris - Examples and Definition of Hubris in Literature (en-US) (2020-12-01).
  4. Webster's New Collegiate Dictionary, p. 63, G. & C. Merriam Company (8th ed. 1976).
  5. Picone, P. M., Dagnino, G. B., & Minà, A. (2014). ". The origin of failure: A multidisciplinary appraisal of the hubris hypothesis and proposed research agenda". The Academy of Management Perspectives 28 (4): 447–68. doi:10.5465/amp.2012.0177. 
  6. What Makes the Arrogant Person So Arrogant? (en).
  7. Stanley J. Grenz, Theology for the Community of God, Pub: Wm. B. Eerdmans Publishing, 2000 - "The Greek word hubris, which occurs occasionally in the New Testament (e.g., Acts 27:10, 21; 2 Cor.12:10). parallels the Hebrew pasha. William Barclay offers a helpful definition of the term. Hubris, he writes, 'is mingled pride and cruelty. Hubris is the pride which makes a man defy God, and the arrogant contempt which makes him trample on the hearts of his fellow men.' [...] Hence, it is the forgetting of personal creatureliness and the attempt to be equal with God."
  8. What Makes the Arrogant Person So Arrogant? (en).
  9. Lewis, C.S. (2001). Mere Christianity : a revised and amplified edition, with a new introduction, of the three books, Broadcast talks, Christian behaviour, and Beyond personality. San Francisco: Harper. ISBN 978-0-06-065292-0.  Unknown parameter |url-access= ignored (help)
  10. Meth 16:18
  11. Andrew Fellows, 2019, Gaia, Psyche and Deep Ecology: Navigating Climate Change in the Anthropocene.
  12. James Mwalubalile, Nguvu ya Kiburi (Dhambi Mama), 2021.