Julius Nyerere
| Mwalimu Julius Nyerere | |
|
|
|
| Muda wa Utawala 26 April 1964 – 5 November 1985 |
|
| Waziri Mkuu | Rashidi Kawawa (1972–77) Edward Sokoine (1977–80) Cleopa Msuya (1980–83) Edward Sokoine (1983–84) Salim A. Salim (1984–85) |
|---|---|
| Makamu wa Rais | Abeid Karume (1964–72) Aboud Jumbe (1972–84) Ali Hassan Mwinyi (1984–85) |
| aliyemfuata | Ali Hassan Mwinyi |
|
Rais wa Tanganyika
|
|
| Muda wa Utawala 9 December 1962 – 25 April 1964 |
|
| Waziri Mkuu | Rashidi Kawawa |
|
Waziri Mkuu wa Tanganyika
|
|
| Muda wa Utawala 1 May 1961 – 22 January 1962 |
|
| Monarch | Elizabeth II |
| mtangulizi | Ofisi iliundwa |
| aliyemfuata | Rashidi Kawawa |
|
Waziri Kiongozi wa Tanganyika
|
|
| Muda wa Utawala 2 September 1960 – 1 May 1961 |
|
| Monarch | Elizabeth II |
|
|
|
| tarehe ya kuzaliwa | 13 Aprili 1922 Butiama, Tanganyika |
| tarehe ya kufa | 14 Oktoba 1999 (umri 77) London, Uingereza |
| mahali pa kuzikiwa | Butiama, Tanzania |
| utaifa | Mtanzania |
| chama | |
| ndoa | Maria Nyerere |
| watoto | 7 |
| mhitimu wa | Chuo Kikuu cha Makerere Chuo Kikuu cha Edinburgh |
| Fani yake | Mwalimu |
| dini | Ukristo (Katoliki) |
| tovuti | juliusnyerere.info |
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Butiama, mkoani Mara, pembezoni mwa Ziwa Nyanza, 13 Aprili 1922 - London, Uingereza, 14 Oktoba 1999) alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania, na mara nyingi anatajwa kama "baba wa taifa". Kwa hakika aliiathiri kuliko yeyote yule. Ndiye mwasisi wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea iliyotangazwa hasa katika Azimio la Arusha.
Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni mwalimu. Kazi hiyo ndiyo iliyompatia jina ambalo lilimkaa maisha yake yote la "Mwalimu."
Kwanza aliongoza Tanganyika toka mwaka 1961 hadi 1964 kama waziri mkuu, halafu kama rais; baada ya muungano wake na Zanzibar, aliongoza Tanzania kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1985 kama rais.
Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiari baada ya kutawala kwa muda mrefu, akiwa bado anapendwa na wananchi walio wengi.
Alipostaafu urais mwaka 1985 alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo. Hata hivyo aliendelea kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
Kwa ruhusa ya makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, Jimbo Katoliki la Musoma linashughulikia kesi ya kumtangaza mwenye heri na hatimaye mtakatifu. Kwa sababu hiyo anaitwa pia "mtumishi wa Mungu".
Yaliyomo |
Maisha yake [hariri]
Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule: Tanganyika).
Alikuwa mmojawapo kati watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabila la Wazanaki.
Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga mifugo ya baba yake; katika umri wa miaka 12 aliingia shule akitembea kilomita 30 hadi Musoma.
Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusomea shule ya wamisionari Wakatoliki huko Tabora.
Katika umri wa miaka 20 alibatizwa akawa Mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.
Mapadri wakiona akili yake kubwa walimsaidia kusomea ualimu huko Makerere, Kampala, Uganda kuanzia mwaka 1943 hadi 1945.
Akiwa Makerere alianzisha tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika, pia alijihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA).
Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akifundisha shule ya St.Mary.
Mwaka 1949 alipata [[skolashipu[[ ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uskoti, Ufalme wa Muungano, akapata M.A. ya historia na uchumi (alikuwa Mtanganyika wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanganyika).
Aliporejea kutoka masomoni, alifundisha Historia, Kiingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis iliyo karibu na Dar es Salaam.
Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.
Mwaka 1954 alibadilisha jina la chama cha TAA kwenda chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho pia kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kikawa tayari chama cha siasa kinachoongoza nchini Tanganyika.
Uwezo wa Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni akalazimika kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akijisemea kuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.
Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima ya Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta umoja katika kupigania uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship Council na Fourth Committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York.
Uwezo wake wa kuongea na wa kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu.
Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa wakati huo, Richard Turnbull, ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.
Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1960.
Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake na tarehe 9 Desemba 1961 Nyerere alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika huru; mwaka mmoja baadaye akawa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika.
Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.
Tarehe 5 Februari 1977 aliongoza chama cha TANU kuungana na chama tawala cha Zanzibar Afro Shirazi Party na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi) akiwa mwenyekiti wake wa kwanza.
Nyerere aliendelea kuongoza taifa hadi 1985 alipomwachia nafasi rais wa pili, Ali Hassan Mwinyi.
Aliacha kuongoza Tanzania ikiwa ni mojawapo kati ya nchi maskini zaidi duniani, ingawa yenye huduma za elimu na afya zilizoenea kwa wananchi wengi.
Hata hivyo aliendelea kuongoza CCM hadi mwaka 1990 na kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
Kwa mfano, inasadikika kuwa Nyerere alishawishi uteuzi wa Benjamin W. Mkapa kama mgombea wa urais mwaka 1995, ambaye alichaguliwa kuwa rais kwenye uchaguzi.
Nyerere alikaa muda mwingi kwake Butiama akilima shamba lake. Pamoja na haya alianzisha taasisi yenye jina lake; mwaka 1996 alionekana akiwa mpatanishi wa pande mbalimbali za vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi.
Tarehe 14 Oktoba 1999 aliaga dunia katika hospitali ya St Thomas mjini London baada ya kupambana na kansa ya damu.
Mafanikio na kasoro [hariri]
Mafanikio [hariri]
Kati ya mafanikio makubwa ya Nyerere kuna: kujenga umoja wa taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha amani ya muda mrefu tofauti na hali ya nchi jirani, iliyofanya Tanzania iitwe "kisiwa cha amani".
Pia kustawisha utamaduni wa Kiafrika pamoja na lugha ya Kiswahili, kushinda ubaguzi wa rangi, kutetea usalama wa taifa katika vita dhidi ya mvamizi Idi Amin wa Uganda.
Kutoa mchango kwa vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrika kama vile: Zimbabwe (ZANU), Afrika Kusini (ANC na PAC), Namibia (SWAPO), Angola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo).
Ukosoaji dhidi yake [hariri]
Nyerere analaumiwa kwa siasa yake ya kiujamaa kuwa ilichelewesha maendeleo ya kiuchumi wa Tanzania. Siasa yake ya ujamaa ilishindikana kwa kiasi kikubwa baada ya mwaka 1976 kwa sababu mbalimbali za nje na za ndani ya nchi.
Baada ya kuona kuwa uchumi wa Tanzania hautaweza kusimama kwa siasa ya kijamaa na kuwa hataweza kuvumilia kuendesha nchi kwa siasa nyingine ambazo yeye hakuwa na imani nazo, Nyerere kwa hiari yake mwenyewe aliamua kustaafu nafasi ya urais kuanzia uchaguzi wa mwaka 1985 na kumwachia usukani Ali Hassan Mwinyi, aliyetawala kwa siasa ya uchumi wa soko huria.
Katika hali ya kukubali ukweli, Nyerere katika tafrija ya kumwaga alitamka juu ya siasa yake upande wa uchumi: “Nimefeli. Tukubali hivyo.”
Kosa lingine ambalo wengine wanaona Nyerere alilifanya ni kumhadaa aliyekuwa Rais wa Zanzibar Mzee Abeid Amaan Karume kwa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar, na kuanza kupora mamlaka ya Zanzibar kidogokidogo. Kwa hivi sasa Wanzanzibari wengi wamechoka na Muungano huo, na wanataka uhuru wa nchi yao ili wapumue. Hata upande wa bara wananchi wengi wanalalamikia kutoweka kwa Tanganyika na serikali yake.
Pia kuna makundi ya Waislamu wanaomtuhumu kwa kuendesha kwa siri vita dhidi ya dini yao na kupendelea Wakristo katika utoaji wa elimu na madaraka,japo wasomi wengi kwa kipindi cha utawala wake walikuwa Wakristo.
Sifa zake [hariri]
Pamoja na hayo, Nyerere bado anakumbukwa na Watanzania hasa wa hali ya chini kutokana na sera zake za kujali utu. Pia ataendelea kukumbukwa na Waafrika barani kote hasa kwa mchango wake mkubwa wakati wa harakati za kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika.
Ni mmoja wa viongozi wachache waadilifu waliokwepa kujilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi ya 24.
Mwishoni mwa maisha yake Nyerere aliishi kama mkulima wa kawaida kijijini kwake Butiama. Alipatwa na kansa ya damu (leukemia) akafariki Uingereza wakati wa kutibiwa katika mji wa London tarehe 14 Oktoba 1999.
Alizikwa mahali pa kuzaliwa kwake, kijiji cha Butiama.
Heshima na tuzo alizopewa [hariri]
Heshima [hariri]
Cuba: Order of José Marti, 1974
Mexico: Order of the Aztec Eagle (Collar), 1975
Guinea-Bissau: Medal of Amílcar Cabral, 1976
Mozambique: Eduardo Mondlane Order, 1983
Angola: Order of Agostinho Neto, 1985
Kisha kufa
South Africa: Order of the Companions of O. R. Tambo (Gold), 2004[1]
Zimbabwe: The Royal Order of Munhumutapa, 2005[2]
Uganda: The Most Excellent Order of the Pearl of Africa, 2007[3]
Uganda: The Order of Katonga, 2007[4]
Rwanda: National Liberation Medal (Uruti Medal), 2009[5]
Rwanda: Campaign against Genocide Medal (Umurinzi Medal), 2009[5]
Namibia: The Most Ancient Order of the Welwitschia Mirabilis, 2010[6]
Tanzania: Order of Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, December 2011
Burundi: National Order of the Republic of Burundi, 2012[7]
Tuzo [hariri]
- 1973: Jawaharlal Nehru Award for International Understanding[8]
- 1982: the Third World Prize
- 1983: Nansen Refugee Award
- 1986: Sir Seretse Khama SADC Medal
- 1987: Lenin Peace Prize
- 1988: Joliot-Curie Medal of Peace
- 1992: International Simón Bolívar Prize
- 1995: Gandhi Peace Prize
Kisha kufa
- 2000: Statesman of the 20th century by the Chama cha Mapinduzi
- 2009: World Hero of Social Justice by the 63rd President of UNGA, Miguel d'Escoto Brockmann[9]
- 2011: Tanzania Professional Network Award[10]
Machapisho ya mwl.Julius K. Nyerere [hariri]
- Freedom and Unity (Uhuru na Umoja): Mkusanyiko wa maandiko na hotuba, 1952–1965 (Oxford University Press, 1967)
- Freedom and Socialism (Uhuru na Ujamaa). Mkusanyiko wa maandiko na hotuba, 1965-1967 (1968)
- Ndamo zimo: "The Arusha Declaration"; "Education for self-reliance"; "The varied paths to socialism"; "The purpose is man"; and "Socialism and development."
- Freedom & Development (Uhuru na Maendeleo). Mkusanyiko wa maandiko na hotuba, 1968-73 (Oxford University Press, 1974)
- Ndani zimo mada za elimu kwa watu wazima; uhuru na maendeleo; kujitegemea; na miaka kumi ya uhuru.
- Ujamaa - Essays on Socialism' (1977)
- Crusade for Liberation (1979)
- Julius Kaisari. Tafsiri ya mchezo wa William Shakespeare unaoitwa Julius Caesar
- Mabepari wa Venisi. Tafsiri ya mchezo mwingine wa William Shakespeare, The Merchant of Venice
Tanbihi [hariri]
- ↑ Government Gazette (PDF). info.gov.za (11 June 2004). Rudishwa juu ya 9 February 2013.
- ↑ The Royal Order of Munhumutapa. SADC Today (4 October 2005). Rudishwa juu ya 9 February 2013.
- ↑ President Museveni to honour Nyerere. New Vision (4 July 2007). Rudishwa juu ya 9 February 2013.
- ↑ Museveni honours Nyerere. New Vision (10 July 2007). Rudishwa juu ya 8 February 2013.
- ↑ 5.0 5.1 Museveni, Zenawi, Nyerere to receive national honours. The New Times (3 July 2009). Rudishwa juu ya 9 February 2013.
- ↑ Tanganyika: Africa’s mecca for liberation movements. Daily News (28 November 2011). Rudishwa juu ya 9 February 2013.
- ↑ Museveni gets prestigious Burundi award. New Vision (4 July 2012). Rudishwa juu ya 9 February 2013.
- ↑ List of the recipients of the Jawharlal Nehru Award. Indian Council for Cultural Relations. Rudishwa juu ya 8 February 2013.
- ↑ Morales Named “World Hero of Mother Earth” by UN General Assembly. Latin American Herald Tribune. Rudishwa juu ya 8 February 2013.
- ↑ Kikwete urges local experts to embrace integrity. Daily News (4 December 2011). Rudishwa juu ya 9 February 2013.
Viungo vya nje [hariri]
- Taasisi ya Mwalimu Nyerere
- Contemporary Africa Database - People/ Nyerere
- http://www.nathanielturner.com/juliuskambaragenyerere.htm
- Mohamed Said: Mwalimu in 1950s Dar (East African October 12 2008)
- Nyerere's remarks on Ali Hassan Mwinyi Corrupt practices
- PBS Interview with Nyerere on the Great Lakes crisis, December 26, 1996
- Infed.org article on Nyerere and his views on education in Tanzania
- Jerry Atkin's Nyerere tribute, from InMotion Magazine
- SouthCentre Nyerere Memorial Site
- A translation of Merchant of Venice into KiSwahili
- Nyerere Obituary from the ANC
- NPR Weekend Edition reflection on Nyerere
- Julius Nyerere Fellowship
- Called to greatness MercatorNet, 10 November 2006
- Beatification inquiry for Tanzania's Nyerere (from Catholic World News)
- Is Nyerere's process to sainthood timely? (from IPP Media)
- The Julius Nyerere Intellectual Festival Week by Gacheke Gachihi, All Africa, 11 June 2009
- The Julius Nyerere Master's Scholarships (University of Edinburgh)
| Orodha ya Marais wa Tanzania | |
| Julius Nyerere • Ali Hassan Mwinyi • Benjamin Mkapa • Jakaya Kikwete |