Julius Caesar

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Gaius Julius Caesar (100 - 44 KK) alikuwa kiongozi Mroma wa kisiasa na wa kijeshi. Amekumbukwa hasa kwa mafanikio mbalimbali yanayoonekana hadi leo.

Kati ya mafanikio haya ni:

  • Waroma wa Kale walimheshimu kushinda viongozi wote waliomfuata au kutangulia akatangaziwa kuwa mungu na jina lake lilikuwa neno kwa ajili ya cheo cha watawala wa Kiroma walionfuata. Kutoka na badiliko hili la jina "Caesar" kuwa cheo lugha mbalimbali walipokea cheo hiki kama vile Kijerumani ("Kaiser"), Kirusi ("Tsar") na Kiswahili ("Kaisari" - kutokana na neno la Kijerumani).
  • Katika historia ya Roma alifunga kipindi cha Jamhuri - kilichofuata ni Dola la Roma aliloiwekea misingi

Kupanda ngazi[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa katika familia ya makabaila wenye nafasi katika Senatus ilivyoitwa bunge la Roma. Aliingia katika siasa akachaguliwa kwa vyeo mbalimbali kwa vipindi vya kawaida wa miezi kadhaa hadi mwaka moja.

Cheo chake muhimi cha kwanza kilikuwa mkuu wa koloni ya Kiroma ya Hispania. Alifaulu kushinda ghasia ya Wahispania wenyeji waliojaribu kuwafukuza Waroma kutoka nchi yao. Caesar aliporudi Roma alitajirika na kujipatia sifa kama kiongozi wa kijeshi pia mwanasiasa aliyeokoa koloni muhimi ya Hispania.

Baadaye Caesar alijiunga na wanasiasa wawili wengine Gnaeus Pompeius Magnus aliyekuwa mkuu wa wanajeshi na Marcus Licinius Crassus aliyekuwa mtajiri kushinda Waroma wote. Wote watatu waliunda umoja ulioitwa "triumviratus" yaani umoja wa wanaume watatu wakashika mamlaka katika dola. Caesar alichaguliwa kwa cheo kikuu yaani Konsul kwa mwaka 59 KK. Baada ya mwisho wa kipindi chake alijipatia cheo cha Prokonsul au gavana wa eneo la Gallia ya Kiroma (Italia ya Kaskazini na eneo ndogo ya Ufaransa ya Kusini).

Vita ya Gallia[hariri | hariri chanzo]

Alitumia nafasi hii kuanzisha vita dhidi ya makabila ya Gallia huru yaani eneo lote la Ufaransa, Uswisi na Ubelgiji ya leo. Katika miaka nane ya 58 - 51 KK alitwaa Gallia yote. Aliingia pia ndani ya Germania (Ujerumani) na kuvuka bahari aliposhambulia kusini ya Britannia. Aliandika kitabu cha "De bello gallico" (Vita ya Gallia) akieleza mapigano yake. Kitabu hiki ina habari muhimu za kihistoria juu ya utamaduni wa makabila ya Gallia, Germania na Britannia aliyopigania nayo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kufanikiwa Gallia na kujenga jeshi kubwa tena hodari wanasiasa wengine huko Roma walimwogopa walijaribu kumzuia asirudi Italia. Mwenzake Crassus alikuwa amekufa tayari vitani katika mashariki ya dola; mwenzake Pompeius aliomwogopa Caesar akajaribu kushawishi viongozi wengine kumsimamisha. Lakini mwaka 49 Caesar aliongoza wanajeshi lake wakirudi Italia. Pompeius na wapinzani wake walitoka Roma wakaenda Ugiriki iliyokuwa jimbo la kiroma. Mwaka 48 Caesar akachaguliwa tena kuwa Konsul. Akamfuata Pompeius kwa jeshi lake akamshinda katika mapigano. Pompeius alikimbia kwenda Misri lakini mfalme Ptolemaio XIII. alimwogopa Caesar akamwua Pompeius akampatia Caesar kichwa chake alipofika Misri. Caesar alikutana na dadake Ptolemaio Kleopatra akampenda na kuzaa mwana wake wa pekee naye. Akamsaidia Kleopatra kuwa malkia na mtawala wa Misri.

Achaguliwa dikteta - kifo[hariri | hariri chanzo]

Caesar alikuwa mwanadamu wa kwanza aliyeonyeshwa kwenye sarafu za Roma

Caesar alirudi Roma kutoka Misri akiwa mshindi dhidi ya wapinzani wote. Bunge la Senatus lilimpa cheo na madaraka ya dikteta kwa miaka 10. Baada ya ushindi mwingine dhidi ya wapinzani huko Hispania bunge lilibadilisha azimio hili kumpa cheo cha dikteta wa maisha. Caesar alipokea azimio hili. Sasa sehemu ya wabunge waliogopa ya kwamba nia yake ilikuwa kuwa mfalme wa Rome - jambo lililokuwa marufuku katika jamhuri ya Roma. Kikundi cha wabunge -wote makabaila wa familia za kale- waliunga mikono wakamwua Caesar bungeni tar. 15. 03. 44 KK kwa kumdunga kisu mara 23. Caesar anasemekana alimtambua mpwa wake Brutus akamwuliza kwa maneno yake ya mwisho: "Hata wewe mwanangu?".

Caesar hakuwa na watoto bali na huyu mwana wa Kleopatra asiyekuwa Mroma. Kabla ya kifo chake alikuwa amempanga mtoto mpwa wake Oktaviano. Huyu Oktaviano -aliyejulikana baadaye kama Augusto na mtawala wa kwanza wa Dola la Roma- alilipiza kisasi chake katika kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe na kuua wapinzani wote wa Caesar.

Miaka miwili baada ya kifo chake bunge lilimtangaza Caesar ndiye mungu.