Mkataba wa Helgoland-Zanzibar

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Mkataba wa Helgoland-Zanzibar ulifanywa kati ya Ujerumani na Uingereza tarehe 1 Julai 1890. Pande zote mbili zilielewana juu ya mipaka ya koloni zao au maeneo walimotaka kuwa na athira kuu katika Afrika.

Mkataba yalihusu maeneo katika Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kusini-Magharibi na Afrika ya Magharibi (Togo) pamoja na kisiwa cha Helgoland mbele ya pwani la Ujerumani katika Bahari ya Kaskazini.

Shabaha ya Mkataba[hariri | hariri chanzo]

Shabaha kuu ya mkataba ilikuwa kuondolewa kwa hatari za magongano kati ya Ujerumani na Uingereza. Leo von Caprivi alikuwa chansella mpya wa Ujerumani tangu Machi 1890 akimfuata Otto von Bismarck. Caprivi alitaka kujenga uhusiano mwema hasa na Uingereza.

Wakati huohuo uhusiano ule ulikuwa mashakani kidogo kutokana na matendo ya Karl Peters aliyejaribu kupanusha eneo la Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki hadi Uganda kinyume cha mapatano ya mwaka 1886 kati ya Ujerumani na Uingereza juu ya mipaka ya maeneo chini ya athira yao katika Afrika ya Mashariki.

Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

Uingereza ilikubali koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (Tanganyika, Rwanda, Burundi. Waingereza waliahidi kumshawishi Sultani ya Zanzibar ili awaachie Wajerumani haki za Zanzibar Tanganyika bara.

Ujerumani ilifuta mipango yake katika Uganda na Zanzibar ambako Mjerumani Karl Peters aliwahi kusaini mapatano ya ushirikiano na Sultani na Kabaka.

Pia iliwaachia Waingereza Usultani ya Witu iliyokuwa tayari chini ya ulinzi wa Ujerumani tangu 1885 na madai yake kwenye pwani la Kenya katika eneo la funguvisiwa ya Lamu na pwani la Somalia hadi Kismayu.

Afrika ya Kusini-Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Pande zote mbili zilipatana kuhusu utawala wa Kijerumani katika eneo ambalo lilikuwa Namibia baadaye. Wajerumani walikubali kutovuka mstari wa mto Oranje upande wa kusini na kukubali utawala wa Waingerezea juu ya Botswana. Wajerumani walipewa pia njia ya kufikia Mto Zambezi katika kanda lililoitwa baadaye Kishoroba cha Caprivi.

Afrika ya Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Pande zote mbili zilipatana mipaka kati ya koloni zao za Togo ya Kijerumani na "Pwani la dhahabu la Kiingereza" (Ghana) halafu kati ya Kamerun na "eneo la Kiingereza linalopakana" (Nigeria).

Ulaya[hariri | hariri chanzo]

Uingereza iliachia Ujerumani kisiwa cha Helgoland katika Bahari ya Kaskazini. Kisiwa hiki kiliwahi kuchukuliwa na Uingereza wakati wa vita dhidi ya Napoleon mwaka 1807 ikawa koloni ya Kiingereza. Kisiwa kilidaiwa na Ujerumani kwa sababu kihistoria ni sehemu ya jimbo la Frisia ya Kaskazini lililokuwa sehemu ya Ujerumani baada ya kuhamishwa mara kadhaa kati ya Ujerumani na Denmark.