Karatasi
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Karatasi (kutoka Kigiriki Χαρτί kharti kupitia lugha ya Kiarabu قرطاص qartas) ni laha bapa na nyembamba ya konge za mimea zilizokandamizwa na kushikana. Watu huandika kwenye karatasi, vitabu na magazeti hufanywa kwa karatasi na vipande vikubwa vya karatasi hutumiwa kwa kufunga vitu ndani yake. Karatasi hunywa kiowevu hivyo hutumiwa pia kwa shughuli za kusafisha.
Karatasi hutengenezwa hasa kutokana na ubao uliosagwa lakini inawezekana kutumia konge za mimea mingine pia. Inawezekana kutumia pia karatasi iliyotumiwa kwa kutengezea karatasi mpya kwa mfano magazeti ya kale.
Kwa matumizi mengine kuna pia karatasi nene kama bapa inayotumiwa kutengezea maboksi ya kubebea vifaa.
Watu wa kwanza wa kutengeneza karatasi walikuwa Wachina.
[hariri] Karatasi ya wadudu
Aina ya karatasi asilia hutengenezwa na nyigu na wadudu wengine kwa kujenga mzinga wao. Zinatafuta ubao ulioanza kuoza na kuitafuna halafu kuijenga kwa kuchanganya na mate. Inakauka kuwa kuta za mzinga na sega.
[hariri] Kutengeneza karatasi
Ubao husagwa halafu kuchanganywa na maji kuwa aina ya uji. Karatasi ya kuandikia huongezwa madawa ya kuondoa rangi yote ili karatasi inatokea nyeupenyeupe. Uji inatandikwa na kusukumwa kuwa laha bapa inayofaa kwa ukurasa. Baadaye kukatwa vipande-vipande jinsi vinavyotakiwa. Karatasi kwa matumizi kwenye mashine kubwa za kuchapa hutengenezwa mfululizo kwa umbo la kanda ndefu linaloviringishwa kuwa vikuto vikubwa. Mashine za kutengeneza karatasi hukausha uji la konge njiani kwa kuipasha joto.
Madawa mbalimbali huongezwa kwenye uji la karatasi kuipa sifa zinavyotakiwa kama uso wa kung'aa au rangi mbalimbali.
Karatasi za kusafishia kwa mfano karatasi ya choo inatakiwa kuwa laini sana.
[hariri] Matumizi ya karatasi
Karatasi hutumiwa kwa madhumini mengi:
- Karatasi ya kuandikia hutumiwa kwa madaftari na laha zinazouzwa kwa rimu
- Karatasi ya kuchapisha vitabu na magazeti hutengenezwa kwa vikuto
- Karatasi ya kusafishia hutengenezwa pia kwa vikuto
- Karatasi kwa pesa inatakiwa kudumu muda mrefu inaungwa pia na nyuzi za metali zinazotakiwa kuifanya vigumu kutengeneza pesa bandia
- Karatasi nene kiasi yenye rangi na bombwe hutumiwa kama mapambo ya nyumba ikipakwa kwenye kuta za nyumba
- Karatasi ni muhimu kwa kufunga bidhaa katika masanduku ya karatasi nene
- Katika utamaduni wa Asia kuta za vyumba mara nyingi ni karatasi tu

