Uajemi
| |||||
Kaulimbiu ya taifa: Kiajemi: Esteqlāl, āzādī, jomhūrī-ye eslāmī ("Uhuru, Huria, Jamhuri ya Kiislamu") | |||||
Wimbo wa taifa: Sorūd-e Mellī-e Īrān | |||||
Mji mkuu | Tehran | ||||
Mji mkubwa nchini | Tehran | ||||
Lugha rasmi | Kiajemi (Farsi) | ||||
Serikali | Jamhuri ya Kiislamu Ali Khamenei (سید علی خامنهای) Ebrahim Raisi (سیدابراهیم رئیسی) | ||||
Mapinduzi imetangazwa |
11 Februari 1979 | ||||
Eneo - Jumla - Maji (%) |
1,648,195 km² (ya 18) 0.7% | ||||
Idadi ya watu - 2013 kadirio - 1996 sensa - Msongamano wa watu |
78,192,200[2] (ya 18) 60,055,488 [1] 48/km² (ya 162) | ||||
Fedha | Rial (ريال) (IRR )
| ||||
Saa za eneo - Kiangazi (DST) |
(UTC+3.30) not observed (UTC+3.30) | ||||
Intaneti TLD | .ir | ||||
Kodi ya simu | +98
- |
Uajemi (kutokana na Kiarabu العجم- al-'ajam) ni nchi ya Asia ya Magharibi. Kimataifa inajulikana zaidi kwa jina Iran (ايران).
Jina rasmi ya nchi ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran au Uajemi. Uajemi imejulikana tangu kale kama nchi iliyochangia mengi katika historia ya binadamu.
Imepakana na Afghanistan, Armenia, Azerbaijan, Iraq, Pakistan, Uturuki na Turkmenistan.
Upande wa kusini kuna mwambao wa Ghuba ya Uajemi (Bahari Hindi) na upande wa kaskazini ni mwambao wa Bahari ya Kaspi.
Tehran ni mji mkuu, pia mji mkubwa nchini.
Historia
Tangu mwaka 500 KK makabila madogo ya nchi yaliunganishwa, na hii ilikuwa mwanzo wa milki ya Uajemi. Mfalme Koreshi II aliunganisha Uajemi wote chini ya mamlaka yake akavamia sehemu za Uturuki wa leo na Babeli na kuunganisha nchi hizo.
Waandamizi wake walipanua milki hadi Misri, Uhindi na Ugiriki.
Milki hiyo ilikwisha baada ya kushindwa na Aleksanda Mkuu; lakini nasaba za Waparthia na Wasasanidi waliendelea kufufua milki ya Uajemi tena na tena.
Baada ya uvamizi wa Waarabu Ujaemi wkatawaliwa kwa muda kama sehemu ya ukhalifa wa Uislamu lakini baada ya karne kadhaa nasaba za kieneo zilichukua utawala kwa jina la khalifa ila hali halisi kama watawala wa kujitegemea.
Baada ya uvamizi wa Wamongolia nasaba ya wana wa Timur iliunganisha Uajemi pamoja na Afghanistan na Asia ya Kati.
Tangu mwaka 1600 kitovu cha utawala kilirudi Uajemi wenyewe chini ya nasaba za Safawi na Khadjari.
Baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia afisa wa kijeshi Reza Khan alimaliza utawala wa Wakhadjari akaanzisha nasaba ya Pahlavi. Alijaribu kuleta matengenezo ya kimaendeleo nchini akaiga katika mengi mfano wa Atatürk katika Uturuki jirani.
Utawala wa kifalme ulikwisha mwaka 1979 wakati wa mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatollah Khomeini yaliyoanzisha Jamhuri ya Kiislamu.
Kipindi kifupi baada ya mapinduzi Uajemi ilishambuliwa na Iraki na vita vya miaka 8 ilisababisha vifo vingi.
Uhusiano na nchi za magharibi, na hasa Marekani, umekuwa mgumu tangu mapinduzi, hasa baada ya wanafunzi Waajemi kushambulia ubalozi wa Marekani mjini Teheran na kuwateka Wamarekani kama makole. Fatwa ya Ayatollah Khomeini kudai kifo cha mwandishi Salman Rushdie iliongeza sifa za ukali za Uajemi.
Tangu uchaguzi wa Rais Mahmoud Ahmadinejad mwaka 2006 aliyetamka matishio dhidi ya nchi ya Israeli kuna mashaka juu ya mipango ya Uajemi kupanua teknolojia yake ya kinyuklia kwa hofu ya kwamba serikali yake inalenga kujenga bomu ya nyuklia. Mapatano yalichukua miaka hadi kufikiwa mwaka 2015.
Utawala
Uajemi ni Jamhuri ya Kiislamu inayoongozwa na katiba yenye sehemu za kidemokrasia na sehemu za kidini.
Mamlaka kuu iko mikononi mwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi anayesimamia siasa ya nchi kwa jumla; yeye ni amiri jeshi mkuu na msimamizi mkuu wa huduma ya usalama; pia anaratibu siasa ya nje. Anateua wakuu wa jeshi, redio na televisheni, viongozi wa salat wa msikiti mkuu katika kila mji, jaji mkuu na mwendesha mashataka mkuu halafu nusu ya wajumbe wa Halmashauri ya Walinzi wa Katiba wanaokubali au kukataa sharia zote zilizopitishwa bungeni wakiwa na mamlaka kusimamisha wagombea kwa uchaguzi wa kitaifa. Anaweza kumwachisha rais. Kiongozi mkuu huchaguliwa na Mkutano wa Wataalamu wa Uongozi kwa muda wa maisha yake. Ayatollah Khamenei ni Kiongozi Mkuu wa pili tangu mapinduzi ya Kiislamu.
Serikali inayoongozwa na rais wa Uajemi aliye na nafasi ya pili baada ya Kiongozi Mkuu. Huchaguliwa na wananchi wote kwa kipindi cha miaka 4 na anaweza kuchaguliwa upya. Wagombea wanahitaji kukubaliwa na Halmashauri ya Walinzi wa Katiba. Rais anaongoza serikali na kazi yake. Katika mambo ya siasa ya nje, jeshi na siasa ya nyuklia yuko chini ya mamlaka ya kiongozi mkuu.
Bunge inayoitwa "majlis" ina wabunge 290 waliochaguliwa kwa muda wa miaka 4. Wagombea wote wanahitaji kibali cha Halmashauri ya Walinzi wa Katiba. Majlis inatunga sheria za nchi na kukubali makisio ya serikali na mikataba ya kimataifa. Sheria zote zilizopita bungeni zinahitaji tena kibali cha halmashauri ya walinzi.
Halmashauri ya Walinzi wa Katiba ni chombo muhimu sana kinachohakikisha mamlaka kuu ya kiongozi mkuu. Ina wajumbe 12 ambao ni wanasheria. 6 wanateuliwa moja kwa moja na Kiongozi Mkuu. 6 wengine wanachaguliwa na bunge kati ya majina wanaopelekwa mbele na jaji mkuu - anayeteuliwa na Kiongozi Mkuu. Kwa hiyo kiongozi mkuu anaamua juu ya wajumbe wote waliomo katika halmashauri hii, hakuna anayeweza kuwa mjumbe bila kibali chake ama moja kwa moja au kupitia jaji mkuu aliyeteuliwa naye.
Mikoa
Uajemi umegawiwa kwa mikoa 31 inayoitwa "ostan" chini ya gavana anayeteuliwa na rais. Kila mkoa huwa na wilaya (shahrestan) na ngazi ya chini zaidi ni mitaa (bakhsh). Chini ya mitaa kuna kata (dehestan) zinazojumlisha vijiji kadhaa.
Watu
Iran ina mchanganyiko wa makabila na dini uliounganishwa na utamaduni na lugha ya Kiajemi, ambayo inatumiwa na wananchi walio wengi na ndiyo lugha rasmi, ikifuatwa na lugha nyingine za jamii ya Kihindi-Kiulaya, lakini pia za jamii nyingine kama Kiazeri (16%) na Kiarabu (2%) (angalia orodha ya lugha za Uajemi).
Dini
Uajemi iliwahi kuwa na dini zake za Uzoroasta na Umani.
Kuanzia karne ya 4 BK idadi ya Wakristo ilikua.
Tangu karne ya 7 Waarabu Waislamu walivamia Uajemi na kuifanya polepole kuwa nchi ya Kiislamu. Katika karne ya 16 Uislamu wa Kishia ulitangaziwa kuwa dini rasmi nchini.
Leo hii takriban asilimia 90 za wakazi ni Waislamu Washia. Karibu 10% ni Wasunni, hasa katika maeneo karibu na mipaka; kiutamaduni Wasunni wengi ni Wakurdi, Wabaluchi au Waturkomani.
Wafuasi wa dini nyingine kwa jumla ni kama 1% ya wakazi wote. Kundi kubwa ni Bahai lakini dini yao ilipigwa marufuku baada ya mapinduzi ya Kiislamu. Kundi linalofuata ni Wakristoː kati hao kundi kubwa ni Waarmenia, halafu Wakaldayo. Wayahudi wa Uajemi ni kundi kubwa kati ya nchi zote za Kiislamu wa mashariki ya kati (0.01%). Wazoroasta wamebaki pia (0.03%). Kundi dogo sana ni Wamandayo wanaoitwa pia wafuasi wa Yohane Mbatizaji.
Tazama pia
Tanbihi
- ↑ Statistical Centre, Government of Iran. ""Population by Religion and Ostan, 1375 Census (1996 CE)"". Iliwekwa mnamo 2006-04-14.
- ↑ "official population clock as of March 17, 2015". http://www.amar.org.ir/.
Viungo vya nje
- The e-office of the Supreme Leader of Iran
- The President of Iran
- Iran.ir Ilihifadhiwa 17 Mei 2009 kwenye Wayback Machine.
- Iran entry at The World Factbook
- Uajemi katika Open Directory Project
- Wikimedia Atlas of Iran
Nchi na maeneo ya Asia |
Afghanistan | Armenia2 | Azerbaijan | Bahrain | Bangladesh | Bhutan | Brunei | China | Falme za Kiarabu | Georgia2 | Hong Kong3 | Indonesia | Iraq | Israel | Jamhuri ya China (Taiwan) | Japani | Kamboja | Kazakhstan | Kirgizia | Korea Kaskazini | Korea Kusini | Kupro2 | Kuwait | Laos | Lebanoni | Macau3 | Malaysia | Maldivi | Mongolia | Myanmar | Nepal | Omani | Pakistan | Palestina | Qatar | Saudia | Singapuri | Sri Lanka | Syria | Tajikistan | Timor ya Mashariki | Turkmenistan | Uajemi | Ufilipino | Uhindi | Urusi1 | Uthai | Uturuki1 | Uzbekistan | Vietnam | Yemen | Yordani |
1. Nchi ina maeneo katika Asia na Ulaya. 2. Nchi iko Asia lakini inahesabiwa pia kati ya nchi za Ulaya kwa sababu za historia au utamaduni. 3. Eneo la pekee la China. |
Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Uajemi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |