Kemal Atatürk

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Atatürk)
Picha halisi ya Atatürk.

Mustafa Kemal Atatürk (Thesalonike, leo nchini Ugiriki, 1881; Istanbul, Uturuki, 10 Novemba 1938) alikuwa mwanzilishi na rais wa kwanza wa Jamhuri ya Uturuki. Jina lake lilikuwa Mustafa Kemal. Baadaye alipewa cheo cha "Atatürk", kinachomaanisha "Baba wa Waturuki".

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa mjini Thesalonike katika Ugiriki ya Kaskazini iliyokuwa sehemu ya Milki ya Osmani hadi 1913.

Alipata kuwa mwanajeshi. Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia aliongoza utetezi wa Waturuki dhidi ya mashambulio ya Uingereza na Ufaransa kwenye mlango wa bahari ya Dardanili na kujipatia sifa nyingi. Baada ya kuporomoka kwa Milki ya Osmani wakati wa mwisho wa vita Atatürk aliongoza upinzani wa kitaifa dhidi ya majaribio ya Ugiriki kujipatia sehemu kubwa ya Anatolia ya magharibi.

Atatürk alimpindua Sultani, alitangaza Uturuki kuwa jamhuri na kuhamisha mji mkuu kwenda Ankara kutoka Istanbul. Baadaye alifuta cheo cha Khalifa kilichokuwa kiliunganishwa na cheo cha Sultani tangu mwaka 1517.

Atatürk aliamini ya kwamba sababu za kushindwa kwa Uturuki vitani zilikuwa desturi na imani za kale. Hivyo aliamua kubadilisha tabia za taifa lake.

Alifuta sharia ya Kiislamu na mahakama ya kadhi. Badala yake alianzisha sheria mpya zilizofuata mifano ya Uswisi na Italia. Sheria ilitangaza usawa wa jinsia na kuwapa wanawake haki ya kupiga kura.

Shule zilianzishwa kwa watoto wote. Mwaka 1928 ilifutwa alfabeti ya Kiarabu iliyotumiwa kuandika Kituruki na vitabu vipya vilionyesha maandishi ya lugha ya taifa kwa alfabeti ya Kilatini. Idadi ya watu waliojifunza kusoma ilipanda kutoka 20% kufikia 90%.

Tarehe 10 Novemba 1938 alikufa mjini Istanbul.

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kemal Atatürk kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.