Wasuba (Kenya)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Wasuba (au Abasuba, jinsi wanavyojiita katika lugha yao) ni kabila la watu nchini Kenya wanaoongea lugha ya Kisuba japo wengi wao huongea Kijaluo.

Kwa hakika jina 'Suba' nchini Kenya hutumika kurejelea makundi matatu tofauti ya watu wanaoishi kusini magharibi mwa Kenya katika eneo la Nyanza Kusini, nayo ni Suba (Abasuba), Irienyi (Abirienyi) na Kunta (Abakunta).

Wasuba halisi[hariri | hariri chanzo]

Kundi la Suba au Suna ndilo kabila la Wasuba na waliingia Kenya kutoka eneo la Mara, Tanzania. Ingawa Wasuba huchukuliwa kama kabila, wao ni kabila dogo tu lililokuwa chini ya kabila kubwa la Wagirango lililowajumuisha pamoja na makabila mengine madogo kama vile Wategi na Wagire. Kwa hiyo basi wao hujulikana pia kama Wasuba-Girango au Wasuna-Girango.

Wasuba wanaishi viungani vya mji wa Migori na wamegawanyika katika koo tatu, nazo ni : Wasweta inayojumuisha koo ndogo za Wakadika, Wakatiga na Wakakrao; Wasimbete inayojumuisha koo ndogo za Wahiri Kiberi (Bahiri Kiberi), Wahiri Ng'ong'o (Bahiri Ng'ong'o), Wahiri Nkena (Bahiri Nkena), Wamiaro na Wanchogu; na Wawiga inayojumuisha Wakwena, Wanyasasi, Wawanje, Wanyathocho na Wakamsuru. Lugha yao asilia ni Kisuba iliyokaribiana na lugha ya Kikuria. Kabila la Wasuba walihamia Afrika Mashariki, wakitokea maeneo yanayojulikana kama Misri kaskazini mwa Afrika.

Haya yaliyoandikwa ya kizazi cha Wasuba tangu walipohama Misri: Ragwe<--Siora<--Montheya<--Girango<--Musuba

Girango ndiye mkale wa Wasuba halisi. Wasuba ni wajukuu au kizazi wa Musuba. Musuba ni mtoto wa Girango. Girango alikuwa na wavulana wengi kama vile Musuba, Tegi na Gire. Na kwa sababu wajukuu wa Musuba ndio jamii yenye idadi kubwa ya kabila ya Wagirango, wao mara nyingi hujitambulisha tu kama kabila la Wasuba.

Mtegi ni mototo mwingine wa Girango, na walitoka Uganda sehemu ya Kitgum na wakatembea mpaka Karachuonyo. Na hapo walikaa kwa muda mrefu na wakahama mpaka nchi ya Wakipsigis. Na hapo walikaa sana, ndipo Tegi alipotengana na wenzake wakina Ongombe na Muruga. Na hapo ndipo Ongombe akahamia huko Kamagambo, ambapo hata hivi sasa bado wengi wao wanaishi huko na wanajulikana kama Wategi, ukoo wa Kamagambo au Kanyingombe. Wategi walianza kutelemka hadi wakafikia Kanyamkago na pale wakakaa kwa muda mrefu. Na kutokana na vita vya makabila walifukuzwa wakaja hadi Kanyamwa. Wategi walizidi kuja wengi kutoka huko nyuma walipokuwa wanabaki baki na wakajaa Nyandiwa na kuenea Mataro hadi Rasira Nyatambe. Mke wa Girango alikuwa binti wa Kijaluo kutoka Acholi na alizaa Gire kwao huko Kitgum–Uganda Kaskazini, kabla hajaolewa. Mke wa Girango alikuwa akiitwa Miluha.

Kuna kabila la watu nchini Tanzania, Wilaya ya Rorya, mkoani Mara wanaojiita Wasuba. Ingawa hakuna uhakika iwapo ni baadhi ya kabila moja au la, watu hawa haswa hujulikana kwa pamoja kama Wasuba-Simbiti na wao ni Wahacha, Wakine, Warieri, Wasimbiti, Wasurwa na Wasweta.

Tukiangazia Wasweta katika kundi hili la Wasuba-Simbiti kama mfano, kwa sababu wao ndio hupatikana hata nchini Kenya, tunapata kuwa Wasweta ni Waluhya (Maragori). Walitoka sehemu ya Masaba , huko Uganda. Safari yao hiyo iliwafikisha sehemu ya Umaragoli (Vihiga). Jina hili la Wasweta walilipata njiani wakati wakija na kupitia sehemu nyingi. Na jina hilo lilitokana na jina la matunda ya miti inayoitwa amasweto, na matunda hayo walikuwa wakila wakiwa na njaa huko porini. Matunda hayo hupatikana kando kando ya mito na hupendwa sana na nyani na miti yake hukuwa sana kwenda juu ambavyo ni vigumu mtu kupanda. Watu hawa walikuwa wanangojea wakiona nyani wamepanda juu ya mti huo, nao wanakwenda pale chini ya miti na matunda huanguka chini kwa kuchumwa na nyani ndipo watu wanaokota na kula. Basi Wasweta waliishi kwa kula matunda hayo wakati wakisafiri, ndipo waliona kwamba nyani ni ndugu yao na wakaamua kwamba hawawezi kamwe kuuwa nyani wala kumtesa kwa njia yoyote.

Baadhi ya Wasweta walibaki huko Vihiga hadi leo, na unaweza kuwatambua hata kwa mwiko wao wa kutokugusa nyani au kumwua. Wengine waliendelea hadi Kisii na kuishi baina ya Wajaluo na Wakisii ambapo wachache wao walibaki. Waliobaki katika eneo hili walimezwa kabisa na Wajaluo na kwa sasa wao ndio mlango wa Wajaluo unaojulikana kama Jowasweta au Jogamba katika wilaya ndogo ya Oyugis. Hata hivyo wengine walilinda lugha pamoja na desturi zao za Kiluhya na walirejelewa kama Maragol na Waluo huku Wakisii wakiwaita Abaragori. Baadaye katika mwaka wa 1961 wakati mpaka wa Luo/Kisii ulipokuwa ukibuniwa baada ya Wilaya ya Nyanza Kusini kugawanywa," Maragol (Wasweta) wote waliokuwa upande wa Ujaluo walisukumwa na kuwekwa upande wa Wakisii. Leo wanapatikana kwenye maeneo ya Gesieka, Mosocho na Kodera, na wao huongea lugha ya Oluluhya na Ekegusii. Na Wasweta waliendelea na safari hadi Suna na Uriri, sehemu ya Migori. Na pale Suna, Wasweta wachache waliobaki walimezwa na Wajaluo wa Suba-Girango. Wao haswa ndio wamejenga ukoo wa Wasweta katika jamii ya Wasuba. Wale waliobaki sehemu ya Uriri walitunza lugha na tamaduni zao. Baada ya Kenya kupata uhuru, Wamaragoli wengine wachache walitoka Vihiga na kujiunga na Wasweta waliobaki sehemu za Uriri na Gesieka. Wasweta wengine waliendelea hadi sehemu ya Bwiregi (Iregi), nchi ya Wakuria. Pia wachache sana walibaki pale. Hatimaye walimezwa na Wakuria ambapo kwa sasa wanajulikana kama ukoo wa Wasweta/Abasweta katika kabila la Wakuria. Na Wasweta wengine waliendelea hadi nchini Tanzania ambapo kwa sasa wametapakaa katika maeneo ya Mara na Mwanza. Hawa ndio Waluhya (Maragori) ambao husemekana kwamba wako nchini Tanzania. Hata hivyo, koo walizojenga kwenye makabila ya Wasuba-Girango na Wakuria hufanya wengine kudhani kwamba kabila la Wasweta huko eneo la Mara ni Wasuba, hasa Wasuba-Simbiti.

Licha ya hayo, Wasuba walimezwa na majirani yao na lugha yao ya Kisuba pamoja na mila zao kutokomea kabisa. Kwa sasa Wasuba-Girango wote huongea Dholuo. Idadi yao nchini Kenya inakadiriwa kuwa 200,000 na wao ndio wakazi wa wilaya ndogo za Suba Mashariki na Suba Magharibi katika Halmashauri ya Wilaya Migori.

Kumezwa kwa kabila la Wasuba na Wajaluo kulitokana na kuoana kwani tokea ujio wa Wajaluo, watu hawa ni majirani. Isitoshe, kabila la Wajaluo wa Kenya na Tanzania si Waniloti halisi, bali ni mchanganyiko wa Wabantu na Waniloti. Wao ni mkusanyiko wa Wajaluo waliotawanyika kutoka kwa makundi mbalimbali ya Waluo ndiyo maana hawana jina maalum la kujitabulisha kama vile makabila ya Wajaluo wa Uganda na Sudan. Mkusanyiko huu ulichanganya damu na Wabantu kutokana na uhamiaji na ufugaji. Walitangamana na Wabantu kuanzia Bunyoro, Uganda Magharibi , hadi Magharibi mwa Kenya.

Baadhi ya jamii ya Wajaluo wanaoaminika kwamba walikuwa Wabantu na walibadilika kuwa Wajaluo kwa namna sawa na ile ya Wasuba ni Wakasgunga, Wakamagambo, Wasaki, Wagamba (Wasweta), Wanjare, Wayimbo, Wasidho, Wamasamaro, Wamatabori, Wausonga, Waholo n. k. Wajaluo wa Kasgunga na Kamagambo wanadhaniwa walikuwa ndugu ya Wagirango kabla ya wao kusambaratika katika maeneo tofauti ya Nyanza Kusini. Pia koo za Wajaluo waliochanganya damu sana na Wabantu hujumuisha Wamuksero, Wakonyango Rabala, Waalego, Wagem, Waugenya, Wakano na nyinginezo. Inadhaniwa kuwa hii ndiyo sababu kuu iliyochangia hawa Wajaluo kuishi na Wabantu kama Wasuba kwa kuelewana.

Wasuba wengi hujitambulisha kama Waluo kwani wameasili (wameathiriwa na kuridhia) mila na desturi za Kiluo. Katika jamii ya Wajaluo, wao huwekwa kwenye kikundi kinachojulikana kama Joka Jok pamoja na Kamagambo, Kasgunga, Konyango Rabala, Muksero, Kanyamkago, Nyakach, Kisumo, Kano n. k.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Uchumi wa Wasuba hutegemea kilimo, ufugaji na wengine ni wafanyibiashara pia. Mazao wanayolima ni mahindi, mtama, mawimbi, mihogo, viazi vitamu, mboga na matunda n.k.

Pia wao walikuwa wafugaji hodari wa mifugo mbalimbali, kama vile ng'ombe, mbuzi na kondo, jambo ambalo waliliiga kutoka kwa majirani wao Waluo. Ijapokuwa Wajaluo kwa sasa hawathamini sana ufugaji, Wasuba bado wanaegemea biashara hii ya ufugaji, hasa katika wilaya ndogo ya Suba Magharibi ambapo wizi wa mifugo wa mara kwa mara hushuhudiwa baina ya Wasuba na majirani yao Wakuria.

Wasuba wengi pia hufanya biashara mbalimbali katika mji wa Migori kadhalika miji mingine nchini Kenya. Mji huu ndio mji mkubwa katika enea la kusini mwa Nyanza. Mji wenyewe unapatikana katika wilaya ndogo ya Suba Mashariki na una wawekezaji wengi mno. Kituo cha kibiashara cha Masara kilichoko katika wilaya ndogo ya Suba Magharibi pia ni Kituo muhimu cha kibiashara.

Itikadi[hariri | hariri chanzo]

Itikadi za Wasuba kadhaa zinafanana na za Wakuria. walikuwa na bado wanathamini mpaka sasa mila za tohara, kutia watoto jandoni, hususan watoto wakiume. Kwa kiasi kikubwa taratibu zao za Itikadi ya tohara zilifanana na zile za majirani wao Wakuria. Namna ya pombe inayojulikana kama togwe au busa ilitumika katika kuandaa sherehe hizi. Kuwa na marika yanayozunguka vizazi hata vizazi na kujirudia. Na pia kuwa na 'kisero' kama kundi la watu waliotahiriwa wakati mmoja, ambayo ilikuwa na msingi wa majina kama vile nginaro, misungu, gitang'osa, kirina n.k.

Hata kama Wasuba waliathirika kimila, bado wanathamini majina yao. Wengi wao hutumia majina yao ya kijadi, na majina hayo kwa kiasi hufanana na majina ya Wakuria. Kwa mfano: chacha, marwa, matiku, mbusiro, matinde, mwabe n.k.

Majimbo ya bunge[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka wa 2013, jami ya Wasuba ilikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo :

Suna Mashariki husimamia wilaya ndogo ya Suba Mashariki ilhali Suna Magharibi husimamia ile ya magharibi.

Wasuba mashuhuri[hariri | hariri chanzo]

  • Eliakim Otieno Marwa - aliyekuwa mwenyekiti wa Suna Girango Welfare Association
  • Chacha Maucha - chifu wa ukoloni wa kata ya Suna
  • Nyironge - mzee Suna Girango
  • Mguru Mwene - aliyekuwa shujaa wa vita
  • Owino Likowa - aliyekuwa mbunge wa Migori.
  • Riogi Riogi - mzee wa jamii ya Suna Girango (Simbete)
  • zerubabbel Baraza Odenge - aliyekuwa chifu wa Suna
  • John Pesa - aliyekuwa mbunge wa Migori
  • Princes Jully - mwanamuziki wa Benga
  • Elijah Maucha Gaoria - daktari

Wairienyi[hariri | hariri chanzo]

Wairienyi ni kabila la bantu waliohamia Kenya kutoka kusini (leo Tanzania) na kufanya makazi kando ya Ziwa Viktoria kwenye vilima vya Gosi au Gwassi, katika Halmashauri ya Wilaya Homa Bay. Katika kuhama kwao waliongozwa na shujaa aliyejulikana kama Murienyi wakiwemo viongozi wengine.

Wairienyi wenyewe hujulikana kama Abirienyi ama Abhiirienyi jinsi inavyokuwa katika maneno sanifu ya lugha hiyo. Lugha yao ni Ekirienyi, na wanafanana na kabila la Wakisii kwa lugha. Ekirienyi ina lahaja mbili ambazo zinaeleweka na kila kikundu, nazo ni Ekikune na Ekigassi.

Licha ya kabila la Wairienyi kuhamia Kenya kutoka kusini kama Wasuba halisi, na pia kujiita Wasuba, hawana uhusiano wowote wa karibu na kabila la watu wa Wagirango. Maeneo wanamokaa Wairienyi hujulikana kama wilaya ndogo ya Gwassi au Suba. Vile vile kuna Wairienyi waliojiunga na kundi la watu kutoka kabila la Wakunta waliokuwa wakihama kuelekea upande wa kusini kutoka masiwa ya Mfangano na Rusinga. Kwa sasa wanaishi kando ya Ghuba ya Muhuru ya Ziwa Viktoria katika eneo la Nyatike karibu na mpaka wa Tanzania. Wengine walivuka mpaka na kuingia nchini Tanzania na kwa sasa wao huishi kama ndugu na Wasimbiti katika eneo la Suba I, Wilaya ya Tarime.

Wairienyi walioingia Tanzania walikaa sehemu inayoitwa Kahenge na wakasogea mpaka Surubu na kusukumwa na mambo ya vita, wakasogea hadi sehemu ya Suba I. Baada ya Wairienyi Kusukumwa na makabila mengine, walisogezwa hadi milima ya Nyaihara. Baadaye walienea katika sehemu nyingi kama vile sehemu ya Konene, Nyamuhumba na sehemu ya Ruhu. Watu wa Irienyi wao hawana ukoo na Wasimbiti, ila Simbiti alioa binti wa Irienyi. Huyo binti jina lake ni Nyaikunya. Papo hapo ndipo undugu wao ukatokea. Na baada ya kuoa, Simbiti alihama kutoka kwao na akaacha ndugu yake Muhacha/Hacha, akaja akaishi na wakwe zake wa Irienyi. Baada ya kukaa kwa siku nyingi wakawa amekuwa kama mtu na ndugu yake. Milango ya Wairienyi nchini Tanzania ni: Wabarimba, Wakibarobi, Wakihenge, Wabamocha na Wabagumbwe. Kwa sasa milango hii ya Wairienyi huchukuliwa kwa pamoja kama ukoo wa Irienyi chini ya kabila la Wasimbiti, na wanashikilia kwamba wao walihamia eneo hilo kutoka vilima vya Gosi (Gwassi) na eneo la Mhoru (Muhuru).

Kabila la Wairienyi wanakadiriwa kuwa watu 80,000 hivi, na wanajulikana katika eneo la ziwa kwa wasichana warembo. Kabila hili la Wairienyi wamegawanyika katika makabila madogo manne, nayo ni Wakaksingri, Waregi (Uregi), Wangoe (Ungoe) na Wagassi.

Watu wa Uregi wako kundi moja na Kaksingri, na wao hujulikana kwa pamoja kama Wakune (Abakune). Wao ndio wazungumzaji wa lahaja ya Ekikune. Lahaja ya Ekikune imeathiriwa sana na lugha ya Olukunta inayozidi hata kuiangamiza. Lahaja ya Ekikune inayo maneno kadhaa za mkopo kutoka lugha ya Olukunta. Kuna uwezekano wa Ekikune kumezwa na Olukunta miaka michache ijayo.

Kwa upande mwingine, Wangoe ndio wakazi wa Ungoe au Ngeri na wao huzungumza lahaja ya Ekingoe, ilhali Wagassi ambao ndio watu wenye idadi kubwa katika tarafa ya Gwassi huzungumza Ekigassi. Lahaja hizi mbili hazijaathiriwa na lugha ya Olukunta na huchukuliwa tu kama lahaja moja ya Ekigase (Ekigassi), kwani tofauti ndogo zilizoko katika lahaja ya Ekingoe na Ekigassi ni za kijiographia tu. Lahaja ya Ekigassi inakaribiana na lugha ya Ekegusii.

Idadi ya Wagassi ni kubwa ikilinganishwa na makabila mengine madogo ya Wairienyi. Pia wao wamegawanyika katika koo mbili, huku koo kubwa ikijulikana kama kubia. Fasihi simulizi hushikila kwamba Wagassi walimeza kundi moja la Wakunta waliohamia Tarafa ya Gwassi kutoka Siwa la Mfangano, yani wajukuu wa Kiboye. Vile vile ni kwa sababu hii ambapo wanahistoria wengine hudhania kwamba Wagassi ni Wakunta. Hata hivyo changamoto iliyoko ni kwamba, tofauti na Wakune ambao wengi wao huzungumza Ekirienyi, Wagassi wengi huzungumza Dholuo. Ni watu wa Wagassi wachache peke ndio huzungumza lugha ya Ekirienyi.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Wairienyi ni wakulima na wafugaji, huku wakiegemea sana kwa kilimo. Baadhi ya mazao yanayofanya vizuri katika vilima vya Gwassi ni mahindi inayojulikana katika lugha yao kama amasori. Mengine ni mtama, mboga na matunda n. k. Pia wao hufuga ng'ombe, mbuzi, kondoo na kuku. Isitoshe, wao pia wanatambulika kama wavuvi.

Wairienyi pia huthamini biashara. Baadhi ya vituo muhimu vya kibiashara vinavyopatikana katika maeneo yao ni Nyandiwa, Sindo, Magunga, na hata mji wa Karungu unaopatikana katika wilaya ndogo ya Sori Bay.

Itikadi[hariri | hariri chanzo]

Wairienyi huthamini mila na tamaduni zao, ingawa wengine wao huishi maisha ya Kiluo na Kikunta. Koo nyingine za Wairienyi walitahiri wanaume kwa wanawake, ingawa itikadi hiyo ilikuja ikapotea.

Koo baina ya Wairienyi walikuwa na majukumu ya kutekeleza tohara, kuchinja kafara na kutatua mizozo. Matambiko yalitolewa katika sehemu maalum ambazo nyingine bado zipo hadi wa leo, mfano ikiwa Kaya Mungusa (Mungusa shrine) katika tarafa ya Kaksingri na Kaya Kiboye (Kiboye shrine) ilioko tarafa ya Gwassi.

Jimbo la bunge[hariri | hariri chanzo]

Wilaya ndogo ya Gwassi imejulikana kisiasa kama Jimbo la Gwassi kwa muda wa miongo miwili sasa. Mbunge wa sasa ni John Mbadi wa chama cha ODM.

Baadhi ya Wairienyi mashuhuri[hariri | hariri chanzo]

  • Zadock Syongoh (kutoka tarafa ya Gwassi) - aliyekuwa Mbunge wa Gwassi
  • Peter Nyakiamo (kutoka Tarafa ya Kaksingri - aliyekuwa Mbunge wa Mbita na waziri
  • Stakus Seko - aliyekuwa chifu mashuhuri kutoka Magunga
  • Felix Nyauchi - aliyekuwa Mbunge wa Gwassi

Wakunta[hariri | hariri chanzo]

Wakunta ni kabila la bantu wanaoishi katika wilaya ndogo ya Mbita, magharibi mwa Halmashauri ya Wilaya Homa Bay. Mbita hupakana na Gwassi upande wa kaskazini. Wakunta hujiita Abakunta na lugha yao ni Olukunta. Waganda ni kikundi walio karibu nao na kuelewana nao kilugha. Lugha yao pia kwa kiasi inakaribiana na Luluhya.

Watu hawa wanaishi kwenye masiwa ya Elusinga (Rusinga); na Ebuang'ano (Mfangano) pamoja na visiwa vinavyo lizingira kama vile Etakawiri (Takawiri), Elemba (Remba) na Ekibuogi (Kibuogi). Wachache wao Wanaishi katika eneo lisilokuwa kisiwa, yaani pwani ya kusini mwa Hori ya Winam katika wilaya ndogo yiyo hiyo, kwenye eneo linalojulikana kama Gembe.

Vile vile, kuna kundi la Wakunta waliohamia eneo la kusini na kufanya ulimwengu wao katika tarafa ya Muhuru kwenye Wilaya ndogo ya Nyatike, Halmashauri ya Wilaya Migori. Utengano huo ulisababisha kuweko kwa lahaja mbili ya lugha ya Olukunta, yaani lahaja ya kusini inayojulikana kama Olumuulu, na lahaja ya kaskazini ya Olwebwang'ano ambayo ndiyo lahaja Kuu ya lugha hii. Bali na Siwa la Mfangano, lahaja ya Olwebwang'ano pia huzungumzwa katika maeneo la Takawiri, Kibwogi, Ragwe na Kisegi.

Lugha ya Olukunta huzungumzwa sana kwenye maeneo ya Ghuba ya Muhuru na Siwa la Mfangano pamoja na visiwa vinavyolizingira, yakifuatwa na eneo la Gembe. Hata hivyo Wakunta wa Siwa la Rusinga huongea lugha ya Dholuo kutokana na athari ya majira yao Waluo wanaotangamana nao.

Idadi ya Wakunta kwa sasa inakadiriwa kuwa 45,000. Watu hawa wamegawanyika katika koo kadhaa. Baadhi ya koo hizo ni: Wakula (Abakula), Wasoklo (Abasoklo), Wakinga (Abakinga), Wakakiimba (Abakakiimba), Waware (Abaware), Wakamasengre (Abakamasengre), Wakaswanga (Abakaswanga), Wanyama (Abanyama) na Wangose (Abangose).

Jamii ya Wakunta wanaaminika kuwa kabila la mwisho lililohamia nchini Kenya. Wakunta waliingia Kenya kama wahamiaji waliokuwa wakitoroka vita vikubwa vilivyozuka katika Ufalme wa Buganda. Fasihi simulizi hueleza kwamba mnamo miaka ya 1760, Kabaka Junju, mfalme wa 26 katika Ufalme wa Buganda aliuawa katika vita kuu. Mfalme huyu alifishwa na ndugu yake, Semaakookiro, kwa usaidizi wa maakida wawili kutoka kabila la Wakunta, Witewe na Kiboye. Hawa watu wawili walikuwa vigogo wa ukoo wa Wakula. Kulikuwa na ushindani mkali katika utawala wa Buganda, baina ya Mfalme Njunju na huyu ndugu yake, jambo lililomfanya Junju kumtuma nje ya utawala.

Baada ya Semaakookiro kufanikiwa kunyakuwa kiti cha utawala wa Buganda, aliunda njama ya kisiri kunyamazisha Witewe na Kiboye ili ukweli usije ukadhihirika. Kwa bahati nzuri, Mkunta aliyekuwa afisa anayesimamia ngoma katika kasri la kabaka, Mwembe, alipata fununu juu ya jambo hilo na kutahadharisha maakida hao wawili. Usiku huo huo, wote watatu walichukuwa mashua na kutoroka Buganda pamoja na watu wa jamaa yao. Tukio hili liliwafanya jamii zima ya Wakunta kuhofia maisha yao, kwani mfalme angewaangamiza viongozi hao wawili, sembuse wao. Hawakuwa na budi kutawanyika kupitia Ziwa Viktoria.

Semaakookiro alipokuja kugundua kwamba Witewe na Kiboye walikuwa katika safari ya kutorokea sehemu za Busoga kupitia ziwa, alituma wanajeshi wake upande wa Busoga ili kuwazingira, jambo ambalo lilifanya Wakunta kugeuza safari yao kuelekea upande wa mashariki. Ni safari hii yao kuelekea mashariki ambayo mwishowe iliwafikisha katika Siwa la Mfangano. Witewe na Kiboye walikuwa viongozi wa ukoo wa Wakula katika utawala wa Buganda. Hata hivyo tukio hili la uhamiaji liliwafanya kuwa viongozi wa kundi zima la kabila la Wakunta, kwani hao ndio waliongoza msafara wa Wakunta kutoka Uganda. Ndio maana watu wa kabila la Wakunta wakati mwingine hujiita kama Abachukulu ba Kiboye na Witewe, yaani kizazi cha Kiboye na Witewe.

Fasihi simulizi huendelea kueleza kwamba Kiboye alifika Siwa la Mfangano kama mseja. Hali hii ilichangia kuhama kwake kutoka Siwa la Mfangano kuelekea upande wa bara, na hatimaye kufika kwenye vilima vya Gwassi. Kiboye alijenga chengo chake katika pahali iliyojulikana kama Kisegi ambapo aliishi pamoja na Wairienyi wa kundi la Wagassi, waliokuwa wenye idadi ndogo nyakati hizo. Huko pia alifanikiwa kupata mke. Huyo mkewe alikuwa binti wa mtu aliyejulikana kwa jina kama Wiga. Ingawa Mzee Wiga alizungumza lugha ya Kiluo, inaaminika kuwa alikuwa wa kabila la Wairienyi, hasa Mgassi. Ukoo wa Mzee Wiga waliwarejelea kizazi cha Kiboye kama Wawiga. Baada ya miaka kadhaa, wajukuu wa Kiboye walimezwa na ukoo wa Mzee Wiga na wakawa Wagassi. Hii ndiyo sababu Wairienyi kutoka kundi la Wagassi pia hujulikana kama Wiga, na pia kufanya Kiboye mwenyewe kuhusishwa na hata Wakisii ambao hukaribiana kilugha na Wagassi. Licha ya hayo, baadhi ya vikundi kutoka ukoo wa Wakula waliohamia eneo hili pamoja na Kiboye wote hawakumezwa na Wagassi. Wao bado wanapatikana katika tarafa ya Gwassi hadi wa leo. Kutokana na haya, baadhi ya watu husema kuwa Wagassi ni Wakunta, na tena ni ndugu ya ukoo wa Wakula, dai ambalo ni uongo mtupu. Isitoshe, wanahistoria wengine hudai kuwa Witewe na Kiboye ndio waanzilishi wa vikundi viwili vya Wakula na Wagassi kama vilivyofuatana, dai ambalo halina msingi wowote. Ukoo wa Wakula tayari ulitambulika katika utawala wa Buganda, na vigogo hawa wawili walikuwa baadhi ya watu chini ya ukoo huo.

Kuna historia ya vita Kati ya Wakunta na majirani wao Wajaluo, mahasimu wao wakuu wakiwa Wasaki. Wasaki, kama Wagamba (Jogamba) wanaopatikana katika wilaya ndogo ya Oyugis, ni Wajaluo wenye asili ya Kiluhya (Maragoli). Wakunta, hasa ukoo wa Waware, walipigana na Wasaki. Inaaminika kuwa ukoo wa Waware umetapakaa kwa sababu ya uvamizi wa Wasaki. Waware hupatikana kwenye masiwa yote mawili ya Mfangano na Rusinga. Na wale walioelekea upande wa mashariki walimezwa na Wajaluo, na kwa sasa wao huishi pamoja na Waluo, hasa Wasakwa ambao ni Waluo wenye asili ya Kiluhya (Wanga), katika wilaya ndogo ya Awendo inayopatikana kaskazini mwa mji wa Migori.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Uchumi wa Wakunta umekuwa ukitegemea uvuvi wa Samaki na utengenezaji wa vyombo vya kusafiria ziwani kama vile madau na mashua tangu jado. Vilevile, watu wa kabila hili walikuwa wawindaji hodari ya wanyama wanaojulikana kama viboko.

Kwa sasa biashara ya kilimo hukuwa sana kwa haraka baina ya Wakunta. Wao hukuza mazao kama vile mahindi, mtama, maharagwe mboga na mengineyo. Pia wao hufuga mifugo kama ng'ombe wanaotumia, hususan kulipa mahari.

Itikadi[hariri | hariri chanzo]

Mila za Wakunta kwa kiasi kikubwa hufanana na mila za Waganda, ikiwemo kutokuwa na tohara. Waliamini kuwepo kwa Mungu mkuu aliyeumba mbingu na dunia wanayeita Katonda. Pia Wakunta walitoa kafara kwa miungu wao na pia kugonya koma. Mizimu ya ukoo ilijulikana kama emisambwa. Waliamini kuhusu mizimu au pepo za ukoo, mfano ukiwa mzimu wa Gumba katika koo za Wakamasengre, Wakaswanga na Wanyama pamoja na mzimu wa Nundu wa Wakula na Waware. Maswala ya utawala na usalama yalikuwa majukumu ya koo. Wanaume wa kabila la Wakunta walithamini kuoa wake wengi, na kuoana baina yao na Waluo, ambao wau huwarejelea Abaswanya kwa Olukunta, kulikuwa jambo la kawaida.

Hata hivyo, Wakunta wa Muhuru huchukuliwa na wanahistoria wengine kama uko wa kabila la Wakuria.

Kwa sasa Wakunta wengi ni Wakristo, wengi wao wakiwa waumini wa kanisa la Waadventisti wa Sabato (SDA).

Wakunta mashuhuri[hariri | hariri chanzo]

  • Lilian Ojwang' - mtangazaji wa KBC Kisumu
  • Tomb Mboya - mwanasiasa mashuhuri aliyeshiriki katika siasa za ukombozi wa Kenya kutoka kwa utawala wa ukoloni. Aliweza kuwakilisha jimbo la Nairobi katika bunge la wakoloni.
  • S. F. Onyango - mbunge wa kwanza wa Jimbo la Mbita.
  • Milly Odhiambo - mbunge wa Mbita

Maelezo zaidi[hariri | hariri chanzo]

Wakunta na Wairienyi ni makabila ya watu wanaoongea lugha za Kibantu. Wako chini ya kundi la Kibantu linalojulikana nchini Kenya kama Western Bantus, pamoja na vikundi walio karibu nao kama vile Waluhya, Wagusii/Wakisii na Wakuria. Kama makabila haya matatu, Wakunta na Wairienyi pia walihamia maeneo wanamokaa saa hii kutoka eneo la nchini Kongo.

Kama Wagirango, Wakunta na Wairienyi pia wameathiriwa na majirani wao Waluo, hadi kwa kiwango cha lugha zao kubadilika. Kwa hiyo, lugha zao ni miongoni mwa lugha ambazo zimedhaniwa kuwa katika hatari ya kupotea. Licha ya kubadilika kwa lugha, Wakunta na Wairienyi wamedumisha lugha na mila zao, ingawa wengine wao hufuata mila za Waluo.

Watu wa kabila la Wakunta hujivuni mila na itikadi zao. Mara nyingi wao hujitambulisha na maneno haya: Abakunta ne enkola ziabu, yaani Wakunta na tamaduni zao. Nakala nyingi na vitabu kadhaa vimechapishwa katika lugha ya Olukunta. Hata Bibilia Takatifu hivi majuzi ilinakiliwa katika lugha ya Olukunta. Bibilia hii hujulikana kama Endagano Empia na imeweza kurahisisha njia za kumwabudia Mungu baina ya watu hawa.

Katika siasa[hariri | hariri chanzo]

Ijapokuwa Ekirienyi na Olukunta ni lugha mbili tofauti na wazungumzaji wa lugha hizo hawaelewani kwa urahisi, wakati wa mwamko wa demokrasia nchini Kenya mwaka wa 1991, serikali ya Kenya ilichukua makabila mawili ya Wairienyi na Wakunta na kuwaweka chini ya kabila moja la Wasuba. Kitendo ambacho kiliibua hisia kali ya kisiasa hususan kwa upinzani uliokichukua kama njama ya kueneza ukabila nchini.

Wairienyi na Wakunta hawakuwa Wasuba, hata hivyo ni majirani wao Waluo waliotumia neno 'Suba' kuwarejelea watu wa makabila hayo mawili na hatimaye likaenea kiasi kwamba hata wanahistoria wa kwanza waliwarejelea Wairienyi na Wakunta kwa pamoja kama Luo Abasuba, maana yake makabila hayo walikuwa na historia finyu nyakati hizo.

Miaka minne baadaye, serikali ilibuni wilaya katika eneo la Wairienyi na Wakunta na kuiita Suba. Hii pia ilileta pingamizi kali kwa wale ambao waliona kuwa serikali inatumia neno hili Suba kisiasa. Katika sensa ya mwaka 2009, Jumla ya watu 139,000 kotaka makabila ya Wairienyi na Wakunta, pamoja na vikundi vingine vya Wajaluo kama vile Kasgunga, walihesabiwa kama kabila la Suba.

Tangu kubuniwa kwa kabila la Suba, Olukunta ndiyo hutumika kama lugha ya kabila hilo na kwa sasa hujulikana kama Olusuba. Isitoshe, redio ya KBC Kisumu inayomilikiwa na serikali hutangazia kabila hilo katika lugha ya Olusuba. Hayo huchangia pakubwa Olusuba kumeza lugha ya Ekirienyi ambayo kwa sasa huitwa Ekisuba , na lahaja zake Ekisuva (Ekikune) na Ekisuba (Ekigassi). Huenda baada ya muda hakutakuwa na lugha ya Ekisuba, hasa Ekisuva, kwani itakuwa imemezwa na Olusuba na kupotea kabisa.

Changamoto inayokumba kabila hilo la Suba ni kwamba mara nyingi hutumiwa kama kifaa cha siasa. Na pia kutokana na siasa ya ukabila nchini Kenya, wanasiasa kutoka kabila hilo, hasa Wakunta hufanya juhudi kuleta Wasuba/Wagirango na vikundi vingine wa Waluo chini ya hilo kabila lao la Suba. Wengi wao kwa sasa huvuruga hata historia ili kuhusisha Wairienyi na Wakunta na jamii ya Wasuba pamoja na vikundi wa Wajaluo kama Kasgunga.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Okoth-Okombo, Duncan (1999) 'Language and ethnic identity: the case of the Abasuba', Kenya Journal of Sciences (Series C, Humanities and Social Sciences) 5, 1, 21-38.
  • Kunta oral history
  • Kenya national archive
  • Suna oral history
  • Heine, Bernd & Brenzinger, Mathias (eds.) (2003) 'Africa', in UNESCO Red Book of Endangered Languages . (Suba entry)
Makala hii kuhusu utamaduni wa Kenya bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wasuba (Kenya) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.