Thomas Aquinas Mtakatifu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Mchoro wake uliofanywa na Fra Bartolomeo
Mtakatifu Thoma wa Akwino
Ngome ya Monte San Giovanni Campano, ambapo kijana Thoma alifungwa asiweze kufuata wito wa kitawa
Mchoro wake uliofanywa na Carlo Crivelli
Ukurasa wa Summa theologiae

Mtakatifu Thomas Aquinas (Roccasecca, katika eneo la watawala wa Aquino, leo katika wilaya ya Frosinone, Italia, 1224 au 1225 - Fossanova, wilaya ya Latina, Italia, 7 Machi 1274) alikuwa mtawa wa Shirika la Wahubiri na padri wa Kanisa Katoliki.

Mnyofu, mkimya, aliyekuwa tayari kutumikia, kiutu alipendwa na wote, naye alipendelea watu wa chini, akihubiria mafukara kwa usahili na wema hata zaidi ya mara moja kwa siku.

Kuliko wengine wote, Thoma aliona elimu na masomo kama njia ya kufikia utakatifu; ni kati ya watu bora upande wa nadharia, hasa wa teolojia ya shule, iliyofikia kilele chake katikati ya karne XIII.

Mwanafunzi wa Alberto Mkuu, alitumia hasa mawazo ya mwanafalsafa wa Ugiriki Aristoteli na ya Waarabu waliomtafsiri, lakini pia ya Plato: ili kufafanua imani, alikubali ukweli ulioweza kutolewa na yeyote, kwa sababu kweli zote zinatoka kwa Mungu; kinyume chake alikanusha udanganyifu wowote.

Hivyo aliweza kufanya usanisi mpana ambao mpaka leo Kanisa Katoliki linautambua kama tokeo bora la mafundisho yake lenyewe.

Anajulikana hasa kwa vitabu vyake “Jumla ya Teolojia” (kwa Kilatini Summa theologiae) na “Jumla dhidi ya Wapagani” (kwa Kilatini Summa contra gentiles).

Alitangazwa na Papa Yohane XXII kuwa mtakatifu tarehe 18 Julai 1323, halafu na Papa Pius V kuwa mwalimu wa Kanisa mwaka 1568. Kwa Kilatini anaitwa Doctor Angelicus (Mwalimu wa Kimalaika) au Doctor Communis (Mwalimu wa wote).

Ni msimamizi wa wanateolojia, wanachuo, watoaji na wauzaji wa vitabu, wanafunzi na shule.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 28 Januari.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alikuwa mtoto wa Landolfo, sharifu mwenye asili ya Kilombardi, na mke wake, Teodora.

Akiwa mtoto wa miaka 5 tu, alitumwa kuishi na Wabenedikto katika Abasia ya Monte Cassino ili apate malezi ya kitawa.

Alipofikia umri wa miaka 14 alihamia Napoli, aliposoma katika chuo kikuu, karibu na konventi ya San Domenico Maggiore (Napoli). Ingawa alipingwa sana na familia, mwaka 1244 aliamua kujiunga na Wadominiko.

Wakubwa wa shirika, kisha kuhisi ukuu wa akili yake, walimtuma Paris aweze kukamilisha masomo yake, lakini kabla hajafika huko alikamatwa na wanafamilia na kufungwa katika ngome ya baba yake huko Monte San Giovanni Campano alipokaa mwaka mzima, akishinikizwa aoe.

Hatimaye alitoroka au alifunguliwa kwa ombi la Papa Inosenti IV.

Baada ya kukaa kidogo Napoli na Roma, mwaka 1248 alifika Cologne (Ujerumani) ili kufundishwa na Alberto Mkuu, mwanasayansi, mwanafalsafa na mwanateolojia wa shirika lake aliyejaribu kulinganisha Ukristo na falsafa ya Aristoteli.

Baadaye, Thoma aliamua kutekeleza mpango huo wa mwalimu wake.

Kuanzia mwaka 1252 alifundisha kwenye Chuo kikuu cha Paris, akianza kama baccalarius biblis, na baada ya miaka 4 aliweza kufundisha kama profesa.

Wakati huo Thoma alipinga falsafa ya wafuasi wa Mwarabu Averroe waliosema imani haiwezi kupatana na akili: "Imani ni kwa watu wanyofu, falsafa ni kwa wasomi".

Thoma alipambana pia na Waagustino ambao walifuata falsafa ya Plato hata kusema ile ya Aristoteli haipatani na imani.

Mwaka 1259 alirudi Italia na kushirikiana na Papa Urbano IV, akiishi kwenye konventi ya Orvieto. Kwa agizo lake, Thoma alitunga au kupanga matini ya liturujia yote ya sikukuu mpya ya Corpus Domini (Mwili na Damu ya Kristo) iliyoanzishwa tarehe 8 Septemba 1264. Kati ya matini hayo, maarufu zaidi kimataifa mpaka leo ni utenzi Pange Lingua, hasa sehemu ya mwisho inayoanzia na maneno Tantum Ergo (Sakramenti Kubwa Hiyo).

Halafu alihamia Roma ili kupanga kozi za chuo cha Santa Sabina na mwaka 1267 Papa Clemens IV alimuita kwake Viterbo, alipohubiri mara nyingi katika kanisa la Santa Maria Nuova.

Akiwa Italia ndipo alipoandika vitabu vingi kama vile Summa contra gentiles, De regimine principium, De unitate intellectus contra Averroistas na sehemu kubwa ya kazi yake bora, Summa Theologiae, inayotumika hadi leo katika teolojia.

Mwaka 1269 alirudishwa Paris akaanza kutetea kiteolojia mashirika ya ombaomba na kupinga Uplato mpya wa Waagustino.

Mwaka 1272, akiitwa na mfalme Karolo I wa Angiò, alirudi Napoli na kupanga upya masomo ya teolojia kwenye chuo kikuu karibu na konventi yake asili.

Tarehe 6 Desemba 1273, katika kanisa la San Domenico Maggiore, alitoka nje ya nafsi yake na tangu siku hiyo aliacha kuandika, akimueleza ndugu Reginaldo wa Piperno, msaidizi na muungamishi wake: «Yale yote niliyoyandika naona ni fungu dogo la majani makavu kulingana na yale ambayo nimeyaona na kufunuliwa. Ndio mwisho wa kuandika kwangu na natumaini umekaribia pia mwisho wa maisha yangu.»

Ndiyo sababu Summa Theologiae haikukamilika (inaishia kwenye mada ya Kitubio).

Mnamo Januari 1274 Papa Gregori X alimuagiza ashiriki Mtaguso wa pili wa Lyon, na Thoma akafunga safari ingawa hali yake haikuwa nzuri.

Alilazimika kusimama kwenye ngome ya Maenza, lakini alipoona hali inazidi kuwa mbaya asiweze kufikia konventi ya shirika, akitaka kufia monasterini, aliagiza aletwe kwenye abasia ya Waciteaux ya Fossa Nuova (leo Fossanova, karibu na Priverno), ambapo alifariki baada ya wiki chache.

Masalia yake yanatunzwa katika konventi ya Wadominiko des Jacobins huko Tolosa (Ufaransa).

Sala yake[hariri | hariri chanzo]

Mungu wa wema wote, utujalie tutamani motomoto, tutafute kwa busara, tujue kwa hakika na kutekeleza kikamilifu matakwa yako matakatifu kwa utukufu wa jina lako.

Maandishi yake[hariri | hariri chanzo]

 • Ad Bernardum
 • Aurora Consurgens
 • Compendium theologiae
 • Contra errores Graecorum
 • Contra impugnantes Dei cultum
 • Contra retrahentes
 • Contra Saracenos
 • De aeternitate mundi
 • De alchemia
 • De anima
 • De articulis Fidei
 • De ente et essentia
 • De forme absolutionis
 • De lapide philosophico
 • De malo
 • De motu cordis
 • De operationibus occultis
 • De perfectione
 • De potentia
 • De principiis naturae
 • De rationibus Fidei
 • De regimine principum
 • De spiritualibus creaturis
 • De substantiis separatis
 • De unione Verbi Incarnati
 • De unitate intellectus contra Averroistas
 • De veritate
 • De virtutibus
 • Summa contra Gentiles
 • Summa theologiae

Marejeo kwa Kiswahili[hariri | hariri chanzo]

 • GEROLD SCHMID, Toma na Marieta – ed. Benedictine Publications Ndanda-Peramiho – Peramiho 1978

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Maisha yake[hariri | hariri chanzo]

Kuhusu mafundisho yake[hariri | hariri chanzo]

Maandishi yake[hariri | hariri chanzo]