Optatam Totius

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Siku ileile (28-10-1965) ambayo Mtaguso wa pili wa Vatikano uliyotoa hati kuhusu uchungaji wa maaskofu na kuhusu urekebisho wa watawa, ilitolewa nyingine tena inayohusu malezi ya kipadri: toka mwanzo hayo yanatiwa maanani sana kwa kusema urekebisho unaotumainiwa wa Kanisa lote unategemea kwa kiasi kikubwa upadri ukitimizwa kwa roho ya Yesu Kristo.

Hati hiyo ilipata kura 2318 dhidi ya 3 tu kati ya washiriki wa mtaguso huo, ikatolewa na Papa Paulo VI. Jina lake kwa Kilatini ni "Optatam Totius", yaani "Kuchagua Yaliyo Bora".

Kuhusu malezi hayo mtaguso mkuu ulikusudia kulinganisha mang’amuzi ya karne zilizopita na mahitaji mapya.

Kwa kuwa malezi yanapaswa kuwa tofauti kwa kila mtu na kila aina ya watu, basi maagizo ya hati hiyo yanayolenga kulinda umoja wa upadri, yatekelezwe kwa namna tofauti kadiri ya mazingira, madhehebu na aina ya mapadri (watawa, wanajimbo waseja na wenye ndoa).

Kwanza jumuia nzima inapaswa kuwajibika kwa malezi ya vijana na ustawi wa miito hasa kwa njia ya sala. Wakurugenzi wa miito wasishindanie vijana, bali tujifunze wote kuwa na mtazamo wa Kikanisa na wa kimataifa. Njia ya kawaida ya kuotesha mbegu za miito ni seminari ndogo. Hizo si za lazima, kinyume na seminari kuu ambapo malezi yote yanalenga upadri moja kwa moja. Walezi wachaguliwe kati ya mapadri bora, kwa kuwa malezi yanawategemea hasa wao. Waseminari waendelee kuchambuliwa kwa imani ya kwamba Mungu hatakubali Kanisa likose wahudumu ikiwa wasiofaa wanaelekezwa kwingine.

Namba nyingine zinahusu malezi ya kiroho, upendo kwa Kanisa, malezi ya kijinsia, ukomavu wa kiutu na uwezekano wa marekebisho ya sheria. Yanafuata maagizo kuhusu masomo yenyewe ambayo moyo wake uwe ni Biblia, na masomo ya juu. Pia inasisitizwa kuwa masomo na malezi hayo yote yanalenga uchungaji katika nyanja zote.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]