Vita ya Abushiri

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Vita vya Abushiri)
Kiongozi Abushiri ibn Salim al-Harthi
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Vita ya Abushiri ilikuwa jaribio la wenyeji wa pwani ya Tanganyika kuzuia utawala wa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki mwaka 1888/1889 lililokandamizwa na jeshi la Wajerumani. Wajerumani waliita "Uasi wa Waarabu".

Viongozi[hariri | hariri chanzo]

Viongozi wake waliojulikana zaidi walikuwa Abushiri ibn Salim al-Harthi kutoka Pangani na Bwana Heri wa Saadani.

Hali ya pwani hadi 1888[hariri | hariri chanzo]

Pwani za Tanganyika na Kenya pamoja na visiwa kama Unguja au Mafia vilikuwa chini ya Omani tangu mwaka 1698 wakati Waomani waliwafukuza Wareno kutoka Mombasa.

Mnamo 1840 Sultani Said bin Sultan alihamisha mji mkuu wa utawala wake kutoka Maskat kuja Zanzibar mjini. Alidai pia ubwana juu ya miji yote ya Waswahili ilikuwepo kwenye pwani. Hali halisi miji ya Waswahili ilijitegemea kwa kiasi kikubwa vilevile makabila ya pwani na kanda la bara lililopo karibu na pwani. Lakini kwa jumla wote walikubali aina ya utawala wa juujuu wa sultani.

Katika miji muhimu Sultani aliweka maliwali au kumkubali mkubwa wa mji kuwa liwali wake. Liwali alikuwa na wajibu wa kukusanya ushuru kwa ajili ya sultani na hii ilikuwa muhimu hasa kwa mabandari ambako watumwa na pembe za ndovu walifanyiwa biashara.

Sultani wa Zanzibar alidai pia namna ya utawala kuhusu sehemu za ndani zaidi, hasa katika eneo la njia za misafara baina ya pwani na Tabora - Ujiji - Ziwa Tanganyika. Lakini usultani haukuwa na mamlaka halisi hapa isipokuwa penye maboma ya Waswahili au Waarabu na misafara yao.

Kwa kipindi kifupi Tippu Tip aliweza kuunganisha wafanyabiashara Waarabu katika mashariki ya Tanganyika na magharibi ya Kongo kukubali kwa jina ukuu wa Sultani wa Zanzibar.

Kufika kwa Wajerumani[hariri | hariri chanzo]

Mnamo 1884 Mjerumani Karl Peters alifika Zanzibar akiwa mwakilishi wa Shirika kwa Ukoloni wa Kijerumani akaendelea kuvuka bahari na kufanya mikataba ya ulinzi na machifu kadhaa wa Tanganyika. Hakujaribu kufanya mikataba katika eneo la pwani lenyewe ilhali alijua ilikuwa eneo la Kizanzibari. Hata hivyo sultani alipinga mikataba akidai ya kwamba machifu hao waliwahi kukubali ukuu wake, kwa hiyo Peters alikuwa alivunja eneo la Kizanzibari.

Lakini serikali ya Ujerumani, iliyowahi kupinga mipango ya Peters, hatimaye ilikubali na kutoa waraka wa ulinzi kwa ajili ya maeneo ya mikataba ya Peters. Serikali ya Sultani ilipokataa kukubali madai yale ililazimishwa kuvumilia kwa kufika kwa manowari wa Kijerumani mbele ya mji wa Zanzibar.

Lakini madai ya Wajerumani juu ya sehemu za bara zilikuwa bure kama pwani yote ilikuwa chini ya Sultani na bidhaa zote zilifika au kutoka katika maeneo haya zilipaswa kupitia mabandari ya sultani na kupigwa ushuru hapo.

Mwaka 1886 Uingereza na Ujerumani zilipatana kati yao kugawa maeneo ya bara na wakati uleule walitambua eneo la sultani kwenye bara kuwa kanda lenye upana la maili 10 pekee kuanzia mto Ruvuma hadi Mogadishu. Sultani Bargash alipaswa kukubali kwa huzuni.

Uingereza iliahidi kumshawishi sultani ili kampuni ya Kijerumani ipate haki ya kutumia Pangani na Dar es Salaam (zilizokuwa katika eneo la sultani) kama mabandari yake. Sultani Bargash hatimaye alikubali yote kwa matumaini ya kuwa na hakika zaidi juu ya eneo lake.[1]

Lakini mwaka uliofuata (1887) tayari alikubali dai la Uingereza kukodisha pwani ya Kenya kwa shirika la Kiingereza; baadaye alianza kushauriana na Karl Peters juu ya mkataba wa aina hiyohiyo. Mkataba huu ulikwisha kusainiwa na mfuasi wake sultani Khalifa bin Said mnamo mwaka 1888.

Kufutana na mkataba kampuni ya Kijerumani ilipokea haki ya kusimamia kanda la pwani kati ya mto Ruvuma hadi Vanga kwa jina la sultani. Eneo hili lingeendelea kuwa sehemu ya Zanzibar na chini ya sheria ya Zanzibar, Kampuni ingetawala ushuru na kuwa na haki ya kuanzisha makazi na mashamba au vituo vingine vya kiuchumi katika eneo hili. Sultani aliona faida ya kwamba angepata mapato ya kutegemea na Wajerumani jinsi alivyopata na Waingereza bila haja ya kumbuana na wakazi wa pwani.

Mapatano yalianza kutekelezwa mnamo Agosti 1888. Wenyeji wa pwani, ambao hawakuulizwa, wakashtuka walipoona maafisa Wajerumani waliofika na kupandisha bendera yao kando ya bendera ya sultani. Walishtuka zaidi juu ya ukali walioonyesha wawakilishi wa kampuni ya Kijerumani.[2]

Pwani ya Kaskazini[hariri | hariri chanzo]

Uasi ulianza Pangani tarehe 3 Septemba 1888 ambako mwakilishi wa Kampuni ya Kijerumani Emil von Zelewski (aliitwa "Bwana Nyundo") alikataza kuonyeshwa kwa bendera ya Sultani na kudai kodi kubwa kwa bidhaa zilizofika bandarini. Zelewski aliumiza hisia ya wenyeji alipoingia msikitini pamoja na mbwa wake wakati wa ibada ya Idd el Hajji (mnamo tarehe 18 Agosti 1888). Tarehe 3 Septemba alikataza kutolewa kwa mzigo wa baruti kutoka kwenye jahazi bandarini. Hapo alishambuliwa na kundi la wananchi waliomkamata na kumfunga ndani, lakini aliokolewa na wanajeshi wa Sultani waliofaulu kumpeleka hadi jahazi alipoweza kuondoka Pangani na kufikia manowari ya Kijerumani.

Huko Tanga Wajerumani walifungwa pia na kuokolewa na wanajeshi Wajerumani wa manowari ndogo "SMS Moewe".[3]

Tarehe 22 Septemba watu wa Bagamoyo walishambulia boma la Wajerumani lakini walizuiliwa na silaha za manowari "Leipzig". Wajerumani katika boma waliendelea kushambuliwa lakini waliweza kijitetea kwa msaada wa askari wa manowari.

Pwani ya Kusini[hariri | hariri chanzo]

Uasi ulienea kusini mnamo 25 Septemba 1888. Maafisa wa kampuni katika Kilwa Kivinje waliuawa. Wajerumani walikimbia kutoka Lindi na Mikindani.

Katika Januari 1889 wamisionari Wakatoliki watatu waliuawa huko Pugu / Dar es Salaam.

Kushindwa kwa kampuni na kuingilia kwa serikali[hariri | hariri chanzo]

Meja von Wissmannm jemadari wa serikali ya Ujerumani aliyefaulu kukomesha upinzani ya Abushiri

Kampuni ilishindwa kukandamiza upinzani huo ikaomba serikali ya Berlin kuingilia kati.

Serikali ilichukua koloni mikononi mwake. Wanamaji wa manowari za Ujerumani zilizokaa katika Bahari Hindi walifika Bagamoyo na Dar es Salaam wakafaulu kutetea vituo hivyo dhidi ya mashambulio.

Afisa Mjerumani Hermann von Wissmann aliagizwa kukusanya jeshi akipewa makisio ya mark milioni 2; Wissmann aliajiri maafisa 21 na maafande 40 kutoka Ujerumani akaelekea Afrika.

Njiani alipitia Misri akawaajiri askari Wasudan 600 kutoka jeshi la Misri (walioachishwa kazi wakati ule kutokana na kupungukiwa kwa jeshi la Misri baada ya vita ya Mahdi).

Baadaye askari 150 Wazulu waliajiriwa katika Msumbiji kama nyongeza.

Jeshi hilo lilijulikana kama "Wissmanntruppe" (kikosi cha Wissmann). Walipewa usaidizi na manowari za Kijerumani zilizokaa katika Afrika ya Mashariki.

Kikosi hicho kilichokuwa na silaha za kisasa kama bombomu kilifaulu kukomesha upinzani wa wenyeji wa pwani.

Kwa jumla makabila ya bara hayakushiriki sana katika vita ya watu wa pwani.

Kikosi cha Wissmann kilibadilika baadaye kuwa Schutztruppe yaani jeshi la kikoloni la serikali ya Ujerumani.

Mwisho wa vita[hariri | hariri chanzo]

Abushiri alikamatwa na kunyongwa tarehe 16 Desemba 1889. Bwana Heri alipaswa kujisalimisha. Kufikia Agosti 1889 vita ilikuwa imekwisha.

Eeno la awali la kampuni likawa koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. "Schwarz-weiss-rot über Ostafrika !",von Jutta Bückendorf, 1997, p 255-57
  2. 2. der Afrikanische Widerstandm u, 337 Jutta Bückendorf, "Schwarz-weiss-rot über Ostafrika !"]
  3. linganisha The German conquest, uk. 92, A Modern History of Tanganyika by John Iliffe

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Pugu Hadi Peramiho - kimehaririwa na P. Gerold Rupper, OSB, BPNP, Peramiho 1988, ISBN 9967 67 031 1