Mark (pesa)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kwa mji wa Uswidi tazama makala ya Mark (manispaa)
Mark 1 ya 1875 (fedha)
Mark 10 za 1880 (dhahabu)
Reichsmark 1 ya 1933 (nikeli)
D-Mark 1 ya 1967 (nikeli)
Mark der DDR ya 1979 (alumini)

Mark ilikuwa jina la pesa ya Ujerumani pamoja na nchi kadhaa za Ulaya kwa kipindi kirefu hadi kuja kwa Euro mwaka 2002.

Kiasili "mark" ilikuwa jina la kipimo cha dhabau na fedha katika Ulaya. Asili ya jina ni Kilat. marca iliyomaanisha alama ya kipimo iliyothebitisha ya kwamba kipande cha dhahabu au fedha ilikuwa na uzito uliotakiwa. Ilianza kutumiwa pia kama jina la sarafu katika maeneo mbalimbali za Ulaya hasa Ujerumani ikilingana na kiasi cha dhahabu cha gramu 200 - 280, hasa mnamo gramu 230.

Baada ya maungano ya Dola la Ujerumani mwaka 1871 mark ilianzishwa kama pesa ya Ujerumani yote kuanzia 1873. Mwanzoni ilikuwa sarafu ya dhahabu; ilikuwa na Pfennig 100. Tangu vita kuu ya kwanza ya dunia pesa hii haikutolewa tena kama dhahabu au fedha.

Sarafu zilipatikana kama mark 1, 2, 3, 5, 10 na 20. Pesa ya karatasi ilitolewa kwa mark 5, 10, 20, 50, 100 na 1000.

Sarafu za nusu mark (Pfenning 50) hadi mark 5 zilikuwa za dhahabu. Pesa za mark 10 na 20 zilikuwa za dhahabu.

Mark ilikuwa pia pesa halali katika koloni za Ujerumani isipokuwa katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ambako Wajerumani walitoa pesa iliyoitwa rupia. Rupia 15 zilingana na mark 20.

Jina la Mark ya dhahabu ilibadilihswa kuwa "Reichsmark" (yaani mark ya dola) hadi 1948. Tangu kugawiwa kwa Ujerumani katika nchi mbili katika kipindi cha vita baridi baada ya vita kuu ya pili ya dunia kila sehemu ilikuwa na mark yake. Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani ilikuwa na "Deutsche Mark" iliyojulikana kimataifa kama D-Mark. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani ilikuwa na "Mark der DDR" hadi kuungana na Shirikisho mwaka 1990.

Mark ilikwisha 2002 wakati Ujerumani ilipojiunga na pesa mpya ya pamoja ya Ulaya Euro.

Jina la mark (Kifini: markka; Kiswidi: mark) ilitumiwa pia kwa pesa ya Ufini tangu 1860 hadi 2002 nchi ilipojiunga Euro.