SMS Möwe
SMS Möwe ilikuwa manowari ya Ujerumani iliyotumiwa na Jeshi la Majini la Dola la Ujerumani kuanzia mwaka 1880 hadi 1905.
Matumizi katika uenezaji wa ukoloni
[hariri | hariri chanzo]Manowari hii ilitumwa kwenda safari mbalimbali zilizolenga kuanzisha makoloni ya Ujerumani.
Mwaka 1884 SMS Möwe ilimbeba mpelelezi Mjerumani Gustav Nachtigal aliyefanya kwa niaba ya serikali yake mikataba na watawala kwenye pwani ya Afrika ya Magharibi na hivyo kuweka misingi wa makoloni ya Togo na Kamerun.
Mwaka 1885 Möwe ilikuwa sehemu ya kundi la manowari chini ya kamanda Eduard von Knorr aliyemtisha Sultani Sayyid Barghash wa Zanzibar kukubali kuanzishwa kwa koloni la Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki katika sehemu za bara.
Mwaka 1889 wakati wa Vita ya Abushiri SMS Möwe ilikaa miezi kadhaa katika bandari ya Dar es Salaam ambako wanamaji wake walisaidia kutetea majengo yaliyoimarishwa (pamoja na Boma la Kale) dhidi ya mashambulio ya wenyeji waliopinga utawala wa Wajerumani.
Mwishoni Möwe ilikaa Tsingtau (koloni la Kijerumani huko China) ambako ilibomolewa na kuuzwa mwaka 1905.
Jina
[hariri | hariri chanzo]"Möwe" inamaanisha shakwe ambayo ni aina ya ndege wa baharini wanaopatikana kote duniani. Kifupi "SMS" kinamaanisha "Seiner Majestät Schiff" (inayolingana na Kiingereza "HMS": His/Her Majesty`s Ship) na kilikuwa kinaonyesha hii ilikuwa manowari ya jeshi la majini ya Ujerumani zamani za ufalme.
Tabia
[hariri | hariri chanzo]SMS Möwe ilikuwa na urefu wa mita 52,2 na upana wa mita 8,90. Ilikuwa na wanamaji 127. Ukubwa wake ulikuwa tani GT 845.
Muundo wake ulikuwa kiunzi cha chuma kilichofunikwa na mbao zilizofunikwa tena kwa mabati ya zinki.
Ilikuwa na tanga lakini ilipokea mwendo wake hasa kutokana na injini ya mvuke yenye silinda 3 zilizotoa kW 652 za kusukuma rafadha yenye kipenyo cha mita 3.23. Ilifikia kasi ya noti 11.7.
Akiba yake ya makaa ilikuwa tani 100 na ilitosha kwa maili 1200. Haikuwa na umeme.
Silaha
[hariri | hariri chanzo]SMS Möwe ilikuwa na mizinga 4 - 5 yenye kipenyo cha sentimita 12 iliyobadilishwa mara kadhaa pamoja na mabadiliko ya teknolojia. Iliweza kubeba ramia 600 hivi.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Erich Gröner, Dieter Jung, Martin Maass: Die deutschen Kriegsschiffe 1815–1945, Vol 1. Bernard & Graefe, München, 1982, ISBN 3-7637-4800-8.
- Hans H. Hildebrand, Albert Röhr, Hans-Otto Steinmetz: Die deutschen Kriegsschiffe Vol 4, Herford 1982, ISBN 3-7822-0235-X, uk. 126 ff.
Makala bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |