Nenda kwa yaliyomo

Emil von Zelewski

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Emil von Zelewski

Emil von Zelewski (13 Machi 1854 - 1891) alikuwa afisa wa jeshi la Ujerumani. Alipokuwa kamanda ya kwanza wa jeshi la ulinzi la kikoloni katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani aliongoza jeshi hilo katika vita dhidi ya Wahehe alipouawa.

Luteni wa jeshi la Prussia

[hariri | hariri chanzo]

Von Zelewski alizaliwa katika jimbo la Prussia ya Magharibi (wakati ule: Ujerumani; leo: Poland) akajiunga na jeshi la Prussia akasoma shule ya kijeshi akafikia cheo cha luteni.

Afisa wa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki mjini Pangani

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1886 aliondoka katika jeshi akajiunga na Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki alipoona nafasi ya kuendelea haraka zaidi.

Mwezi Agosti 1888 alitumwa kama mwakilishi wa kampuni kwenda mji wa Pangani kwenye mwambao wa Bahari Hindi. Watu wa Pangani walimpa jina la "Nyundo"[1]. Pangani ilikuwa sehemu ya kanda la barani la Usultani wa Zanzibar lililokodishwa na Zanzibar kwa Kampuni ya Kijerumani. Hapa alisababisha kwa ukali wake uasi wa wenyeji uliokuwa chanzo cha vita ya Abushiri yaani jaribio la watu wa pwani kuwafukuza Wajerumani.

Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki ilifaulu mwaka 1887 kuingia katika mkataba na sultani wa Zanzibar aliyewapa haki ya kutawala kanda la pwani lililokuwa barani chini ya Zanzibar kwa niaba ya Sultani na kukusanya ushuru kwenye bandari zake. Kwa msingi wa haki hiyo kampuni ilitakiwa kulipa kodi kwa sultani. Mkataba huo ulipingwa na viongozi wa wenyeji waliojisikia wameachwa na sultani wakamtazama sasa kama msaliti. Wawakilishi wa kampuni walitakiwa kutekeleza wajibu wao kwa ushirikiano na maliwali wa sultani kila mji wakionyesha bendera ya Zanzibar pamoja na bendera ya kampuni.

Uasi wa Pangani

[hariri | hariri chanzo]

Zelewski tangu mwanzo alionyesha ukali mkubwa mno pamoja na dharau dhidi ya wenyeji. Alisimamisha bendera ya kampuni pekee mbele ya nyumba yake bila bendera ya sultani; alijaribu kumtumia liwali wa sultani kama mtumishi wake bila kumwonyesha heshima.

Konsuli wa Austria aliandika katika taarifa yake kwa serikali ya Vienna wakati ule: "Mwakilishi wa Kampuni ya Kijerumani alifanya kosa la kumtafuta liwali wa Pangani ndani ya msikiti na kwa bahati mbaya hapa nchini majengo ya aina hii hayaruhusiwi kwa wasio Waislamu. Kwa bahati mbaya tena mwakilishi alifuatwa na mbwa wake waliomfuata hadi ndani ya msikiti..." Taarifa ilionyesha pia ya kwamba hakuvua viatu wakati wa kuingia msikitini. Tukio hili likatokea siku ya Idd el Hajj yaani mnamo 18 Agosti 1888.[2]

Matendo hayo yalisababisha viongozi wa Pangani kukutana wakaamua kuchukua hatua dhidi yake. Tarehe 3 Septemba Zelewski alikataza kutolewa kwa mzigo wa baruti kutoka kwenye jahazi katika bandari. Hapo umati wa wananachi walimfunga Zelewski ndani ya nyumba yake na bendera ya kampuni ilichomwa. Aliachishwa na wanajeshi wa Sultani wa Zanzibar. Baada ya siku kadhaa alikombolewa na kikosi cha wanajeshi Wajerumani kutoka manowari. Uasi wa Pangani ulikuwa mwanzo wa harakati kubwa ya upinzani dhidi ya Wajerumani iliyoenea kote kwenye pwani na kuendelea kuwa vita ya Abushiri. Utawala wa kampuni ya Kijerumani iliyokosa jeshi lake uliporomoka haraka; serikali ya Berlin iliamua kuingia kati na kumtuma meja Hermann von Wissmann aliyepewa pesa ya kuajiri wanajeshi wa kukodiwa hasa kutoka Sudan na Afrika Kusini pamoja na maafisa Wajerumani.

Emil von Zelewski alijiunga na jeshi la von Wissmann mwaka 1889 akaongoza mwanzoni vikosi vidogo akashiriki kubomoa boma la Abushiri na kutwaa miji ya Pangani na Saadani.

Baada ya vita alikuwa mkuu wa jeshi huko Kilwa.

Kamanda wa Jeshi la Ulinzi ka Koloni

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1891 serikali ya Ujerumani ilibadilisha hali ya eneo la kampuni kuwa koloni kamili la Dola la Ujerumani. Machi 1891 jeshi la Wissmann lilipewa cheo cha kuwa sehemu rasmi ya jeshi la Ujerumani kwa jina la "Schutztruppe" yaani jeshi la ulinzi la koloni. Wissmann alipoitwa kuwa gavana wa kwanza wa Ujerumani katika Afrika ya Mashariki Zelewski alikuwa kamanda wa jeshi la ulinzi.

Shabaha ya Wajerumani ilikuwa upanuzi wa utawala wao ndani ya maeneo ya Tanganyika barani. Mwanzoni waliona umuhimu kuangalia njia ya misafara iliyoelekea kutoka pwani kwenda Ujiji kando ya Ziwa Tanganyika. Hapo mipango ya Wajerumani iligongana na uenezi wa Wahehe waliowahi kupanuka katika Nyanda za Juu za Kusini chini ya watemi Munyigumba Muyinga na Mkwawa. Vikosi vya Wahehe walizunguka hadi kufikia njia ya misafara wakashambulia pia makabila waliyowahi kukubali utawala wa Wajerumani.

Hapa serikali ya koloni iliamua kuvunja uwezo wa Wahehe na Zelewski alipewa amri ya "kuwaadhibu" yaani kumshambulia ma kumnyamazisha Mkwawa.

Ushinde wa Lugalo

[hariri | hariri chanzo]

Kazi ya kwanza ya Zelewski kama kamanda wa Schutztruppe ilikuwa pia kazi yake ya mwisho. Mwezi wa Julai 1891 aliondoka Dar es Salaam akiongoza kikundi cha kombania 3, jumla maafisa na maafande 13 Wajerumani, askari wa kukodiwa Waafrika 320 na wapagazi 170 waliobeba mizinga miepesi na bunduki za mtombo.

Walipokaribia Uhehe Zelewski alianza kuangamiza vijiji kadhaa akitumia silaha zake za kisasa. Tarehe 30 Julai aliandika katika taarifa yake "tuliangamiza kijiji chenye ukuta kwa ramia 20 za mzinga na risasi 850 za mtombo". Tarehe 5 Agosti na 6 Agosti alichoma nyumba 25, tarehe 15 Agosti na 16 Agosti tena nyumba 50.[3]

Wakati huohuo Mkwawa alikusanya jeshi lake akasubiri Wajerumani kufika mahali palipofaa kwa maoteo. Zelewski alijisikia salama akisadiki silaha zake na kudharau Wahehe kama maadui, hivyo aliendelea bila kutanguliza wapelelezi. Tarehe 17 Agosti Zelewski aliongoza kikundi chake moja kwa moja ndani ya jeshi la Wahehe waliomsubiri karibu na kijiji cha Lugalo wakijificha ndani ya manyasi marefu pande zote mbili za njia nyembamba iliyotumiwa na Wajerumani. Kutokana na njia nyembamba Wajerumani walipaswa kutembea kwa umbo la msafa, kwa hiyo kila mahali walikuwa wachache waliposhambuliwa na Wahehe 3,000. Baada ya dakika kumi Zelewski mwenyewe pamoja na idadi kubwa ya watu wake waliuawa tayari.

Sehemu ya kombania ya nyuma iliyoongozwa na maluteni 2 na maafande 2 Wajerumani, maefendi 2 pamoja na askari 62 na wapagazi 74 waliweza kukutana pamoja kwenye kilima walipojitetea kwa bunduki ya mtombo na kujiokoa.[4]

Wenyeji wa Lugalo wanamkumbuka Zelewski kwa jina la "Nyundo".

Mengineyo

[hariri | hariri chanzo]

Kati ya watoto wa mdogo wake Zelewski alikuwepo Erich von dem Bach-Zelewski. Huyu alipanda ngazi nchini Ujerumani wakati wa utawala wa Adolf Hitler akawa jenerali wa jeshi la "SS silaha" akisimamia miradi mbalimbali ya kuwaua Wayahudi na raia nchini Urusi. Mwaka 1944 aliongoza kampeni ya kukandamiza jaribio la upinzani la wakazi wa Warszawa dhidi ya Wajerumani. Wataalamu walioandika juu ya Bach-Zelewski walitoa hoja ya kwamba maisha ya mjomba Emil von Zelewski aliyeshindwa na Waafrika yalikuwa aibu kwa familia na aibu hii ilikuwa sababu moja kwa ukali wa Erich aliyekuwa tayari ya kutekeleza matendo ya kinyama.

  1. kwa tahajia ya Kijerumani "Njundo"; alitajwa hivyo katika taarifa ya la Oscar Baumann kuhusu majadiliano na Abushiri ; In Deutsch-Ostarfrika während des Aufstandes, uk. 138
  2. Köfler-Sauer a.a.O. bei Anm. 39 und 40
  3. Morlang uk. 2
  4. Maelezo zaidi pamoja na majina angalia en:Hehe

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]