Idd el Hajj
Idd el Hajj (pia: Idi el Haji, Eid el Hajj) ni sikukuu ya Uislamu wakati wa mwezi wa Dhul Hijjah ambao ni mwezi wa Hajj. Sherehe hii inatunza kumbukumbu ya sadaka ya Ibrahimu.
Eid al-Adha Inaangukia tarehe 10 Dhu al-Hijja, mwezi wa kumi na mbili na wa mwisho wa kalenda ya Kiislamu. Sherehe na maadhimisho kwa ujumla huendelezwa kwa siku tatu zifuatazo, zinazojulikana kama siku za Tashriiq[1].
Eid al-Adha pia wakati mwingine huitwa Eid II au Idd Kubwa. Kama ilivyo kwa Eid al-Fitr, sala ya Eid inasaliwa asubuhi ya Eid al-Adha, baada ya hapo udhiyah, au dhabihu ya kiibada ya kondoo, inaweza kufanywa. Katika mapokeo ya Kiislamu, inaheshimu utayari wa Ibrahimu kumtoa mwanawe kama tendo la utii kwa amri ya Mungu. Kutegemeana na simulizi, ama Ishmaeli au Isaka wanarejelewa kwa jina la heshima Sadaka ya Mungu. Mahujaji wanaohiji kwa kawaida hufanya tawaf na saee ya Hajj siku ya Eid al-Adha, pamoja na ibada ya kumpiga mawe shetani siku ya Idi na siku zinazofuata.
Majina ya sikukuu
Kati ya Waislamu duniani sikukuu hii hujulikana kwa majina mbalimbali ambayo hutafsiriwa pia kwa lugha mbalimbali kama vile:
- Idd-al-Adhha (kwa Kiarabu: عيد الأضح) yaani sikukuu ya sadaka
- Idd-al-Qorban (kwa Kiarabu: عید قربان) sikukuu ya sadaka (kwa kutumia neno tofauti ya "sadaka" katika Qurani); kwa Kituruki: Kurban Bayramı; kwa Kikurdi "Cejna Kûrbanê";
- Idd-al-Kabir (kwa Kiarabu: عيد الكبير) au "sikukuu kubwa"; "Bari Eid" huko Uhindi na Pakistan; jina hili hutumiwa kwa sababu kati ya sikukuu mbili zinazoamriwa katika Qurani hii ni sikukuu kubwa zaidi.
Sadaka ya Ibrahimu
Idd husheherekewa kama kumbukumbu ya sadaka ya Ibrahimu (Abrahamu) ambaye kufuatana na taarifa za Biblia na za Qurani alikuwa tayari kumchinja mwanawe kama sadaka kwa Mungu. Lakini Mungu alimzuia asimchinje akampatia kondoo badala yake. Habari zake kati Qurani ziko sura al-Hajj aya 37, katika Biblia Mwanzo 22.
Katika mapokeo ya Biblia huyu mwana alikuwa Isaka. Qurani haitaji jina lake lakini Waislamu walio wengi huamini aliyemaanishwa ni Ismaeli, mwana wa Ibrahimu na Hagar.
Ibada zake
Sherehe huanza na sala ya idd katika msikiti. Mara nyingi hufuatwa na baraza au mkutano wa Waislamu. Katika nchi nyingi huwa na kawaida ya kutembelea pia makaburi ya marehemu.
Kila Mwislamu mwenye uwezo hupaswa kumchinja mnyama wa sadaka siku hiyo, mara nyingi kondoo, lakini kuna pia sadaka za mbuzi, ng'ombe au ngamia kufuatana na uwezo na kawaida ya nchi.
Sehemu ya nyama ya sadaka hizo hugawiwa kwa maskini wasio na uwezo. Nyingine hutumiwa kwa karamu ya familia.
Tarehe za Idd
Idd husheherekewa kati ya tarehe 10 hadi 13 ya mwezi wa Dhul Hijjah wa kalenda ya Kiislamu. Tarehe hali halisi hutegemea kuonekana kwa hilali au mwezi mwandamo. Hapa hutokea tofauti za kila mwaka kati ya Waislamu. Kimsingi mapokeo ya Kiislamu hudai mwezi kuonekana kwa macho.
Tofauti za makadirio kati ya Waislamu
Sehemu za Waislamu hukubali ya kwamba inawezekana kukadiria tarehe hii kisayansi, lakini huko Saudia husisitizwa kuona kwa macho. Maadamu Saudia ni mahali pa miji mitakatifu ya Maka na [Madina]], Waislamu wengine hupenda kufuata kawaida ya kule.
Zamani hapakuwa na tatizo sana kwa sababu kila nchi ilikuwa na azimio lake. Mitambo ya kisasa huonyesha siku hizi kama Waislamu wameshaanza kusheherekea nchi moja lakini nchi nyingine bado. Katika nchi mbalimbali, hasa kule ambako Waislamu walihamia juzi tu kama Ulaya, kuna tarehe tofauti kandokando kama wengine hufuata matangazo ya Uturuki yanayokadiriwa kisayansi na wengine matangazo ya Saudia yanayofuata kuonekana kwa macho. Matangazo ya Saudia yamepingwa mara nyingi kwa sababu tarehe zilitangazwa ambapo hapakuwa na uwezekano kuona hilali kisayansi.
Kubadilika kwa tarehe katika kalenda ya jua
Katika kalenda ya Gregori, ambayo ni kalenda ya kawaida, tarehe za Kiislamu hubadilika kila mara kwa sababu mwaka wa Kiislamu hufuata kalenda ya mwezi lakini kalenda ya kawaida hufuata jua. Kalenda ya Kiislamu ina takriban siku 11 pungufu kuliko kalenda ya jua. Kila mwaka tarehe ya Idd huweza kutokea kwa siku mbili tofauti za kalenda ya Gregori kwa sababu kawaida ya Uislamu hufuata kuonekana kwa mwezi kunakopatikana tofauti duniani.
Orodha inyaofuata yaonyesha tarehe rasmi za Idd-al-Hajj kwa nchi ya Saudia jinsi ilivyotangazwa hadi 2007 na halmashauri kuu ya Majlis al-Qadā’ al-A‘lā . Tarehe za miaka 2008 na kuendelea ni tarehe zinazokadiriwa kulingana na kalenda ya Kiislamu jinsi ilivyo kawaida katika nchi kama Uturuki. Tofauti zitaendelea kutokea kulingana na maelezo hapo juu kuhusu tofauti ya makadirio na kuonekana kwa hilali
- 1426 BH: 10 Januari 2006
- 1427 BH: 30 Desemba 2006 (jinsi ilivyotangazwa - tarehe ya kukadiriwa: 31 Desemba 2006)
- 1428 BH: 19 Desemba 2007 (jinsi ilivyotangazwa - tarehe ya kukadiriwa: 20 Desemba 2007)
- 1429 BH: 8 Desemba 2008 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1430 BH: 27 Novemba 2009 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1431 BH: 16 Novemba 2010 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1432 BH: 6 Novemba 2011 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1433 BH: 26 Oktoba 2012 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1434 BH: 15 Oktoba 2013 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1435 BH: 4 Oktoba 2014 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1436 BH: 23 Septemba 2015 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1437 BH: 11 Septemba 2016 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1438 BH: 1 Septemba 2017 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1439 BH:21 Agosti 2018 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1440 BH: 11 Agosti 2019 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1441 BH: 31 Julai 2020 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1442 BH: 20 Julai 2021 (tarehe ya kukadiriwa)
- 1443 BH: 10 Julai 2022 (tarehe ya kukadiriwa)
Viungo vya nje
- Background to Eid ul Adha Ilihifadhiwa 11 Februari 2008 kwenye Wayback Machine.
- Moonsightings for different regions or their following after some other region
- tarehe ikikadiriwa and (jinsi ilivyotangazwa dates for days of the Islamic Calendar
Makala hii kuhusu Uislamu bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |
- ↑ Kadi, Samar. "Eid al-Adha celebrated differently by Druze, Alawites", 25 September 2015. Retrieved on 1 August 2016. Archived from the original on 2017-12-12.