Nenda kwa yaliyomo

Utumwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha ya mvulana mtumwa huko Zanzibar, 1890 hivi.

Utumwa ni mfumo unaotoa fursa kwa binadamu kummiliki binadamu mwenzake kama mali yake. Binadamu anayemilikiwa anakuwa na hadhi sawa na chombo au kifaa chochote kinachoweza kuuzwa.

Mfumo huu ulianza kabla ya uandishi kubuniwa, ukawa maarufu hasa kabla ya harakati za ukoloni duniani, mathalani kuanzia karne ya 15, ambapo watumwa walihitajika katika shughuli za kilimo na uchimbaji madini katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, hasa Amerika, ingawa katika sehemu nyingine, hasa Uarabuni, walitafutwa hasa watumwa wanawake kwa ajili ya uasherati.

Mfumo huu huunda matabaka ya "mabwana" ambao humiliki watumwa na "watwana" ambao ni watumwa wenyewe.

Utumwa tofautitofauti

Katika historia zilitokea aina mbalimbali za utumwa.

Kulikuwa na utumwa wa muda (yaani mtu huwa mtumwa kwa miaka kadhaa) au kwa maisha yote.

Kulikuwa na utaratibu ambao watoto wa mtumwa walikuwa watumwa tena, hivyo kuzaliwa watumwa; kulikuwa pia na utaratibu wa kwamba watoto wa watumwa walitazamiwa kama watu huru.

Kulikuwa na jamii ambako watumwa hawakuwa na haki kabisa, yaani mabwana waliweza kuwatendea jinsi walivyotaka, hata kuwaua; lakini kulikuwa pia na jamii zilizojua haki fulani za watumwa: hapo watumwa waliweza kuwa na mali ya binafsi na kwa njia hii hata kununua uhuru wao kutoka kwa mabwana.

Watumwa katika utumishi wa watawala waliweza kupata nafasi muhimu katika jamii; mfano ni Wamameluki wa Misri waliokuwa watumwa wanajeshi wakatawala nchi hiyo kwa karne kadhaa.

Chanzo cha utumwa

Mtumwa huko Brazil.

Chanzo cha utumwa kilikuwa mara nyingi ama vita ama madeni.

Vitani waliotekwa wakauzwa kama watumwa wakihesabiwa kama sehemu ya uwindo wa washindi.

Sababu kuu nyingine ilikuwa madeni ya watu waliokamatwa na kuuzwa ili madeni yalipwe kwa njia hii.

Mahitaji ya kiuchumi ya kupata watumwa wengi yalisababisha biashara ya watumwa.

Uchumi wa Roma ya Kale ulitegemea watumwa waliokamatwa na kusafirishwa kutoka pande zote za mazingira ya Bahari Mediteranea.

Milki za makhalifa wa Uislamu ziliendelea kutegemea watumwa. Waosmani walichukua watoto wa Kikristo, hasa kutoka nchi za Balkani, na kuwapeleka kama watumwa katika sehemu za kusini za milki yao kama Misri walipofanya kazi kama wanajeshi.

Biashara ya Waarabu kuhusu watumwa ilidumu miaka 1,300, na kupeleka mamilioni ya Waafrika upande wa Asia.

Mahitaji ya uchumi wa kimataifa tangu karne ya 15 yalisababisha kuongezeka kwa biashara ya watumwa hasa kutoka Afrika; mamilioni walikamatwa na watawala wa milki kwenye pwani za Afrika au Waarabu na kuuzwa kwa wafanyabiashara Wazungu waliowapeleka Amerika walipohitajika kwa kazi kwenye mashamba makubwa ya miwa na pamba.

Biashara hii ilianza kupingwa zaidi tangu mwisho wa karne ya 18. Mkutano wa Vienna (1814-1815) ulikuwa mapatano ya kwanza ya kimataifa yaliyolenga kukataza biashara ya watumwa kutoka Afrika.

Hata hivyo iliendelea kwa miaka kadhaa hasa upande wa bahari Hindi ambako wanafayabiashara Waislamu kama Tippu Tip waliendelea kukamata watumwa na kuwapeleka pwani na Zanzibar kulikokuwa na soko la watumwa kubwa kuliko yote.

Ukoloni ulimaliza kwa kiasi kikubwa biashara hiyo Afrika pia, ingawa Mauritania ilifanya utumwa kuwa kosa la jinai mwaka 2007 tu.

Tangu karne ya 20 utumwa na pia biashara ya watumwa zimepigwa marufuku katika mapatano ya kimataifa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Lakini miaka ya hivi karibuni imeona biashara mpya inayotumia nafasi za usairi wa kisasa; hata kama duniani hakuna utumwa kisheria tena, ni hasa wanawake na mabinti wanaouzwa kwa kazi haramu ya ukahaba kati ya nchi na nchi.

Uislamu na utumwa

Uislamu ulikubali utumwa, hivyo katika nchi zinazofuata dini hiyo utumwa ulichelewa zaidi kufutwa.

Lakini Waislamu walifundishwa masharti fulani kama kuwatendea watumwa vizuri. Walifundishwa pia kwamba ni tendo jema mbele ya Mungu (Allah) kumwacha huru mtumwa.(Habari hii inatakiwa kuthibitishwa kwa kuonyesha vyanzo)

Ukombozi wa watumwa

Tazama makala kuu Wendo wa ukomeshaji wa utumwa

Watawa Wamersedari walijitosa kukomboa watumwa (mchoro wa mwaka 1637).

Katika historia ndefu za utumwa, kulitokea juhudi za kukomboa waliotekwa, hasa kwa kuwanunua ili kuwaacha huru.

Kati ya Wakatoliki yalianzishwa hata mashirika maalumu ya kitawa kwa lengo hilo, kwa mfano Watrinitari na Wamersedari.

Ukristo na utumwa

Kwa muda mrefu utumwa ulikuwa utaratibu wa kijamii katika sehemu nyingi za dunia.

Habari za kwanza za kimaandishi juu ya Afrika Mashariki (karne ya 2 K.K.) zilisema: "wanaleta kutoka pwani ile ndovu, dhahabu na watumwa".

Kule Ulaya kuna kundi la mataifa linaloitwa tangu zamani "Waslavi" (kama vile Warusi, Wapolandi, Waserbia n.k.). Kumbe neno "slavi" kiasili linamaanisha "watumwa": watu wa mataifa yale walikamatwa zamani na kuuzwa kama watumwa katika sehemu nyingine za Ulaya, Asia na pia Afrika Kaskazini.

Hali hiyo ni mbaya sana, hailingani kabisa na utu na heshima ya kibinadamu, wala haipatani na Ukristo unaokiri na kulenga udugu wa watu wote. Lakini watu walioishi zamani katika mazingira yenye utumwa walikuwa wamezoea hali hiyo.

Habari za watumwa tunaweza kuzisoma hata katika Biblia. Ilikuwa jambo la kawaida katika mazingira ya Israeli ya Kale. Mtu aliweza kukamatwa na kuuzwa utumwani ili kulipia madeni yake. Mara nyingi watumwa walikuwa watu waliokamatwa vitani. Kwa mfano wakazi wote wa Yerusalemu walifanywa watumwa baada ya mji huo kutekwa na wanajeshi Waroma mwaka 70 B.K. Wakati wa Biblia asilimia 20 hivi za wakazi wa Dola la Roma walikuwa watumwa. Lakini katika nchi ya Israeli hali ilikuwa tofauti. Sheria ya Musa ilimwacha mtumwa awe huru baada ya miaka 7 (Kut 21:2). Kwa sababu hiyo hawakuwapo watumwa wengi katika Israeli. Labda ndiyo sababu Yesu hakufundisha juu ya utumwa kwani walikuwa wachache sana katika mazingira yake.

Mtume Paulo aliishi zaidi nje ya eneo la Israeli. Katika miji mikubwa kama Antiokia, Korintho, Efeso au Roma watumwa walikuwa wengi. Paulo alifundisha ni wajibu wa mabwana Wakristo kuwatendea watumwa wao vizuri. Kwa nini hakupinga utumwa?

Wataalamu wengi hudhani kwamba Paulo alitegemea kurudi kwake Yesu na mwisho wa dunia kuwa karibu sana, hivyo hakuona umuhimu wa kubadilisha taratibu za kijamii. Lakini alisititiza kwamba ndani ya Kanisa ni marufuku kutofautisha kati ya watumwa na walio huru. Ukristo uliweza kuvuta watumwa wengi, kwani uliwakubali kuwa binadamu wenye utu na heshima kamili. Wapinzani wa Ukristo waliuita "Dini ya watumwa". Walau mtumwa mmoja alichaguliwa kuwa Askofu wa Roma. Kanisa Katoliki linamkumbuka kama Mtakatifu Papa Kalisti I.

Baada ya uenezaji wa Ukristo utumwa ulipungua sana Ulaya. Vilevile walimu wengi Wakristo walipinga utumwa wenyewe. Hatimaye mabadiliko ya uchumi yaliondoa faida ya kutumia watumwa.

Hali hii ilibadilika baada ya kuanzishwa kwa ukoloni Amerika. Wareno na Wahispania walioteka nchi za huko walivutwa na tamaa ya dhahabu.

Mataifa ya Ulaya yalipeleka ng'ambo mara kwa mara wafungwa wao kwa nia ya kusafisha jamii zao na kupunguza gharama za magereza. Watu waliona kule mbali hawawezi kusababisha hasara. Kumbe hawakujali hali ya wenyeji walioteswa na wale wakorofi walioona nafasi ya kujitajirisha.

Hata maafisa wa serikali za kikoloni walishindwa kuwadhibiti vizuri kwani waliwategemea katika kuwatawala wenyeji ambao hawakunyamaza kwa hiari. Ndipo wamisionari walipojitahidi kupambana na ukorofi uliokuwepo, lakini kiasi: jinsi mapato kutoka makoloni yalivyokuwa muhimu kwa makisio ya serikali za Ulaya, haikuwa rahisi kupambana na unyonyaji katika makoloni ya mbali.

Kanisa Katoliki halikukubali rasmi biashara ya watumwa, lakini Mapapa waliona hawana nguvu ya kuizuia. Walijaribu zaidi kuweka masharti jinsi ya kuwatendea watumwa. Mataifa kadhaa yalifuata mafundisho ya Kanisa: k.mf. Hispania na Ufaransa zilikataa kuwa na soko la watumwa lakini zilifunga macho raia wao wakiendesha biashara hiyo nje ya mipaka yao. Wengine kama Wareno hawakuona tatizo kufanya biashara hiyo.

Watumwa wa kwanza kutoka Afrika waliingia Ureno wakati Mfalme wa Ureno alipokubali kupokea kutoka kwa Waarabu wa Moroko watumwa kadhaa kama malipo ya madeni. Wapelelezi Wareno walioanza kuzunguka pwani za Afrika walileta tena na tena wafungwa kama watumwa. Lakini mpaka wakati ule walikuwa wachache kwani Ulaya soko lilikuwa dogo.

Kumbe baada ya kuanzishwa kwa makoloni Amerika watumwa walitafutwa sana kwa ajili ya kulima mashamba makubwa na kuchimba madini kule. Hivyo ukoloni Amerika ulisababisha kukua kwa mahitaji ya watumwa.

Hapo utaratibu wa kale wa utumwa ulipanuka kuwa mbaya sana kuliko awali. Milioni nyingi za Waafrika waliuawa katika vita vya kukamata watumwa na nyingine nyingi wakapelekwa wamefungwa kule Amerika katika hali ya kutisha.

Vurugu iliyoharibu jamii nyingi za Kiafrika ndiyo iliyosababisha vilevile uharibifu wa misheni za Kikristo katika karne za 16-18. Uharibifu wa taratibu za kijamii ulikuwa mbaya zaidi katika maeneo ya pwani yaani kulekule walipoingia wamisionari.

Si ajabu kwamba Waafrika wengi walishindwa kutambua tofauti kati ya wamisionari Wareno na wafanyabiashara ya watumwa kutoka taifa lilelile. Hali ilikuwa mbaya zaidi wamisionari wenyewe walipojiingiza katika mambo ya utumwa kama walivyofanya wengine.

Kwa jumla ni aibu kubwa kwamba Wakristo wengi walitumia muda mrefu mno kutambua kwamba Ukristo na utumwa havipatani.

Mwanzoni awamu mpya ya utumwa haikuonekana kwa watu wengi kule Ulaya, maana uliendeshwa hasa Afrika na Amerika. Lakini habari zake zilienea. Mara walijitokeza waliopinga utumwa au waliojaribu kupunguza nguvu yake. Lakini wakati ule katika nchi mbalimbali za Ulaya hata wakulima wengi hawakuwa huru kweli (ingawa si watumwa).

Katika karne ya 17 kule Uingereza Wakristo wa madhehebu ya "Marafiki" (waliitwa pia "Quakers") waliamua kwamba utumwa haupatani na Ukristo, hivyo mwenye watumwa anajitenga nayo. Polepole wengine wakaunga mkono hoja hiyo hata likajitokeza tapo la kufuta utumwa.

Wakristo wa tapo hilo walimshtaki Mwingereza mlowezi katika Visiwa vya Karibi aliyetembelea Uingereza akiwa na mtumwa. Mwaka 1772 hakimu aliamua si halali kuwa na watumwa katika nchi hiyo.

Wapinzani wa utumwa wakaendelea kusukuma Bunge la Uingereza. Lakini matajiri wa Liverpool (waliofaidika na utumwa kama wenye meli au kwa sababu waliendesha biashara ya watumwa wenyewe) walitetea vikali hali halisi. Katika karne ya 19 polepole utumwa na biashara ya watumwa vilikomeshwa katika sehemu nyingi za dunia.

Mtawanyiko ndani ya Kanisa ulikuwa jambo wa kusikitisha sana. Kumbe hapa tumepata mfano jinsi Mungu alivyotumia vikundi vidogovidogo kuelimisha Wakristo wote. Maana madhehebu makubwa yalikosa nguvu ya kupinga vikali utumwa kwa kuwa karibu mno na serikali, tena matajiri. Ni Wakristo wa madhehebu madogo kama Marafiki au Wamethodisti waliotangulia na kusaidia Wakatoliki, Waanglikana na Wareformati kutambua ukweli.

Hali nyingine iliyosaidia kukomesha utumwa ni mabadiliko ya uchumi. Umuhimu wa kazi ya watumwa ulipungua sana kutokana na njia mpya za kuzalisha mali. Si tena wafanyabiashara ya "Biashara kati ya Amerika, Ulaya na Afrika" (Triangular trade) waliokuwa na pesa nyingi (hivyo na athari pia) katika jamii ya Uingereza. Waliopata uzito zaidi ni mabepari ambao waliendesha viwanda wakitumia wafanyakazi huru na si watumwa. Hivyo ubepari ulibadilisha mkazo ndani ya jamii mbalimbali.

Tazama pia

Marejeo

Ya jumla

  • Bales, Kevin, Disposable People: New Slavery in the Global Economy (1999)
  • Campbell, Gwyn, Suzanne Miers, and Joseph C. Miller, eds. Women and Slavery. Volume 1: Africa, the Indian Ocean World, and the Medieval Atlantic; Women and Slavery. Volume 2: The Modern Atlantic (2007)
  • Davies, Stephen (2008). "Slavery, World". In Hamowy, Ronald. The Encyclopedia of Libertarianism. Thousand Oaks, CA: SAGE; Cato Institute. pp. 464–9. ISBN 978-1-4129-6580-4
      . LCCN 2008009151
       . OCLC 750831024
      . http://books.google.com/books?id=yxNgXs3TkJYC.
  • Davis, David Brion. The Problem of Slavery in the Age of Revolution, 1770-1823 (1999)
  • Davis, David Brion. The Problem of Slavery in Western Culture (1988)
  • Drescher, Seymour. Abolition: A History of Slavery and Antislavery (2009) highly regarded history of slavery and its abolition, worldwide
  • Finkelman, Paul, ed. Encyclopedia of Slavery (1999)
  • Gordon, M. Slavery in the Arab World (1989)
  • Greene, Jacqueline. Slavery in Ancient Egypt and Mesopotamia, (2001), ISBN 0-531-16538-8
  • Joseph, Celucien L. Race, Religion, and The Haitian Revolution: Essays on Faith, Freedom, and Decolonization (CreateSpace Independent Publishing Platform, 2012)
  • Joseph, Celucien L. From Toussaint to Price-Mars: Rhetoric, Race, and Religion in Haitian Thought (CreateSpace Independent Publishing Platform, 2013)
  • Lal, K. S. (1994). "Muslim Slave System in Medieval India". ISBN 81-85689-67-9. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-05-12.
  • Miers, Suzanne, and Igor Kopytoff, eds. Slavery In Africa: Historical & Anthropological Perspectives (1979)
  • Morgan, Kenneth. Slavery and the British Empire: From Africa to America (2008)
  • Postma, Johannes. The Atlantic Slave Trade, (2003)
  • Rodriguez, Junius P., ed., The Historical Encyclopedia of World Slavery (1997)
  • Rodriguez, Junius P., ed. Slavery in the United States: A Social, Political, and Historical Encyclopedia (2007)
  • Shell, Robert Carl-Heinz Children Of Bondage: A Social History Of The Slave Society At The Cape Of Good Hope, 1652–1813 (1994)
  • Westermann, William Linn The Slave Systems of Greek and Roman Antiquity (1955), ISBN 0-87169-040-3
Vyanzo visivyotajwa
  • Hogendorn, Jan and Johnson Marion: The Shell Money of the Slave Trade. African Studies Series 49, Cambridge University Press, Cambridge, 1986.
  • The Slavery Reader, ed. by Rigas Doganis, Gad Heuman, James Walvin, Routledge 2003
Marekani
      . LCCN 2008009151
       . OCLC 750831024
      . http://books.google.com/books?id=yxNgXs3TkJYC.
Nyakati zetu

Viungo vya nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Zamani

Nyakati zetu