Nenda kwa yaliyomo

Ukoloni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kikoloni)
Ramani ya Ukoloni duniani kabla ya Vita ya Miaka Saba mnamo mwaka 1754
Ramani ya ukoloni duniani mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945.

Ukoloni ni mfumo wa taifa moja kuvuka mipaka yake na kutawala maeneo ya mbali yanayokaliwa na watu wengine kwa nyanja za uchumi, utamaduni na jamii. Maeneo hayo yanaweza kuitwa makoloni ya kawaida au maeneo lindwa tu.

Neno "koloni" linatokana na Kilatini colonia (kupitia Kiingereza colony). Ni kwamba Roma ya Kale ilipanua eneo lake kwa kuanzisha miji mipya ya nje kwa kuteua raia na kuwapa ardhi kwa ajili ya mashamba huko. Hiyo iliitwa koloni.

Milki nyingine za kale zilitumia mtindo huohuo kama vile Wagiriki wa Kale na Wafinisia.

Neno hilo la Kilatini lilitumiwa baadaye kwa ajili ya kutaja makazi mapya ya watu kutoka eneo moja katika eneo la mbali. Ilhali hatua hii ilimaanisha mara nyingi pia upanuzi wa utawala wa eneo mama, neno likataja baadaye pia eneo linalotawaliwa na nchi ya mbali.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Ukoloni ni hasa ule wa kipindi tangu karne ya 15 ambako Ureno na Hispania zilianza kueneza himaya zao Afrika na Amerika ya Kusini na kudumu pengine hadi baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Lakini kulikuwa na vipindi vya ukoloni pia zamani katika historia kama vile ukoloni wa Roma ya Kale, ukoloni wa Waarabu na wengine. Ukoloni kwa maana hii unaweza kuwa tofauti na kuundwa kwa koloni katika vipindi mbalimbali vya historia ambapo maeneo bila wakazi au yenye wakazi wachache sana yaliingiliwa na watu kutoka sehemu nyingine.

Ukoloni mamboleo ni aina ya nchi au kundi la nchi fulani kutawala nchi nyingine kinyemela kwa kuweka vikwazo na masharti yatakayowafanya watawaliwa waendelee kuwa na uchumi tegemezi ili watajirishe zaidi hao wanaowatawala kinyemela.

Utawala wa kikoloni

[hariri | hariri chanzo]

Utawala wa kikoloni ni utawala ulioanzishwa hasa na Wazungu kwa lengo la kunyonya na pengine kuwabagua Waafrika na watu wengine wenyeji wa Asia, Oseania na Amerika.

Utawala huo ulitegemea hali ya taifa husika pamoja na hali ya jamii zilizokuwa zinatawaliwa.

Baada ya kuanzisha utawala huo wakoloni walibadilisha utawala wa jadi na kuufanya utawale kwa masilahi ya wakoloni; pia utawala huo uliharibu hadhi ya utawala wa jadi na misingi ya jadi.

Muundo wa utumishi

[hariri | hariri chanzo]

Muundo wa utumishi katika utawala wa kikoloni ulikuwa wa kibaguzi na kinyonyaji:

(a) Kazi katika ngazi za juu zilifanywa na Wazungu, hasa kazi zilizohitaji ujuzi.

(b) Kazi katika ngazi za chini zilifanywa na wenyeji kama vile ukarani, utarishi, ufagizi na ukorokoroni.

(c) Wakoloni walitoa elimu duni kwa wenyeji ili waendelee kuwaajiri katika ngazi za chini.

Makoloni yaliyokuweko Afrika

[hariri | hariri chanzo]

Nchi za Afrika ziliwekwa rasmi chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya mara baada ya Mkutano wa Berlin wa 1885 ulioitishwa na chansella wa Ujerumani Bismarck mwaka 1884-1885.

Nchi zilizojenga ukoloni huo Afrika zilikuwa Uingereza, Ufaransa, Ureno, Ujerumani, Uhispania, Italia na Ubelgiji. Uholanzi karne za nyuma ilikuwa na Afrika Kusini.

1. Ubelgiji ilikuwa na maeneo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda ya leo

2. Uingereza ilikuwa na Afrika Kusini, Botswana, Cameroon ya Kiingereza, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Misri, Nigeria, Shelisheli, Sierra Leone, Somaliland, Sudan, Swaziland, Tanganyika, Uganda, Zanzibar, Zambia, Zimbabwe na sehemu nyingine kwa muda.

3. Ufaransa ilikuwa na Algeria, Benin, Cameroon, Chad, Cote d'Ivoire, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jibuti, Komoro, Gabon, Guinea, Madagaska, Mali, Mauritania, Moroko, Niger, Senegal, Togo, Tunisia na sehemu nyingine kwa muda.

3. Ujerumani ilikuwa na Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani (leo Namibia), Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (tangu 1922 Burundi, Rwanda na Tanganyika), Kamerun na Togo, lakini baada ya vita vikuu vya kwanza ilinyang'anywa kila mojawapo; zilikuwa maeneo ya kudhaminiwa kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa na kuweka chini ya Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji na Afrika Kusini.

4. Italia ilikuwa na Eritrea, Libya na Somalia ya Kiitalia; pia Ethiopia kwa miaka mitano tu (1936-1941).

5. Ureno ilikuwa na Angola, Cape Verde, Guinea-Bissau, Msumbiji, Sao Tome na Principe

6. Hispania ilikuwa na Guinea ya Ikweta, sehemu za Moroko na Sahara Magharibi.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]