Nguvu (adili)
Maadili bawaba |
---|
Nguvu (kwa Kigiriki ἀνδρεία - andreia; kwa Kilatini fortitudo; kwa Kiingereza courage) ni adili la kiutu linalomfanya mtu awe imara na kudumu kulenga mema hata katika matatizo.
Linathibitisha nia ya kushinda vishawishi na mapingamizi katika njia ya uadilifu. Linawezesha kushinda hofu hata ya kifo na kuvumilia majaribu na dhuluma. Hivyo mtu anakuwa tayari hata kuuawa ili kutetea jambo la haki.
Kuanzia Plato nguvu inatajwa kati ya maadili manne yanayoitwa maadili bawaba kwa kuwa yanategemeza maadili mengine yote ya kiutu.
Subira na ustahimilivu, nguzo za maisha ya Kikristo
[hariri | hariri chanzo]Nyakati hizi ngumu inafaa tuyakumbuke maneno ya Yesu kuhusu adili la nguvu linalohitajika ili tusiogope tishio lolote wala kuzuiwa na pingamizi lolote kwenye njia ya wokovu: “Kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu” (Lk 21:19). Subira ndiyo namna ya kawaida zaidi ya kutekeleza nguvu katika matatizo ya maisha.
Subira ni adili ambalo linategemea nguvu na kuzuia mtu asiache kufuata akili iliyoangazwa na imani akishindwa na matatizo na huzuni; linamfanya avumilie mabaya asivurugwe nayo. Asiye na subira, hata akiwa mkali, ni dhaifu tu: kwa kweli anapofoka ameshindwa kiadili. Kinyume chake, mwenye subira anavumilia baya lisiloepukika ili aendelee kupanda kwa Mungu. Hiyo ni tofauti na ugumu wa wale wanaovumilia mapingamizi mradi wafikie matamanio ya kiburi chao. Kwa adili hilo mtu anatawala dhoruba za hisi zilizopatwa na huzuni. Wafiadini wanajitawala na kuwa huru kwa namna bora. Katika subira tunakuta sehemu ya tendo kuu la adili la nguvu: kuvumilia tabu bila kushindwa nazo. Kuvumilia kwa muda mrefu kinachopingana na umbile ni kugumu na kustahili kuliko kumshambulia adui kwa muda mfupi wa ari. Basi, ikiwa nguvu inavumilia mapigo yanayomuua askari vitani na hasa mfiadini, adili la subira linavumilia matatizo ya maishani bila kuyajali. Hivyo linalinda maadili mengine dhidi ya vurugu na kutegemeza jengo la Kiroho. Lakini ili subira iwe na msimamo ni lazima mtu awe na neema inayotia utakatifu, yaani upendo unaomjali Mungu kuliko yote na kwa vyovyote: “Upendo huvumilia” (1Kor 13:4).
Matatizo yakidumu muda mrefu mfululizo, inavyomtokea mtu anayepaswa kuishi na mkorofi, linahitajika adili ambalo linafanana na subira na kuitwa ustahimilivu, kutokana na urefu wa majaribu, mateso na dharau. Ili tutekeleze adili hilo Kikristo tukumbuke mara nyingi subira ya Mwokozi msalabani, inayopita wazo lolote la kibinadamu. “Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo” (2Thes 3:5). Kwa upendo wetu alivumilia mateso ya mwili makali mno, pamoja na yale ya roho yaliyomjia kutoka kwa watu wake na hata kwa kujisikia amelaaniwa na Mungu kwa niaba ya dhambi alizozibeba. “Kumbukeni mara nyingi kuwa Bwana wetu ametuokoa kwa kuteseka na kuvumilia, na kuwa vivyo hivyo sisi tunapaswa kuufikia uzima wa milele kwa njia ya mateso na huzuni, kwa kuvumilia dharau, upinzani na masikitiko kwa upole mkubwa iwezekanavyo… Wapo wanaokubali tu mateso yanayoleta heshima, k.mf. kujeruhiwa vitani… Aliye mvumilivu kweli na mtumishi wa Mungu anavumilia vilevile tabu zinazoleta aibu ya kusemwa, kulaumiwa na kutendwa vibaya na watu wema, marafiki, ndugu… Upinzani unaotoka kwa watu wema unavumilika vibaya zaidi, lakini unatokea mara nyingi sana” (Fransisko wa Sales). Tabu zilizovumiliwa vizuri ndizo matofali yanayojenga wokovu wetu, fungu la wana wa Mungu hapa duniani na dalili ya uteule, kwa kuwa “imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (Mdo 14:22). Pengine tendo moja la subira kubwa kufani linatosha kutupatanisha na Mungu. Tujifunze kuteseka kwa utulivu, pasipo manung’uniko. Watakaoshiriki zaidi mateso ya Yesu watatukuzwa zaidi pamoja naye.
Upole wa Kikristo na matunda yake
[hariri | hariri chanzo]Upole unaotakiwa kuendana na subira unatofautiana nayo kwa kuwa tokeo lake maalumu ni kuzuia vurugu za hasira, si kuvumilia tabu. Adili la upole ni tofauti na silika ya upole kwa sababu linaratibu kwa mwanga wa akili (na wa imani) hisi zilizotikiswa na hasira. Adili hilo ni bora kuliko tabia hiyo ya kisaikolojia, kama vile usafi wa moyo ulivyo bora kuliko elekeo la haya, na adili la huruma kuliko ulaini wa moyo. Mara nyingi tabia ya upole inajitokeza kwa watu wanaopendeza, lakini inaendana na ukali kidogo kwa wasiopendeza. Kumbe adili la upole linaondoa ukali na uchungu kwa wote na katika nafasi yoyote. Tena linaingiza utulivu fulani hata unapotakiwa ukali: kwa kuwa linategemea adili la kiasi, linapenda kutozidisha.
Upole huo unakusudiwa kutawala si maneno na mwenendo tu, bali moyo pia, la sivyo ni bandia. Ukisababishwa na lengo lipitalo maumbile na ukitekelezwa hata kwa watu wakali, upole ni “ua la upendo” (Fransisko wa Sales). Katika mmea ua ndiyo sehemu ya kuvutia zaidi, na ingawa ni dhaifu lina kazi muhimu ya kutunza tunda linaloundika ndani yake. Vivyo hivyo upole ndio unaovutia zaidi katika utekelezaji wa upendo. Ndiyo sura yake ambayo inajitokeza katika macho, tabasamu, mwenendo na maneno, ikizidisha thamani ya huduma inayotolewa. Pia unatunza matunda ya upendo na ari, kwa kufanya mashauri na maonyo yapokewe vizuri. Tunaweza tukawa na ari kwa jirani, lakini tusipotumia upole hatutaonyesha tunawapenda, na nia zetu njema zitashindikana kwa sababu tutaonekana kusema kwa hasira kuliko kwa busara na hekima.
Upendo unastahili kwa namna ya pekee unapotumiwa kwa wanaotutesa; hapo kwa hakika si wa kibinadamu, bali unatoka kwa Mungu na pengine unamgusa aliyetukasirikia bure. Sala ya Stefano (taz. Mdo 7:60) ilimvutia Saulo neema ya uongofu, na upole unawaondolea silaha wakatili. “Hakuna kinachoweza kumtuliza tembo aliyekasirika kuliko sura ya mwanakondoo, na hakuna kinachozuia nguvu ya mzinga kuliko sufu” (Fransisko wa Sales). Pengine upole wa Kikristo unaogeuza shavu la pili unamtuliza mwenye hasira walau kidogokidogo.
“Ni afadhali kuunda watubu kwa kutumia upole kuliko kuunda wanafiki kwa kutumia ukali… Mjitahidi kutekeleza upole mnyenyekevu unaowapasa kwa wote, kwa kuwa ndio adili bora alilotusisitizia Bwana wetu. Ikiwatokea kukosa dhidi yake, msifadhaike, bali kwa tumaini kubwa muinuke tena na kuendelea na safari kwa amani na upole kama awali” (Fransisko wa Sales). Tunashika nzi wengi zaidi kwa tone la asali kuliko kwa pipa la siki. Inahitajika ari, lakini yenye upole na subira. Basi, tuepe ari chungu ya kukaripia daima ambayo inasababishwa na kiburi na iliharibu marekebisho mengi utawani. Dhidi yake Yohane wa Msalaba alisema, “Pasipokuwa na upendo wa kutosha, mpatie upendo, nanyi mtavuna upendo”.
Heri ya upole inahusiana na kipaji cha ibada ambacho kinatutia mvuto wa upendo wa kitoto kwa Mungu tuzidi kumuona kama Baba mpendwa; hivyo kinatufanya tuone watu kuwa ndugu, watoto wa Baba yuleyule, si watu tusiohusiana nao wala wapinzani. Kipaji hicho kinatusemesha kwa dhati zaidi na zaidi, “Baba yetu uliye mbinguni…”, tukitamani ufalme wake uimarike ndani yetu na ya ndugu zetu; hamu hiyo inasababisha upole unaong’aa kwa jirani.
Ili tutekeleze vizuri adili hilo, tunapaswa kulizingatia lilivyo ndani ya Yesu, upole upitao maumbile ambao umetokana na ari ya kuokoa watu bila kuipunguza, kama alivyotabiriwa, “Hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima” (Isa 42:2-3). Alipobatizwa alishukiwa na Roho Mtakatifu kwa sura ya njiwa, akatambulishwa kuwa “Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu” (Yoh 1:29). Hatimaye msalabani akawasamehe watesi wake kwa kuwaombea. Ndio upole katika tendo kuu la nguvu; tabasamu ya Msulubiwa ndiyo sura bora ya wema hapa duniani. Upole wa namna hiyo ni moja ya dalili zinazobainisha zaidi wafiadini wa kweli. Watu wengine wanayafia mawazo yao, na kiburi kinawafanya wavumilie mateso; ndani mwao haupatikani ulinganifu wa maadili yanayoonekana kupingana. Kumbe wafiadini ni wapole hata kwa watesi na wanawaombea; sasa kusahau mateso yao wenyewe ili kufikiria wokovu wa watesi ni dalili ya upendo mkuu unaolinganisha maadili yote ndani yake.
Tumuombe Bwana adili hilo pamoja na unyenyekevu wa moyo; tumuombe kwenye komunyo, katika ule muungano wa dhati wa roho yetu na yake, wa akili yetu na yake, wa moyo wetu na wake uliofurika upendo. Tumuombe mara nyingi, halafu tukipata nafasi tuyatekeleze maadili hayo kwa bidii. Hapo yatatimia maneno yake: “Mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu” (Math 11:29). Wakati wa ukinaifu na mahangaiko tung’amue raha hiyo kwa kusamehe kabisa waliotukosea. Kwa msaada wa neema tutarudi mahali petu mbele ya Bwana na ya jirani, kwenye utulivu wa utaratibu tuliopangiwa na kwenye amani ya dhamiri nyofu iliyounganika na Mungu wake. Katika upendo tutaona amani itokayo kwa Mungu, tofauti na ile ya nje tu inayopatikana ulimwenguni kwa kukubaliana na maadui wa Mungu na maelekeo yetu mabaya, kwa kutengana na waadilifu na kusambaratika kwa ndani: hiyo ni amani ya mauti inayoendana na uwozo. Kumbe amani aliyotuachia Bwana ni ya dhati na inadai tupambane mfululizo na tabia zetu mbovu, na ulimwengu na shetani: “Sikuja kuleta amani, bali upanga” (Math 10:34). Hakika, hatuwezi kuwa wanyenyekevu na wapole kwa wote tusipotumia nguvu juu yetu. Lakini, hata kama upendo wake una masharti makali, tunang’amua ukweli wa maneno yake: “nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi” (Math 11:30). Uzito wa mzigo huo unapungua kadiri yanavyostawi maadili ambayo ni namna za upendo. “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote; hutumaini yote, hustahimili yote” (1Kor 13:4-7). Upole huo wa Kimungu unaandaa kuzama katika sala, ni utangulizi wa heri isiyo na mwisho.
Ushujaa wa adili la nguvu
[hariri | hariri chanzo]Ndani ya mtu aliyekamilika unyenyekevu na upole vinaendana na maadili ya nguvu na moyo mkuu ambayo yanaonekana kuwa kinyume chake, kumbe yanakamilishana navyo.
Nguvu ni adili la kiutu linalotuimarisha katika kulenga mema magumu tusiogope mapingamizi makubwa. Inatawala hofu yetu mbele ya hatari, kazi za kuchosha, lawama na yale yote yanayoweza kupooza juhudi za kuelekea mema; halafu inatuzuia tusisalimu amri tunapopaswa kupambana. Nguvu inaratibu pia ushupavu na uchangamfu usiofaa ambavyo vinaelekeza kutenda bila kujali lolote. Matendo yake makuu ni mawili: kukabili hatari na kustahimili magumu. Tunapaswa kuyavumilia kwa upendo wa Mungu, na kwa hakika ni vigumu kustahimili muda mrefu kuliko kujitosa wakati wa kuchangamka.
Nguvu inaendana na subira katika kuvumilia huzuni za maishani bila kuhangaika wala kulalamika, halafu inaendana na ustahimilivu unaovumilia muda mrefu, na udumifu katika kutenda mema ambao ni kinyume cha ukaidi katika kutenda mabaya. Adili la nguvu linahusiana pia na moyo mkuu unaosukuma kutenda makuu katika maadili yote, ukikwepa ulegevu pasipo kuangukia makosa ya kujiamini, kujivuna au kutaka kuringa.
Kipaji cha nguvu kinaliongezea ukamilifu wa juu zaidi na kutuandaa tupokee uvuvio wa Roho Mtakatifu ukija kututegemeza mbele ya hatari, na kuondoa hangaiko la kujisikia hatuwezi kutimiza wajibu mkubwa wala kuvumilia majaribu yanayotukabili. Kipaji hicho kinadumisha “njaa na kiu ya haki” katika hali yoyote.
Ushujaa wa adili la nguvu unadhihirishwa hasa na kifodini kinachovumiliwa ili kutetea ukweli wa imani au adili fulani. Nje ya kifodini, adili la nguvu na kipaji cha nguvu, pamoja na subira na moyo mkuu vinatumika kila palipo na haja ya kutenda kishujaa au kuvumilia makubwa. Nguvu hiyo ya Kikristo inatofautiana na uvumilivu wa mwenye kiburi, kwa sababu inaendana na unyenyekevu, upole na unyofu mkubwa. Huo wa mwisho ni wa kishujaa unapopenda ukweli hata kukwepa kila undumakuwili, uongo, ulaghai, utata, ingawa unajua kutunza siri usiseme yale yote yaliyomo moyoni.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Aristoteles. 2014. Éthique à Nicomaque. Ed. Pierre Pellegrin. Lutetiae: Éditions Flammarion.
- Aultman, Julie. 2008. "Moral Courage Through a Collective Voice." The Journal of Positive Psychology 8 (4): 67–69. doi:10.1080/15265160802147140.
- Avramenko, Richard. 2011. Courage: The Politics of Life and Limb. University of Notre Dame Press.
- Becker, Ernest. 1973. The Denial of Death. Novi Eboraci: The Free Press.
- Bussey, K. 1992. "Lying and truthfulness: Children's definitions, standards, and evaluative reactions." Child Development 63, 129–37.
- Deci, E. L., R. M. Ryan. 2000. "The 'what' and 'why' of gal pursuits: Human needs and the self-determination of behavior." Psychological Inquiry 4: 227–68.
- Deutsch, M. 1961. "Courage as a concept in social psychology." The Journal of Positive Psychology 55 (1): 49–58. doi:10.1080/00224545.1961.9922158.
- Eisenberger, R. 1992. "Learned industriousness." Psychological Review 99: 248–67.
- Evans, P. D., et D. G. White. 1981. "Towards an empirical definition of courage." Behaviour Research and Therapy 19: 419–24.
- Fleury, Cynthia. 2010. La fin du courage: la reconquête d'une vertu démocratique. Lutetiae: Fayard.
- Hobbes, Thomas. 1972. De Homine et De Cive, ed. Bernard Gert. Indianapoli: Hackett Publishing Company. ISBN 978-0-8446-4756-2.
- Hobbes, Thomas. 1991. Leviathan, ed. Richard Tuck. Cantabrigiae: Cambridge University Press.
- Hume, David. 1751. An Enquiry Concerning The Principles Of Morals. Lanhamiae Terrae Mariae: Start Publishing LLC.
- Hume, David. 2009. A Treatise On Human Nature: Being an Attempt to Introduce the Experimental Method of Reasoning into Moral Subjects. The Floating Press.
- Jeanmart, G., L. Blésin, eds. 2009. "Figures du courage politique dans la philosophie moderne et contemporaine, numéro thématique de la revue Dissensus." Revue de philosophie politique de l'Université de Liège 2 (autumnus).\ Editio interretialis. Archived 30 Mei 2013 at the Wayback Machine.
- Kerfoot, K. M. 2012. "Courage as a concept in social psychology." Nursing Economics 30 (3): 176–78.
- Kühne, Ulrich, ed. 2006.l Mutige Menschen: Frauen und Männer mit Zivilcourage. Monaci: Elisabeth Sandmann Verlag.
- McDonnell, Myles. 2006. "Roman Manliness: 'Virtus' and the Roman Republic." Cantabrigiae: Cambridge University Press. ISBN 978-0-5218-2788-1.
- Meyer, Gerd. 2007. Lebendige Demokratie: Zivilcourage und Mut im Alltag: Forschungsergebnisse und Praxisperspektiven. Ed. 2a. Baden-Baden: Nomos. ISBN 3-8329-0444-1.
- Miller, William Ian. 2000. The Mystery of Courage. Cantabrigiae Massachusettae: Harvard University Press. ISBN 978-0-674-00826-7.
- Nietzsche, Friedrich. 1989. Beyond Good and Evil: Prelude to a Philosophy of the Future. Novi Eboraci: Vintage. ISBN 978-0-521-77078-1.
- Osho. 1999. Courage: The Joy of Living Dangerously. Londinii: Macmillan. ISBN 978-0-312-20517-1.
- Palmquist, Stephen. 2000. "Angst and the Paradox of Courage." The Tree of Philosophy. Hong Kong: Philopsychy Press.
- Pianalto, Matthew. 2012. "Moral Courage and Facing Others." Philosophical Studies 20 (2): 165–84. doi:10.1080/09672559.2012.668308.
- Plato. 1997. Complete Works, ed. John M. Cooper et D. S. Hutchinson. Indianapoli: Hackett Publishing. ISBN 978-0-87220-349-5.
- Peterson, C., et M. E. P. Seligman. 2004. Character Strengths and Virtues: A Handbook and Classification. Novi Eboraci: Oxford University Press.
- Pury, Cynthia L. S., et J. Lopez Shane 2010. "The Psychology of Courage: Modern Research on an Ancient Virtue." Decade of behavior. American Psychological Association.
- Putman, Daniel. 2001. "The Emotions of Courage." Journal of Social Philosophy 32 (4): 463–70. doi:10.1111/0047-2786.00107.
- Rate, Christopher R., Jennifer A. Clarke, Lindsay Sternberg, et Robert J. Sternberg. 2007. "Implicit theories of courage." The Journal of Positive Psychology 2 (2): 80–98. doi:10.1080/17439760701228755.
- Rousseau, Félicien. 1985. Courage ou résignation et violence. Lutetiae: Editions Le Cerf.
- Ryan, R. M., et C. Frederick. 1997. "On energy, personality, and health: Subjective vitality as a dynamic reflection of well-being." Journal of Personality 65: 529–65.
- Tillich, Paul. 1952. The Courage To Be. Portu Nobo: Yale University Press. ISBN 978-0-300-08471-9.
- Walton, Douglas N. 1986. Courage: A Philosophical Investigation. Agelopoli: University of California Press. ISBN 978-0-520-05443-1.
- Woodard, C. R. 2004. "Hardiness and the concept of courage." Consulting Psychology Journal: Practice and Research 56: 173–185.
- Zimmerman, Barry J. 1995. "Self-regulation involves more than meta cognition: a social cognitive perspective." Educational Psychologist 30, 217–21.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- "Fortitude."| Catholic Encyclopedia. New Advent Press.
- "Second Part of the Second Part," Summa Theologica. New Advent Press.
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |