Beda Mheshimiwa
Beda maarufu kama Mheshimiwa tangu enzi za uhai wake (Wearmouth-Jarrow, Northumbria, leo nchini Uingereza, 672 au 673 – 25 Mei - Wearmouth-Jarrow, 735) alikuwa mmonaki, padri, mwanateolojia na mwanahistoria nchini Uingereza.
Mtumishi wa Kristo monasterini tangu umri wa miaka minane hadi kifo chake, alitumia maisha yake yote kutafakari na kufafanua Biblia; pamoja na kushika kila siku nidhamu ya kimonaki na kumuimbia Mungu kanisani, alipenda daima kujifunza, kufundisha na kuandika.
Hasa anafahamika kwa kitabu chake “Historia ya kikanisa ya taifa la Waingereza” (kwa Kilatini: Historia ecclesiastica gentis Anglorum). Akiona Kanisa lilivyozidi kustawi kati ya mataifa mapya, alipenda kuonyesha lisivyobanwa na ustaarabu mmoja, bali linakumbatia kila aina ya utamaduni ili kuikamilisha katika Kristo.
Beda alichangia kwa kiasi kikubwa uenezaji wa hesabu ya miaka baada ya Kristo kuzaliwa.
Mwaka 1899 alitangazwa na Papa Leo XIII kuwa mtakatifu na mwalimu wa Kanisa.
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Mei[1].
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Vyanzo
[hariri | hariri chanzo]Karibu yale yote tunayoyajua kuhusu maisha ya Beda yamo katika sura ya mwisho ya Historia Ecclesiastica, aliyoimaliza mwaka 731 hivi, ambapo anadokeza kuwa yuko katika mwaka wa 59 wa maisha yake, hivyo alizaliwa 672–673.
Habari nyingine tunazipata katika barua ya mwanafunzi wake Cuthbert kuhusu kifo chake.
Asili na wito
[hariri | hariri chanzo]Beda hasemi kitu kuhusu asili yake, lakini kuna dalili kuwa familia yake ilikuwa na hali nzuri katika jamii.
Kumbe anataja mahali alipozaliwa kama "maeneo ya monasteri hii", yaani monasteri pacha ya Wearmouth na Jarrow, Northumbria, leo Uingereza Kaskazini Mashariki.
Abati wake wa kwanza alikuwa Benedikto Biscop.
Alipofikia umri wa miaka 7, alitumwa monasterini ili apate malezi kutoka kwa abati huyo, halafu kwa Ceolfrith. Beda haelezi kama lengo la awali lilikuwa awe mmonaki baadaye. Lakini ndivyo ilivyotokea, akatumia maisha yake yote huko “kuimbia sifa za Mungu, kusoma, kufundisha na kuandika”, alivyosema mwenyewe.
Mmonaki na padri
[hariri | hariri chanzo]Alipofikia miaka 19 tu, (692 hivi), alipewa daraja takatifu ya ushemasi, na alipofikia miaka 30 (702 hivi) alipata upadrisho.
Mtaalamu wa biolojia na historia, lakini hasa teolojia, alifaulu kufanya Biblia ieleweke kwa urahisi kupitia mahubiri yake sahili iliyofuata mfano wa mababu wa Kanisa.
Alipata kuwa kati ya wasomi wakuu wa Karne za Kati za mwanzo, akifaidika na magombo mengi muhimu aliyoletewa na maabati wake kutoka safari zao nyingi za ng’ambo.
Sifa ya ufundishaji na uandishi wake ilisababisha afanye urafiki na watu bora kadhaa wa wakati huo, ambao walimtia moyo kudumu kati kazi hiyo kwa faida ya wengi.
Mwaka 701 hivi aliandika vitabu vyake vya kwanza, De Arte Metrica na De Schematibus et Tropis; vyote viwili kwa ajili ya madarasa.
Aliendelea kuandika maisha yake yote, akimaliza vitabu zaidi ya 60, vingi vikiwepo hadi leo.
Biblia ilikuwa daima chanzo kikuu cha teolojia yake. Baada ya kuchunguza nakala ipi ni sahihi zaidi, aliifafanua Kikristo, akijitahidi kuelewa vizuri maneno yanasema nini, lakini kwa mwanga wa Kristo aliye ufunguo wa Maandiko yote katika umoja wake wa dhati. Kwake matukio ya Agano la Kale na ya Agano Jipya yanakwenda pamoja kuelekeza kwa Kristo.
Mada nyingine aliyoipenda sana ni historia ya Kanisa, kutokana na imani ya kwamba Roho Mtakatifu anazidi kufanya kazi ndani yake. Hivyo alipitia wakati wa Mitume, halafu mababu wa Kanisa na Mitaguso mikuu sita ya kwanza na kulinganisha tarehe za matukio mengi na ujio wa Yesu Kristo, akichangia kufanya wote wakubali kalenda iliyoenea sasa kila mahali, ikihesabu miaka "baada ya Kristo kuzaliwa".
Vilevile alihesabu kitaalamu tarehe sahihi ya Pasaka, iliyo kiini cha mwaka mzima wa liturujia, akihimiza Wakristo wenyeji wa Uingereza na Ireland wakubali wote utaratibu wa Roma kuhusu mambo hayo. Kweli alichangia kuunganisha katika Ukristo mataifa ya Ulaya.
Hotuba zake zilifaulu kuongoza waamini waadhimishe vema mafumbo ya imani na kuyatekeleza maishani, huku wakitarajia ujio wa pili wa Yesu ili kuingizwa naye katika liturujia ya mbinguni.
Akifuata masisitizo ya mababu kama Ambrosi, Augustino na Sirili wa Aleksandria, alifundisha kwamba sakramenti hazimfanyi mtu “awe Mkristo tu, bali Kristo mwenyewe”. Kila anayepokea kwa imani Neno la Mungu kwa mfano wa Bikira Maria anaweza kumzaa Kristo upya. Na Kanisa, kila linapobatiza watu, linakuwa “Mama wa Mungu” kwa kuwazaa kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Alihimiza walei wawe na bidii katika kupata mafundisho ya dini na kuwashirikisha mapema watoto wao. Pia wasali mfululizo kwa kutolea matendo yao yote kama sadaka ya kiroho pamoja na Kristo.
Mwanashairi, aliandika tenzi kwa Bikira Maria ambazo ni kati ya zile bora zaidi zilizowahi kuandikwa.
Mwaka 708 baadhi ya wamonaki wa Abasia ya Hexham walimshtaki kuwa mzushi, lakini alifaulu kujitetea.
Mwaka 733 alisafiri hadi York, Lindisfarne na sehemu nyingine.
Alipougua, hakuacha kazi yake, akidumisha furaha ya dhati iliyojitokeza katika kusali na kuimba.
Alifariki tarehe 26 Mei 735 akazikwa Jarrow lakini masalia yake yakahamishiwa kwenye kanisa kuu la Durham katika karne ya 11.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Bede (1969). Colgrave, Bertram and Mynors, R. A. B. (mhr.). Bede's Ecclesiastical History of the English People. Oxford: Clarendon Press. ISBN 0-19-822202-5.
{{cite book}}
: CS1 maint: multiple names: editors list (link) (Parallel Latin text and English translation with English notes.) - Bede (1991). Ecclesiastical History of the English People. Translated by Leo Sherley-Price, revised R. E. Latham, ed. D. H. Farmer. London: Penguin. ISBN 0-14-044565-X.
- Bede (1994). McClure, Judith and Collins, Roger (mhr.). The Ecclesiastical History of the English People. Oxford: Oxford University Press. ISBN 0-19-283866-0.
{{cite book}}
: CS1 maint: multiple names: editors list (link) - Bede (1943). Jones, C. W. (mhr.). Bedae Opera de Temporibus. Cambridge, MA: Mediaeval Academy of America.
- Bede (2004). Wallis, Faith (trans.) (mhr.). Bede: The Reckoning of Time. Liverpool: Liverpool University Press. ISBN 0-85323-693-3.
- Swanton, Michael James (trans.) (1998). The Anglo-Saxon Chronicle. New York: Routledge. ISBN 0-415-92129-5.
- Abels, Richard (1983). "The Council of Whitby: A Study in Early Anglo-Saxon Politics". Journal of British Studies. 23 (1): 1–25. doi:10.1086/385808.
- Behr, Charlotte (2000). "The Origins of Kingship in Early Medieval Kent". Early Medieval Europe. 9 (1): 25–52. doi:10.1111/1468-0254.00058.
- Blair, Peter Hunter (1990). The World of Bede (tol. la Reprint of 1970). Cambridge: Cambridge University Press. ISBN 0-521-39819-3.
- Brown, George Hardin (1987). Bede, the Venerable. Boston: Twayne. ISBN 0-8057-6940-4.
- Brown, George Hardin (1999). "Royal and Ecclesiastical rivalries in Bede's History". Renascence. 51 (1): 19–33.
- Cannon, John (1997). The Oxford Illustrated History of the British Monarchy. Oxford University Press. ISBN 0-19-822786-8.
{{cite book}}
: Unknown parameter|coauthors=
ignored (|author=
suggested) (help) - Farmer, David Hugh (1978). The Oxford Dictionary of Saints. Oxford, UK: Oxford University Press. ISBN 0-19282-038-9.
- Goffart, Walter A. (1988). The Narrators of Barbarian History (A. D. 550-800): Jordanes, Gregory of Tours, Bede, and Paul the Deacon. Princeton, N.J.: Princeton University Press. ISBN 0-691-05514-9.
- Higham, N. J (2006). (Re-)Reading Bede: The Historia Ecclesiastica in Context. Routledge. ISBN 978-0415353687.
- McCready, William D (1994). Miracles and the Venerable Bede: Studies and Texts. Pontifical Institute of Mediaeval Studies #118. Toronto: Pontifical Institute of Mediaeval Studies. ISBN 0-88844-118-5.
- Mayr-Harting, Henry (1991). The Coming of Christianity to Anglo-Saxon England. University Park, PA: Pennsylvania State University Press. ISBN 0-271-00769-9.
- Meyvaert, Paul (1996). "Bede, Cassiodorus, and the Codex Amiatinus". Speculum. 71 (4): 827–883. doi:10.2307/2865722.
- Opland, Jeff (1980). Anglo-Saxon Oral Poetry: A Study of the Traditions. New Haven and London: Yale U.P. ISBN 0-300-02426-6.
- Thacker, Alan (1998). "Memorializing Gregory the Great: The Origin and Transmission of a Papal Cult in the 7th and early 8th centuries". Early Medieval Europe. 7 (1): 59–84. doi:10.1111/1468-0254.00018.
- Tyler, Damian (2007). "Reluctant Kings and Christian Conversion in Seventh-Century England". History. 92 (306): 144–161. doi:10.1111/j.1468-229X.2007.00389.x.
{{cite journal}}
: Unknown parameter|month=
ignored (help) - Ward, Benedicta (1990). The Venerable Bede. Harrisburg, PA: Morehouse Publishing. ISBN 0-8192-1494-9.
- Wright, J. Robert (2008). A Companion to Bede: A Reader's Commentary on The Ecclesiastical History of the English People. Grand Rapids, MI: Eerdmans. ISBN 978-0-8028-6309-6.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Ecclesiastical History of the English People Ilihifadhiwa 30 Agosti 2009 kwenye Wayback Machine., Books 1-5, L.C. Jane's 1903 Temple Classics translation. From the Internet Medieval Sourcebook.
- Bede's Ecclesiastical History and the Continuation of Bede (pdf), at CCEL, edited & translated by A.M. Sellar.
- Bede's World: the museum of early medieval Northumbria at Jarrow
- The Venerable Bede
- The Venerable Bede from In Our Time (BBC Radio 4)
- Bede the Venerable Ilihifadhiwa 14 Aprili 2011 kwenye Wayback Machine.
- Saint Bede Ilihifadhiwa 18 Aprili 2007 kwenye Wayback Machine. at The Online Library of Liberty
- Bede the Venerable at Find a Grave