Nenda kwa yaliyomo

Mpira wa miguu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Soka)
Mechi ya kandanda ya Angola dhidi ya Moroko mwaka 2013.

Mpira wa miguu (pia soka au kandanda) ni mchezo unaochezwa na jumla ya wachezaji ishirini na wawili katika timu mbili, kila timu ikiwa na wachezaji kumi na mmoja.

Lengo hasa la mchezo huu ni wachezaji kuumiliki mpira kwa kutumia miguu na kufunga goli, yaani kuuingiza mpira katika wavu wa wapinzani mara nyingi zaidi.

Matumizi ya mikono ni marufuku isipokuwa kwa mlinda mlango katika eneo maalumu na wakati wa kurudisha mpira baada ya kutoka nje ya uwanja.

Historia

Mchezaji wa mpira wa miguu, Ugiriki ya Kale.

Michezo mbalimbali ya kuchezea mpira inaweza kupatikana katika kila uwanja wa jiografia na historia. Wachina, Wajapani, Wakorea na Waitalia, wote hao walikuwa wakicheza mpira zamani kabla ya enzi zetu. Wagiriki na Waromania walitumia michezo hiyo kuwaandaa wapiganaji kabla ya vita.

Hata hivyo, ni nchini Uingereza ambapo umbo la soka la kisasa lilianza kulipuka.

Ilianza wakati mashirikisho mawili (Shirikisho la Mpira wa miguu na Mpira wa Ragbi) yalipotawanyika. Shirikisho la kwanza lilibakia Uingereza. Mnamo Oktoba 1963, Vilabu 11 vya London vilituma wawakilishi katika mkutano wa Freemasons ili kujadili na kuweka kanuni zilizokubalika kusimamia mechi zilizochezwa kati yao.

Mkutano huu ulipelekea kuanzisha kwa Shirikisho la Kandanda (Football Association).

Miongoni mwa kanuni zilizowekwa ni zile za kukataa utumiaji wa mikono kushika mpira na kunyang'anyana kwa nguvu. Soka na Ragbi zilifarakana tarehe hiyo.

Miaka minane baada ya kuanzishwa, Shirikisho la Kandanda (FA) lilikuwa na wanachama 50. Shindano la kwanza la kandanda - Kombe la FA - lilianza mwaka huo, likifuatiwa na lile la Ligi ya Ubingwa miaka 17 baadaye.

Wachezaji wawili wa Klabu ya Darwin, John Dove na Fergus Suter walikuwa wa kwanza kulipwa kwa mchezo wao. Kitendo hiki kilikuwa mwanzo wa soka la kulipwa iliyohalalishwa mwaka wa 1885.

Mwamko huu ulipelekea kuanzishwa kwa Mashirikisho ya kitaifa nje ya Uingereza (Great Britain). Baada ya Shirikisho la Kandanda la Uingereza, Mashirikisho yaliyofuatia ni ya Uskoti (1873), Wales (1875) na Eire (1880).

Kutokana na ushawishi mkuu wa Uingereza katika mataifa ya dunia, soka ilisambaa kote duniani.

Mataifa mengine mengi yalianzisha Mashirikisho ya Kandanda kufikia 1904 wakati Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilipoanzishwa. Tangu hapo, kandanda ya kimataifa imekuwa ikikua licha ya vikwazo mbalimbali.

Kufikia 1912, FIFA ilikuwa na uanachama wa mashirikisho 21, idadi iliyoongezeka na kufikia 36 mwaka 1925.

Kufikia 1930 - mwaka ambapo kwa mara ya kwanza kulikuwa na mashindano ya Kombe La Dunia, FIFA ilikuwa na wanachama 41. Idadi hii ilizidi kuongezeka na kufika 51 mnamo 1938 na 76 kufikia 1950.

Baada ya Kongamano la FIFA la mwaka 2000, kulikuwa na wanachama 204 na idadi hii inazidi kukua kila mwaka.

Kanuni

Maagizo ya Kandanda hupitiwa na kufanyiwa mabadiliko kila mwaka (Mwezi Julai) na Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA).[1]

Uwanja

Vipimo vya uwanja wa soka.

Uwanja una umbo la mstatili. Hakuna kipimo kamili, ila kanuni zinasema urefu ni baina ya mita 90 na 120, upana baina ya mita 45 na 90. Kwa michezo ya kimataifa urefu uwe baina ya mita 100 - 110 na upana baina ya mita 64 na 75.

Goli ziko kwenye pande fupi zaidi. Kuna alama ya bendera kwenye kona za uwanja. Mwaka 2008 IFAB ilijaribu kusanifisha vipimo kuwa mita 105 kwa 68, lakini kanuni hii ilisimamishwa baadaye.

Mstari ni mpaka wa uwanja. Wakati mpira uko kwenye mstari hata kwa kiasi kidogo unahesabiwa bado uko ndani ya uwanja. Kwa goli kukubaliwa sharti mpira uwe umepita mstari wa goli kabisa.

Mpangilio wa wachezaji

[2] [3] Kuna wachezaji wa aina tatu: beki, kiungo na washambuliaji au straika na golikipa .

Ni uamuzi wa kocha kuhusu idadi ya wachezaji wa kulinda lango, wa kiungo au wa mbele, ikitegemea mfumo uliotumika. Mfumo wa 4-4-2[4] umekuwa maarufu miongoni mwa timu nyingi. Mfumo huu hujumlisha walinzi wanne pamoja na mlinda lango, wachezaji wanne wa kiungo na wawili wa mbele. mshambuluaji lazima akawa mtu mwenye ujuzi mkubwa na mwenye nguvu za kushambulia

Utunukizi wa Alama

Golikipa akiokoa mpira uliopigwa shuti ndani ya eneo la penati

Katika ligi za kitaifa na kimataifa, alama hutunukiwa kwa timu baada ya mchezo. Timu iliyoshinda hupewa alama tatu huku timu zilizotoka sare hupewa alama moja kila moja.

Ikiwa ni lazima mshindi apatikane, hasa kwenye mechi za fainali, mchezo huwa na muda wa ziada kama timu hizo ziko sare. Iwapo sare hiyo huendelea mchezo huamuliwa kwa mikwaju ya penalty.

Shirikisho la Kandanda Duniani

[5] Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ndilo shirikisho kuu linalosimamia kandanda duniani. Wanachama wake ni mashirikisho ya kandanda ya nchi mbalimbali. Kufikia mwaka wa 2000, lilikuwa na wanachama 204 kutoka pembe zote za dunia. Shirikisho hili huandaa mashindano mbalimbali ya soka kama vile Kombe la Dunia la FIFA na pia huwatunuku wachezaji.

Orodha ya Wachezaji Maarufu Duniani

Orodha ifuatayo inaonyesha baadhi ya wanasoka maarufu duniani, lakini haiashirii usanjari huu kulingana na ubora. Wapo wengine wengi ambao hawajatajwa hapa.[6]

Orodha ya wachezaji duniani waliofunga zaidi ya magoli 500

Mchezaji Magoli Michezo G/M Miaka
1 Ureno Cristiano Ronaldo 838 1184 0.71 2001
2 Argentina Lionel Messi 823 1063 0.77 2003
3 Austria Josef Bican 812 522 1.56 1931-1957
4 Brazil Romario 772 994 0.78 1985-2009
5 Brazil Pelé 767 812 0.94 1956-1977
6 Hungaria Ferenc Puskas 746 754 0.99 1943-1966
7 Ujerumani Gerd Muller 735 793 0.93 1962-1981
8 Uholanzi Abe Lenstra 676 777 0.87 1936-1963
9 Poland Robert Lewandowski 641 913 0.70 2005
10 Uswidi Zlatan Ibrahimovic 579 994 0.58 1999
11 Hungaria Ferenc Deak 576 510 1.13 1940-1957
12 Brazil Tulio Maravilha 575 794 0.72 1988-2019
13 Ujerumani Uwe Seeler 575 592 0.97 1953-1978
14 Zambia Godfrey Chitalu 569 811 0.70 1964-1982
15 Poland Ernst Willimowski 554 474 1.17 1934-1955
16 Ureno Eusebio 552 639 0.86 1957-1980
17 Uskoti Jimmy McGrory 550 547 1.01 1922-1938
18 Ujerumani Franz Binder 546 430 1.27 1930-1949
19 Ureno Fernando Peyroteo 544 354 1.54 1937-1950
20 Mexiko Hugo Sánchez 541 895 0.60 1976-1998
21 Uruguay Luis Suárez 540 896 0.60 2005
22 Ujerumani Fritz Walter 539 572 0.94 1937-1959
23 Hungaria Jozsef Takacs 523 526 0.99 1917-1934
24 Hungaria Gyula Zsengeller 522 641 0.81 1935-1953
25 Brazil Zico 522 788 0.66 1971-1994
26 Argentina Alfredo Di Stefano 514 706 0.73 1945-1966
27 Austria Hans Krankl 514 655 0.78 1970-1989
28 Uswidi Gunnar Nordahl 513 561 0.91 1937-1958
29 Brazil Roberto Dinamita 512 825 0.62 1971-1992
30 Uingereza Jimmy Greaves 511 812 0.63 1957-1971
31 Hungaria Ferenc Bene 508 946 0.54 1961-1979

Mpira wa miguu barani Afrika

Mchezo ulipelekwa Afrika na Waingereza wakati wa ukoloni. Mechi za kwanza zilizorekodiwa mwaka 1862 huko Cape Town na Port Elizabeth[7].

Ilhali ulikuwa mwanzoni mchezo wa kizungu ulienea haraka kati ya vijana Waafrika kupitia shule, jeshi na wafanyakazi wa reli. Kwa mfano kisiwani Unguja walikuwa wafanyakazi Wazungu na Wahindi waliocheza soka pamoja wakitazamiwa na wenyeji, halafu wanafunzi wa shule ya misioni St Andrew's ya UMCA. Khamis Fereji alikumbuka jinsi gani mnamo 1910 soka ilichezewa na watoto na vijana kote Zanzibar mjini wakitumia mipira ya tennis mtaani au mwambanoni wakati wa jioni ilhali wazee walitazama. Vivyi hivyo aliandika Dr. Nmandi Azikiwe katika kumbukumbu ya maisha yake ya kwamba alipokuwa mtoto Calabar (Nigeria) kabla ya Vita Kuu ya Kwanza walicheza mpira kila mahali kwa kutumia maembe, machungwa au mipira ya tennis[8]

Mchezo ukaendelea kupanuka na kuendeshwa na wenyeji katika klabu zilizoundwa wakati miji ilikua na kuwa na wakazi wengi Waafrika[9].

Tangu uhuru soka ilipanuka sana katika nchi huru za Afrika. Baada ya kujiunga na FIFA wawakilishi wa nchi huru za Afrika waliweza kuhakikisha ya kwamba Afrika Kusini ilitengwa kwa sababu ya siasa yake ya apartheid (ubaguzi wa rangi).

Tangu 1970 mpango wa kombe la dunia ulibadilishwa kuhakikisha nafasi kwa kila bara na Afrika ilipewa nafasi 1 ya hakika. 1986 zilikuwa nafasi 2, 1998 nafasi 4 na tangu kombe la 2002 kuna nafasi 5 kwa timu kutoka Afrika. [10]

Kwa Tanzania na nchi nyingi za Afrika kuna uhaba wa wafadhiliː hiyo husababisha timu ambazo hazina uwezo wa kiuchumi kukata tamaa. Tatizo kubwa ni uhamisho wa wachezaji vijana wenye uwezo kuhamia nje ya Afrika. Wakati wa kombe la dunia idadi kubwa wachezaji wa timu za kitaifa kutoka Afrika wanaajiriwa na klabu huko Ulaya; wakati wa kombe la dunia dunia 2010 walikuwa asilimia 80 za wachezaji Waafrika kwenye kombe la dunia waliocheza kwa klabu za Ulaya. Hali hii inashusha uwiano wa soka katika ligi za kitaifa kwa sababu wachezaji bora wako ng'ambo wakipatikana tu kwa mechi za kimataifa wakishiriki katika timu ya kitaifa.[11]

Mpira wa miguu nje ya kanuni za kawaida

Video inaonyesha namna nyingi jinsi gani mpira unachezewa duniani.
Katika mpira wa miguu, madhumuni ya msingi ya mashabiki ni kuhamasisha timu yao wakati wa mechi.

Hali halisi kuna namna nyingi kucheza soka hata pasipo na wachezaji 22 au uwanja kamili. Kila mahali dunaini watu hasa vijana hucheza barabarani au shambani kwa kila idadi ya wachezaji, ilhali fimbo au mawe mawili hudokeza goli. Pasipo na mpira kamili vijana hujitengenezea kifaa kwa karatasi au plastiki iliyoshikwa kwa kamba katika umbo la kufanana na tufe.

Kwa mazingira ya pekee kuna pia mapatano juu ya kanuni maalumu kwa timu ndogo (kwa mfano wachezaji 5/5) au mahali kama mchanga wa mwabaoni (beach soccer), katika ukumbi (indoor soccer) au kwa wachezaji walemavu.

Tanbihi

  1. Kanuni za Soka, www.fifa.com [1] Archived 9 Julai 2014 at the Wayback Machine.
  2. Soccer Formations, www.soccerhelp.com [2]
  3. Formations, www.expertfootball.com [3] Archived 22 Novemba 2012 at the Wayback Machine.
  4. Mfumo wa 4-4-2, www.soccer-training-guide.com [4] Archived 31 Mei 2023 at the Wayback Machine.
  5. Kuhusu FIFA, www.fifa.com [5] Archived 7 Julai 2014 at the Wayback Machine.
  6. Orodha ya Wachezaji Maarufu wa Soka, www.soccer-fans-info.com [6] Archived 25 Septemba 2014 at the Wayback Machine.
  7. C. Clarey, Soccer Returns to Its Roots in Africa New York Times 9-06-2010, iliangaliwa 6-12-2016
  8. Peter Alegi, African Soccerscapes: How a Continent Changed the World’s Game uk. 6. ilitazamiwa kupitia google books tarehe 9-12-2016
  9. .Alegi u. 18
  10. Soccer in Africa, iliangaliwa 9-12-2016
  11. Mahojiano na profesa Peter Alegi, npr.org tar. 9-06-2010, ikiangaliwa tarehe 9-12-2016

Tazama pia

Viungo vya nje