Wagikuyu
Wagikuyu (pia: Wakikuyu) ni kabila kubwa nchini Kenya lenye watu milioni 8.1 au asilimia 17 za Wakenya wote[1]. Wenyewe hujiita Agĩkûyû. Neno Gikuyu linatokana na mti wa mkuyu (kwa Kik: mũkũyũ). Lakabu ya Wakikuyu ni Nyũmba ya Mũmbi, tafsiri yake ikiwa ni: nyumba ya Muumba.
Wao hukaa hasa katika nyanda za juu za Kenya ya Kati katika mazingira ya Nairobi hadi mlima Kenya. Mlima huu katika lugha yao huitwa "Kĩrĩma kĩrĩ Nyaga". Mlima huu wenye umaarufu kwa kuwa na kimo cha juu ni mahali ambapo wazee, walitolea kafara Mungu wao "Ngai".
Historia
[hariri | hariri chanzo]Asili
[hariri | hariri chanzo]Wakikuyu ni Wabantu wa kaskazini mashariki. Wanahusiana na makabila jirani: Wameru, Waembu, Wambeere na Wakamba ambao waliishi karibu na Mlima Kenya. Inaaminika kuwa, pamoja na makabila hayo, Wakikuyu walihama kutoka beseni la mto Kongo na kuweka makazi kadhaa na mwishowe kuishi karibu na Mlima Kenya katika tukio linalojulikana kama uenezi wa Wabantu[2].
Kabla ya mwaka 1880
[hariri | hariri chanzo]Taifa
[hariri | hariri chanzo]Wakikuyu walikuwa waliishi kama watu huru na walitawala eneo waliloishi kati ya Mlima Kenya, Safu za Nyandarua (Kik: Mĩtambũrũko ya Nyandarwa), Vilima vya Ngong' (Kik: Kĩrĩma kĩa Mbirũirũ) na Mlima Ol Donyo Sabuk (Kik: Kĩrĩma kĩa Njahĩ)[3]. Hawakufanya biashara ya watumwa na hawakukuwa na utumwa katika jamii. Hata hivyo, walisimilisha kabila la Dorobo ambao walikuwa wenyeji katika baadhi ya misitu kwa njia ya ndoa za kabila tofauti[4]. Kwa njia hiyo, pamoja na kuchukua milki ya misitu, waliweza kupanua mipaka kufikia na zaidi ya eneo lliokuwa Mkoa wa Kati. Walikuwa wakulima na wafanyabiashara. Walifanya biashara na makabila jirani; Wamasai na Wakamba. Pia, walihusika katika utengenezaji chuma na kamba[4].
Utawala
[hariri | hariri chanzo]Vijana, waume na wake, walitahiriwa. Kikundi cha watahiriwa wa pamoja kiliitwa rika (kik: riika)[5]. Marika kadhaa ya waume yalitengeneza rejimenti. Mviga wa kutahiriwa ulifanywa kwa muda wa miaka 9 na rejimenti na jeshi kuundwa na marika hayo. Kwa miaka minne na nusu au misimu 9, mviga wa kutahiriwa haukufanywa. Rejimenti kadhaa ziliunda kizazi ambacho kingetawala kwa takriban miaka 35. Kizazi cha mwisho kutawala kilikuwa Riika rĩa Mwangi, ambacho kilipatiwa mamlaka na Riika rĩa Maina mwaka 1898 katika sherehe ya kubadilisha mamlaka inayoitwa Ituĩka[6]. Hakuna kizazi kingine kimetawala kwani wakoloni walikatiza mfumo wa kutahiri na kutoa mifumo ya utawala katika jamii ya Wakikuyu[7][5].
Baraza la kitaifa la wazee halikutekeleza mamlaka yoyote ya kisiasa, ila kazi yake kuu ilikuwa kutoa hukumu, kutangaza vita na kuwa ishara ya ummoja wa taifa na utamaduni wake. Mamlaka yalikuwa yamegatuliwa katika koo ndogo (kik: mbarĩ), ambazo ziliongozwa na mwanamme mzee zaidi[7][5].
Jamii
[hariri | hariri chanzo]Wakikuyu waliishi kama koo tisa. Hakukuwa na mipaka kati ya koo ingawa kila ukoo ulijulikana kufanya kazi maalum katika jamii. Kwa kuwa watu wa ukoo mmoja walihusiana kupitia damu, haikuwa inaruhusiwa kuoa ndani ya ukoo. Kulikuwa na koo ambazo hazikuwa na viongozi katika taifa. Hata hivyo, Taifa lote lilitawaliwa na baraza ambalo liliongozwa na kiongozi aliyekuwa akiitwa mũthamaki[4].
Dini
[hariri | hariri chanzo]Wakikuyu walimwamini Mungu mmoja, jina lake Ngai au Mũrungu au Mwene Nyaga (mwenye utakatifu) au Mwathi (Bwana). Kafara, pamoja na maombi, kwa Mungu zilitolewa chini ya mti wa mkuyu au mtini (Kik: Mũgumo). Maombi yalielekezwa Mlima Kenya kwani waliamini kuwa ni mojawapo ya makazi ya Mungu akiwa duniani.
Milima katika dini
[hariri | hariri chanzo]Katika kisasili cha Wakikuyu, Mungu alimwumba binadamu, jina lake Gikuyu. Alimpeleka juu ya Mlima Kenya na kumwonyesha nchi. Alimwambia kuwa nchi yote kati ya milima minne; Milima Nyandarua, Milima Ngong', Mlima Kenya na Mlima Ol Donyo Sabuk, ni yake na vizazi vyake. Pia, alipatiwa maagizo kuwa atakapopata shida yoyote, amwite Mungu kwa kufanya sadaka chini ya mti wa mtini akitazama Mlima Kenya na Mungu angemsaidia[7]. Iliaminika kuwa Mungu alipowatembelea viumbe wake, aliishi katika Milima hiyo minne. Mojawapo ya sababu ya kuwepo na radi, ilikuwa kwamba Mungu alikuwa anahama kati ya makazi yake manne[7].
1889-1963
[hariri | hariri chanzo]Maisha na utamaduni wao vilivurugwa wakati wakoloni walifika wilaya ya kale ya Kabete (leo, Kaunti ya Kiambu)[5]. Kabla ya Wazungu kufika, nabii Mugo wa Kibiru alikuwa ametabiri kuwa "nyoka wa chuma atatoka majini na kufika katika nchi yao na vipepeo weupe". Aliwaambia kuwa wageni watafika katika nchi yao. Ilikuwa jukumu la wenyeji kuwatunza na kuwakaribisha. Wenyeji walifanya hivyo kwa matumaini kuwa reli itaendelea na kuwaacha[7]. Hata hivyo, wakoloni waliwabughudhi wenyeji na kuwakosea hadhi. Kwa sababu ya usaliti huo, Wakikuyu wa kusini, wakiongozwa na Chifu Waiyaki wa Hinga, walikaidi mkataba waliokuwa wameweka na Frederick Lugard wa IBEAC. Ngome ya Frederick ilichomwa na misafara iliyokuwa inaelekea kaskazini kuvamiwa. Wakikuyu walikataa kuwauzia wakoloni bidhaa[7]. Miaka miwili baadaye, Waiyaki wa Hinga alikamatwa na kuuawa.
Utawala wa moja kwa moja ulifanywa wakati IBEAC ilifilisika na serikali ya Uingereza kutengeneza Afrika Mashariki ya Kiingereza. Wakikuyu walifukuzwa kutoka mashamba yao na walowezi kutwaliwa ardhi hiyo iliyokuwa na hali nzuri ya ukulima wa kahawa na majani chai. Waliipinga sera hii na kuwauwa wenyeji wale waliunga mkono na kuwasaidia wakoloni[8]. Baada ya kushindwa kuwakandamiza, wakoloni walitumia polisi na jeshi la wamasai, ambao mara nyingi hawakusikizana na Wakikuyu, kutuliza hali kwa njia ya vita[4][7]. Wakikuyu hawakufanikiwa na hivyo wakaanza kutumia njia ya kisiasa kupinga ukoloni.
Wakikuyu, pamoja na Waafrika kutoka makabila mengine, walitumiwa kama askari wasaidizi (kwa Kiingereza: Carrier Corps) katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kwa kuwa walikuwa wamezoea mandhari ya nchi. Walipata tajriba na wengi wao walijiunga na Muungano wa Wakikuyu Wachanga (kwa Kiingereza: Young Kikuyu Association), kiongozi wao akiwa Harry Thuku mwaka 1921. Muungano huo uliwapa uzalendo na kuwatia moyo kuiasi serikali ya Koloni la Kenya.
Ili kulinda maslahi yao, walowezi waliweka sera ya kukataza wenyeji kukuza kahawa, kutoza ushuru wa boma na kupunguza ukubwa wa ardhi iliyopewa kwa wasiokuwa na ardhi. Sera hizo zilifanya wengi wahamie mijini.
Wanajeshi wakikuyu wa King's African Rifles waliorudi nyumbani kutoka Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939-1945) walikuwa wametiwa motisha kupigania uhuru. Wakati huo, mwaka 1944, Harry Thuku alikuwa ameanzisha chama cha kisiasa cha kitaifa, Kenya Afican Study Union (KASU) ambacho kiliendelea kuwa Kenya African Union (KAU). Eliud Mathu, mwanachama wa KAU, alikuwa Mwafrika wa kwanza katika Baraza la Kutunga Sheria (LegCo). Jomo Kenyatta alifanywa mwenyekiti wa KAU mwaka 1947.
Kufikia mwaka 1952, juhudi za KAU kutaka Waafrika watendewe haki kuhusiana na ardhi, hazikuwa zimefaulu. Kwa hivyo, chini ya uongozi wa Jemedari Dedan Kimathi, waasi wa Mau Mau walianza vita dhidi ya wakoloni Waingereza na wasaidizi wao wenyeji. Dedan Kimathi alikamatwa mwaka 1956, kuashiria kushindwa kwa Mau Mau.
Mwaka 1961, Jomo Kenyatta aliachiliwa huru na kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya mwaka 1964. Tangu mwaka huo, Wakikuyu wametoa marais watatu wa Kenya, ikiwemo Emilio Stanley Mwai Kibaki na Uhuru Muigai Kenyatta.
Utamaduni
[hariri | hariri chanzo]Lugha
[hariri | hariri chanzo]Lugha ya Wakikuyu ni Kikuyu. Ni lugha ya kibantu inayokaribiana na lugha za jamii za Mlima Kenya.
Vyakula
[hariri | hariri chanzo]Vyakula vya Wakikuyu ni kama vile, githeri, mukimo (vyakula vilivyopondwa), mutura (matumbo yaliyojazwa nyama na damu, kisha kuchomwa), uji, njahi, sukumawiki na mchicha.
Wakikuyu mashuhuri
[hariri | hariri chanzo]Tofauti na awali kwa miaka mingi wamejenga makazi kwingineko. Kama makabila mengi nchini, wao wanakabiliwa na tishio la kuacha tamaduni na mila zao. Wagikuyu wanaojulikana zaidi kimataifa ni
- Jomo Kenyatta (Rais wa kwanza wa Kenya)
- Uhuru Kenyatta (Rais wa sasa wa Kenya)
- Wangari Maathai (mwenye Tuzo ya Nobel ya Amani ya mwaka 2004)
- Ngugi wa Thiong'o (mwandishi anayeishi Marekani)
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Kenya Population 2020, ilingaliwa Machi 2020
- ↑ "Wayback Machine" (PDF). 2011-08-13. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2011-08-13. Iliwekwa mnamo 2018-08-01.
- ↑ "Mukurwe wa Nyagathanga – Gikuyu Eden?", Gīkūyū Centre for Cultural Studies (kwa American English), 2011-05-21, iliwekwa mnamo 2018-08-01
- ↑ 4.0 4.1 4.2 4.3 SCORESBY., ROUTLEDGE, W (2016). WITH A PREHISTORIC PEOPLE, THE AKIKUYU OF BRITISH EAST AFRICA : being some account of the method... of life and mode of thought found existent amongst. [S.l.]: FORGOTTEN BOOKS. ISBN 1333670974. OCLC 990964726.
{{cite book}}
: CS1 maint: multiple names: authors list (link) - ↑ 5.0 5.1 5.2 5.3 "Kikuyu | Encyclopedia.com". www.encyclopedia.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2018-08-04.
- ↑ Godfrey,, Muriuki, (1974). A history of the Kikuyu, 1500-1900. Nairobi,: Oxford University Press. ISBN 0195723147. OCLC 1094498.
{{cite book}}
: CS1 maint: extra punctuation (link) CS1 maint: multiple names: authors list (link) - ↑ 7.0 7.1 7.2 7.3 7.4 7.5 7.6 Jomo., Kenyatta, (2015). Facing Mount Kenya : the traditional life of the Gikuyu. Nairobi: Kenway Publications. ISBN 0435902199. OCLC 933580405.
{{cite book}}
: CS1 maint: extra punctuation (link) CS1 maint: multiple names: authors list (link) - ↑ Boyes, John (190-?]). How I became King . . . of the Wa-Kikuyu. University of California Libraries. [Nairobi : W. Boyd & Co.
{{cite book}}
: Check date values in:|date=
(help)
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Kayû ka muingi Kameme FM Listen Live
- Mûûgî nî mûtaare
- Gikuyu Language
- Kikuyu Names
- Kikuyu.com
- Kikuyu origin
Makala hii kuhusu utamaduni wa Kenya bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wagikuyu kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |