Waiyaki wa Hinga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Waiyaki wa Hinga alikuwa mpiganaji na kiongozi wa Wakikuyu (mũthamaki) katika Kabete ya kale[1].

Aliongoza vita dhidi ya Wamasai na harakati dhidi ya wakoloni[2].

Alifariki mwaka 1892, akiwa mikononi mwa wakoloni.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Haijulikani bayana mahali alipotoka au wakati alipozaliwa. Baadhi ya vizazi vyake husema alikuwa wa nasaba ya Wakikuyu ilhali baadhi ya wanahistoria wanaamini alikuwa Mmasai kutoka Ngong aliyekuwa amehama hadi Dagoretti kwa sababu ya maafa asilia[3].

Waiyaki alipewa jina Hinga, maana yake ikiwa mnafiki, kwa sababu hakuwa na uwazi na alikisiwa kuwa jasusi kutoka kwa Wamasai. Wamasai pia hawakumwamini kwa kuwa alikuwa ameongoza vita dhidi yao na kuteka ng'ombe wengi. Jina Waiyaki linaaminika kutokana na neno Koiyaki kutoka Kimaasai[4].

Alikuwa tajiri aliyekuwa ameoa wanawake kumi. Kama kiongozi, alikuwa kabaila mwenye ushawishi mkuu. Makazi yake yalikuwa na vijumba tofauti, vya bibi zake na kimoja cha wageni. Hapo ndipo walipatana na Frederick Lugard tarehe 10 Oktoba 1890[3][2].

Uasi na kifo[hariri | hariri chanzo]

Lugard alikuwa na jukumu la kuhakikisha ushawishi wa Uingereza na usalama wa misafara ya wafanyabiashara katika Afrika ya Mashariki. Kwa sababu hiyo, alikuwa akitengeneza mikataba na makabila tofauti katika ziara ya kwenda Uganda. Kampuni aliyokuwa akiifanyia kazi, IBEAC, ilikuwa ikiasisi ngome njiani[5]. Waiyaki alikubali ngome, ambayo pia ilikuwa kituo cha misafara ya Waingereza, ijengwe katika ardhi aliyoitoa. Lugard alijenga ngome, mahali ambapo Kanisa la P.C.E.A. la Kihumo limejengwa[6][3]. Ili apatiwe shamba, Lugard alifanya mkataba na Waiyaki kwa njia ya uchale. Walikubaliana kwamba Wazungu hawangenyakua ardhi au mali yoyote kutoka kwa Wakikuyu[2].

Mwezi mmoja baada ya Lugard kuendelea na safari yake, askari na wachukuzi walioachwa chini ya usimamizi wa George Wilson walianza kuvamia mashamba ya wenyeji na kuiba mazao ya shamba, mifugo na hata kuwadhulumu wanawake[3][5]. Matukio hayo yaliwakasirisha sana wenyeji. Waiyaki aliongoza shambulizi katika ngome hiyo mwaka 1891. Walipofika katika ngome, walipata kuwa George na wadogo wake walikuwa wametoroka kwa kuwa walikuwa wameonywa kuhusu shambulio hilo. Washambuliaji waliichoma ngome[5][3].

Mwaka 1892, msafara uliokuwa umeongozwa na Erick Smith ulitumwa Kabete. Smith alijenga ngome nyingine ambayo iliitwa Ngome ya Smith (kwa Kiingereza: Fort Smith) bila idhini. Kulikuwa na vuta nikuvute kati ya wageni na wenyeji. Waingereza walikuwa wametumwa kulipiza kisasi kwa kushambulia kijiji cha Riuki, Githunguri. Waiyaki aliwaonya wanakijiji, wakaweza kuondoka pamoja na mifugo yao kabla ya shambulizi kutendwa. Waingereza walichoma vijiji 30 na kuharibu mazao ya mashamba[1]. Waiyaki alipokwenda kulalamikia Waingereza katika Ngome ya Smith, alipatana na W. P. Purkis. Purkis alidai kuwa Waiyaki alikuwa amejaribu kumvamia kwa kutumia kisu na kwa hiyo, Waiyaki akakamatwa[7]. Baada ya kuteswa, alipelekwa katika mahakama ya muda, iliyokuwa kando ya ngome[1]. Mahakama ilimpata kuwa na kosa akahukumiwa kuhamishiwa Pwani.

Haijulikani bayana kilichomfanyikia alipokuwa katika msafara, ila tu hakuweza kuendelea na safari alipofika Kibwezi. Baadhi ya vyanzo husema kuwa msafara ulipofika Kibwezi, Waiyaki hangeweza kuendelea kwa kuwa alikuwa na majeraha mabaya kichwani[7]. Wengine husema kuwa alipigwa risasi. Rekodi rasmi zinaonyesha kuwa aliachwa katika hospitali ya misheni ambapo alifariki akazikwa katika makaburi ya hospitali hiyo[5][1]. Vyanzo vingine husema kuwa alizikwa hai, mwaka 1892[3][7][8].

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 "122 years later, family seeks hero’s burial for Waiyaki wa Hinga". nation.co.ke (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2018-10-17. 
  2. 2.0 2.1 2.2 Jestice, Phyllis G. (2004). Holy People of the World: A Cross-cultural Encyclopedia (kwa Kiingereza). ABC-CLIO. ku. 905–906. ISBN 9781576073551. 
  3. 3.0 3.1 3.2 3.3 3.4 3.5 Standard, The, "How legend was buried alive for resisting takeover", The Standard (kwa Kiingereza), iliwekwa mnamo 2018-10-17 
  4. "PressReader.com - Connecting People Through News". www.pressreader.com. Iliwekwa mnamo 2018-10-17. 
  5. 5.0 5.1 5.2 5.3 "Oldest edifice of colonial era left to rot in Kikuyu". www.businessdailyafrica.com. Iliwekwa mnamo 2018-10-17. 
  6. Wanjohi Mutunga. "How pioneers set the pace" (PDF). The Torch bearer. Iliwekwa mnamo 17 October 2018.  Check date values in: |accessdate= (help)
  7. 7.0 7.1 7.2 History and Government Form 2 (kwa Kiingereza). East African Publishers. uk. 53. ISBN 9789966253330. 
  8. Worger, William H.; Clark, Nancy L.; Alpers, Edward A. (2010). Africa and the West: From colonialism to independence, 1875 to the present (kwa Kiingereza). Oxford University Press. uk. 119. ISBN 9780195373134.