Nenda kwa yaliyomo

Mohandas Karamchand Gandhi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mahatma Ghandi)
Gandhi kama mwanafunzi London
Gandhi na Kasturba mnamo 1902
Wakili Gandhi mwaka 1906 katika Afrika Kusini
Gandhi akitembelea London mwaka 1931
Gandhi akishika chumvi kando ya bahari kwenye maandamano ya chumvi

Mohandas Karamchand Gandhi (kwa Kigujarati: મોહનદાસ કરમચંદ ગાંધી; 2 Oktoba 1869 - 30 Januari 1948), maarufu zaidi kwa jina la Mahatma Gandhi, alikuwa mwanasheria, mwanafalsafa, mwanaharakati wa haki za binadamu na kiongozi wa siasa nchini Uhindi.

Anajulikana hasa kama kiongozi wa harakati za uhuru wa Uhindi aliyepinga na kushinda ukoloni kwa njia ya amani bila ya matumizi wa mabavu au silaha.

Gandhi alizaliwa katika eneo la Gujarat kama mtoto mdogo wa Karamchand Gandhi na mama Putali Bai. Baba yake alikuwa waziri mkuu katika serikali ya maharaja wa nchi lindwa ndogo ya Porbandar wakati ilipokuwa sehemu ya Uhindi wa Kiingereza.

Familia yake ilifuata dini ya Uhindu, madhehebu ya Wavishnu, lakini nyumba ya Gandhi ilitembelewa pia na Waislamu na Wajain.

Mwaka 1883 akiwa na umri wa miaka 13 aliozwa kwa mke wake Kasturba wakazaa watoto 4.

Masomo katika Uingereza

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1888 alisafiri kwenda Uingereza akasoma sheria kwenye chuo kikuu cha London, akapokewa kama wakili kwenye mahakama za juu kuanzia 1891.

Huko Uingereza alisoma mengi juu ya Ukristo, akipendezwa hasa na mahubiri ya Yesu na hotuba ya mlimani, lakini hakuvutwa na nafasi ya pekee Yesu anayopewa katika imani ya Kikristo.

Wakati uleule alianza kusoma vitabu vitakatifu vya Uhindu, hasa Bhagavad Gita iliyoendelea kuwa mwongozo wa kiroho maishani mwake.

Afrika Kusini

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya mtihani alirudi Uhindi akafanya kazi kama wakili mjini Bombay. Mwaka 1893 alitumwa Afrika Kusini kwa kesi moja tu, lakini alibaki huko hadi 1914.

Katika Afrika Kusini Gandhi alijenga falsafa yake, akaanza kujishughulisha na masuala ya siasa na haki za binadamu. Alihamasishwa kufanya hivyo na mang'amuzi ya ubaguzi wa rangi.

Gandhi alisimulia katika kitabu juu ya maisha yake ya kwamba siku chache baada ya kufika Afrika Kusini alisafiri kwa treni akishika tiketi ya daraja la kwanza. Abiria Wazungu walilalamika juu yake akaambiwa ahamie kwenye behewa la mizigo. Gandhi alikataa akaondolewa na polisi akabaki kituoni.

Baadaye alipata mang'amuzi mengine alipofukuzwa katika basi kwa sababu Mzungu aliyeingia alidai kiti kilichokaliwa na Gandhi.

Hivyo Gandhi alifungua ofisi katika Afrika Kusini mjini Durban kwenye jimbo la Natal akaanza kupigania haki za Wahindi katika Afrika Kusini waliobaguliwa kwa sheria za nchi. Wakati ule Wahindi walikuwa raia wa Milki ya Kiingereza wenye haki zote wakifika Uingereza yenyewe, lakini katika Afrika Kusini iliyokuwa pia sehemu ya milki ya Kiingereza walibaguliwa kutokana na rangi ya ngozi yao.

Mwaka 1894 aliunda chama cha Natal Indian Congress akifuata mfano wa Indian National Congress huko Uhindi. Chama hicho kilidai haki sawa kwa Wahindi katika Afrika Kusini.

Wakati wa Vita ya pili ya Waingereza dhidi ya Makaburu (1899) na vita dhidi ya Wazulu (1906) aliunda kikosi cha usaidizi kwa Waingereza waliokusanya majeruhi na kuwatunza kwenye hospitali.

Mwaka 1906 serikali ya jimbo la Transvaal ilianzisha sheria iliyodai Wahindi kujiandikisha na kubeba vitambulisho. Gandhi alipinga sheria hiyo akaongoza maandamano na mikutano ya kuchoma vitambulisho. Alihimiza wafuasi wake kukubali kupigwa na kuadhibiwa bila ya kutumia mabavu wenyewe.

Katika miaka iliyofuata Wahindi kwa maelfu walipigwa na polisi, walikamatwa na kufungwa jela pamoja na Gandhi mwenyewe.

Baada ya miaka saba watu wengi walisikitikia matumizi ya nguvu dhidi ya Wahindi walioandamana kwa utulivu, hata serikali ilipaswa kupunguza ukali wa sheria.

Falsafa ya Satyagraha

[hariri | hariri chanzo]

Katika miaka híyo Gandhi alijenga falsafa yake ya upinzani bila ya silaha wala mabavu aliyoitumia baadaye Uhindi.

Imani ya Gandhi iliathiriwa na mafundisho ya Ujain aliyoyajua tangu utoto wake na hasa dai la kutotumia mabavu lakini kufuata njia za amani.

Kiini chake kilikuwa satyagraha inayomaanisha "kusimama upande wa ukweli". Satyagraha kwake ilikuja pamoja na kutokuwa na uhasama na kutotumia nguvu. Alisema "Ukweli haukubali nguvu kwa sababu hakuna mtu mwenye ukweli wote, kwa hiyo hakuna mwenye haki ya kuadhibu wengine."

Dhana nyingine ni "swaraj" inayomaanisha "kujitawala". Gandhi aliona swaraj katika ngazi mbili:

  • swaraj kama kujitawala kwa kila mtu akitawala tamaa zake;
  • swaraj kama haki ya watu kwa pamoja kujiamulia mambo yao na kutotawaliwa kutoka nje (kwa mfano na wakoloni).

Kiongozi Uhindi

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuugua aliondoka Afrika Kusini mwaka 1914 akarudi Uhindi alipopokewa kama shujaa kwa sababu habari zake zilimtangulia.

Aliunda makazi ya pamoja (ashram) alimoishi na watu waliofuata imani yake ya satyagraha. Alianza kuvaa nguo za wakulima wa kawaida.

Mwaka 1920 alikuwa kiongozi wa Indian National Congress akaanzisha kampeni ya kitaifa dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza. Alihimiza Wahindi wengi kutotii sheria za serikali ya Kiingereza bila kutumia nguvu.

Mfano mmoja ni maandamano ya chumvi mwaka 1930. Sheria ya Kiingereza iliweka biashara yote ya chumvi mikononi mwa serikali. Kutengeneza chumvi na kuiuza ilikuwa haki ya serikali iliyokabidhi haki hii kwa kampuni zilizolipa kodi za pekee. Gandhi aliongoza watu kwa maelfu hadi baharini walipochota maji ya bahari wakaichemsha na kupata chumvi kidogo kwa njia hiyo. Kiasi cha chumvi kilikuwa kidogo mno, lakini kwa kufanya hivyo walivunja sheria kwa makusudi. Waingereza walianza kuwakamata wapikachumvi, lakini walishindwa na idadi kubwa ya watu waliokubali kukamatwa. Tena ilikuwa vigumu kuwahamasisha askari walioona kosa lilikuwa dogo sana na wakosaji hawakuwa na hatari yoyote kwao.

Gandhi mwenyewe alikamatwa mara kadhaa akakaa jela jumla ya miaka 8.

Mwishowe watu wengi huko Uingereza walichoka habari za Uhindi na mwisho wa vita kuu ya pili ya dunia serikali mpya ya chama cha Labour iliamua kuipa Uhindi uhuru wake.

Kipindi cha uhuru na ugawaji wa Uhindi

[hariri | hariri chanzo]

Ndani ya Uhindi yenyewe fitina ilianza juu ya nafasi ya Waislamu katika taifa jipya, huku sehemu kubwa ya Waislamu wakidai kugawiwa kwa koloni katika nchi mbili.

Mapigano yalianza na watu elfu kadhaa waliuawa. Mnamo Agosti 1947 nchi mbili za Uhindi na Pakistan zilianzishwa, na Oktoba 1947 vita vikafuata kati ya nchi hizo mbili juu ya jimbo la Kashmir. Vita vikaongeza uadui, na watu milioni kadhaa walifukuzwa yaani Wahindu kutoka Pakistan na Waislamu kutoka Uhindi.

Gandhi alijitahidi kupatanisha viongozi wa pande zote akafunga chakula akitangaza alikuwa tayari kufunga hadi kifo wasipopatana. Heshima kwa Gandhi ilisababisha viongozi wa pande mbalimbali katika Uhindi kukutana na kutafuta njia za kumaliza uhasama.

Tarehe 30 Januari 1948 Gandhi alipigwa risasi na hivyo kuuawa akitembea katika bustani ya nyumba huko Delhi. Mwuaji wake alikuwa Mhindu wa kundi lililofuata itikadi kali. Huyu kijana alikasirishwa na hatua za kupatanisha Waislamu na Wahindu akaamini Gandhi alikuwa msaliti wa Uhindu.

Gandhi alijulikana hasa kwa jina la Mahatma. Neno hili la Kisanskrit lamaanisha "roho kubwa". Aliitwa hivyo mara ya kwanza alipofika Bombay wakati wa kurudi kutoka Afrika Kusini. Gandhi hakupenda jina hilo lakini alishindwa kuzuia matumizi yake.