Maharaja

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Maharaja (Kisanskrit महाराज mahārāja, mtawala mkubwa, mfalme mkubwa) ni cheo cha kihistoria kwa mtawala mkabaila nchini Uhindi. Umbo la kike ni maharani ambaye ni ama mke wa maharaja au mtawala wa kike. Cheo hiki kilitumiwa pia katika madola yaliyoathiriwa na Uhindi katika nchi za Indonesia, Malaysia na Ufilipino za leo.

Wakati wa utawala wa Kiingereza juu ya Uhindi kulikuwa na madola 600 yaliyokuwa na hali ya nchi lindwa ndani ya Uhindi wa Kiingereza uliojumlisha nchi za Uhindi, Pakistan na Bangladesh za leo. Madola haya yalisimamiwa na watawala ya Kihindi na wengi wao walikuwa na cheo cha maharaja, wengine waliitwa raja, sultani na mengine.

Waingereza walitawala theluthi mbili za eneo la Uhindi wa Kiingereza moja kwa moja na theluthi moja ilikuwa sehemu ya madola haya 600. Kila maharaja au mtawala alikuwa na mshauri mkazi Mwingereza aliyekuwa na uwezo wa kusimamisha maazimio ya serikali ya dola au kumshawishi mtawala kuitikia mapendzi ya serikali kuu.

Hali halisi cheo cha "maharaja" hakikulingana mara nyingi na uwezo halisi wa watawala kwa sababu wengi wao walikuwa na maeneo madogo lakini Waingereza walikubali kuwapa vyeo vikubwa badala ya madaraka halisi.

Kati ya maharaja waliotawala maeneo makubwa walikuwa wale wa Mysore na wa Jammu na Kashmir. Mtawala wa dola kubwa kabisa la kujitawala hakutumia cheo cha maharaja alikuwa Nizam wa Hyderabad.

Wakati wa uhuru wa Uhindi na Pakistan kama jamhuri madola madogo yalifutwa na cheo cha maharaja kilipigwa marufuku.