Nenda kwa yaliyomo

Historia ya Ukraine

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Ukraine inahusu eneo la Ulaya ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Ukraine (au Ukraina).

Historia ya kale

[hariri | hariri chanzo]
Dola la Kiev, chanzo cha Urusi.

Ukraine ulianza polepole pamoja na Urusi huko makabila ya wasemaji wa Kislavoni cha Mashariki walikoanza kujenga maeneo yao kuanzia karne ya 8 BK.

Waviking waliunda dola la kwanza katika eneo la Kiev, wakalitawala kama dola la Kislavoni. Wenyewe waliingia haraka katika lugha na utamaduni wa wenyeji, lakini waliacha jina lao kwa sababu "Rus" kiasili ilikuwa jina la Waskandinavia wale kutoka Uswidi ya leo.

Mwaka 988 Kiev ilipokea Ukristo wa Kiorthodoksi kutoka Bizanti. Tukio hilo liliathiri moja kwa moja utamaduni na historia yote iliyofuata.

Dola la Kiev liliporomoka kutokana na mashambulio ya Wamongolia baada ya Jingis Khan, na maeneo madogo zaidi yalijitokeza yaliyopaswa kukubali ubwana wa Wamongolia.

Upanuzi wa utemi wa Moscow

[hariri | hariri chanzo]
Utemi wa Moscow 1390 - 1525

Katika karne ya 14 sehemu kubwa ya maeneo ya Milki ya Kiev ya awali ilifikishwa chini ya utawala wa Polandi na Lithuania. Tawi moja la familia ya watawala wa Kiev lilidhibiti Moscow katika mashariki-kaskazini. Hapa viongozi wake walifaulu kuimarisha utawala na kupanua eneo lake. Hata askofu mkuu wa Kiev, aliyepaswa kuondoka baada ya kuchomwa kwa mji wake, hatimaye alihamia Moscow. Hivyo watawala wa utemi wa Moscow walijitazama kama wafuasi halali wa Dola la Kiev wakaendelea kutumia jina "Rus" lililoendelea kuwa chumbukizo la jina Urusi. Hatimaye watemi wa Moscow walifaulu kushinda pia Wamongolia na kupata uhuru.

kutoka katikati ya karne ya 15 hadi katikati ya karne ya 18, ardhi ya kati na kaskazini mwa Ukraine ilidhibitiwa na Cossacks ya Kiukreni, kiongozi wao wa kwanza alikuwa Ostafy Dashkevich (mkuu wa jiji la Cherkasy) na wa mwisho alikuwa Petro Kalnyshevskyi.

Maeneo makubwa ya Ukraine ya leo yalikuwa chini ya utawala wa Lithuania na Polandi na baadaye ya Ufalme wa Maungano ya Poland-Lithuania. Mwaka 1696 watawala wa Polandi walishawishi sehemu ya maaskofu Waorthodoksi kukubali maungano na kanisa katoliki na hii ilikuwa chanzo cha kutokea kwa Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraina.

ardhi zilizodhibitiwa na Cossacks za Kiukreni wakati wa Khmelnytskyi

Kuanzia 1648 hadi 1657, vita vya ukombozi vilipiganwa nchini Ukraine chini ya uongozi wa Bohdan Khmelnytsky dhidi ya Poland, alijaribu kuunda serikali huru kwa Waukraine, lakini kwa sababu ya usawa wa nguvu, alilazimika kuhitimisha muungano na Moscow. Ukraine ilipokea haki za taasisi inayojitegemea, lakini serikali ya Urusi ilipunguza polepole uhuru huu, hadi mnamo 1775 Cossacks za Kiukreni ziliharibiwa. Hati zao zote za thamani, ambazo ni ushahidi wa historia ya Ukraine katika karne ya 15-18, zilihifadhiwa kwa muda mrefu katika ngome ya St. Elizaveta (leo mji wa Kropyvnytskyi).

Sehemu ya Ukraine upande wa mashariki wa mto Dnestr ilitawaliwa na Moscow. Katika karne ya 18 Polandi iligawanywa kati ya majirani yake. Ugawaji huo uliongeza sehemu za Ukraine zilizofika chini ya utawala wa Urusi. Ila sehemu ya kusini-magharibi ilikuwa sehemu ya milki ya Austria. Katika maeneo chini ya Urusi Wakatoliki walipaswa kurudi katika Kanisa la Kiorthodoksi. Lakini katika maeneo yaliyochukuliwa na Austria tangu mwaka 1772, serikali iliwapa Wakatoliki Waukraine haki sawa na Kanisa la Kilatini; liliweza kuunda seminari na vyuo; taasisi hizo zikawa chimbuko la kukua kwa lugha ya Kiukraine na utaifa wa Kiukraine.

Miaka mia ya mwisho

[hariri | hariri chanzo]

Miaka 1918 - 1921, baada ya mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na ya kuporomoka kwa Dola la Urusi, nchi ilikuwa na kipindi kifupi cha uhuru na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Miaka 1922 - 1991 Ukraine ilikuwa jamhuri mwanachama wa Umoja wa Kisovyeti. Jamhuri hiyo ilikuwa moja ya nchi wanachama walioanzisha Umoja wa Mataifa.[1] Hali halisi haikuwa na madaraka ya pekee kwa sababu ilikuwa chini ya usimamizi wa serikali kuu ya Moscow.

Baada ya kuporomoka kwa Umoja wa Kisovyeti nchi ilijipatia tena uhuru wake kama Jamhuri ya Ukraine, ingawa Russia haikuridhika wala kukubali mipaka.

Mwaka 1991 Urusi na Ukraine ziliutia sahihi mkataba wa urafiki walipoahidiana kuheshimiana kama majirani wema.

Kwa msingi huo, mwaka 1994 Ukraine ilikabidhi Urusi silaha za nyuklia iliyowahi kurithi kutoka jeshi la Kisovyeti na kwenye Mkataba wa Budapest Urusi, Marekani na Uingereza ziliahidi kulinda Ukraine katika mipaka yake dhidi ya mashambulizi yoyote[2].

Hata hivyo, baada ya mwaka 2000 majadiliano ndani ya Ukraine kuhusu kujiunga na umoja wa NATO ilianza kuleta ugumu katika uhusiano na Urusi.

Mwaka 2013 yalitokea maandamano na mapigano kwa sababu rais Viktor Yanukovich aliamua ghafla kukataa mapatano ya kujiunga na Umoja wa Ulaya yaliyokwisha kukubaliwa tayari. Waandamanaji kwa mamia waliuawa na polisi na hatimaye rais alikimbilia Urusi. Hapo bunge liliamua kumwondoa madarakani na kuwa na uchaguzi mpya wa rais.

Katika hali hiyo Urusi ilivamia Krim kwa njia ya kuficha. Wanajeshi wasio na sare walitokea kwenye miji ya Krim wakivamia majengo ya serikali pamoja na bunge la kieneo[3]. Idadi isiyojulikana ya wabunge la jimbo la Krim waliamua tarehe 5 Februari kuondoa serikali ya jimbo wakaitisha kura za wananchi. Tarehe 11 Februari walitangaza uhuru wa Krim, na kura ya wananchi ya tarehe iliyoendeshwa na mamlaka mpya ilitangaza kuwa na kura nyingi za kujiunga na Urusi. Ombi hilo lilikubaliwa na Urusi.

Mnamo Aprili 2014 waandamanaji walivamia majengo ya serikali huko Donetsk wakidai pia kura kuhusu kujitenga na Ukraine. Baada ya kuondolewa na polisi, waandamanaji wenye silaha walitangaza maeneo ya Donetsk na Luhansk kuwa "jamhuri za kujitegemea". Serikali ya Ukraine iliongeza polisi na pia jeshi. Mapigano yalianza ambako jeshi la Urusi lilisaidia waasi, kwanza kwa siri na baadaye waziwazi. Mapigano hayo yalikuwa mwanzo wa Vita ya Donbas iliyoendelea hadi mwaka 2022.

Mwaka 2022 rais wa Urusi alitangaza kwamba yeye haoni Ukraine kama nchi halisi akaamuru jeshi lake kuvamia Ukraine tarehe 24 Februari.

  1. "Activities of the Member States - Ukraine". United Nations. Iliwekwa mnamo 2011-01-17.
  2. https://treaties.un.org/doc/Publication/UNTS/Volume%203007/Part/volume-3007-I-52241.pdf Memorandum on security assurances in connection with Ukraine’s accession to the Treaty on the Non-Proliferation of Nuclear Weapons, Tovuti ya treaties.un.org, iliangaliwa Machi 2022
  3. Gunmen Seize Government Buildings in Crimea, gazeti la New York Times ya 27 Februari 2014
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Ukraine kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.