Historia ya Austria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Austria inahusu eneo la Ulaya ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Austria.

Kwa muda mrefu wa historia yake Austria ilihesabiwa kama sehemu ya Ujerumani. Kwa karne nyingi watawala wake walishika cheo cha Kaisari wa Dola takatifu la Roma lililojumlisha Ujerumani wote.

Austria ilitawala pia sehemu kubwa za Ulaya ya Mashariki. Watawala wa Austria walishika pia vyeo vya kifalme vya nchi za Bohemia na Hungaria.

Wakati wa vita za Napoleoni Kaisari Franz II alilazimishwa kujiuzulu kama Kaisari wa Ujerumani wote mwaka 1806 akabaki na cheo cha Kaisari wa Austria tu. Baada ya Napoleoni Austria ilikuwa nchi muhimu katika shirikisho la Ujerumani.

Mwaka 1866 Austria ilishindwa katika vita dhidi ya Prussia ikatoka katika siasa ya Ujerumani. Baada ya vita hiyo Kaisari Franz-Josef alipaswa kuwakubalia Wahungaria cheo sawa na Wajerumani ndani ya milki yake. Kuanzia hapo milki ilijulikana kama Austria-Hungaria

Hadi Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Austria-Hungaria iliendelea kutawala nchi za Ulaya ya Mashariki pamoja na Ucheki, Slovakia, Slovenia, Kroatia, Bosnia-Herzegovina, na sehemu kubwa ya Poland ya Kusini, pia sehemu zilizopo sasa katika kaskazini mwa Italia.

Mwisho wa vita dola hili lilisambaratishwa. Sehemu zake zote zikawa nchi huru. Nchi ndogo ambayo ilikaliwa na Waaustria Wajerumani ilibaki. Washindi wa vita walizuia Waaustria wasijiunge na Ujerumani, hivyo Jamhuri ya Austria ilianzishwa.

Mwaka 1938 dikteta wa Ujerumani Adolf Hitler (aliyekuwa Mwaustria mwenyewe) alivamia Austria kwa jeshi lake na kuiunganisha na Ujerumani. Wakati ule sehemu kubwa ya Waaustria walikubali.

Baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia Austria ilirudishwa kuwa nchi ya pekee ikabaki hivyo.

Mwaka 1995 Austria ikajiunga na Umoja wa Ulaya.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Austria kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.