Historia ya Monako

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Monako inahusu eneo ambalo siku hizi linaunda Ufalme mdogo wa Monako.

Historia ya Monako imekuwa sawa na historia ya familia ya Grimaldi tangu mwanzo wake.

Akina Grimaldi walikuwa matajiri katika mji wa Genova (Italia) waliopaswa kukimbia nchi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1296 BK. Walinunua cheo cha kitemi pamoja na maeneo madogomadogo ya utawala katika Italia ya Kaskazini hadi Ufaransa Kusini.

Kati ya maeneo hayo yote ni Monako pekee iliyobaki mikononi mwao tangu kuondoa mji mikononi mwa Genova mwaka 1419.

Watemi wa Grimaldi walifaulu kwa siasa yenye busara kupata kibali cha Wafalme wa Ufaransa kuwa eneo la kujitegemea bila mamlaka ya kifalme juu yao. Wakati ule palikuwapo na nchi nyingi ndogo sana za aina hiyo katika Ulaya, hasa Italia na Ujerumani.

Busara ya akina Grimaldi iliwawezesha kutunza uhuru wao katika karne zilizofuata, hasa wakijenga uhusiano mzuri mara na huyu mara na huyu kati ya majirani wakubwa.

Kati ya 1425 hadi 1641 akina Grimaldi waliweka nchi yao chini ya ulinzi wa Hispania wakiwalipa Wahispania pesa kwa kuweka kikosi cha wanajeshi katika boma la Monako. Tendo hilo lilikuwa utetezi dhidi ya wafalme wa Ufaransa ambao wakati mwingine walielekea kumeza nchi ndogo.

Baada ya kuchoka na Wahispania walifanya mapatano na Wafaransa waliolazimisha Hispania kuondoka.

Wakati wa mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789 utawala wa kifalme na kitemi ulifutwa kabisa Ufaransa na serikali ya mapinduzi haikuheshimu tena mapatano ya kukubali uhuru wa eneo la akina Grimaldi.

Lakini baada ya kipindi cha Napoleon Bonaparte, aliyerithi matunda ya mapinduzi, mataifa ya Ulaya kwenye mkutano wa Vienna mwaka 1815 yalipatana kurudisha hali jinsi ilivyowahi kuwa awali. Hivyo Wagrimaldi walirudi Monako wakiendelea kutawala hadi leo.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Monako kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.