Nenda kwa yaliyomo

Historia ya Ubelgiji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Ubelgiji inahusu eneo ambalo siku hizi linaunda Ufalme wa Ubelgiji.

Jina la "Belgii" lilikuwa jina la wakazi wa kale wa kaskazini mwa Gallia, na Gallia Belgica ilikuwa jimbo la Dola la Roma.

Wakati wa Zama za Kati maeneo yake yalikuwa chini ya Dola Takatifu la Kiroma na tangu mwaka 1477 yalitawaliwa na nasaba ya Habsburg. Watawala hao walikuwa Wakatoliki, hivyo walizuia uenezaji wa Matengenezo ya Kiprotestanti.

Hata hivyo mikoa ya kaskazini ilifaulu kwa njia ya vita kujipatia uhuru na kuanzisha Jamhuri ya Nchi za Chini (Uholanzi) tangu mwaka 1648. Mikoa iliyoendelea kuwa Ubelgiji ya baadaye ilibaki chini ya Habsburg hadi Mapinduzi ya Kifaransa na utawala wa Napoleon aliyeiingiza katika Ufaransa.

Baada ya Mkutano wa Vienna wa mwaka 1815 Ubelgiji iliunganishwa pamoja na Uholanzi kuwa sehemu ya Ufalme wa Muungano wa Nchi za Chini na hapo ilikuwa sehemu ya kusini ya ufalme huo. Tofauti na sehemu za kaskazini, zilizokuwa na Waprotestanti wengi, mikoa ya Ubelgiji ilikaliwa na Wakatoliki. Tena, wenyeji wa mikoa ya kusini kabisa waliongea Kifaransa, na pia katika sehemu nyingine, ambako watu waliongea Kiholanzi, lugha ya Kifaransa ilikuwa lugha iliyopendwa na tabaka za juu na wasomi.

Tofauti hizi za kiutamaduni zilichangia hisia ya kubaguliwa kati ya watu wa kusini na katika mapinduzi ya 1830 mikoa ya kusini ilijitenga na Ufalme wa Muungano wa Nchi za Chini na kuanzisha ufalme mpya wa Ubelgiji.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Ubelgiji kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.