Nenda kwa yaliyomo

Surinam

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Suriname)
Republiek Suriname
Jamhuri ya Surinam
Bendera ya Surinam Nembo ya Surinam
Bendera Nembo
Kaulimbiu ya taifa: Kilatini: Justitia - Pietas - Fides
("Haki - Imani - Uaminifu")
Wimbo wa taifa: Opo kondreman
Lokeshen ya Surinam
Mji mkuu Paramaribo
5°50′ N 55°10′ W
Mji mkubwa nchini Paramaribo
Lugha rasmi Kiholanzi
Serikali Demokrasia
Chan Santokhi
Uhuru
Tarehe

25 Novemba 1975
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
163,821 km² (ya 92)
1.10%
Idadi ya watu
 - Julai 2014 kadirio
 - 2012 sensa
 - Msongamano wa watu
 
573,311 (ya 167)
541,638
2.9/km² (ya 231)
Fedha Dollar ya Surinam (SRD)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
ART (UTC-3)
(haifuatwi) (UTC-3)
Intaneti TLD .sr
Kodi ya simu +597

-



Ramani ya Surinam (maeneo yanayodaiwa na Surinam lakini kutawaliwa na majirani yana rangi kijani-nyeupe)

Surinam ni nchi huru upande wa kaskazini wa Amerika Kusini. Zamani za ukoloni ilijulikana kama "Guyana ya Kiholanzi".

Imepakana na Guyana, Guyana ya Kifaransa na Brazil.

Kuna pwani ya bahari ya Atlantiki.

Mji mkuu ni Paramaribo.

Jiografia

[hariri | hariri chanzo]

Surinam ni nchi ndogo ya Amerika Kusini ikiwa na eneo la km² 163,820 pekee.

Mlima wa juu ni Julianatop wenye kimo cha mita 1,280 juu ya UB.

Kwa jumla kuna kanda mbili nchini:

  • kaskazini penye mashamba na idadi kubwa ya wakazi (takriban 20% ya eneo)
  • kusini penye misitu minene na savana lakini wakazi wachache (80% ya eneo)

Hali ya hewa ni ya kitropiki.

Mvua hunyesha mara mbili kila mwaka: mvua kubwa kati ya Aprili hadi Agosti na mvua ndogo kati ya Desemba hadi Februari. Usimbishaji ni kuanzia millimita 1,500 kwa mwaka karibu na pwani hadi millimita 3,000 kusini-mashariki mwa nchi.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Wakazi asilia wa Surinam walikuwa Waindio hasa Waarawak na Wakaribi waliokalia sehemu za pwani na savana.

Waindio, Wahispania na Waingereza

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1498 Kristoforo Kolumbus alipita mwambaoni akifuatwa mwaka 1499 na Amerigo Vespucci. Msafara wa upelelezi sehemu za bara ulifanywa na Wahispania mwaka 1500.

Mwaka 1651 Waingereza walijenga kituo cha kwanza cha kudumu kwenye mdomo wa mto Surinam (karibu na Nieuw Amsterdam wa leo) kilichotekwa na Waholanzi mwaka 1667. Kutokana na mkataba wa amani ya Breda wa mwaka uleule eneo hili lilibadilishwa na eneo la New York (Marekani) ya leo iliyowahi kukaliwa na Waholanzi.

Utawala wa Uholanzi

[hariri | hariri chanzo]
Mtumwa apigwa kwenye shamba la miwa.

Hivyo Surinam ya leo imekuwa koloni la Uholanzi tangu mwaka 1667 kwa jina la "Guyana ya Kiholanzi". Wakati ule ilikuwa pamoja na Guyana ya leo (1815-1966: Guyana ya Kiingereza).

Waholanzi waliendeleza biashara ya mashamba makubwa ya miwa, pamba, kokoa na kahawa wakitumia kazi ya watumwa Waafrika.

Kati ya miaka 1799 hadi 1815 Uholanzi ilivamiwa na Ufaransa na kutawaliwa kama sehemu ya himaya ya Napoleoni. Wakati ule Uingereza ilitwaa makoloni ya Uholanzi na kuyatawala.

Baada ya Mkutano wa Vienna (1815) Surinam ilirudishwa lakini Guyana ya leo ilibaki kama koloni la Guyana ya Kiingereza.

Utumwa na kutokea kwa Wabusinenge

[hariri | hariri chanzo]
Kijiji cha Wabusinenge kwenye mto Surinam mnamo 1955.

Kati ya Waafrika wengi waliolazimishwa kuwafanyia kazi mabwana wa mashamba makubwa wengine walifaulu kutoroka na kukimbia porini. Huko walianzisha makazi yao na kuishi maisha huru. Katika Guyana waliitwa Wabusinenge au "Bosneger" ("Weusi wa porini"). Walianzisha makabila mapya na kuchagua viongozi wao.

Historia yao ilianza baada ya Waingereza kuanzisha mashamba ya kwanza walipotumia kazi ya watumwa. Kuna taarifa ya mwaka 1690 ya kuwa kikosi cha Weusi wa porini walishambulia shamba la Imanuel Machato kwenye mto Cassewijne, kumwua na kuondoka na watumwa wake. Waholanzi na pia Waingereza walijaribu mbinu mbalimbali kuwashinda wale Weusi wa porini walioonekana kuwa tishio kwa utaratibu wa utumwa na uchumi wa kikoloni.

Lakini kuanzia mwaka 1749 Waholanzi walijaribu kupatana na Wabusinenge na mwaka 1760 kukawa na mkataba wa amani wa kwanza ambamo serikali ya kikoloni ilikubali uhuru wa kabila moja la Wabusinenge. Wale waliahidi kutopokea watumwa wapya wakimbizi bali kuwarudisha kwa Waholanzi.

Katika koloni jirani la Kiholanzi la Berbice (leo: Guyana) kulitokea uasi mkubwa wa watumwa dhidi ya mabwana wao kuanzia tarehe 23 Februari 1763. Wazungu wote waliacha mashamba yao na kukimbilia mjini walipoweza kujihami. Watumwa wengi waliondoka na kujificha porini baada ya kufika kwa wanajeshi Waholanzi waliokuja kukandamiza ghasia hiyo.

Mwisho wa utumwa na wafanyakazi kutoka Asia

[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 1 Julai 1863 Uholanzi ulifuta utumwa na watumwa 35,000 walipewa uhuru lakini walipaswa kuendelea kama wafanyakazi kwa muda wa miaka 10.

Baadaye wengi wao hawakutaka tena kufanya kazi mashambani. Hivyo wafanyakazi walitafutwa Uhindi, Uchina na katika koloni la Uhindi ya Mashariki ya Kiholanzi (leo: Indonesia). Ndiyo asili ya sehemu kubwa ya wakazi wa Surinam ya leo.

Mwaka 1954 Surinam pamoja na Antili za Kiholanzi ilipewa madaraka ya kujitawala.

Tangu mwaka 1973 kulikuwa na majadiliano kuhusu uhuru kamili uliopatikana tarehe 25 Novemba 1975. Serikali za kwanza zilikuwa na matatizo ya kisiasa. Wakazi wengi sana -jumla 1/3 ya wananchi- walihamia Uholanzi kwa hofu ya kwamba mambo yatakuwa mabaya.

Udikteta na vita ya wenyewe kwa wenyewe

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya miaka minne ya kwanza kulitokea mapinduzi ya kijeshi tarehe 25 Februari 1980. Serikali ya kijeshi iliongozwa na soli Desi Bouterse.

Awali wananchi wengi na pia serikali ya Uholanzi walikubali watawala wapya. Lakini tangu mwaka 1982 mbinu za mabavu na unyama zilionekana kwa kuuawa kwa wapinzani mbalimbali.

Mwaka 1985 kikundi cha Wabusinenge chini ya Ronnie Brunswijk waliojiita "Jungle Comando" kilianza vita vya msituni dhidi ya serikali. Vita vilipigwa kwa ukatili na unyama miaka miwili hadi shinikizo kutoka nchi za nje -hasa Uholanzi- lililazimisha serikali kukubali uchaguzi huru.

Uchaguzi wa Novemba 1987 ulileta ushindi wa vyama vya upinzani vilivyoanzisha serikali mpya chini ya Ramsewak Shankar. Lakini Bouterse alifanya mapinduzi tena na kumwondoa Shankar madarakani tarehe 24 Desemba 1990.

Hali ya wasiwasi iliendela hadi uchaguzi mpya wa 1991 ulioleta serikali ya Ronald Venetiaan.

Mnamo Agosti 1992 mkataba wa amani ulisainiwa na wapinzani wa "Jungle Comando" na kumaliza kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakazi wa Surinam ni wa asili mbalimbali kutokana na historia ya nchi.

Nyumba za zamani ya Uholanzi mjini Paramaribo.

Wakazi asilia ni wachache sana (3.8%). Wengine wote ni watoto wa wahamiaji waliofika wakati wa ukoloni.

Vikundi vikubwa ni:

Wasurinam wanaoishi Uholanzi ni karibu sawa na idadi ya wanaoishi bado nchini.

Lugha rasmi ni Kiholanzi: inatumika katika ofisi za serikali, bungeni na shuleni na katika lahaja ya Kisurinam ni lugha mama ya 60% ya wananchi, na lugha ya pili kwa 20-30%.

Pamoja na Kiholanzi kuna lugha za Krioli za Kiingereza (Kisranan-Tongo inayotumiwa na sehemu kubwa ya wananchi na nyingine 2 za Wabusinenge), halafu Kihindustani cha Surinam, Kijava, lugha 4 za Waindio na lahaja mbalimbali za Kichina.

Zinatumika pia Kiingereza, Kihispania, Kireno na Kifaransa ingawa si lugha mama za wenyeji.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Nchi na maeneo ya Amerika Kusini

Argentina | Bolivia | Brazil | Chile | Ekuador | Guyana | Guyani ya Kifaransa | Kolombia | Paraguay | Peru | Surinam | Uruguay | Venezuela

Makala hii kuhusu maeneo ya Amerika Kusini bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Surinam kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.