Nenda kwa yaliyomo

Mateso ya Wakristo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mateso ya Wakristo ni ukandamizaji wa kiserikali au wa kijamii kwa Wakristo kwa sababu ya dini yao. Kuna mifano mingi ya kihistoria na ya kisasa ya madhulumu inayoathiri jumuiya hiyo, pamoja na mateso dhidi ya dini nyingine.

Sala ya Mwisho ya Wakristo katika Circus Maximus, mchoro wa mafuta na Jean-Léon Gérôme (1863–1883)

Katika historia ya Kanisa, taarifa kuhusu mateso ya Wakristo zilipatikana tangu karne ya 1. Pale mwanzoni Ukristo ulionekana kama kundi katika Uyahudi lenye mafundisho yasiyokubalika. Hivyo Wakristo wa kwanza walitazamwa kama wakosaji Wayahudi waliovumiliwa mara nyingi (linganisha Mdo 5:34 n.k.) au kuadhibiwa (linganisha Mdo 7, hukumu ya Stefano) kulingana na utaratibu wa jumuiya hiyo. Ndani ya jumuiya za Kiyahudi walitengwa katika miji kadhaa na kuadhibiwa, ingawa kwa jumla walivumiliwa.

Mateso ya kidini yalitokea kwa wingi kwanza katika Dola la Roma tangu mwaka 64 B.K. hadi Hati ya Milano ya mwaka 313 yanajulikana kama mateso ya Wakristo. Katika kipindi hicho kirefu, vilirudia tena na tena vipindi vya mateso vikifuatana na vipindi vya amani. Lakini miaka yote Ukristo ulikuwa dini haramu, hivyo kila mara mateso yaliweza kuanza upya. Katika hali hiyo Wakristo walijenga utaratibu mzuri wa kufundishana na kusaidiana katika matatizo. Halafu wakakazia sana mafundisho ili waumini wasimame imara katika matatizo na dhuluma. Kuanzia katikati ya karne ya 2 ulipangwa ukatekumeni mrefu kwa wanaoomba ubatizo ili wajue la kusadiki na la kufanya. Wakajitahidi kuonyesha kwa maisha na matendo yao kwamba Ukristo ni imani yenye amani na upendo isiyoharibu umma. Waliofanya dhambi kubwa walitengwa na jumuia hadi atakapofanya kitubio cha hadhara na hatimaye kupokewa tena na askofu. Wakaendelea kuombea serikali na watu wote, hasa wakati wa ibada ya ekaristi, ambayo ilitiwa maanani sana na kuzidi kupambwa kwa namna mbalimbali. Kwa ajili hiyo walikutana katika nyumba za watu binafsi, au kwenye "katakombu" yaani mahandaki chini ya ardhi walipotengeneza makaburi yao, yakiwemo ya watakatifu waliofia dini. Walipokutana huko kwa ajili ya ibada, waliimarisha imani yao na utayari wa kuifia kama hao.

Nyakati za kale

[hariri | hariri chanzo]

Mateso ya Wakristo mikononi mwa vyombo vya Dola la Roma yalianza pia katika karne ya 1 yakaendelea hadi mwanzo wa karne ya 4, wakati Kaizari Konstantino alipokubali Ukristo kuwa dini halali.

Dola la Roma

[hariri | hariri chanzo]

Dola la Roma lilikuwa na eneo kubwa sana katika nchi zinazozunguka Mediteranea katika mabara matatu. Mataifa mengi waliishi chini ya utawala wake. Utawala huo ulianza kabla ya Yesu kuzaliwa ukaendelea mpaka karne ya 5 baada ya Kristo upande wa magharibi wa bahari ya Kati na hadi karne ya 15 upande wa mashariki.

Katika utamaduni wa Kibantu hakuna wazo la miungu mingi. Katika mapokeo hayo Mungu ni mmoja, ila kuwasiliana naye ni kwa njia ya mizimu hasa, si moja kwa moja. Kumbe katika sehemu nyingi za dunia utamaduni wa asili ulikuwa na imani ya miungu mingi. Dini hizo zilikuwa kawaida Afrika Kaskazini, Ulaya na sehemu nyingi za Asia kabla ya uenezaji wa Ukristo, hivyo ziliathiri mazingira ya taifa la Israeli hata wakati wa Yesu na wa Kanisa lake. Kati ya miungu mingi iliyoabudiwa kila mmoja aliaminika kuwa na idara yake alipotawala hasa, kama vile hali ya hewa, vita, kifo, uponyaji, mavuno, mifugo, biashara, uzazi n.k. Miungu iliyomaanisha nyota au sayari kama vile Jua, Mwezi na Zohali ilikuwa mapokeo ya Roma. Lugha ya Kiingereza inatunza mpaka leo kumbukumbu ya miungu mingi iliyoabudiwa katika utamaduni wa Ulaya wa Kale kabla ya kuingia kwa Ukristo, maana siku za juma zina majina ya miungu ambayo iliaminiwa kuzisimamia.

Kwa jumla serikali ya Roma iliwaachia watu uhuru waendelee na desturi au mila zao ila tu ilikuwa lazima walipe kodi na kukubali utawala mkuu. Watu wengi sana walikuwa na imani ya miungu mingi. Waliabudu mahekaluni mbele ya sanamu za miungu ile. Walikuwa na imani ya kwamba miungu ni mikubwa na yenye nguvu kuliko watu na inaishi milele. Hata hivyo waliamini miungu kuwa na tabia nyingi zinazofanana na zile za binadamu. Serikali iliona ni muhimu kuabudu miungu yote kwani ingekuwa hatari mungu fulani angesahauliwa hata kusababisha akasirike.

Matendo ya Mitume 17:16-23 inasimulia kwamba Paulo alishangaa kuona sanamu nyingi za miungu kule Athene. Kati ya sanamu hizo aliona madhahabu (altare) yaliyotengwa kwa ajili ya “Mungu asiyejulikana". Kumbe serikali ya Athene iliogopa kumsahau mungu yeyote ikatoa sadaka za tahadhari.

Kwa upande mwingine watu waliamini kwamba hata mtu anaweza kupanda ngazi na kuwa kama mungu akiwa na sifa za kutosha zinazokubalika mbele za miungu yote na hasa mungu mkuu. Ndiyo asili ya kumtangaza mtawala mkuu au Kaisari wa Roma kuwa na sifa za kimungu. Raia walitakiwa kushiriki ibada za kumtolea sadaka mbele ya sanamu zake. Kwa watu wengi waliozoea kuabudu miungu mingi haikuwa vigumu kumwingiza Kaisari kama mungu wa nyongeza katika mawazo yao: kwao ilikuwa kuongeza tu jina moja katika orodha ya miungu iliyoabudiwa. Lakini kwa Wakristo haikuwezekana kushiriki ibada hizo. Imani ya Kikristo hukataa kuwepo kwa miungu mingi, vilevile hukataza kuiabudu. Kwa hiyo walionekana kama maadui wa serikali. Walikamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani waadhibiwe kama waasi watakaosababisha hasira ya miungu juu ya watu wote. Juu yao iliandikwa, “Mto Tiber ukifurika ama Naili unakosa maji, nchi ikifunikwa na giza au inatetemeka, tena njaa, vita au tauni vikitokea, mara moja sauti husikika: ‘Wakristo watupwe kwa samba! Wakristo wauawe’”.

Wakristo waliweza wakahumiwa bila kusikilizwa, lakini ikiwa baraza lilikaa, uamuzi ulijulikana toka mwanzo. Mara nyingi walipelekwa kwenye viwanja vya michezo kama kile cha Nero kilichokuwa palipo leo basilika la Mt. Petro katika mtaa wa Roma unaoitwa Vatikano. Huko waliachwa peke yao bila chochote kupambana na askari wenye silaha au wanyama wakali, huku watazamaji wakishangilia damu inapomwagika. Baadhi ya waandishi Wapagani walieleza juu ya wingi wa Wakristo waliouawa na juu ya ukatili uliotumika dhidi yao. Usiku mmoja Nero mwenyewe alizunguka karibu na ikulu huko mitaa ikiangazwa na watu waliopakwa mafuta na kuwashwa moto wawe kama mienge.

Maonyesho hayo yalikusudiwa kutisha watu waogope kuwa Wakristo. Lakini yakageuka kampeni kwa ajili ya Ukristo, kwa sababu watazamaji walianza kujiuliza: Je, watu hao wana kosa gani? Ni imani gani inayowapa nguvu ya kusimama mbele ya wanyama mwitu na kuuawa badala ya kutoa sadaka mbele ya sanamu? Kwa nini wale wanaokufa hivyo wanajulikana kuwa watu wasioiba wala kusema uongo lakini wengine wenye tabia mbaya hawana matatizo wakitoa sadaka tu mbele ya sanamu? Kumbe damu ya mashahidi ilikuwa mbegu ya kukua kwa Kanisa.

Ni kwamba nje ya suala la kidini Wakristo walikuwa raia wema, lakini waliweza kuchukiwa kwa sababu mbalimbali: walichanganywa na Wayahudi waliochukiwa tayari kwa jinsi walivyojibagua na kudharau wengine wote, waliwazibia riziki waliofaidika na sadaka za Kipagani, walitiwa shaka sana kwa kufanya ibada zao kwa siri n.k.

Wakristo walionekana si watu wa kawaida kwa sababu walikaa mbali na sadaka na ibada za miungu mahekaluni. Katika miaka ya kwanza walivumiliwa kiasi kwa sababu walitazamwa kama kundi la Kiyahudi na Wayahudi walitambuliwa na serikali kuu kama dini halali na kuruhusiwa kutoshiriki katika ibada za miungu. Hata hivyo walitazamwa na wengine kwa mashaka na chuki, sawa na Wayahudi. Mashambulio yaliweza kutokea kutokana na chuki hiyo. Mateso ya aina hiyo yanatajwa katika Waraka wa kwanza wa Petro[1].

Mateso chini ya Nero na Domitiano

[hariri | hariri chanzo]

Mateso ya kwanza mikononi mwa serikali yalitokea mjini Roma chini ya Kaizari Nero (54–68). Nero aliogopa hasira ya watu wa Roma kwa sababu ya moto ulioteketeza sehemu kubwa ya mji ambao wengi waliona ndiye aliyewahi kuusababisha. Hapo alishtaki Wakristo kuwa waanzilishi wa moto huu. Mwanahistoria Mroma Tacitus aliandika:

Kwa hiyo, ili kuondoa uvumi (kuwa yeye mwenyewe alisababisha moto ule) Nero alishtaki kundi lililochukiwa kwa sababu ya machukizo yao, lililoitwa na watu „Wakresto“, na kuwatesa sana. Kristo, ambaye jina hilo lilitokana naye, alipatwa na adhabu kuu wakati wa utawala wa Tiberio mikononi mwa mmoja wa magavana wetu, Pontio Pilato. Imani potovu kabisa iliyodhibitiwa kwa muda huo, ilizuka tena si katika Yudea pekee, penye chanzo cha awali cha uovu huo, lakini hata huko Roma, ambapo mambo yote ya kuchukiza na ya aibu kutoka kila sehemu ya dunia hupata kituo chao na kuwa maarufu.
Kwa hiyo, kwanza walikamatwa wote waliokiri hatia; basi, kwa habari yao, umati mkubwa sana ulitiwa hatiani. Walishtakiwa si kwa sababu ya jinai ya uchomaji tu bali chuki dhidi ya ubinadamu. Kejeli za kila namna ziliongezwa kwenye vifo vyao.
Walifunikwa kwa ngozi za wanyama, wakararuliwa na mbwa hadi kufa, au walipigiliwa misumari kwenye misalaba, au walitupwa motoni na kuchomwa, ili kutumika kama nuru ya usiku, wakati mwanga wa mchana ulikwisha.[2].

Hakuna dalili kwamba mateso hayo yalienea nje ya mji wa Roma.

Katika mapokeo ya Wakristo wa kale inafuata taarifa kuhusu wimbi la madhulumu chini ya Kaizari Domitiano (81-96) linaloakisiwa katika Waraka wa kwanza wa Petro[3]. Katika madhulumu hayo Wakristo hawakutafutwa lakini ilitosha kushtakiwa kama Mkristo. Domisyano alianza kudai ibada za kimungu kwake mwenyewe. Popote katika Dola la Roma watu waliitwa kusimamisha sanamu zake na kumwabudu. Kwa wakazi wengi jambo halikuwa geni sana maana kwao lilikuwa kuongeza tu jina moja katika orodha ya miungu iliyoabudiwa. Lakini kwa Wakristo tendo hilo lilikuwa gumu mno. Imani ya Kikristo hukataa kuwepo kwa miungu mingi, vilevile hukataza kuiabudu.

Basi, Wakristo walikataa kuabudu sanamu za Kaisari. Tendo hilo lilionekana kama kusaliti serikali. Wakuu wa mikoa na majimbo walianza kuwaadhibu. Lakini katika mwendo wa miaka ibada za sanamu za Kaisari zikaongezeka. Matatizo yakakua, vita vikaongezeka, uchumi na biashara vikashuka chini. Thamani ya fedha ikapungua. Watu wengi wakaanza kukata tamaa na kutafuta msaada katika dini mbalimbali. Hivyo mafundisho ya kidini yalizidi. Hapo wazo lilikua la kuwa anayekana kuwepo kwa miungu ni hatari kwa umma. Ni mwasi atakayesababisha hasira ya miungu juu ya watu wote: ni lazima aadhibiwe.

Mateso chini ya makaisari waliofuata

[hariri | hariri chanzo]

Mateso ya aina hiyo yaliendelea chini ya makaisari waliofuata, yakitegemea uhusiano baina ya Wakristo na wananchi katika mazingira yao na pia msimamo wa mahakimu na magavana wa Kiroma katika maeneo mbalimbali. Kwenye maeneo kadhaa Wakristo waliishi bila matatizo, katika maeneo mengine waliona matatizo na madhulumu.

Kwa jumla, kadri idadi ya Wakristo ilivyoongezeka, chuki kati ya wananchi dhidi yao ilikua katika maeneo mengi. Wakristo walitazamiwa kama wakanamungu, kama watu wanaojitenga na jamii na kawaida zote, wenye desturi mbaya na hatari kwa jamii na dola. Uvumi mbalimbali zilisambaa, eti Wakristo wana mikutano ya siri ambako wanalevya, kushiriki katika ngono kati ya wote hata wanachinja watu na kula nyama yao. Makaizari wa kipindi kile walisisitiza mara kadhaa si halali kama Wakristo wanapigwa na kuuawa na umati wa watu bali baada ya kuendesha kesi kwa utaratibu pekee. [4]

Ukali wa mateso ulitegemea siasa ya wakuu wa mikoa ya Kiroma. Wakati mwingine waliweza kujipatia sifa wakitoa taarifa ya kwamba wamekamata Wakristo wengi na kuwahukumu. Wakati mwingine waliona afadhali kuwaacha Wakristo na kutosababisha vurugu katika mkoa. Nje ya suala la kidini Wakristo walikuwa raia wema. Kutoka nyaraka za Plinio Kijana (61 - 113) inaonekana kwamba walihukumiwa wakisisitiza kuwa Wakristo hata kama hakuna kosa lingine; walipewa nafasi ya kukana imani hiyo na kutoa sadaka mbele ya miungu halafu walisamehewa.[5]

Mnamo mwaka 200 gavana wa Afrika Kaskazini alihukumu Wakristo wafe katika uwanja wa michezo waliporaruliwa na wanyama wa pori mbele ya watazamaji maelfu. Mwandishi Mkristo Tertuliani aliandika kuhusu hasira dhidi ya Wakristo katika mji wake Karthago: “Kama mto Tiber unafurika mji, kama Mto Nile haifuniki mashamba kama kawaida, mvua isiponyesha au tetemeko ikitikisika, kama kuna njaa au majanga, mara moja tunasikia kilio: Wakristo mbele ya simba!“[6]

Wakati Roma ilipotawala Wakristo wengi walionyesha uhodari kwa kutokana imani yao na kufa kama mashahidi wa Yesu. Mfano huo ulisababisha Wapagani wengi kuwa Wakristo. Lakini si wote walisimama imara mbele ya vitisho. Wengi wakatoa sadaka mbele ya sanamu wakatubu baadaye na kuomba wasamehewe udhaifu huo. Wengine waliwahonga maafisa wa serikali wakanunua vyeti vilivyothibitisha ya kwamba walitoa sadaka zile ingawa haikuwa kweli.

Mateso chini ya Decius na Valerian
[hariri | hariri chanzo]

Kati ya dhuluma nyingine ambazo zilifuata, kali zaidi ni ile ya kaisari Decius miaka 250-251, halafu ile ya Valeriani mwaka 257.

Ni kwamba mnamo mwaka 249 Decius alifaulu katika uasi dhidi ya kaizari aliyekuwepo. Mwaka 250 , akilenga kuimarisha utawala wake, aliagiza raia wote washiriki katika ibada za kuombea dola na utawala wake. Kushiriki kulithibitishwa kwa hati. Wakristo waliokataa walikamatwa na kufungwa gerezani, wakisisitiza wakapokea hukumu ya mauti. Maaskofu wa Yerusalemu, Antiokia na Roma walikufa gerezani. Wengi walitoa sadaka hizo baada ya kutishwa, wengine walikimbia, walijificha au kuhonga maafisa ili wapate hati ya uthibitisho bila kushiriki hali halisi. Amri ya Decius haikulenga Wakristo[7] lakini ilikuwa pigo kubwa kwao. Idadi ya wahanga haikuwa kubwa sana kwa sababu Decius alikufa mapema vitani.[8]

Valerian aliyemfuata alitazamiwa mwanzoni kirafiki na Wakristo lakini aliendelea kuanzisha mateso upya[9] akilenga kanisa moja kwa moja. Maaskofu na mapadre walitafutwa, majengo ya makanisa na makaburi ya Wakristo kukamatwa. Katika awamu la kwanza adhabu ya maaskofu na makasisi waliokataa sadaka ilikuwa uhamisho kwa gereza ya mbali na kwa njia hiyo kaizari alilenga kutenganisha sharika na viongozi wao. Baada ya mwaka mmoja amri mpya iliagiza adhabu ya mauti kwa hao waliokataa sadaka[10].

Pia hapa ilikuwa kifo cha mapema ya kaizari kwenye mwaka 260 wakati wa vita dhidi ya Uajemi iliyomaliza mateso na mwana wake alibatilisha amri zake.

Mawimbi hayo mawili yalisababisha mafarakano ndani ya sharika za Wakristo; wale waliokataa sadaka lakini hawakuawa bado walitoka gerezani baada ya mateso na kudai kipaumbele juu ya hao waliowahi kujificha, kuhonga maafisa au kutoa sadaka. Kwa jumla maaskofu walisisitiza hao wote wasamehewe wakitubu lakini hata hivyo makundi kadhaa walijitenga na umoja wa Wakristo, maarufu kati yao alikuwa Novatiano wa Roma.

Katika karne ya 3 mateso yalikuwa makali hasa kule Misri. Katika miji mikubwa kama Aleksandria watu wengi walikuwa Wakristo. Machoni pa wakuu wa serikali hali hiyo ilikuwa uasi. Wakaona lazima kuzima uasi huo. Kati ya miaka 302 na 308 B.K. maelfu wakauawa kule Aleksandria. Wakakatwa vichwa na maaskari, wakapelekwa katika kiwanja cha michezo mbele ya wanyama mwitu, wakachomwa moto. Lakini idadi ya Wakristo waliokuwa tayari kufa ilizidi uwezo wa serikali wa kuwaua.

Mateso chini ya Dioklesyano
[hariri | hariri chanzo]

Lakini ni hasa Kaisari Dioklesyano aliyejaribu kwa nguvu zote kuharibu Kanisa na kufuta Ukristo katika mateso ya miaka 303-305. Maelfu waliuawa: walikatwa vichwa na maaskari, walipelekwa katika kiwanja cha michezo kwa wanyamapori, walichomwa moto n.k. Mateso yalikuwa makali hasa kule Misri. Katika miji mikubwa kama Aleksandria watu wengi walikuwa Wakristo. Machoni pa wakuu wa serikali hali hiyo ilikuwa uasi, wakaona lazima kuuzima. Lakini idadi ya Wakristo iliendelea kuongezeka kote katika Dola la Roma na waliokuwa tayari kufa ilizidi uwezo wa serikali wa kuwaua.

Hatimaye mwaka 313 ulileta ukombozi: Kaisari mpya, jina lake Konstantino Mkuu, alitangaza mwisho wa mateso: “Tunataka mtu yeyote anayetamani kufuata dini ya Kikristo aweze kufanya hivyo bila hofu yoyote ya kusumbuka kwa ajili hiyo. Wakristo wawe na uhuru tele kufuata dini yao”.

Lakini mwisho wa dhuluma za serikali haukuwa mwisho wa matatizo yote: badala ya hatari za nje, sasa zilijitokeza zaidi hatari za ndani, hasa mafundisho ya kizushi yaliyogawanya waumini.

Mateso chini ya Juliani Mwasi
[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Konstantino Kanisa lilikua sana. Watu wengi walijiunga na Ukristo. Zamani ilikuwa hatari kuwa Mkristo, kumbe sasa imekuwa faida, hata watu wenye imani haba waliosita zamani wakajiunga na Kanisa. Makaisari wenyewe walikuwa Wakristo, isipokuwa Juliani Mwasi (361-363) aliyejaribu kurudisha Upagani kwa kuwadhulumu tena.

Milki ya Uajemi

[hariri | hariri chanzo]

Katika Milki ya Wasasani, Ukristo ulienea kwa nguvu katika Mesopotamia lakini pia kwenye nyanda za juu za Iran. Katika milki hiyo, dini rasmi ilikuwa Uzoroasta. Uajemi ilikuwa na mashindano na mara kwa mara uhusiano wa kiadui na Dola la Roma. Tangu utawala wa Kaizari Konstantino Ukristo ulianza kuwa muhimu zaidi upande wa Roma na hii ilisababisha hofu upande wa watawala wa Uajemi kuhusu ushirikiano wa raia zao wa Kikristo na adui aliye Mkristo. Kutokana na hofu hiyo mfalme Shapur II alianza kudhulumu Wakristo katika mji mkuu wake. [11]

Umma wa Waislamu

[hariri | hariri chanzo]

Dunia nzima ilishangaa kusikia habari ya kwamba Waarabu kutoka jangwani walifaulu kuwashinda wanajeshi hodari wa Kiroma (636) na wa Kiajemi (642). Lakini Waarabu walikutana na maadui waliokosa nguvu: katika miaka iliyotangulia dola hizo mbili kubwa ziliwahi kupigana vita virefu na vikali. Wananchi wote na wanajeshi wao walichoka. Uchumi ulidhoofika baada ya miaka 20 ya vita. Tena wenyeji wa Misri na Siria walisikitikia utawala wa Kaisari wa Bizanti. Walidai tangu muda mrefu uhuru wa kitaifa lakini wakagandamizwa.

Uislamu ulienea haraka sana kwa nguvu ya kijeshi katika nchi hizo zilizokuwa na Wakristo wengi. Mwanzoni walikuja Waarabu kadhaa tu: walichukua madaraka ya serikali kuu na kujenga makambi ya kijeshi katika kila nchi. Vijana wa Kiarabu walifuata baba zao wakiitikia wito wa dini uliokuja pamoja na nafasi ya kupata maisha nafuu. Mbali ya nguzo tano za Uislamu, walifundishwa kwamba ikiwa watakufa katika vita vitakatifu alifundishwa kwamba ikiwa watakufa vitani watapokewa na Mungu kama mashahidi wa imani na kuingia Paradiso moja kwa moja. Lakini wasipokufa vitani watakuwa matajiri wakitawala nchi mpya na kupokea kodi za wenyeji wasio Waislamu. Imani ya aina hii iliwapa nguvu kweli na iliendelea kuvuta Waarabu wengi kutoka kwao kuhamia Afrika Kaskazini na Asia ya Kati.

Kwa kawaida Wakristo hawakulazimishwa kuacha imani yao. Viongozi wa Waarabu washindi walifanya mikataba na maaskofu wa Kikristo katika maeneo waliyoyateka. Wakristo waliahidiwa ulinzi wa makanisa yao wakiambiwa wanaweza kuendelea na mila na desturi walivyozoea. Lakini hawakuwa na haki zote za uraia. Wasio Waislamu walijiona wanabaguliwa mbele ya Waislamu. Walitozwa kodi kubwa ya pekee. Mahakamani hawakuweza kushuhudia dhidi ya Mwislamu, walilazimishwa kuvaa nguo za pekee tofauti na Waislamu, walikataliwa kupanda farasi, kujenga makanisa mapya, au kutumia kengele makanisani. Waislamu walipata kipaumbele katika mambo yote. Hivyo polepole wenyeji walianza kutumia lugha ya Kiarabu pamoja na kujiunga na Uislamu. Bila shaka wazazi wengine walitumaini kuwasaidia watoto wao wapate maendeleo maishani wakifuata dini ya watawala.

Masharti ya kujiunga na Uislamu ni rahisi. Hakuna mafundisho magumu, mwanzoni inatosha kutamka "shahada" ya Kiislamu ambayo ni fupi sana: As-haddu inna la ilaha ila allah, wa Muhamad rasul ullah. (Nakiri ya kwamba Mungu ndiye mmoja tu, na Mohamad ni mtume wa Mungu). Lakini baadaye haiwezekani kurudi katika Ukristo maana sheria ya Kiislamu inaruhusu Mkristo kugeuka Mwislamu lakini inakataza kwa adhabu ya kifo Mwislamu asitoke katika imani hiyo na kufuata dini nyingine.

Sababu kubwa ya udhaifu wa Wakristo hao ilikuwa mafarakano kati yao, na hasa majaribio ya serikali ya Bizanti kuwalazimisha wote kufuata uongozi wake, wakiitumia na kuitawala dini kama nguzo ya siasa yake. Lakini mambo ya imani hayafai kulazimishwa. Hivyo katika nchi kama Misri Wakristo waliotaka uhuru wa kisiasa walilazimishwa kuwa chini ya Askofu wa Bizanti, wakajisikia wanagandamizwa kidini pia, si kisiasa tu. Baadhi yao waliwapokea Waislamu kwa matumaini ya kuwa watamaliza utawala wa kidikteta wa Bizanti. Jeshi la Bizanti lilishindwa kwa kukosa msaada wa wazawa. Kiongozi Mwislamu aliahidi madhehebu yote yataheshimiwa. Alifanya mkataba na Wakristo waendelee na ibada zao na desturi zao. Ahadi hiyo ilitimizwa kwa namna tofauti. Baada ya muda Wamisri walijikuta wamekuwa watu wa ngazi ya chini. Mabwana wapya walianza kubadilisha utamaduni wa nchi. Aliyejiunga na Uislamu na kujifunza Kiarabu alikubaliwa lakini Wakristo wenyeji waliotunza urithi wao walibaguliwa. Majaribio yote ya kupigania uhuru yaligandamizwa vikali.

Baadaye Waislamu waliteka sehemu iliyobaki ya Afrika Kaskazini kama Tunisia na Algeria. Huko Ukristo ulikuwa dhaifu kutokana na mafarakano mengi ya miaka ya nyuma na dhuluma za kidini. Nguvu zake za ndani zilivunjika wakati wa mateso makali ya Wadonato kwa mikono ya Wakatoliki, yakifuatwa na mateso makali ya Wakatoliki kwa mikono ya Wakristo Waario. Baada ya karne za kulaumiana na kuuana kati ya Wakristo, wengine walikuwa na wasiwasi juu ya ukweli wa mafundisho ya Kanisa. Si ajabu kwamba huko Ukristo ulipotea baada ya karne chache za utawala wa Kiislamu. Pamoja na matatizo yaliyowapata Wakristo chini ya utawala huo, kwa muda mfupi wenyeji wengi wa sehemu hizo walisilimu. Tena katika nchi za jirani (Italia na Hispania) vita vikali vilipigwa kati ya Waarabu walioshambulia na Wakristo waliojitetea; labda hali hiyo iliongeza moyo wa Waislamu kutovumilia uwepo wa Wakristo. Kanisa la Afrika Kaskazini-Magharibi lilikoma baada ya karne chache, tofauti na Misri ambako Wakristo walishika imani yao katika karne zote ingawa kwa matatizo makubwa chini ya serikali ya Kiislamu.

Mara kwa mara upande wa watawala na wakubwa yalijitokeza matendo mabaya, kama makanisa kubomolewa au kugeuzwa misikiti, n.k. Kwa mfano msikiti mkuu wa Dameski (Siria) ulikuwa zamani Kanisa la Mt. Yohane Mbatizaji. Mwanzoni Waarabu waliahidi kuliheshimu, lakini mtawala aliyefuata alitaka jengo kubwa lililopatikana mjini kwa ajili ya ibada yake. Ndivyo ilivyotokea Waturuki walipoteka Konstantinopoli: Kanisa Kuu la Hagia Sofia (Hekima Mtakatifu) liligeuka msikiti.

Vipindi vya kulazimisha vilitokea tena na tena, hasa baada ya mataifa mapya kuwa Waislamu. Waarabu wenyewe walionyesha ustahimilivu zaidi kwa wenye imani nyingine (Wakristo, Wayahudi n.k.). Katika maeneo kama Misri au Siria Kanisa liliweza kuendelea na ibada ya Kikristo ingawa kwa matatizo. Lakini huko Asia makabila na mataifa mapya walipokea Uislamu, mara nyingi kwa njia ya vita. Waturuki, Waajemi na Wamongolia baada ya kuwa Waislamu walikuwa wakali kuliko Waarabu wenyewe. Walilazimisha wote waliokuwa na imani tofauti (Wakristo, Wabuddha au wafuasi wa dini za jadi) wawe Waislamu. Mtawala Mwislamu wa Wamongolia, Tamerlano, aliua Wakristo lukuki na kubomoa makanisa elfu kadhaa alipofanya vita vyake Asia ya Kati. Katika vita hivyo Ukristo wa Asia ya Kati uliharibika kabisa. Maeneo makubwa yalichomwa moto, watu walilazimishwa kwa upanga kuwa Waislamu au kuuawa. Mnamo mwaka 1400 Ukristo wa Asia ulibaki katika Mashariki ya Kati tu (Asia ya Magharibi) pamoja na India Kusini. Kumbe uzito wa Ulaya uliongezeka katika Kanisa kwani ni huko tu lilipoweza kuendelea bila maadui wa nje.

Hasa vipindi vya vita vya msalaba kati ya Wakristo kutoka Ulaya na Waarabu viliongeza uchungu kwa Wakristo waliokuwa chini ya utawala wa Kiarabu. Katika vipindi hivyo Wakristo chini ya Waislamu waliweza kuangaliwa kama wasaliti na kuteswa, makanisa yao kubomolewa n.k.

  1. J. N. D. Kelly (1969), A Commentary on the Epistles of Peter and of Jude, London, A. & C. Black 1969, ISBN 0-7136-1285-1, uk. 10, online hapa
  2. Tacitus, Annales
  3. Die Lage der Christen im römischen Reich nach dem 1. Petrusbrief: Zum Problem einer Domitianischen Verfolgung Author(s): Joachim Molthagen, Source: Historia: Zeitschrift für Alte Geschichte, Bd. 44, H. 4 (4th Qtr., 1995), pp. 422-458, Stable URL: http://www.jstor.org/stable/4436394
  4. Origins to Constantine, ed. by Frances M. Young, Margaret M. Mitchell ; assistant editor K. Scott Bowie. (The Cambridge history of Christianity; v. 1) ISBN 0 521-81239-9, uk 508 ff
  5. https://faculty.georgetown.edu/jod/texts/pliny.html Pliny, Letters 10.96-97, tovuti ya Chuo Kikuu cha Georgetown, iliangaliwa Oktoba 2022
  6. Origins to Constantine, uk 511
  7. Kinyume aliona Eusebi wa Kaisarea kwamba sababu ya amri ya Decius ilikuwa chuki yake dhidi ya mtangulizi wake Kaizari Filipo, lakini wataalamu hawakubali. Ona Eusebius Caesariensis – Historia ecclesiastica - The Church History Of Eusebius, online http://www.ccel.org/ccel/schaff/npnf201.html , ukurasa 590 Mhariri Schaff anaeleza kwamba sababu inayotajwa hapa na Eusebio si sahihi.
  8. Origins to Constantine, uk 513 f.
  9. Eusebio uk. 632 anaeleza badiliko la msimamo wa kaizari ulisababishwa na ushawishi wa "wamagi" wa Misri.
  10. Origins to Constantine, uk. 515
  11. Ona Persian Martyrs katika Encyclopedia Iranica.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mateso ya Wakristo kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.