Plinio Kijana

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Plinio Kijana (kwa jina kamili la Kilatini Gaius Plinius Caecilius Secundus; alizaliwa Gaius Caecilius Cilo, 61 - 113 hivi) alikuwa mwanasheria, mwandishi, na seneta wa Roma ya Kale. Mjomba wake Plinio Mzee, alisaidia kumlea na kumsomesha.

Plinio Kijana aliandika mamia ya barua, ambazo 247 zimesalia hadi leo. Barua zake zina thamani kubwa ya kihistoria. Baadhi zao zilielekezwa kwa watawala kama Kaizari Traiano au watu mashuhuri kama vile mwanahistoria Tacitus.

Utotoni[hariri | hariri chanzo]

Plinio Kijana alizaliwa Novum Comum (leo Como, Italia Kaskazini) mnamo mwaka 61 BK, akiwa mwana wa Lucius Caecilius Cilo na wa mke wake Plinia Marcella, dada wa Plinio Mzee. [1] Alikuwa mjukuu wa seneta na mmiliki wa mashamba makubwa Gaius Caecilius. Alimpenda sana mjomba wake, Plinio Mzee aliyekuwa maarufu sana wakati ule na katika barua moja alieleza jinsi mjomba alivyofanya kazi kwenye Naturalis Historia. [2]

Baba yake alifariki akiwa na umri mdogo. Baada ya kufundishwa nyumbani, Plinio alikwenda Roma kwa masomo zaidi. Huko alifundishwa balagha. Ni wakati huo ambapo Plinio alizidi kuwa karibu na mjomba wake Plinio Mzee. Kwenye mwaka 79 BK, wakati Plinio Mdogo alipokuwa na umri wa miaka 17 au 18, mjomba wake Plinio Mzee alifariki akijaribu kuwaokoa wahathiriwa wa mlipuko wa volkeno Vesuvio. Katika wasia wa Mzee, Plinio Kijana alirithi mali yake na kuasilishwa naye. Hivyo alibadilisha jina lake kutoka Gaius Caecilius Cilo hadi Gaius Plinius Caecilius Secundus. [3]

Ndoa[hariri | hariri chanzo]

Plinio Kijana alioa mara tatu. Mke wa kwanza aliyemwoa alipokuwa mdogo sana (takriban miaka 18), alifariki akiwa na umri wa miaka 37; mke wa pili kwa tarehe isiyojulikana, na mara ya tatu Calpurnia. Kuna barua zinazoonyesha kwamba alimpenda sana mke wake akihuzunika wakati mimba ya mtoto wao iliharibika. [4]

Kifo[hariri | hariri chanzo]

Tarehe ya kifo chake haijulikani; anadhaniwa kufariki ghafla mnamo mwaka 113, kwa kuwa hakuna matukio yoyote yaliyorejelewa katika barua zake baadaye. [5]

Nyaraka zake kuhusu Wakristo[hariri | hariri chanzo]

Kati ya nyaraka zake ziko hasa mbili ambazo zimekuwa maarufu. Moja inahusu mlipuko wa Mlima Vesuvio alioushuhudia, na nyingine ni barua yake kuhusu jinsi ya kuwatendea Wakristo pamoja na jibu la Kaizari Traiano.

Alipokuwa gavana wa jimbo la Kiroma la Bithinia-Ponto (leo katika Uturuki), Plinio alimwandikia barua Kaizari Traian mnamo mwaka 112 na kuomba ushauri jinsi ya kushughulikia Wakristo. Katika barua hiyo ( Epistulae X.96 ), Plinio alieleza kwa kina jinsi alivyoendesha kesi za watu walioshukiwa kuwa Wakristo akaomba mwongozo wa Kaizari jinsi wanavyopaswa kutendewa. [6]

Alieleza kwamba hakuwa na uhakika Wakristo wanapaswa kushtakiwa kuhusu nini, na jinsi wanavyotendewa wakitubu. Kama washtakiwa walipelekwa mbele yake, aliwauliza kama ni Wakristo; wakikubali aliwaambia waache au watakufa; hii alifanya mara tatu na wasipotubu aliwahukumu wafe, isipokuwa kama ni raia Waroma, hapo aliwatuma Roma. Kama walikuwa tayari kutubu aliwaambia watoe sadaka ya ubani na divai kwa sanamu za miungu mbele yake akawaacha. Plinio aliongeza kuwa hana uhakika kuhusu imani yao lakini aliona kiburi cha kukataa maagizo yake kinastahili adhabu.[7]

Plinio hakuwahi kufanya uchunguzi wa kisheria wa Wakristo na hivyo alitafuta maagizo ya Traiano. Barua hizo zimehifadhiwa zikiwa hati za mapema zaidi, nje ya maandiko ya Wakristo wenyewe, zilizorejelea hali yao katika Dola la Roma. [8]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Salway, B. (1994). Journal of Roman Studies 84. ku. 124–145. 
  2. Pliny Letters 3.5.8–12. See English translation (Plinius the Elder (2) Archived 18 Januari 2013 at the Wayback Machine.) and Latin text (C. PLINII CAECILII SECVNDI EPISTVLARVM LIBER TERTIVS).
  3. Radice, Betty (1975). The Letters of the Younger Pliny. Penguin Classics. uk. 13. 
  4. Pliny. Letters. uk. 8.10. 
  5. Hurley, Donna.W (2011). Suetonius The Caesars. Indianapolis/Cambridge: Hackett Publishing Company. ku. x. ISBN 978-1-60384-313-3. 
  6. The Early Christian Church Volume 1 by Philip Carrington (2011) ISBN|0521166411 Cambridge Univ Press p. 429
  7. https://faculty.georgetown.edu/jod/texts/pliny.html Pliny, Letters 10.96-97, tovuti ya Chuo Kikuu cha Georgetown, iliangaliwa Oktoba 2022
  8. St. Croix, G.E.M (Nov 1963). "Why Were the Early Christians Persecuted?". Past & Present 26 (26): 6–38. JSTOR 649902. doi:10.1093/past/26.1.6. 

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]