Yohane wa Dameski

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Mt. Yohane wa Damasko.
Mt. Yohane wa Damasko

Yohane wa Dameski (kwa Kiarabu يوحنا ابن ﺳﺮﺟﻮﻥ Yuḥannā ibn Sarjūn) alikuwa mmonaki, padri na mwanateolojia kutoka Dameski mji mkuu wa Siria (Damasko, 676? - Palestina, 749?).

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1883 Papa Leo XIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Ni msimamizi wa wachoraji.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Desemba.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa Damasko, labda katika familia ya Kiarabu ya Kikristo. Baba yake alikuwa Sarjūn ibn Manṣūr. Babu yake, Manṣūr, alikuwa wa kwanza katika familia kupewa vyeo vikubwa chini ya utawala wa halifa Mu'awiya bin Abi Sufyan na wa waandamizi wake.

Baba yake pia alikuwa mwanasheria, akafuatwa na Yohane ambaye bado kijana alipata kuwa mshauri wa halifa wa Damasko na msimamizi wa mali yake.

Lakini baadaye kidogo akahukumiwa na kukatwa mkono wa kushoto. Hapo alihama mji huo na kujiunga na monasteri ya Mt. Saba, kati ya Bethlehemu na Yerusalemu, ambapo alipewa upadrisho.

Alihubiri na kuandika sana hadi kifo kilipompata akiwa na umri wa miaka 73.

Katika maandishi yake alikusanya mafundisho ya mababu waliomtangulia, yeye akiwa wa mwisho kati yao.

Kitabu chake maarufu zaidi kinaitwa Kuhusu Imani Sahihi. Pia ametuachia tenzi bora kwa ajili ya liturujia.

Alitumia nguvu zake zote hasa kutetea picha takatifu katika Ukristo dhidi ya waliotaka kuziteketeza. Alipewa ushindi na Mtaguso wa pili wa Nisea (787) baada ya kifo chake.

Sala yake[hariri | hariri chanzo]

Wewe, Bwana, ulinitoa katika viuno vya baba yangu; wewe uliniunda tumboni mwa mama yangu; wewe ulinitoa mwangani, mtoto uchi, kwa kuwa sheria za umbile letu zinafuata daima amri zako.

Wewe uliandaa kwa baraka ya Roho Mtakatifu uumbaji wangu na maisha yangu, si kadiri ya matakwa ya mtu wala ya tamaa ya mwili, bali kadiri ya neema yako isiyosemeka.

Uliandaa uzazi wangu kwa matayarisho yanayopita sheria za umbile letu, ulinitoa mwangani kwa kunifanya mwanao, uliniandika kati ya wafuasi wa Kanisa lako takatifu lisilo na doa.

Umenilisha maziwa ya Kiroho, maziwa ya maneno yako ya Kimungu.

Umenitegemeza kwa chakula kizito cha Mwili wa Yesu Kristo, Mungu wetu, Mwanao pekee mtakatifu sana, umenilevya kwa kikombe cha Kimungu cha Damu yake itiayo uzima, aliyoimwaga kwa wokovu wa ulimwengu wote…

Sasa, Bwana, kwa njia ya kuhani wako umeniita nitumikie wanafunzi wako.

Sijui kwa mpango gani umefanya hivi; wewe tu unajua…

Unichunge, Bwana, na uchunge mwenyewe pamoja nami watu wengine, ili moyo wangu usiniinamishe kulia wala kushoto, bali Roho wako mwema unielekeze njia nyofu ili matendo yangu yafuate matakwa yako, na yayafuate kweli mpaka mwisho.

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]