Nenda kwa yaliyomo

Nge (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kundinyota la Nge (pia Akarabu - Scorpius) jinsi linavyoonekana kutoka Tanzania, majina kwa Kiswahili
Ramani ya Nge (pia Akarabu - Scorpius) jinsi linavyoonekana kwa mtazamaji aliye kwenye nusutufe ya kaskazini
Nge - Akarabu jinsi ilivyowazwa na msanii Hall

Nge (pia: Akarabu, Scorpius) ni kundinyota la zodiaki linalojulikana pia kwa jina la kimagharibi Scorpius au Scorpio[1]. Ni moja ya makundinyota yanayotambuliwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia [2]

Kiuhalisia nyota za Nge huwa haziko pamoja kama zionekanavyo kutoka duniani. Kuna umbali mkubwa kati ya nyota na nyota, pia kuna umbali mkubwa kati ya mahali zilipo nyota hizo na duniani bila kujali iwapo kwa mtazamo wetu zaonekana kuwa karibu au mbali. Kwahiyo kundinyota "Nge" linaonyesha eneo la angani jinsi lionekanavyo likiangaliwa kutokea duniani.

Nge ni tafsiri ya Akarabu. Mabaharia Waswahili wamejua nyota hizi kwa muda mrefu kwa ni jina la Akarabu linalotokana na kiarabu عقرب ʿaqrab ambalo linamaanisha "nge". Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa Wagiriki wa Kale waliosema Σκορπιός skorpios. Aidha majina yenye maana hiyo yalitumika pia na mataifa mengine mengi ya kale. Katika mitholojia ya Wagiriki wa Kale, Nge alishindana na mwindaji Orion (Jabari). Katika hadithi hizo Nge alimuua Jabari-Orion, na baadaye Zeus(mungu mkuu wa Wagiriki) aliwapeleka Nge na Jabari angani na kuwapangia majira tofauti ya kuwa huko. Jabari alipangiwa kuwinda majira ya baridi, na yalipofika majira ya kiangazi alikimbia kumpisha Akarabu.

Katika unajimu wa kisasa katika Afrika ya Mashariki jina "Akarabu" limesahauliwa badala yake "Nge" imekuwa jina la kawaida.

Mahali pake

[hariri | hariri chanzo]

Nge iko angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Mizani (Libra) upande wa magharibi na Mshale au Kausi (Sagittarius) upande wa mashariki.

Nyota zilizounda kundinyota la Mizani hapo zamani, leo zinahesabiwa kuwa sehemu ya Nge. Hii inaonekana hadi leo kutokana na majina ya nyota angavu zaidi katika Mizani zinazoitwa Zubani Shimali("Koleo la Kaskazini") na Zubani Junubi("Koleo la Kusini") majina hayo yanamaanisha makoleo ya nge.

Nge ni kundinyota kubwa linaloonekana vema kwenye nusutufe ya kusini mwa dunia kwenye kanda ya njia nyeupe.

Magimba ya angani

[hariri | hariri chanzo]

Nge ina nyota nyingi zinazoonekana kwa macho ya kawaida. Nyota angavu zaidi ni Antara (en:Antares) au Alfa Scorpionis. “Antares” ni jina la kigiriki lenye maana ya “Anti-Ares” yaani mpinzani wa “Ares” aliyekuwa mungu/muungu wa vita. Pia jina la Kigiriki la sayari ya Mirihi lilichaguliwa kwa sababu lina rangi nyekundu sawa na Mirihi (Ares). Antara ni nyotamaradufu zenye mwangaza unaoonekana kwa kubadilikabadilika kati ya mag 0.9 hadi 1.8 ikiwa na umbali wa miakanuru 604. Ni nyotajitu yenye kipenyo mara 700 kuliko jua letu.

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
α 21 Antara (Antares) 0,9 bis 1,8m 604 M1.5 Iab-Ib + B4 Ve
λ 35 Shaula 1,63m 703 B2 IV + B
θ Sargas 1,86m 272 F1 II
ε 26 2,3m 64 K1 III
δ 7 Dschubba 2,29m 402 B0.3 IV
κ 2,41m 464 B1.5 III
β1 8 Acrab 2,56m 530 B1 V
υ 34 Lesath 2,70m 519 B2 IV
τ 23 Alniyat 2,8m ca. 500 B0 V
π 6 2,89m 459 B1 V + B2 V
σ 20 Alniyat 2,9m ca. 600 B1 III + ca. B1 + ca. B7 + B9.5 V
ι1 2,99m 1792 F2 Iae
μ1 3,00m 822 B1.5 V + B6.5 V
G 3,19m 127 K2 III
η 3,32m 72 F3 III-Ivp
μ2 3,56m 517 B2 IV
ζ2 3,62m 151 K4 III
ρ 5 3,87m 409 B2 IV-V
ω1 9 3,93m 424 B1 V
ν 14 Jabbah 4,00m 437 B3 V
  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Scorpius" katika lugha ya Kilatini ni "Scorpionis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Scorpionis, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 360 (online kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]


Makundinyota ya Zodiaki
Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa)

Kaa (Saratani – Cancer )Kondoo (Hamali – Aries )Mapacha (Jauza – Gemini )Mashuke (Nadhifa – Virgo )Mbuzi (Jadi – Capricornus )MizaniLibra )Mshale (Kausi – Sagittarius )Ndoo (Dalu – Aquarius )Nge (Akarabu – Scorpius )Ng'ombe (Tauri – Taurus )Samaki (Hutu – Pisces )Simba (Asadi – Leo )