Mshale (kundinyota)
Kwa habari za sayari (wakati mwingine kwa kosa huitwa pia "Kausi") angalia hapa Neptuni; kwa matumizi mengine ya jina "Sagittarius" angalia hapa Sagittarius
Mshale (pia Kausi, kwa Kilatini/Kiingereza: Sagittarius[1]) ni jina la kundinyota kwenye zodiaki.
Nyota za Mshale huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Mshale" linaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoiona kutoka Duniani.
Jina
Mabaharia Waswahili wamejua nyota hizi kwa muda mrefu kwa jina la "Kausi" linalotokana na neno la Kiarabu Qaws قوس linalomaanisha "upinde". Maana hii ni karibu sawa na jina la Kilatini "Sagittarius" (mpiga upinde). Wataalamu wa kale waliona katika nyota zake picha ya mtu anayekalia juu ya farasi akishika pinde na kulenga mshale.
Jina la "Kaus" limetumiwa pia katika elimuanga ya kimagharibi kutaja nyota kadhaa zilizomo hapa kama vile Kaus Australis, Kaus Medius na Kaus Borealis.
Katika vitabu kadhaa vya shule za msingi nchini Tanzania "Kausi" imetumiwa kwa kosa kutaja sayari ya nane katika Mfumo wa Jua letu yaani Neptuni.
Katika unajimu wa kisasa jina la Kausi limeshasahauliwa na nyota hizi zinajulikana zaidi kwa “Mshale” ambayo inarejelea picha inayotumiwa kama ishara yake.
Kuonekana
Mshale inaonekana pale angani ambako Njia Nyeupe inang'aa zaidi yaani kuelekea kitovu cha majarra yetu.
Mshale ni kati ya makundinyota yaliyojulikana tangu karne nyingi zikitumiwa hasa na mabaharia kutafuta njia baharini wakati wa usiku.
Nyota na magimba ya anga
Katika eneo la Mshale wataalamu wa anga walitambua magimba ya angani kadhaa ya maana. Hizi ni pamoja na
- Alfa Sagittarii ambayo ni chanzo cha mawimbi ya redio; inaaminiwa ya kwamba mawimbi haya ni dalili za kuwepo kwa shimo jeusi kubwa sana linaloitwa "Sagittarius A*"; linatazamiwa kuwa shimi jeusi kuu kwenye kitovu cha galaksi yetu yaani Njia Nyeupe.
- Nebula kadhaa zilizoandikishwa katika orodha ya Messier kama vile Nebula za Wangwa, Bata-Maji, na Buibui Nyekundu.
Jina (Bayer) |
Namba ya Flamsteed |
Jina (UKIA) |
Mwangaza unaoonekana |
Umbali (miaka nuru) |
Aina ya spektra |
---|---|---|---|---|---|
ε | 20 | Kaus Australis | 1,9m | 143 | B9.5 III |
σ | Nunki | 2,05m | 224 | B2.5 V | |
ζ | 38 | Ascella | 2,60m | 89 | A3 IV |
δ | 19 | Kaus Media | 2,72m | ca. 350 | K3 III |
λ | 22 | Kaus Borealis | 2,82m | 78 | K0 IV |
π | 41 | Albaldah | 2,88m | 440 | F2 II/III |
γ | 10 | Alnasl | 2,98m | 96 | K0 III |
η | 3,10m | 149 | M2 III | ||
φ | 27 | 3,17m | 231 | B8.5 III | |
τ | 40 | 3,31m | 120 | K1 / K2III | |
ξ2 | 37 | 3,52m | 372 | G8 / K0II/III | |
ο | 39 | 3,76m | 139 | K0 III | |
μ | 13 | Polis | 3,84m | 3912 | B2 III |
ρ1 | 44 | 3,92m | 122 | F0 III/IV | |
β1 | Arkab Prior | 3,96m | 378 | B9 V | |
α | Rukuba ya Rami (α Sgr) | 3,97m | 170 | B8 V | |
ι | 4,12m | 189 | K0 III | ||
β2 | Arkab Posterior | 4,27m | 139 | F2 III |
Tanbihi
- ↑ Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Sagittarius" katika lugha ya Kilatini ni "Sagittarii" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Sagittarii, nk.
Marejeo
- kuhusu jina: Jan Knappert, The Swahili names of stars, planets and constellations; makala katika jarida la The Indian Ocean Review, Perth, Australia September 1993, uk. 7
Makundinyota ya Zodiaki Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa) |
||
---|---|---|
Kaa (Saratani – Cancer ) • Kondoo (Hamali – Aries ) • Mapacha (Jauza – Gemini ) • Mashuke (Nadhifa – Virgo ) • Mbuzi (Jadi – Capricornus ) • Mizani – Libra ) • Mshale (Kausi – Sagittarius ) • Ndoo (Dalu – Aquarius ) • Nge (Akarabu – Scorpius ) • Ng'ombe (Tauri – Taurus ) • Samaki (Hutu – Pisces ) • Simba (Asadi – Leo ) |