Historia ya Pakistan
Historia ya Pakistan inahusu eneo ambalo leo linaunda jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan.
Historia ya awali
[hariri | hariri chanzo]Binadamu walifika Bara Hindi kutoka Afrika kabla ya miaka 55,000 iliyopita. Uwepo wao wa muda mrefu, kwanza kama wawindaji-wakusanyaji waliozagaa barani, umefanya watu wa eneo hilo wawe na tofauti kubwa kati yao upande wa urithi wa kibiolojia, ambayo inapitwa na Waafrika tu.
Makazi ya kudumu yalianza magharibi, katika beseni la mto Indus, miaka 9,000 iliyopita, hata kuzaa ustaarabu maalumu (Indus Valley Civilisation) katika milenia ya 3 KK.
Kabla ya ukoloni
[hariri | hariri chanzo]Kufikia mwaka 1200 KK, Kisanskrit cha Kale, mojawapo kati ya lugha za Kihindi-Kiulaya, kilikuwa kimeenea India kutoka Kaskazini-Magharibi, kikawa lugha ya Rigveda, mwanzoni mwa dini ya Uhindu. Hivyo lugha za Kidravidi zikakoma kaskazini.
Kufikia mwaka 400 KK, matabaka ya kudumu katika jamii yalikuwa yamejitokeza katika Uhindu. Hapo dini za Ubuddha na Ujaini zilitokea, zikipinga taratibu hizo za kibaguzi.
Kati karne za kwanza baada ya Kristo, dini za Ukristo, Uislamu, Uyahudi na Uzoroastro pia zilitia mizizi katika jamii.
Majeshi kutoka Asia ya Kati yalivamia kwa kwikwi mabonde ya India, hata kuunda usultani wa Delhi na kuingiza India Kaskazini katika umma wa Kiislamu.
Wakati wa ukoloni
[hariri | hariri chanzo]Pakistan ilikuwa sehemu ya Uhindi wa Kiingereza hadi mwaka 1947.
Mwaka 1857 Wahindi walipinga utawala wa Kampuni ya Kiingereza kwa Uhindi wa Mashariki. Matokeo yake utawala ulishikwa na serikali yenyewe ya Uingereza kama koloni (1858).
Mwisho wa karne ya 19 harakati za Wahindi kutafuta uhuru zilianza upya. Mwaka 1885 chama cha INC (Indian National Congress) kiliundwa na Wahindu na Waislamu pamoja waliodai uhuru.
Mwaka 1906 viongozi Waislamu walitoka katika INC na kuunda "Shirikisho la Waislamu".
Mwaka 1917 Uingereza ulitamka ya kwamba ulitaka kuelekea polepole hali ya kujitawala kwa Wahindi. Viongozi wa wenyeji hawakuridhika na mkasi wa mabadiliko. Chini ya uongozi wa Mahatma Ghandi mwendo wa kupigania uhuru bila mabavu ulipata nguvu. Ghandi alipigania hasa umoja wa Wahindu na Waislamu lakini alipingwa na viongozi wenye itikadi kali wa pande zote mbili.
Baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia Waingereza walikubali kujiondoa katika Uhindi. Swali kubwa lilikuwa kama nchi itabaki kama nchi moja au kama maeneo ya Waislamu yatajitenga.
Baada ya uhuru
[hariri | hariri chanzo]Tarehe 14/15 Agosti 1947 utawala wa Uingereza ulikwisha. Bara Hindi iligawanywa katika nchi mbili za Uhindi na Pakistan. Mgawanyo wa Uhindi ulikuja na vita na kumwaga kwa damu nyingi.
Tarehe 30 Januari 1948 Ghandi mwenyewe aliuawa na Mhindu mkali aliyemchukia kwa sababu alitaka usawa wa Waislamu na Wahindu.
Wakati ule ilikuwa nchi moja pamoja na Bangla Desh ya leo, lakini mwaka 1971 hizo pande mbili zilitengana baada ya vita kati yao.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Pakistan kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |