Nenda kwa yaliyomo

Historia ya Timor Mashariki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Timor Mashariki inahusu historia ya eneo ambalo leo linaunda jamhuri ya Timor Mashariki.

Kisiwa cha Timor kilikuwa kituo cha biashara cha Wareno tangu karne ya 16. Visiwa vingine vya Indonesia ya leo vilivamiwa na Waholanzi na Timor ilibaki kisiwa pekee chini ya utawala wa Ureno katika sehemu hii ya dunia.

Katika karne ya 19 Waholanzi walifika pia Timor. Mikataba ya miaka 1859 na 1916 ilithibitisha ugawaji wa kisiwa. Sehemu ya magharibi ilikuwa chini ya Uholanzi (na baadaye sehemu ya Indonesia), lakini sehemu ya mashariki ilibaki koloni la Ureno.

Baada ya mapinduzi ya Ureno ya 1974 Wareno waliondoka Timor bila maandalizi ya kutosha. Viongozi wazalendo walitangaza uhuru. Lakini siku chache baada ya tangazo hilo, jeshi la Indonesia lilivamia nchi ambayo ikatangazwa kuwa jimbo la Indonesia. Hali hiyo haikutambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Vita vikali vya msituni vilifuata kati ya wapigania uhuru na jeshi la Indonesia.

Mabadiliko yalipatikana mwaka 1998 baada ya rais Suharto wa Indonesia kujiuzulu, na rais mpya Bacharuddin Jusuf Habibie kuwa tayari kuipa Timor ya Mashariki hali ya kujitawala ndani ya Indonesia.

Karibu wananchi wote (98 %) walihudhuria katika kura ya maoni ya tarehe 30 Agosti 1999 na zaidi ya robo tatu (78,5 %) walipigia kura uhuru badala ya kuwa jimbo la kujitawala.

Baada ya kura hiyo jeshi la Indonesia lililipiza kisasi kwa kuua watu wengi na kuharibu nyumba, lakini macho ya dunia yalitazama Timor, na serikali ya Indonesia, kwa tishio la kufutiwa mikopo ya benki ya dunia, ililazimishwa kuondoa jeshi lake na kukubali kufika kwa jeshi la Umoja wa Mataifa chini ya uongozi wa Australia.

Tangu tarehe 27 Septemba 2002 Timor Mashariki ni nchi mwanachama wa UM.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Timor Mashariki kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.