Petro Claver

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mt. Pedro Claver, mtume wa Wanegro.

Petro Claver, S.J. (kwa Kihispania: San Pedro Claver Corberó; Verdu, Urgell, Lleida, Catalonia, Hispania, 26 Juni 1581Cartagena, Kolombia, 8 Septemba 1654) alikuwa padri Mjesuiti mmisionari huko Amerika Kusini.

Kutokana na maisha yake aliyoyatoa kwa nadhiri ya kujifanya mtumwa wa watumwa, anaheshimiwa kama mtakatifu msimamizi wa misheni zote za Kanisa Katoliki kwa watu wenye asili ya Afrika.

Katika miaka 40 ya kuhudumia Wanegro wa Kolombia kiroho na kimwili, inakadiriwa aliwabatiza 300,000 hivi.

Papa Pius IX alimtangaza mwenye heri tarehe 16 Julai 1851, na Papa Leo XIII alimfanya mtakatifu tarehe 15 Januari 1888.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 9 Septemba[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Petro Claver alizaliwa mwaka 1581 huko Verdu katika familia tajiri ya wakulima Wakatoliki sana[2], miaka 70 baada ya Mfalme Ferdinando wa Hispania kuanzisha biashara ya watumwa kwa kuruhusu ununuzi wa Waafrika 250 huko Lisbon kwa ajili ya makoloni yake ya Amerika.

Katika karne ya 17 biashara hiyo kutoka Afrika kwenda Amerika ilikuwa kubwa.[3]

Ni katika mazingira hayo kwamba Petro alijisikia kuongozwa na Mungu afanye kazi kwa juhudi zote.

Akiwa mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Barcelona,[2] Petro alijulikana kwa akili na moyo wa ibada.

Baada ya kusomea huko miaka miwili, aliandika hivi katika daftari lake dogo alilolitunza maisha yake yote: "Natakiwa kujitoa nimtumikie Mungu hadi kifo, nikijifananisha na mtumwa."

Baada ya kumaliza masomo yake, Petro alijiunga na Shirika la Yesu huko Tarragona akiwa na umri wa miaka 20. Kisha kumaliza unovisi, alitumwa kusoma falsafa huko Palma, Mallorca.

Akiwa huko alifahamiana na bawabu wa chuo cha shirika, Mt. Alfonso Rodriguez, bradha maarufu kwa utakatifu na kwa karama ya unabii. Rodriguez alijisikia ameambiwa na Mungu kwamba Claver alitakiwa kutumia maisha yake katika makoloni ya Hispania Mpya barani Amerika, akamhimiza mara nyingi kuitikia wito huo.[2]

Claver alijitolea kwenda akatumwa katika ufalme wa Granada Mpya, alipofikia katika bandari ya Cartagena mwaka 1610.[4]

Akitakiwa kusubiri miaka 6 kabla ya kupewa upadrisho wakati wa kusoma teolojia, aliishi katika nyumba za Wajesuiti huko Tunja na Bogotá. Katika miaka hiyo ya maandalizi, aliguswa sana na ukali uliotumika dhidi ya watumwa, pamoja na hali yao ngumu kwa jumla.

Cartagena ilukuwa kituo cha biashara hiyo. Kwa mwaka watu 10,000 walikuwa wanashushwa bandarini kutoka Afrika Magharibi baada ya kusafirishwa melini katika hali ya kutisha, kiasi kwamba inakadiriwa thuluthi moja walikuwa wanakia njiani. Ingawa biashara hiyo iliharamishwa na Papa Paulo III na Urban VIII[3] faida yake kiuchumi ilifanya iendelee kustawi[4]

Mtangulizi wa Claver katika utume wake wa moja kwa moja, padri Alonso de Sandoval, S.J., alimuandaa na kumuongoza hata kwa mfano wake.[4] Sandoval alimuona Claver kuwa mwanafunzi bora. Mwenyewe alikuwa amehudumia watumwa kwa miaka 40 kabla Claver hajafika kumpokea katika kazi hiyo. Sandoval alikuwa amejitahidi kujifunza desturi, ibada na lugha za Waafrika, akafaulu kiasi cha kuweza kuandika kitabu juu ya hayo mwaka 1627 baada ya kurudi Seville.

Petro alipoweka nadhiri za daima katika shirika mwaka 1622, alisaini hivi kwa Kilatini hati ya kujiweka wakfu: Petrus Claver, Aethiopum semper servus (yaani: Petro Claver, mtumwa wa kudumu wa Waafrika).

Kanisa la Mt. Petro Claver huko Cartagena, Colombia, alipoishi na kufanya kazi.

Sandoval alikuwa akitembelea watumwa mahali pa kazi zao, kumbe Claver aliona afadhali kuwasubiri bandarini na kupanda mara melini kuwahudumia walionusurika katika safari, ingawa ilikuwa shida kutembea kati yao kwa jinsi walivyobanana.

Claver alivaa joho alilokuwa tayari kumpa yeyote mwenye shida; baadaye ilisemekana kwamba kila aliyelivaa alipona moja kwa moja maradhi yake.

Baada ya kushushwa ili kupangwa sokoni na kuuzwa baada ya umati wa wanunuzi kuwachunguzachunguza, Claver alikuwa anawapatia dawa, chakula, kileo, limau na tumbaku. Kwa msaada wa wakalimani na picha kubwa aliyoleta, aliwapa mafundisho ya msingi katika imani ya Ukristo.[5]

Claver alishindana na baadhi ya Wajesuiti wenzake waliokubali utumwa, akahimiza wote kuwaona watumwa kama ndugu katika Kristo. Baada ya kuwafundisha na kuwabatiza alijitahidi wapate haki zao kama binadamu na kama Wakristo.

Hata hivyo utume wake ulienea zaidi, kwa kuhubiri barabarani kwa mabaharia na wafanyabiashara pamoja na kwenda vijijini mpaka wakati wa kurudi kuwatembelea aliowabatiza na kuwatetea.

Wakati wa safari hizo, alikuwa anajitahidi kukwepa mapokezi ya wenye mashamba na wanyapara wao, akipendelea kulala katika makazi ya watumwa.

Vilevile alihudumia waliotembelea Cartagena (hata [Waprotestanti]] na Waislamu) na waliohukumiwa adhabu ya kifo, ambao amewaandaa wengi kufa vizuri kiroho; pia alitembelea mara nyingi hospitali za mji huo.

Mwaka hadi mwaka, kazi na ushuhuda wake vilileta nafuu fulani katika hali ya watumwa, naye akawa na sauti iliyosikika.

Mifupa ya Claver chini ya altare ya kanisa lake huko Cartagena

Miaka ya mwisho, Petro alikuwa mgonjwa mno asiweze kutoka chumbani. Kwa miaka 4 alibaki karibu peke yake, akihudumiwa vibaya (hata karibu kuachwa bila chakula) na mtumwa aliyekombolewa ambaye mkubwa wa nyumba alimuagiza kumshughulikia. Petro hakulalamika kamwe, akikubali yote kama malipizi ya dhambi zake.[6]

Alifariki tarehe 8 Septemba 1654.

Heshima baada ya kufa[hariri | hariri chanzo]

Watu wa Cartagena walipopata habari ya kifo chake, walilazimisha waruhusiwe kuingia chumbani ili kumpa heshima ya mwisho. Kutokana na sifa zake, walijipatia vipande vya nguo zake kama masalia hata karibu kumuacha uchi.[6]

Wakuu wa mji, ambao awali walimuona anawasumbua daima kwa kutetea watumwa, waliagiza mazishi ya fahari.

Alitangazwa mtakatifu pamoja na Alfonso Rodriguez, na baada ya miaka minane 1896 Papa Leo XIII alimtangaza pia msimamizi wa umisionari wote katika ya Waafrika.[2]

Mwili wake unatunzwa katika kanisa la Wajesuiti alipokuwa anaishi, ambayo sasa linaitwa kwa jina lake.[7]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]