Bahari ya Chumvi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Mtalii akielea kwenye maji ya Bahari ya Chumvi na kusoma gazeti

Bahari ya Chumvi (Kiebrania: יָם הַ‏‏מֶ‏ּ‏לַ‏ח‎ yam ha-melaḥ "bahari ya chumvi"; Kar.: ألبَحْر ألمَيّت‎ al-bahrᵘ l-mayyit, "bahari ya mauti") ni ziwa lililoko kati ya nchi za Israel, Palestina na Yordani.

Ziwa liko ndani ya bonde la mto Yordani ambalo ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki. Eneo lake ni takriban 600 km².

Mwambao wa ziwa ni mahali pa chini kabisa kwenye nchi kavu ya dunia uko mita 400 chini ya uwiano wa bahari. Kwa sababu hiyo kuna joto kali linalosababisha maji mengi kugeuka mvuke na kuacha chumvi nyingi na kiasi cha chumvi ni mara tisa kulinganisha na chumvi katika maji ya Bahari ya Kati. Kiasi hicho kikubwa cha chumvi kimezuia kuwepo kwa samaki ndani yake; uhai wa pekee ni aina za bakteria na algae.

Kiasi kikubwa cha chumvi kimesababisha densiti ya maji yake kuwa juu; hivyo binadamu huelea katika maji haya tu bila ya kuhitaji jitihada yoyote. Watalii hupenda kufika hapa wakiogelea na kujipakia matope ya ziwa yanayosemekana kuwa nia tabia za kuponya magonjwa ya ngozi.

Israel na Yordani zimeanzisha viwanda vinavyosafisha aina mbalimbali za chumvi kwa matumizi ya kibiashara.

Kwa jumla kiasi cha maji ziwani kimerudi nyuma kwa sababu mto Yordani ambayo ni mto wa pekee unaoingia humo umehamishwa kwa shughuli za umwagiliaji.