Istanbul
Istanbul (kwa Kituruki unatajwa İstanbul) ni mji mkubwa zaidi katika nchi ya Uturuki, ukiwa na wakazi wanaokadiriwa kuwa kati ya milioni 11 na 15, ambao wanaufanya kuwa miongoni mwa miji mikubwa ya dunia. Huu ndio mji mkuu wa Mkoa wa İstanbul.
Eneo la Istanbul linaelekea pande zote mbili za mlangobahari wa Bosporus unaotenganisha Ulaya na Asia. Hivyo ni mji pekee duniani uliopo katika mabara mawili.
Kiini cha kihistoria kipo upande wa Ulaya kwenye sehemu yenye umbo la rasi baina ya Bahari ya Marmara na Pembe ya Dhahabu ambayo ni mkono wa bahari unaoingia ndani ya nchi na hivyo mahali pa mji ulikingwa na bahari pande tatu.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Mji huu umebadilishiwa jina mara kadhaa katika historia yake ya zaidi ya miaka 2,600. Awali jiji hilo liliundwa na Wagiriki mnamo mwaka 660 KK kwa jina la Bizanti. Mnamo mwaka 330 BK Kaisari Konstantino Mkuu aliufanya kuwa mji mkuu wa Dola la Roma akaupanua ukajulikana kama Konstantinopoli (yaani mji wa Konstantino).
Konstantinopoli uliendelea kama mji mkuu wa Dola la Roma na baadaye Roma ya Mashariki uliojulikana pia kama Milki ya Bizanti hadi mwaka 1453 ambapo mji ulitwaliwa na Waturuki. Tangu mwaka ule uliendelea kama mji mkuu wa Milki ya Osmani hadi mwaka 1923. Baadaye serikali ya Uturuki ilihamia Ankara.
Wakati wa Waosmani majina mbalimbali yalitumiwa: Konstantinopoli au kwa kifupi "Konstantiniye", halafu tangu karne ya 18 pia "Istanbul". Tangu mwaka 1873 jina rasmi kwa Kituruki limekuwa "Istanbul".
Kuwepo kwa bandari kumepelekea mji huo kuwa kitovu cha biashara katika Uturuki.
Katika Ukristo ni muhimu kama makao ya Askofu wa pili kwa heshima kati ya Maaskofu wote duniani, kadiri ya orodha iliyotolewa na mitaguso mikuu ya karne ya 4.
Hadi vita vya kwanza vya dunia Istanbul ilikuwa na wakazi wengi Wakristo, hasa Wagiriki na Waarmenia, lakini wakati ule Waarmenia waliteswa wakapungua na baada ya vita Wakristo walibaguliwa kwa jumla, hivyo wengi walihamia Ugiriki. Leo hii Wagiriki waliobaki ni 2000 - 3000 pekee na Waarmenia ni takriban 50,000.
Majengo
[hariri | hariri chanzo]Istanbul huwa na majengo mengi ya kihistoria kama vile
- Hagia Sofia ilikuwa kanisa kuu la Konstantinopoli; ilijengwa kwa amri ya Kaisari Iustiniano na kukamilishwa mwaka 537
- Ukuta wa Theodosio ulioimarishwa kwa amri wa Kaisari huyu na kuwa kinga ya mji hadi uvamizi wa Waturuki
- Makanisa ya kale, mengine kati yake yamebadilishwa kuwa misikiti
- Mnara wa Galata uliojengwa na Waitalia katika sehemu yao ng'ambo ya Pembe la Dhahabu
- Misikiti mikubwa ya Milki ya Osmani kama vile Msikiti wa Suleymaniye, Msikiti wa Sultan Ahmad na majengo mbalimbali ya Mimar Sinan
- Topkapi iliyokuwa ikulu ya masultani hadi mwaka 1923 na leo hii ni kati ya makumbusho muhimu duniani
- Mnara wa Msichana - Kiz Kulesi: kulingana na hadithi nyingi tofauti, Konstantino, mmoja wa viongozi wa Kibizanti, alikuwa na binti yake mrembo ambaye alimpenda sana. Watabiri walitabiri kuwa kifo cha binti huyo kitatokana na kugongwa na nyoka. Katika kumlinda binti yake na janga hilo, mfalme akaagiza kujengwe nyumba katikati ya kisiwa ambapo ndipo Kiz Kulesi ilipo hivi sasa. Lakini mwisho wa siku yule binti aliuawa na nyoka aliyefika kisiwani katika kikapu cha mboga.
Elimu
[hariri | hariri chanzo]Mjini Istanbul kuna vyuo vikuu mbalimbali, kati yake:
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Istanbul Governor's Office Ilihifadhiwa 22 Desemba 2006 kwenye Wayback Machine.
- Istanbul Metropolitan Municipality Ilihifadhiwa 26 Novemba 2005 kwenye Wayback Machine.
- WikiSatellite view of Istanbul at WikiMapia
- Emporis Buildings Database: Historic and modern buildings of Istanbul
- Ottoman architect Sinan's works in Istanbul Ilihifadhiwa 1 Aprili 2008 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu maeneo ya Uturuki bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Istanbul kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |