Twiga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Giraffa)
Twiga
Twiga wa Afrika Kusini
Twiga wa Afrika Kusini
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wanaonyonyesha watoto wao)
Oda: Artiodactyla (Mamalia wanaokanyaga kwa kwato mbili-mbili)
Nusuoda: Ruminantia (Wanyama wanaocheua)
Familia: Giraffidae (Wanyama walio na mnasaba na twiga)
Jenasi: Giraffa (Twiga)
Brisson, 1762
Ngazi za chini

Spishi 11, nususpishi 7:

Msambao wa nususpishi za twiga
Msambao wa nususpishi za twiga

Twiga (kutoka Kimaasai: thwega) ni jenasi ya wanyama ya Afrika katika familia Giraffidae. Wanapatikana hasa kuanzia Nijeri mpaka Afrika Kusini.

Spishi zake nne ni mamalia wenye kwato shufwa na shingo ndefu kuliko ile ya wanyama wote wa nchi kavu. Mwili wao umepambwa kwa madoa yasiyo na umbo maalumu, yenye rangi ya njano mabaka meusi na kutenganishwa na rangi nyeupe, au rangi ya manjano-kahawia.

Twiga huishi hasa maeneo ya savanna na nyika. Hata hivyo wakati chakula kinapokuwa adimu, hupendelea maeneo yenye miti mingi, migunga na vikwata hasa. Hunywa maji mengi sana wakati yanapopatikana ili kukabili ukame ukija. Twiga hutumika kama nembo ya kuiwakilisha taifa la Tanzania.

Mabadiliko ya zamani[hariri | hariri chanzo]

Twiga wana uhusiano na tandala na ng’ombe, lakini wanawekwa kwenye familia yao pamoja na ndugu zao wa karibu okapi. Familia hii hapo awali ilikuwa na wanyama wengi kiasi. Twiga huaminika kuwa walitokana na swala aliyekuwa na urefu wa futi 3 tu, mnamo miaka milioni 30–50 iliyopita.

Kutokea kwa shingo ndefu ya twiga kumezua mjadala mkubwa sana. Hadithi iliyozoeleka ni kwamba ilikuwa ni kutokana na juhudi za twiga kuyafikia matawi ya juu ya miti wakati wa ushindani wa chakula na wanyama wenzie walao majani.

Kulikuwa na nadharia nyingine isemayo kuwa twiga dume ndio waliokuwa na shingo ndefu kuleta tofauti na jike, na kuweza kufikia majani ya juu ili kupata chakula; kukua kwa shingo zao kulikuwa tu ni kama ukuaji wa pili baada ya balehe. Hata hivyo, nadharia hiyo haikubaliki sana na kulingana na tafiti za hivi karibuni, imeonyesha udhaifu mkubwa na kubakiza nadharia ile ya kuanza peke yake.

Hata madoa ya twiga yanaaminika kuwa hapo awali yalikuwa ni ya rangi angavu juu ya mwili wa ngozi nyeusi. Madoa hayo taratibu yaliendelea kuwa ya muundo wa nyota na maua, leo hii yamekuwa hayana umbo maalumu.

Pembe[hariri | hariri chanzo]

Twiga katika zoo
Twiga mama na mtoto
Twiga wakijamiiana

Jinsia zote mbili zina pembe, japo pembe za twiga jike ni ndogo, hivyo kwa pembe hizo unaweza ukatambua jinsia ya twiga kwa urahisi, kwa sababu twiga jike wana nywele juu ya nundu za pembe zao, huku pembe za twiga dume zikiwa na upara tu. Twiga dume wakati mwingine huwa na mkusanyiko wa kalsiamu kwenye fuvu la kichwa, ambao (mkusanyiko) hukua kadiri wanavyoongezeka umri, na kuwa kama nundu nyingine na kufanya jumla ya nundu kuwa tatu.

Shingo[hariri | hariri chanzo]

Twiga wana shingo ndefu wanayoitumia kula majani ya miti mirefu kabisa. Twiga wana pingili saba za mifupa ya shingoni, kama wanyama wengine, japo baadhi ya wataalamu wanadai zipo nane zaidi, mifupa hiyo ina maungio.

Miguu na miondoko[hariri | hariri chanzo]

Twiga wana miguu mirefu sana, kwa kadiri ya 10% zaidi ya miguu ya nyumbu. Mwendo wa twiga ni wa maringo, lakini akiwa anafukuzwa hukimbia sana, mpaka kufikia mwendokasi wa km. 55 kwa saa. Twiga ni kazi kuwindwa, na ni hatari. Wanapenda kujihami kwa teke la nguvu. Teke la twiga mkubwa linaweza kupasua fuvu la kichwa cha simba au hata kuvunja uti wa mgongo. Simba pekee ndio wanyama wanaoweza kuwa tishio kwa twiga.

Mfumo wa mzunguko wa damu[hariri | hariri chanzo]

Moyo wa twiga una uzito wa kg. 10 na una urefu wa sm. 60, na hutakiwa kuzalisha mgandamizo wa damu mara mbili zaidi ukilinganisha na wanyama wa kawaida, ili kusaidia kusukuma damu mpaka kwenye ubongo, kichwani. Karibu na shingo kuna mfumo wa damu tata, unaomida damu nyingi isiende kwenye ubongo wakati twiga anapoinamisha kichwa chake.

Tabia[hariri | hariri chanzo]

Twiga jike hukusanyika pamoja kwenye makundi ambayo wakati mwingine hujumuisha twiga dume wadogo. Twiga dume wadogo hao hupenda kujiunga na dume wakubwa. Utafiti wa mwaka 1920 ulithibitisha kuwa twiga hawachangamani na twiga wasio wa kundi moja. Pia pindi dume atakapo kumpanda jike, basi huchagua yeyote aliye katika kipindi cha joto, kwenye kundi lolote. Twiga dume hutambua twiga jike walio katika kipindi cha joto kwa kuonja ladha ya mikojo yao. Twiga huchangamana vizuri na wanyama wengine wala nyasi. Kuwa pamoja na twiga hawa ni faida kubwa, kwa sababu urefu wao husaidia hata kuona adui tangu wakiwa mbali.

Uzazi[hariri | hariri chanzo]

Twiga hubeba mimba kwa siku 400 mpaka 460 ambapo hatimaye mara nyingi huzaa ndama mmoja, japo mapacha hutokea mara kadhaa. Mama hujifungua akiwa amesimama na kende lake hukatika mtoto aangukapo ardhini. Ndama akizaliwa huwa na urefu wa mita 1.8. Baada ya saa kadhaa, mama huweza kukimbia japo ndani ya wiki mbili za mwanzo ndama hutumia muda mwingi kujilaza chini huku akilindwa na mama yake. Ndama huyo huwa hatamaniwi kuwindwa na simba, chui, fisi wala mbwa mwitu. Ni asilimia 25–50 tu ya twiga ndiyo hufikia kuwa wakubwa. Twiga hukadiriwa kuishi miaka 20–25 wakiwa mwituni na miaka 28 wakifugwa nje ya mbuga.

Kupigana/kusuguana kwa shingo[hariri | hariri chanzo]

Twiga mapiganoni

Kitendo hicho cha twiga kufanywa kwa madhumuni mbalimbali; lengo mojawapo ni kupigana vita, vita vinaweza kuwa kubwa kwelikweli. Kadiri shingo inavyokuwa ndefu, ndipo kichwa nacho kinapokuwa kikubwa zaidi, na nguvu ya kupigana huwa kubwa vilevile. Na imeonekana twiga dume wanaofanikiwa kupata jike wa kujamiiana ni wale twiga dume waliofanikiwa kushinda kwenye vita. Ndiyo maana husikika kuwa, shingo ndefu imetokana na ushindani wa kijinsia, lakini mara nyingine twiga, husuguana tu shingo zao kwa kujipatia raha/ashiki ya kimapenzi. Tena ajabu, twiga dume, wao kwa wao ndio hushiriki zaidi zoezi hilo hasa nyakati za upweke. Mhemko wakati wa shughuli hiyo unaweza kuwa mkubwa mpaka kufikia kileleni.

Kulala[hariri | hariri chanzo]

Twiga ni miongoni mwa mamalia wanaolala kwa muda mdogo kuliko wote, na hulala kwa wastani wa dakika kumi mpaka saa 2 katika masaa 24 ya siku moja na kuwa na wastani wa saa 1 ya kulala kwa siku.

Chakula[hariri | hariri chanzo]

Twiga anayekula

Twiga hula majani ya miti, nyasi nyingi na matunda. Ulimi wake una urefu wa takribani sentimeta 45 na ni mgumu sababu mlo wa twiga huhusisha miiba pia. Twiga anaweza kula mpaka kilo 29 za majani kwa siku, lakini anaweza hata kustahimili kwa kilo 6.8 tu za nyasi. Twiga hula kidogo sana kwa sababu hupata chakula chenye virutubisho vingi sana na pia mfumo wake wa mmeng’enyo wa chakula ni wa uhakika sana. Twiga pia huweza kukaa kwa vipindi virefu bila kunywa maji.

Spishi[hariri | hariri chanzo]

@G. c. rothschildi amechukuliwa kuwa sawa na G. c. camelopardalis siku hizi.

Spishi za kabla ya historia[hariri | hariri chanzo]

  • Giraffa gracilis
  • Giraffa jumae
  • Giraffa priscilla
  • Giraffa punjabiensis
  • Giraffa pygmaea
  • Giraffa sivalensis
  • Giraffa stillei

Picha[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Ili kupata maelezo kuhusu masanduku ya uanapwa ya spishi angalia: Wikipedia:WikiProject Mammals/Article templates/doc.