Kiboko (mnyama)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kiboko
Kundi la viboko mtoni Luangwa (Zambia)
Kundi la viboko mtoni Luangwa (Zambia)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wenye viwele)
Nusungeli: Placentalia (Wanyama wenye mji)
Oda: Artiodactyla (Wanyama wenye kwato mbili kwa kila mguu)
Nusuoda: Whippomorpha (Wanyama kama nyangumi na viboko)
Familia: Hippopotamidae (Wanyama walio na mnasaba na kiboko)
Jenasi: Hippopotamus
Linnaeus, 1758
Spishi: H. amphibius
Linnaeus, 1758
Ngazi za chini

Nususpishi 5:

Kiboko (jina la kisayansi: Hippopotamus amphibius) ni mamalia mkubwa wa familia ya Hippopotamidae. Nyumbani kwake ni bara la Afrika.

Huishi kwenye maji ya mito na maziwa lakini ana uwezo wa kutembea kwenye nchi kavu mbali na maji. Chakula chake ni nyasi fupi.

Kimo cha mbegani kinafikia mita 1.5 na urefu wake hadi mita 4.5. Uzito wake ni kati ya kilogramu 2700 na 4500 kg. Hivyo kiboko inashindana na kifaru juu ya cheo cha kuwa mnyama mzito wa pili kwenye nchi kavu baada ya tembo. Akikimbia hufikia mwendo wa kilomita 48 kwa saa ingawa kwa muda mdogo tu. Viboko huishi majini na nchi kavu, hasa kwenye maziwa na mito ambako viboko dume huishi kwenye sehemu kubwa ya mto na jike na watoto 5 mpaka 30. Wakati wa mchana hubaki wametulia kwa kukaa ndani ya maji au matope; kuzaliana na kuzaa watoto vyote hutokea ndani ya maji. Hujitokeza nyakati za giza kula nyasi. Wakati viboko hupumzika pamoja ndani ya maji, wakati wa kula nyasi hutawanyika na hakuna mipaka.

Kiboko anatambulika kwa kinywa na meno yake makubwa, mwili usio na nywele, miguu mifupi na umbo kubwa. Ni mnyama wa ardhi wa tatu kwa ukubwa akiwa na uzito (kati ya tani 1.5 na 3.5), nyuma ya faru mweupe (tani 1.5 mpaka 4 ) na tembo (tani 3 mpaka 7 ). Licha ya umbo lake la kujaa na miguu mifupi, kiboko huweza kumshinda mbio binadamu kwa urahisi. Kiboko pia katika mbio fupi wanafikia mpaka kasi ya km 29/saa. Kiboko ni miongoni mwa viumbe ambao ni wakorofi kuliko wote an husemekana kama ni mnyama kali kuliko wote Afrika. Kuna kadiri ya viboko 125,000 mpaka 150,000 katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara; Zambia 40,000 na Tanzania 20,000 mpaka 30,000.[1] Viboko bado wapo kwenye tishio la kutoweka kutokana na kutoweka kwa uoto na ujangili kuwinda nyama yao na meno yao chonge ya vipusa.

Uainishaji na asili[hariri | hariri chanzo]

Kiboko ni mnyama wa jenasi Hippopotamus. Kiboko kibete ni wa jenasi Choeropsis. Hapo awali, alikuwa amewekwa katika jenasi Hexaprotodon, ambayo ina idadi ya spishi za viboko zilizotoweka. Jenasi hizi ziko katika familia Hippopotamidae. Familia hii imeainishwa katika oda Artiodactyla pamoja na wanyama wengine wenye kwato mbili. Wana wengine wa Artiodactyla ni pamoja na ngamia, ng'ombe, kulungu na nguruwe, ingawa viboko hawana [[uhusiano[[ wa karibu na vikundi hivi.

Nusupishi za kiboko zimeainishwa kulingana na tofauti zao za maumbo hasa fuvu zao za kichwa na maeneo wanamoishi.[2]

  • H. a. amphibius, Kiboko wa Naili – (nususpishi iliyotawala) iliyoanzia Misri, ambako sasa wametoweka, kusini mpaka Mto Naili hadi Tanzania na Mozambique.
  • H. a. kiboko, Kiboko Mashariki – kwenye pembe ya Afrika, Kenya na Somalia. Kiboko ni neno la Kiswahili.
  • H. a. capensis, Kiboko Kusi – kutoka Zambia mpaka Afrika ya Kusini. Fuvu zao za kichwa nyingi zipo bapa.
  • H. a. tschadensis, Kiboko Magharibi – wanapatikana Afrika Magharibi yote, na kama jina linavyosema, Chad. Wana uso mfupi kiasi na sura pana yenye obiti kuu.
  • H. a. constrictus, Kiboko wa Angola – ndani ya Angola, kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Namibia.

Hapo awali, ilifikiriwa kuwa viboko walikuwa na uhusiano wa karibu na nguruwe na kwa hivyo waliwekwa katika nusuoda Suina. Walakini, ushahidi kutoka protini za damu, ADN[3][4][5] na kumbukumbu ya visukuku sasa unaonyesha kwamba viboko wana uhusiano wa karibu zaidi na nyangumi[6]. Wahenga wao wa pamoja walioishi kwenye maji na nchi kavu waligawanyika kutoka Ruminantia takriban miaka milioni 60 iliyopita. Baadaye, nyangumi walijitenga na viboko[4][7]. Kwa pamoja, vikundi hivi sasa vimepewa nusuoda yao ya Whippomorpha (kutoka whale + hippo + morpha = umbo).

Viboko wa zamani zaidi wanaojulikana walikuwa katika jenasi Kenyapotamus na waliishi Afrika kutoka miaka milioni 16 hadi 8 iliyopita. Ingawa spishi za kiboko za kale zilisambaa Asia na Ulaya kote, hakuna hata moja ambayo imewahi kugunduliwa katika Amerika. Kuanzia miaka milioni 7.5 hadi 1.8 iliyopita, wahenga kadhaa wa kiboko wa kisasa, katika jenasi Archaeopotamus, waliishi Afrika na Mashariki ya Kati[8].

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Kiboko kwenye hifadhi huko Lisbon
Kiboko dume akiwa nje ya maji wakati wa mchana, huko Ngorongoro Crater, Tanzania
Kiboko aliyejizamisha huko katika hifadhi ya Memphis

Viboko ni miongoni mwa mamalia wakubwa. Wanaweza kuishi majini na nchi kavu. Ujazo-nene wao unawaruhusu kuzama na kuogelea chini kabisa mwa mto. Viboko nao huchukuliwa kama wanyama wakubwa, lakini tofauti na wanyama wengine wakubwa, viboko huishi kwenye maji baridi ya mito na maziwa. Kutokana na umbo lao kubwa, ni vigumu kupima uzito wao wakiwa mwituni. Makadirio mengi ya uzito yanatokana na operesheni za kuwapunguza zilizofanyika mnamo 1960. Wastani wa uzito wa kiboko dume ni kg 1500-1800. Viboko jike ni wadogo kidogo wakiwa na wastani wa uzito wa kg 1300-1500. Viboko wakubwa dume wanaweza kuwa wakubwa sana mpaka kufikia kg 3200 na hata mara kadhaa kufikia kg 4500. Viboko dume huendelea kukua muda wote wa maisha yao, huku majike hufikia uzito wa juu wakifikia umri wa miaka 25.

Kwenye kipindi cha “Dangerous Encounters with Brady Barr”, kwenye televisheni ya National Geographic Channel, Dk. Brady Barr alipima mkandamizo wa taya za kiboko mara aumapo na ya kiboko jike na kupata kg 826. Barr alijaribu pia kupima kwa kiboko dume lakini hakufanikiwa kutokana na ukorofi wa kiboko dume.[9]

Viboko wana urefu wa mita 3.3 mpaka 5.2, kujumuisha na mkia wenye urefu wa sm 56, inayojumuisha pembe kubwa na nywele upande wa kulia kulingana na jinsia yake, na urefu wa karibia mita 1.5 kwenye mabega yake. Japokuwa ni wanyama wakubwa, viboko wana uwezo wa kukimbia sana kuliko hata binadamu wakiwa nchi kavu. Makadiriio ya mwendokasi wao ni kutoka km 30 mpaka 40 au hata 50 kwa saa. Kiboko anaweza akabakia na mwendo huu kwa umbali wa walau mita mia kadhaa tu.

Kiboko huishi kwa miaka 40 mpaka 50. Kiboko aitwaye Donna, anayeishi akiwa na umri mkubwa kuliko wote sasa 57, huko Mesker Park Zoo katika Evansville, Indiana. Kiboko aliyewahi kuripotiwa kuwa na umri mkubwa zaidi aliitwa Tanga, aliishi huko Munich, Ujerumani na alifariki mnamo 1995 akiwa na umri wa miaka 61. Macho, masikio na pua za kiboko yapo juu ya fuvu la kichwa. Hii huwaruhusu kuzamisha sehemu kubwa ya mwili wao kwenye maji au matope na kupata ubaridi kujizuia na mwanga mkali wa jua. Mifupa yao imejengwa kuweza kubeba uzito wa mnyama wote. Kama mamalia wengine waishio majini, kiboko pia wana nywele chache za mwilini.

Ngozi zao hutoa majimaji mekendu kwa ajili ya kuzuia kuungua na jua. Majimaji hayo huitwa pia ‘jasho jekundu’, japo si damu wala jasho. Majimaji haya mwanzoni huwa hayana rangi lakini baada ya dakika kadhaa huwa mekundu, na baada ya muda huwa ya kijivu. Kemikali mbili zimetambuliwa ndani yake, ‘hipposudoric acid’ na ‘norhipposudiric acid’ ambazo zote zina asili ya asidi. Kemikali hizi huzuia ukuaji wa bakteria wanaosababisha magonjwa na pia kusharabu pigmenti za mwanga wa jua aina ya ‘ultraviolet’ na kuziua athari za mwanga wa jua. Na viboko wote hata wanaotofautiana milo yao huwa na kemikali hizi za aina moja, hivyo kemikali hizi hazitokani na chakula.

Kiboko akiwa majini

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Kigezo:IUCN2008 Database entry includes a range map and justification for why this species is vulnerable.
  2. Eltringham, S.K. (1999). The Hippos. Poyser Natural History Series. Academic Press. ISBN 0-85661-131-X. 
  3. Ursing, B.M.; Arnason U. (1998). "Analyses of mitochondrial genomes strongly support a hippopotamus-whale clade". Proceedings of the Royal Society 265 (1412): 2251–5. PMC 1689531. PMID 9881471. doi:10.1098/rspb.1998.0567. 
  4. 4.0 4.1 Gatesy, J. (1 May 1997). "More DNA support for a Cetacea/Hippopotamidae clade: the blood-clotting protein gene gamma-fibrinogen". Molecular Biology and Evolution 14 (5): 537–543. PMID 9159931. doi:10.1093/oxfordjournals.molbev.a025790.  Unknown parameter |doi-access= ignored (help)
  5. Geisler, J. H.; Theodor, J. M. (2009). "Hippopotamus and whale phylogeny". Nature 458 (7236): E1–4; discussion E5. Bibcode:2009Natur.458....1G. PMID 19295550. doi:10.1038/nature07776.  Unknown parameter |s2cid= ignored (help)
  6. Sanders, Robert (25 January 2005). Scientists find missing link between the dolphin, whale and its closest relative, the hippo. Science News Daily.
  7. Boisserie, Jean-Renaud; Lihoreau, Fabrice; Brunet, Michel (2005). "The position of Hippopotamidae within Cetartiodactyla". Proceedings of the National Academy of Sciences 102 (5): 1537–1541. Bibcode:2005PNAS..102.1537B. PMC 547867. PMID 15677331. doi:10.1073/pnas.0409518102.  Unknown parameter |doi-access= ignored (help)
  8. Boisserie, Jean-Renaud (2005). "The phylogeny and taxonomy of Hippopotamidae (Mammalia: Artiodactyla): a review based on morphology and cladistic analysis". Zoological Journal of the Linnean Society 143: 1–26. doi:10.1111/j.1096-3642.2004.00138.x.  Unknown parameter |doi-access= ignored (help)
  9. Barr, Brady. "Undercover Hippo," Dangerous Encounters, National Geographic Channel, January 20, 2008.

Ili kupata maelezo kuhusu masanduku ya uanapwa ya spishi angalia: Wikipedia:WikiProject Mammals/Article templates/doc.