Silika kadiri ya sufii

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Upambanuzi huu ni wa zamani, ila mwishoni mwa karne XX imechunguzwa na kutengenezwa upya na wanasaikolojia waliouita enneagram, yaani mchoro wa silika tisa, ambazo zinaitwa kwa tarakimu fulani na kupangwa katika duara. Hizo zinahusiana kwa namna mbalimbali, lakini hasa ni kwamba tatu (5, 6, 7) zinafuata zaidi mawazo ya kichwa, tatu (2, 3, 4) hisi za moyo, na tatu (8, 9, 1) misukumo ya matumbo. Kila mtu anaweza kutumia vitovu vyote vitatu, lakini polepole amependelea kimojawapo hata kikatawala vingine. Hivyo kwa kutegemea urithi na mazingira amepoteza uwiano.

Hakuna namba nzuri au mbaya zaidi: kila moja ina utajiri na udhaifu wake. Tusichague namba fulani kwa sababu tunaipenda, bali tujaribu kujua na kupokea ukweli juu yetu. Ni rahisi kujitambua kwanza tupo katika kundi lipi kwa kuchunguza tunavyojisikia tukifikiria tunatakiwa kuishi katika miji mitatu ifuatayo, ambayo ni ya kubuniwa, lakini tuichukue kama ni ya kweli.

Mji wa kichwa[hariri | hariri chanzo]

Umejengwa kwa mpango kabambe: majengo yote yanalenga kufaa tu, hayana pambo lolote lile, tena karibu yote yako sawa. Vioo vyake ni vyeusi ili watu wa ndani waweze kuona kila kitu nje wasionekane wenyewe. Katika mji huo utajisikia daima unachunguzwa na wenyeji. Kwa namna fulani hofu ndiyo ono linalotawala, hivyo wanahitaji kujikinga na watu na hatari. Nyumba nyingi zimezungukwa na kuta ndefu zenye mageti mazito, watu wasije wakaingia bila ya ruhusa maalumu.

Barabara zote zinakwenda wima tu na kupangwa kama jedwali. Kuna vibao vya kuelekezea, navyo vyote vimechongwa kwa usanifu na kuandikwa namna inayosomeka kwa urahisi. Barabara zina taa za kutosha kuangazia wanaotembea usiku. Lakini hakuna watu wengi njiani, na wale wachache wanakwenda zao bila ya kusimama kwa maongezi marefu: kila mmoja anaonekana kufuata mawazo yake muhimu asitake kusumbuliwa.

Pamoja na hayo wanajali sheria za usalama barabarani na adabu njema, wakiwaachia wenzao njia pasipo ukorofi. Pamoja na kuwa na nidhamu]] ya hali ya juu, wanaweza kupokea na kusaidia wenzao kwa ukarimu, lakini bila ya kushirikisha maoni yao wala kutokeza hisi zao. Usafi ni mkubwa, kwa kuwa watu wa kichwa wanapenda kila kitu kisiwe na doa.

Kuna shule nyingi ajabu, za kila aina, hata vyuo vikuu; tena wanafunzi wake si watoto na vijana tu, bali watu wa makamo na wazee pia. Vilevile maktaba ni nyingi, na watu wanaingia na kutoka mfululizo huko wakibeba vitabu.

Kama Mtume Thoma, Wakristo wa huko wanaonekana kudhani imani ni kuona. Ndani ya kanisa, benchi zimepangwa mistarini kwa utaratibu kamili, nazo zimejaa vitabu vya ibada na tafakuri.

Pamoja na hayo, watu wa kichwa wanatofautiana pia. Katika mji huo tuliwakuta:

• Bibi sita, mshikasheria, ambaye alitupokea vizuri nyumbani na kuzungumzia watoto wake anaowapenda sana. Ameshawapangia maisha ya mbeleni akisukumwa na hofu ya kuwa wataweza wakapatwa na matatizo yasiyoshindikana. Hasa alionyesha kuogopa wakubwa wake wote, hata yuko tayari kuwatii daima na kuwakubalia bila ya kuchanga neno lolote. Anafanya kazi vizuri kwa kutii mamlaka, si kwa kupenda. Mwenyewe anashindwa kuchagua, kuamua na kujituma. Anachotaka hasa ni kuwa mwaminifu.

Kilema chake: Woga. Matatizo yake: kujivunia utiifu wake, kuogopa mabadiliko, kuwa mgumu, shupavu na jeuri, kuhukumu haraka, kutovumilia.

Utatuzi: kutambua kazi ya Roho Mtakatifu, kuwa tayari kwa mambo mapya, kukubali mabadiliko yanawezekana, kuzingatia roho ya sheria, kupokea mapungufu ya wengine, kujitosa zaidi hata katika mambo yasiyo wazi. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 3, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 9.

• Bwana tano, mchunguzi, ni mtu wa nadharia. Anapenda kukaa kimya, kutazama yote, kuwasoma wengine, kujipatia ujuzi mkubwa zaidi na zaidi, kusoma na kusikiliza kwa makini anaowaona wanamzidi elimu. Lakini mwenyewe anahitaji msukumo mkubwa mpaka akubali kutenda, kutoa, kushirikisha ujuzi wake. Baadaye anashangaza kwa jinsi anavyoweza kueleza mambo kinaganaga kwa mpangilio mzuri. Hasa hapendi mikutano ya burudani. Anachotaka hasa ni kuwa na hekima.

Kilema chake: Choyo. Matatizo yake: kulaumu, kuchoma moyo hata kama ni kwa utani, kutojali wengine, kuwa mchoyo, kujitafutia raha. Utatuzi: kushirikisha zaidi nafsi, vipawa na muda wake, kujumuika na wengine, kuonyesha na kueleza hisia za moyo wake, kukubali uwezo wake, kubuni na kuanzisha mambo. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 7, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 8.

• Kumbe sherehe fulani ndiyo nafasi tuliyokutana na bibi saba, mfurahivu. Huyo hawezi kuvumilia mwingine anune, hivyo yuko tayari daima kuigiza na kuchangamsha watu. Vilevile hapendi mazungumzo mazito juu ya hatari, shida na matatizo, hivyo akiyasikia anayakatisha mara na kuanzisha mengine ya burudani. Anapenda kufanya mipango mingi, pasipo hakika ya kuitekeleza kweli; akishindwa atadai wengine waitimize badala yake. Anavaa nguo zinazomtia uzuri. Anachotaka hasa ni kupendeza.

Kilema chake: Ulafi. Matatizo yake: kuwa mlafi, kutokubali maumivu, kuepuka majukumu, kutofuatilia mambo madogomadogo, kufungamana kijuujuu tu, kukosa subira, kuahirisha “mpaka kesho”. Utatuzi: kuishi katika ukweli wa maisha, kuangalia matukio ya sasa, kukabili magumu kwa ustahimilivu, kutimiza kazi na mpango mpaka mwisho, kukubali mipango ya wengine na kujihusisha nayo. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 1, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 5.


Mji wa moyo[hariri | hariri chanzo]

Umejengwa bila ya mpango wowote: kila mtu amejijengea popote alipoona nafasi ni nzuri kwa kuhusiana na watu. Hivyo nyumba zimesimama karibukaribu, bila ya mipaka wala mageti, zimezingirwa na maua mengi ambayo katikati yake kuna matangazo yaliyoandikwa kwa usanii. Mengi yake ni ya sherehe, ngoma na burudani mbalimbali.

Barabara zinazoziunganisha nyumba hizo zinatumika sana, tena sana. Watu wanaonekana wazi kupenda mafungamano, urafiki, maisha ya kijamii. Wanajali sana sura yao, kwa hiyo wanapenda kuvalia mitindo mipya na ya pekee, kuzungumzia uzuri, urembo n.k. Pamoja na hayo wengi wamevaa sare ya unesi na ya huduma nyingine. Kuna makao mengi ya vyama na kujitolea, mbali ya sinema nyingi.

Kuta za kanisa zimepambwa sana nje na ndani, na badala ya benchi kuna mito, makochi nk. Ibada zinaonekana nzuri na za dhati, kwa kuwa waamini wanasali wanavyojisikia kutoka moyoni kuliko kwa kufuata vitabu na taratibu rasmi.

Pamoja na hayo, watu wa moyo pia wanatofautiana. Katika mji huo tuliwakuta:

• Bibi mbili, mtoahuduma, aliyetualika kwa chai na kutuonyesha anavyojali raha ya watu hata hakuweza kukaa nasi walau kidogo. Pamoja na kutuhudumia alipaswa kuitikia simu mfululizo, kwa sababu wengi wanamtafuta awasaidie. Mwenyewe anafurahia sana jambo hilo, ila mara kadhaa analalamika akisema, “Mbona nadaiwa kila kitu mimi?” Anazidisha hisia zake kwa wengine, akiwaonyesha anavyowapenda, akiwabembeleza hata kuwatawala na kuwatumia kwa faida yake. Upande wake anadai sana sifa na shukrani; akizikosa anadhani kuna uhasama dhidi yake. Tulipofaulu kuongea naye alipata habari nyingi kutoka kwetu, lakini hakujifahamisha kweli. Basi, tuligundua anavyotaka kujitawala asiweze kukubali yeye naye anahitaji msaada, wala kuuomba. Kwake ni vigumu kujifahamu kwa dhati. Anachotaka hasa ni kusaidia wote katika yote.

Matatizo yake: kujivuna, kuwa mjanja na mdanganyifu, kukosa subira, kujiona mkombozi, kumiliki wengine. Utatuzi: kukubali mahitaji yake, kupokea msaada, kuacha wengine wawajibike, kutambua mahitaji halisi, kutodhani bure kwamba ametupwa. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 8, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 4.

• Bibi tatu, mtafutavyeo, mkuu wa ofisi fulani. Tulitaka kumuona atueleze kuhusu shoti iliyotokea. Basi, karani wake hodari alituingiza kwake bila ya kuchelewa. Mara akaanza kuzungumzia hali ya ofisi akisisitiza bila ya kuchoka kwamba shoti yoyote haikuweza kutokana na kosa lake, bali mwenyewe amesharekebisha mengi, na kwa hakika baada ya muda mfupi yote yatakwenda sawa. Ni mtu wa juhudi sana, mshindani asiyekubali kushindwa. Ana uwezo mkubwa wa kujumuisha watu katika kazi ya pamoja. Anaonekana kujiamini, lakini hapendi kuonyesha miguso yake, wala udhaifu wowote. Anashughulikia sana afya yake lakini anashindwa kutambua hisia zake na anazitupa juu ya wengine. Anaweza akadanganya mradi afaulu, kwa sababu anachotaka hasa ni kufanikiwa.

Kilema chake: Udanganyifu. Matatizo yake: kupenda ubatili, kuwa mjanja, kufuata njia yoyote ili kufikia lengo, kutokubali kushindwa, kutoamini wengine.

Utatuzi: kujikubali alivyo badala ya kuangalia kazi tu, kujitahidi kuwa namna fulani kuliko kuonekana na kutenda, kugawa madaraka, kukubali mengine hayawezekani, kukiri ameshindwa. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 9, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 6.

• Bwana nne, msanii. Ingawa ni mtu wa makamo hajaoa. Uhusiano wake na wengine ni mgumu, unapitia sanaa, alama na mifano. Nyumba yake ni nzuri sana, ina picha nyingi ukutani. Alipika mwenyewe na kupanga chakula namna ya kupendeza. Mezani tulifurahishwa na miziki myepesi. Anaeleza wazi na kwa dhati kwamba, “hakuna anayeonja miguso mbalimbali kama mimi”. Anapenda mazuri na kuweza na kutaka amshirikishe yeyote. Ila mazungumzo yake yalielekea kulilia mambo yaliyopita, hata huzuni ikatujia. Anajidanganya kuhusu ukweli wake. Anachotaka hasa ni kuwa wa pekee.

Kilema chake: Kijicho. Matatizo yake: kujiona mwema kuliko wengine, kuwashusha, kujitafutia makuu, kujisifu, kuwa na wivu, kukata tamaa, kunung’unika mno.

Utatuzi: kutambua vipawa vya wengine, kufurahia sifa wanazopewa, kusikiliza kuliko kusema, kumtia moyo anayeshindwa kusema, kufurahia mambo ya kawaida ya kila siku. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 2, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 1.

Mji wa matumbo[hariri | hariri chanzo]

Watu wake wanapendelea historia na utamaduni wao: ndiyo sababu kati ya majengo ya kisasa, ambayo ni sahili na ya kufaa kwa starehe, yapo mengine ya zamani yanayoonyesha uzuri wa wakati uliopita, na vilevile nyumba kadhaa za makumbusho. Sehemu kubwa ya ardhi hailimwi, ila kando ya nyumba kuna mabustani ya mboga badala ya maua.

Watu wa mji huu wanavaa nguo yoyote wasijali urembo. Hata chakula kinachaguliwa kulingana na manufaa kwa afya kuliko ladha. Ni watu wa kelele, wanapenda kusema kwa sauti kubwa, kusalimiana motomoto, kupiga muziki na ngoma. Hawajali hukumu ya watu kuhusu namna yao ya kusema, kuvaa au kupanga nyumba. Wanatia maanani haki za binadamu, mahitaji ya kila mtu na hifadhi ya mazingira, kiasi cha kuona uchungu sana mambo hayo yakikosekana. Hata barabarani ni rahisi kukutana na kundi la watu wanaoshirikisha maoni yao juu ya mambo ya haki. Wanafuata na kuheshimu mashindan. Hasa wana busara ya kidunia. Mlangoni pa kanisa kuna orodha ya mahitaji ya watu ili kila mwamini atoe msaada anavyosukumwa kwa ndani.

Mjini huku pia tulikuta watu tofauti:

• Bwana nane, mtawala, anayependa kuongoza. Anajua uwezo wake wa kusababisha mambo mbalimbali hata maishani mwa watu wengine. Anawasukuma wanaomzunguka wajitolee kufanya kazi za hiari, hata mara nyingi ni kama anawalazimisha. Haogopi kumkabili yeyote, anatenda kwa nguvu, pengine kwa ukorofi. Hawezi kuishi bila ya kupigania haki yake na ya ulimwengu]] mzima. Hawezi kupokea chochote anachokiona si halali. Anaogopa kukubali hisani au miguso yoyote ndani mwake, akijisikia anaweza kuishi vizuri pasipo “upuuzi wa namna hii” (anavyosema). Anachotaka hasa ni kuwa na nguvu.

Kilema chake: Uzinifu. Matatizo yake: kuwa na kiburi, kukasirika vikali, kuchoma moyo, kutawala kwa maneno, kutupa wasioweza.

Utatuzi: kukubali mambo yalivyo, kutambua hisia zake, kujipokea na kupokea wengine, kuvumilia wengine wasiokubaliana naye, kutohukumu, kuwa mpole kwake na kwa wengine, kuwawezesha wafanye, kustawisha wema alionao. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 5, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 2.

• Bibi tisa, mpendaamani, anayesikitika mno kusikia maneno makali, hivyo anajitahidi mara kuwatuliza aliyeyatoa na aliyeambiwa. Anajaribu kueleza kwamba sababu ya mlipuko wa hasira si wenyewe. Katika kuleta amani ana kipaji cha pekee. Hapendi ghasia wala haraka; anachelewa karibu kila wakati. Hana bidii, kwa sababu anaridhika na maisha yalivyo, kama kwamba hana lengo maalumu. Ila anajitafutia amani na raha hata kujipatia vingi kwa gharama asije akahitaji tena kwenda kununua. Anachotaka hasa ni kutulia.

Kilema chake: Uvivu. Matatizo yake: kustahimili mno, kukosa shauku, kutojihusisha, kusikia watu bila ya kuwasikiliza, kuahirisha kazi.

Utatuzi: kujikaza, kujihusisha, kuamua, kutambua na kuonyesha hisia, kujithamini na kujali wengine. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 6, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 3.

• Bwana moja, mdaiukamilifu, ambaye kazi yake maalumu ni kusahihisha, kukosoa na kufichua uovu wake na wa yeyote yule. Kwake haki inawafanya wote wawe sawa, asikubali kupendelea wakubwa kwa sababu tu ni wakubwa. Anaona ulimwengu kama mkusanyo wa kasoro, ambazo ni kazi yake mwenyewe kuzirekebisha hata katika mambo madogomadogo. Anapenda kukosoa lakini pia kukosolewa kwa haki. Ni hakimu mkali asiyekubali kusubiri muda unaohitajika kukua. Kabla hajaanza kufanya kitu, anahitaji kuwa na hakika ya kukifanya vizuri. Anadai ukamilifu daima tena mara. Kwake ni shida kubwa kujipokea alivyo pamoja na kasoro zake. Hata akisema bila ya kelele, sauti yake inatokeza hasira iliyomo kwa wingi ndani mwake. Kwa kuwa anaona aibu sana kuionyesha, anaihifadhi ndani hata inakuwa kinyongo. Anachotaka hasa ni jitihada bora za kurekebisha yote.

Kilema chake: Hasira. Matatizo yake: kujivunia ukamilifu, kukosa subira, kuwa shupavu, kuhukumu, kutosikia ya wengine, kutopenda kushirikiana nao katika majukumu.

Utatuzi: kukubali mipaka yake, kutambua na kukubali hasira yake, kupokea wengine walivyo, kutumaini mambo yatakwenda vizuri, kufurahia hatua ndogondogo. Asifuate mwelekeo wa kufanana na namba 4, bali aende kinyume na kujitahidi kufanana na namba 7.