Nenda kwa yaliyomo

Nzige-jangwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Schistocerca gregaria)
Nzige-jangwa
Jike na dume wa nzige-jangwa wakipandana
Jike na dume wa nzige-jangwa wakipandana
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Orthoptera (Wadudu wenye mabawa nyofu)
Nusuoda: Caelifera (Wadudu kama panzi)
Familia: Acrididae (Panzi)
Jenasi: Schistocerca
Stål, 1873
Spishi: S. gregaria
(Forskål, 1775)

Nzige-jangwa ni wadudu wa kundi la panzi katika familia Acrididae wa oda Orthoptera ambao wanaishi jangwani kwa kawaida. Lakini wakiwa wengi sana hujikusanya katika makundi makubwa na kusafiri mbali ndefu hata nje ya jangwa. Tauni za nzige-jangwa wametishia uzalishaji wa kilimo katika Afrika, Mashariki ya Kati na Asia kwa karne nyingi. Riziki za angalau moja ya kumi ya idadi ya watu duniani yanaweza kuathiriwa na wadudu hao walafi.

Mzunguko wa maisha

[hariri | hariri chanzo]

Mzunguko wa maisha wa nzige-jangwa una hatua saba: yai, hatua 5 za tunutu, wanaojulikana kama warukaji, na mpevu mwenye mabawa. Kupandana hufanyika wakati dume aliyekomaa anaporuka juu ya mgongo wa jike aliyekomaa na kumbokora mwili wake kwa miguu. Manii huhama kutoka ncha ya fumbatio ya dume kwenda ncha ya ile ya jike, ambapo huhifadhiwa. Mchakato huo unachukua masaa kadhaa na uingizwaji mmoja wa manii unatosha kwa vibumba vitatu vya mayai.

Kisha jike hutafuta udongo laini unaofaa kwa kutaga mayai yake. Lazima uwe na joto sahihi na kiwango kizuri cha unyevu na kuwa karibu na majike wengine wanaotaga. Anachunguza mchanga kwa fumbatio yake na kuchimba kishimo ambacho ndani chake anaweka kibumba cha mayai kilicho na mayai hadi mia moja. Kibumba cha mayai kina urefu wa sm 3 hadi 4 na ncha ya chini ni takriban sm 10 chini ya uso wa ardhi. Mayai yamezungukwa na povu na hii inakauka mpaka kuwa utando na kuziba kishimo juu ya kibumba cha mayai. Mayai huchukua unyevu kutoka kwa mchanga unaozunguka. Kipindi cha kuatamia kabla ya kujiangua kwa mayai kinaweza kuwa wiki mbili au zaidi sana, kulingana na nyuzijoto.

Kundi zito la tunutu nchini Sudani

Baada ya kutoka kwenye yai tunutu mpya huanza kujilisha punde si punde na, ikiwa ana awamu ya kukaa pamoja na wenzake, anavutiwa na tunutu wengine na wanajikusanya. Wakati wa ukuaji anahitaji kuambua ngozi (kuacha kiunzi-nje chake) mara kwa mara. Ganda lake gumu la nje linapasuka na mwili wake unatanuka wakati kiunzi-nje kipya bado ni chororo. Hatua kati ya maambuaji zinaitwa “instars” na tunutu wa nzige-jangwa hupitia maambuaji matano kabla ya kuwa mpevu mwenye mabawa. Tunutu wa awamu ya kukaa pamoja huunda makundi yanayojilisha, kukota jua na kusonga mbele katika vikosi vinavyoshikamana, wakati wale wa awamu ya kutokaa pamoja hawaundi makundi.

Baada ya uambuaji wa tano mdudu anasemekana kuwa mpevu lakini bado hajakomaa kabisa. Kwanza ana rangi ya pinki na hawezi kukuza mayai au kuzalisha manii. Kufikia ukomavu kunaweza kuchukua wiki mbili hadi nne wakati uwepo wa chakula na hali ya hewa zinafaa, lakini kunaweza kuchukua muda mrefu kama miezi sita wakati hali hizo ni duni. Madume hukomaa kwanza na kutoa harufu ambayo huchochea kukomaa kwa majike (feromoni). Wakikomaa wadudu hao wanageuka kuwa njano na fumbatio ya majike huanza kuvimba na mayai yanayokua.

Ekolojia na kuunda makundi

[hariri | hariri chanzo]

Nzige-jangwa wana awamu mbili: awamu ya "solitaria" na awamu ya "gregaria" (polyphenism). Imeonyeshwa kuwa tunutu na wapevu wa nzige wanaweza kutenda kama gregaria ndani ya masaa machache baada ya kuwekwa katika hali ya msongano, ingawa mabadiliko ya kimofolojia huchukua maambuaji kadhaa ili kuonekana. Nzige wa gregaria wanahitaji kizazi kimoja au zaidi ili kuwa solitaria wakikuzwa katika upweke.

Tunutu wa solitaria nchini Mauritania
Tunutu wa hatua ya tano

Kuna tofauti katika mofolojia na mwenendo kati ya awamu hizo mbili. Katika awamu ya solitaria tunutu hawaundi makundi lakini huzunguka peke yao. Rangi yao kwanza ni kijani, lakini hatua zinazofuata zinaweza kuwa hudhurungi ikiwa uoto kijani huadimika au kukosekana. Wapevu wa solitaria huruka usiku na kuwa hudhurungi ili kufichika katika mazingira yao na wanaweza kuwa njano isiyoiva wakikomaa.

Katika awamu gregaria tunutu hujikusanya pamoja. Hatua ya kwanza ni nyeusi, zile za pili na tatu ni nyeusi na nyeupe na hatua zinazofuata ni njano kali pamoja na mabaka meusi. Wapevu wasiokomaa ni pinki na waliokomaa ni njano. Wanaruka wakati wa mchana katika makundi mazito.

Badiliko kutoka kwa mdudu wa solitaria asiye msumbufu kwenda kwa mdudu mlafi wa gregaria hufuata kwa kawaida kipindi cha ukame, wakati mvua inanyesha na mimea inaibuka katika maeneo makuu ya uzalishaji wa nzige. Idadi ya wadudu inazidi haraka na mashindano kwa chakula huongezeka. Kadiri tunutu wanaposongamana, changamano ya karibu ya miili yao husababisha miguu yao ya nyuma kugongana. Kichocheo hiki husababisha mfululizo wa mabadiliko ya metaboliki na ya mwenendo ambayo husababisha wadudu kubadilika kutoka kwa awamu ya solitaria kwenda kwa ile ya gregaria.

Wakati tunutu wanapokuwa gregaria, rangi yao hubadilika kutoka kwa kijani hadi njano na nyeusi, na wapevu hubadilika kutoka hudhurungi hadi pinki (wasiokomaa) au njano (waliokomaa). Mwili wao huwa mfupi zaid na wanatoa feromoni inayowafanya wavutiane, ambayo huongeza uundaji wa makundi. Feromoni ya tunutu ni tofauti na ile ya wapevu. Wanapofunuliwa na feromoni ya wapevu, tunutu huchanganyikiwa na kufadhaika, kwa sababu inaonekana kwamba hawawezi "kunusana", ingawa vichocheo vya kuona na kugusa vinabaki. Baada ya siku chache makundi ya tunutu hutengana na wale wanaotoroka umbuai huwa solitaria tena. Wanasayansi kadhaa wamejaribu kutumia sehemu kuu ya feromoni hio, benzyl cyanide, ili kusababisha tunutu wa gregaria wakuwe solitaria. Lakini matokeo ya majaribio uwandani walisikitikisha na kemikali hii ilizingitiwa kuwa sumu mbaya. Kwa hivyo mbinu huo wa udhibiti ulisuswa.

Wakati wa vipindi vya utulivu, vinavyoitwa vipindi vya kupunguka au mapungufu, nzige-jangwa hutokea tu ukanda wa km² milioni 16 ambao unaenea kutoka Mauritania kupitia Jangwa Sahara kaskazini mwa Afrika na kupitia Bara Arabu mpaka kaskazini magharibi mwa Uhindi. Katika hali nzuri ya kiekolojia na hali nzuri ya hewa, vizazi kadhaa vinaweza kuandamana na kusababisha makundi kujiunda na kuvamia nchi pande zote za eneo la upungufu, kaskazini hadi Uhispania na Urusi, kusini hadi Nijeria na Kenya na mashariki hadi Uhindi na kusini magharibi mwa Asia. Nchi kama 60 zinaweza kuathiriwa katika eneo la km² milioni 32 au takriban asilimia 20 ya uso wa dunia.

Kundi la nzige-jangwa huko Sahara ya Magharibi

Makundi ya nzige huruka juu ya upepo kwa takriban kasi ya upepo. Yanaweza kupita km 100 hadi 200 kwa siku na yataruka hadi takriban m 2000 juu ya usawa wa bahari (juu ya mwinuko mkubwa zaidi nyuzijoto inakuwa baridi sana). Kwa hivyo makundi hayawezi kuvuka safu za milima mirefu kama Milima ya Atlas, ya Hindu Kush au ya Himalaya. Hayatajiingiza kwenye misitu ya mvua ya Afrika wala katika Ulaya ya Kati. Walakini, mara kwa mara makundi ya mapevu huvuka Bahari ya Shamu kati ya Afrika na Bara Arabu na hata wameripotiwa kuvuka Bahari ya Atlantiki kutoka Afrika mpaka Visiwa vya Karibi katika siku kumi wakati wa tauni ya 1987-89.

Kundi moja linaweza kufunika hadi km² 2000 na linaweza kuwa na nzige milioni 40 hadi 80 kwa km². Kundi la km² 500 kwa hivyo lina nzige bilioni 20 hadi 40 na uzito wa tani 40,000 hadi 80,000 ukizingatia wastani wa gramu mbili kwa nzige. Kutoka kizazi kimoja hadi kingine idadi ya nzige inaweza kuongeza mara 10 hadi 16.

Nzige-jangwa wa solitaria hula mimea yenye majani mapana inayopatikana katika makazi yao ya jangwa. Hawapendi nyasi sana. Lakini wakiwa gregaria hula mimea takriban yote, pamoja na mazao ya binadamu, na sehemu zote za mimea hiyo: majani, maua, matunda, mbegu na gome. Nzige mmoja hula chakula cha uzito sawa na uzito wa mwili wake kila siku. Mpevu ana uzito wa g 2, kwa hivyo kundi la nzige bilioni moja anakula tani 2000 kwa siku.

Udhibiti

[hariri | hariri chanzo]

Kuonya mapema na kudhibiti ili kuzuia milipuko ni mkakati uliopitishwa na nchi zilizoathiriwa na nzige barani Afrika na Asia kujaribu kuzuia tauni za nzige kuendelea na kuenea. Mnamo miaka ya 1920-1930s, udhibiti wa nzige ulikuwa uwanja mkubwa wa ushirikiano wa kimataifa. Taasisi ya Kilimo ya Kimataifa ilitengeneza miradi kadhaa yenye lengo la kubadilishana data kuhusu nzige-jangwa na mikutano ya kimataifa ilifanyika katika miaka ya 1930: Roma mnamo 1931, Paris mnamo 1932, London mnamo 1934, Kairo mnamo 1936 na Brussels mnamo 1938. Milki za kikoloni zilihusika sana katika majaribio haya ya kudhibiti nzige wasumbufu ambao waliathiri sana Mashariki ya Kati na sehemu za Afrika. USSR pia ilitumia udhibiti wa nzige kama njia ya kupanua ushawishi wake katika Mashariki ya Kati na Asia ya Kati.

Huduma ya Taarifa za Nzige-Jangwa (Desert Locust Information Service au DLIS) ya FAO huko Roma, Italia, inafuatilia hali ya hewa, hali ya kiekolojia na hali ya nzige kila siku. DLIS inapokea matokeo ya utendaji wa ukaguzi na udhibiti unaofanywa na timu za kitaifa katika nchi zilizoathirika na inachanganya habari hizi na data za sateliti kama vile MODIS, makadirio ya mvua na matabiri ya joto na mvua ya kimsimu ili kuchanganua hali ya kisasa na kutabiri wakati, kiwango na mahali pa kuzaliana na uhamiaji hadi wiki sita zilizotangulia. Tathmini za hali na matabiri huchapishwa katika majarida ya nzige ya kila mwezi yanayoanzia miaka ya 1970. Hayo yanaongezewa kwa maonyo na chonjo kwa nchi zilizoathirika na kwa jamii ya kimataifa. Yale tangu miaka ya 1990 yanapatikana kwenye tovuti ya FAO Locust Watch. FAO pia hutoa taarifa na mafunzo kwa nchi zilizoathirika na kuratibu ufadhili kutoka kwa mashirika ya wafadhili ikiwa kuna milipuko mikubwa na tauni.

Nzige-jangwa ni msumbufu mgumu kudhibiti na hatua za udhibiti zinatatizwa zaidi na maeneo makubwa yaliyo mbali mara nyingi ( km² milioni 16-30) ambapo nzige wanaweza kupatikana. Miundombinu ya kimsingi isiyosimamiwa katika nchi kadhaa zilizoathirika, rasilimali chache kwa ufuatiliaji na udhibiti wa nzige na msukosuko wa kisiasa ndani na kati ya nchi zilizoathirika hupunguza uwezo wa nchi kufanya shughuli za ufuatiliaji na udhibiti.

Kwa sasa njia kuu ya kudhibiti uvamizi wa nzige-jangwa ni kutumia viuawadudu, haswa fosfati ogania kama fenitrothion, malathion na chlorpyrifos. Hivi vinapulizwa kwa vipimo vidogo vya ukolevu wa juu kwa vyombo vya kupulizia vilivyopandishwa kwenye magari au ndege kwa viwango vya matumizi vya mjao wa chini kabisa (ultra-low volume au ULV). Mdudu hupata kiuawadudu moja kwa moja au kupitia uokotaji wa sekondari (yaani kukanyaga au kula mabaki kwenye mimea). Udhibiti hufanywa na mashirika ya serikali katika nchi zilizoathirika na nzige au na mashirika maalum kama vile Shirika la Udhibiti wa Nzige-Jangwa kwa Afrika ya Mashariki (Desert Locust Control Organization for East Africa au DLCO-EA).

Nzige-jangwa ana maadui wa asili kama vile nyigu na nzi mbuai, nyigu vidusia, lava wa mbawakawa, ndege na watambaazi. Hao wanaweza kuwa na ufanisi katika kudhibiti idadi ya wadudu wa solitaria lakini wana athari ndogo dhidi ya nzige-jangwa wa gregaria kwa sababu ya idadi kubwa sana ya wadudu katika makundi ya wapevu na ya tunutu.

Mara nyingi wakulima hujaribu njia za kimakanika za kuua nzige kama vile kuchimba mitaro na kuzika makundi ya tunutu, lakini hii inahitaji kazi nyuingi na ni ngumu kufanya wakati uvamizi mkubwa umetawanyika kwenye eneo kubwa. Wakulima pia hujaribu kuogofya makundi ya nzige mbali na mashamba yao kwa kufanya kelele, kuchoma tairi au njia nyingine. Hii inaelekea kuhamisha shida kwenye mashamba jirani, na makundi ya nzige yanaweza kurudi tena kwa urahisi kwenye mashamba yaliyotembelewa hapo awali.

Dawa za kibiolojia

[hariri | hariri chanzo]

Dawa za kibiolojia zinajumuisha kuvu, bakteria, uto wa mbegu za mwarobaini na feromoni. Ufanisi wa dawa nyingi za kibiolojia ni sawa na ule wa dawa za kemikali za kawaida, lakini kuna tofauti. Kwa ujumla dawa za kibiolojia huchukua muda mrefu zaidi kuua wadudu, magugu au magonjwa ya mimea, kwa kawaida kati ya siku 2 na 10.

Kuna aina mbili za dawa za kibiolojia, biokemikali na vijidudu. Dawa za biokemikali ni sawa na kemikali zinazotokea kwa asili lakini zina sumu isiyo kali sana au hazina sumu, kama vile feromoni zinazotumiwa kupata wenzake wa jinsia nyingine. Dawa za kibiolojia zenye vijidudu zina bakteria, kuvu, miani au virusi ambayo inatokea kwa asili au imebadilishwa vinasaba. Kuvu viuawadudu hukandamiza wasumbufu kwa uambukizaji kwa ujumla: kusababisha ugonjwa ambao ni maalum kwa wadudu.

Bidhaa za udhibiti wa kibiolojia zimekuwa zikiendelewa tangu miaka ya mwisho ya tisini, haswa bidhaa zilizo na kuvu ya asili iliyo pathojeni wa wadudu (yaani kuvu inayoambukiza wadudu), Metarhizium acridum. Spishi za Metarhizium zinaenea duniani kote na zinaambukiza vikundi vingi vya wadudu, lakini zinaonyesha hatari ndogo kwa wanadamu, mamalia wengine na ndege. M. acridum inaambukiza tu panzi wenye vipapasio vifupi, kikundi ambacho nzige ni wana wake, na kwa hivyo imechaguliwa kama kiambato kiamilifu cha bidhaa hizo. Ni salama mno kwa sababu haitoi sumu kama hufanya spishi nyingine za Metarhizium.

Bidhaa inayopatikana sasa katika Afrika na Asia ya Kati, inaitwa NOVACRID. Bidhaa nyingine, Green Muscle, iliyobuniwa katika mradi LUBILOSA, ilipatikana hapo zamani lakini ikatoweka kutoka soko hadi hivi karibuni, wakati leseni ya uuzaji ilipewa kampuni nyingine. Bidhaa hizo zinatumika kwa njia ile ile kama dawa za kikemikali, lakini haziui haraka kama zile. Kwa vipimo vilivyopendekezwa kuvu inaweza kuchukua wiki mbili hadi tatu kuua hadi 90% ya nzige. Kwa sababu hiyo inashauriwa kutumiwa hasa dhidi ya tunutu. Hao hupatikana zaidi katika jangwa, mbali na maeneo ya mazao, ambapo kuchelewesha kwa kifo hailetei uharibifu wa mazao kwa kawaida. Faida ya bidhaa ni kwamba zinaathiri panzi na nzige tu, ambayo hufanya ziwe salama sana kuliko viuawadudu vya kikemikali. Hasa, inaruhusu maadui wa asili wa nzige na panzi kuendelea na kazi yao ya faida. Hao wanajumuisha ndege, nyigu vidusia na mbuai, nzi vidusia na spishi fulani za mbawakawa. Ingawa maadui wa asili hawawezi kuzuia tauni, wanaweza kupunguza marudio ya milipuko na kuchangia udhibiti wao. Dawa za kibiolojia zinapendekezwa hasa kutumika katika maeneo ya mazingira nyeti kama hifadhi za kitaifa au karibu na mito na miili mingine ya maji.