Tinini (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Tinini (Draco) katika sehemu zao ya angani
Ramani ya Tinini-Draco, kwa macho ya mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia

Tinini (kwa Kilatini na Kiingereza Draco) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kaskazini ya dunia yetu.

Jina

Tinini ni jina lililotumiwa tangu zamani na mabaharia Waswahili waliojua njia yao baharini wakati wa usiku wakiangalia nyota[2]. Jina hili waliwahi kupokea kutoka Waarabu walioiita التنين at-tinniin na hili ni tafsiri ya Kigiriki Δράκων drakon (Draco kwa tahajia ya Kilatini).

Draco ilikuwa moja ya makundinyota 48 yaliyoorodheshwa na Klaudio Ptolemaio. Ilipokelewa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia katika orodha ya makundinyota 88 ya kisasa iliyotolewa mwaka 1930. [3] Kifupi rasmi ni ‘Dra’.[4]

Katika mitholojia ya Ulaya na Mashariki ya Kati Tinini au dragoni ni mnyama mkubwa mwenye umbo kama nyoka au mjusi, akiwa na miguu minne na mabawa mawili anayeweza kutema moto. Katika mitholojia ya Kigiriki ni Herakles alipambana pia na dragoni. Kundinyota Rakisi linalolingana na lile ya kumkumbuka Herakles (lat. Hercules) liko jirani na Tinini (Draco).

Mahali pake

Tinini - Draco iko katika karibu na ncha ya anga ya kaskazini, hivyo inaonekana kisehemu tu katika Afrika ya Mashariki na sehemu za nyota zake huwa chini ya upeo wa macho.

Inapaka na makundinyota jirani ya Dubu Mdogo (Ursa Minor), Dubu Mkubwa (Ursa Major), Bakari (Bootes), Rakisi (Hercules), Kinubi (Lyra), Dajaja (Cygnus) na Kifausi (Cepheus).

Nyota

Tinini - Draco ni kundinyota kubwa lenye nyota nyingi.

γ Gamma Draconis au “Etanin" ni nyota angavu zaidi. Ina mwangaza unaoonekana wa 2.2 ikuwa na umbali unaokadiriwa kuwa miakanuru 148[5]. Mwendo wake katika anga-nje unaelekea kwetu na katika miaka milioni 1.5 itakaribia hadi umbali wa miakanuru 28 na kuwa nyota angavu kabisa angani[6].


Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
γ 33 Etamin au Eltanin 2,23m 150 K5 III
η 14 Aldhibain, Al Dhibain 2,74m 80 G8 III
β 23 Alwaid 2,79m 400 G2 II
δ 57 Altais 3,07m 100 G9 III
ζ 22 Aldhibah 3,17m 300 B6 III
ι 12 Edasich 3,29m 102 K2 III
χ 44 3,57m 25 F7 V
α 11 Thuban 3,65m 300 A0 III
ξ 32 Grumium 3,7m ca. 110 K2 III
ε 63 Tyl 3,83m 147 G7 + K5
λ 1 Gianfar 3,8m ca. 330 M0 III

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Draco" katika lugha ya Kilatini ni "Draconis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Draconis, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Oktoba 2017
  4. "The IAU list of the 88 constellations and their abbreviations" ya mwaka 1922, kwenye tovuti ya Ian Ridpath, iliangaliwa Mei 2017
  5. Draco, tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. Eltanin (Alfa Draconis), Tovuti ya Prof. Jim Kaler

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 202 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331